ENDELEA KUPOKEA ADVENTIST WORLD KISWAHILI

Tunawathamini na kuwatambua wote waliojisajili na tuna taarifa mpya na za kusisimua kuhusu jinsi mnaweza kuendelea kusoma na kupata Adventist World.

KULIPATA KWENYE WHATSAPP

Kwa sababu ya umaarufu wa kulipata jarida hilo kwenye WhatsApp, tunahamia kwenye mfumo mpya wa kutangaza ambao utatuwezesha kuwasiliana nanyi mara kwa mara. Bonyeza kiungo kilicho hapo chini kujiunga na chaneli ya WhatsApp Broadcast ambapo tutakujulisha toleo jipya linapokuwepo.

KULIPATA KWENYE TOVUTI

Lipate jarida hilo kwenye tovuti yetu, kwa kukibonyeza kiungo kilicho hapo chini:

Tovuti hiyo vilevile inabeba Adventist World kwa lugha anuwai.

KULIPATA KWENYE FACEBOOK

Kiungo cha toleo la hivi karibuni la Adventist World huwekwa kwenye Ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi. Kwa “Liking” ukurasa huu utapokea taarifa zetu mpya na kuweza kututumia jumbe ukiwa na majibu yoyote.

HIFADHI MAKTABA YA JARIDA LA KISWAHILI KWENYE SIMU YAKO AU KOMPYUTA

Tumetengeneza maktaba ya kidijitali ya majarida yote ya Adventist World. Ili kulipata kusanyo hili kwa urahisi kwenye simu yako, fuata hatua zilizo hapo chini:

 

Bonyeza kiungo kilicho hapo chini ili kuipata maktaba.

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 

AU

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 


Kwa maoni yoyote au majibu, tafadhali jiskie huru kututumia barua pepe kwenye kwambokaj@ecd.adventist.org. Tunapenda kusikia kutoka kwako na tunatazamia uhusiano mzuri na wasomaji wetu wa Adventist World-Kiswahili.

Asante sana na Mungu awabariki,
Timu ya Adventist World-Kiswahili

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa kwambokaj@ecd.adventist.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

Picha ya jalada: artplus / iStock / Getty Images Plus / Getty Images

Mkusanyiko wa Kiulimwengu wa Patakatifu 

Na Justin Kim

Kati ya mafundisho yetu yote, mada ya patakatifu ni moja ambayo tumeanza tu kugundua ukweli wa kiroho. Ellen White alisema, “[Patakatifu] palifungua mfumo kamili wa ukweli, ulioshikamana na kuafikiana, ukionyesha kuwa mkono wa Mungu uliongoza vuguvugu kuu la marejeo na ulifunua wajibu wa sasa kwa kuonyesha nafasi na kazi ya watu Wake. . . . Nuru kutoka katika hekalu iliangazia wakati uliopita, wakati uliopo, na wakati ujao.”1

 

Somo kuu linalotokana na patakatifu lina usawa. Mara nyingi tunaona kama nguzo mbili na kupima katikati kama kituo. Lakini patakatifu panatoa, si ishara mbili tu, bali tatu: uga, mahali patakatifu, na patakatifu pa patakatifu. Hapa kuna baadhi ya mahusiano ambapo pembe tatu inaonekana:

Kama mpangilio wa kinabii wa nyakati za mwisho, uga unawakilisha huduma ya Kristo alipokuwa duniani, akitoa damu ya ukombozi ili kuanzisha mfumo wa wokovu wa hekalu la mbinguni. Mahali patakatifu palikuwa mahali ambapo Kristo alihudumu tangu kupaa Kwake hadi mwaka 1844, wakati patakatifu palipotakaswa. Patakatifu pa patakatifu panahusiana na hukumu ya upelelezi ya utakaso huu inayoelekea mwisho wa nyakati. Kwa kuwa hakuna chumba cha nne, Kuhani Mkuu anatoka kwa njia ile ile aliyopitia kuingia, akirudi duniani. 

 

Katika wokovu, uga unalingana na kuhesabiwa haki, ambapo damu na maji vinawakilisha kuhesabiwa haki. Mahali patakatifu panahusiana na utakaso, ambapo mkate na nuru vinawakilisha haki inayotolewa ndani yetu. Patakatifu pa patakatifu panaelekeza kwenye utukufu, ambapo sisi, kupitia sifa za Kuhani wetu Mkuu, tutapata fursa ya kumwona Mungu moja kwa moja siku moja.

 

Hatimaye, jumuiya mbalimbali za kanisa la Kikristo huwa zinazingatia vipengele vya sehemu tofauti za hekalu. Waprotestanti wanahimidi kwa haki msalaba wa Kristo, kama inavyoonekana katika Mwanakondoo wa Mungu aliyewakilishwa na uga, lakini mara nyingi huishia hapo mapema mno. Wakatoliki wa Roma wanasisitiza chombo cha kanisa lao katika mchakato wa utakaso kupitia sakramenti (kwa mfano, mkate wa Ekaristi) na vitu vya kidini kama mishumaa (nuru) na ubani. Wapentekoste na wakarismatiki wanatangaza enzi ya nguvu, wakitazamia utukufu kupitia uhusiano wa karibu wa ana kwa ana na Mungu.

 

Waadventista wako wapi? Si katika moja, si katika mbili, bali zote tatu zinapaswa kuwa na uwiano sahihi. Tunasherehekea dhabihu ya Yesu, upatanishi wa Yesu na hukumu ya Yesu. Tunahakikisha uwiano kati ya kuhesabiwa haki, utakaso na utukufu. Tunajulishwa kiunabii kwamba mkusanyiko wa watu hawa wa damu, wa watakatifu, na wenye nguvu wataunganishwa kwa msingi wa patakatifu pa duniani.2 Basi na tuwaunganishe wafuasi wa Yesu kutoka pande zote za ulimwengu na kuwaelekeza kwenye huduma ya Kristo katika hekalu la mbinguni.

1 Ellen G. White, Pambano Kuu (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1911), uk. 351. 

 

2 Ellen G. White, Maranatha (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1976), uk. 190.

Picha: Adventist Record

Zaidi ya Waadventista 1,200 kutoka Visiwa vya Vanuatu, Solomon na New Caledonia walikusanyika pamoja katika bandari ya Vila kwa ajili ya Mkutano wa Ustawi wa Nchi ya Vanuatu kutoka Desemba 6 hadi 15. Wakati wa mkutano washiriki pia walishiriki katika kuifikia jamii, kama inavyoonekana hapa.

“Ukarimu wa watu wetu unatia moyo. Kwa kweli wanaishi kwa kusudi letu la kubadilisha maisha kila siku kupitia afya ya mtu na walikusanyika pamoja ili kusaidia wale waliowahitaji katika jamii tunayoihudumia.”

— Todd Saunders, meneja mkuu mtendaji wa Santariamu nchini Australia na New Zealand, akizungumzia wafanyakazi wa kampuni ya chakula ambao walichangia zaidi ya dola za Kimarekani 3,400 kwa ajili ya kampeni ya kila mwaka ya Coast Shelter. Zaidi ya hayo, Santariamu ilishangaza shirika hilo kwa donge la dola za Kimarekani 12,400 ili kuhakikisha kuwa programu zake muhimu zinaendelea katika mwaka 2025 na kuendelea. Coast Shelter inafanya kazi katika Pwani ya Kati ya New South Wales, Australia, ikitoa huduma na msaada kwa watu wanaokutana na tatizo la ukosefu wa makazi au unyanyasaji wa kijinsia na familia.

Maombi na Mitandao ya Kijamii

Washiriki wa kanisa ulimwenguni kote waliulizwa kama wanaomba au wanashiriki katika maombi kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.

“Eneo hili lilianzishwa kwa nia ya kuwafanya watu wawe karibu na Mungu na kuweka mazingira ya amani, tafakari, sifa na ushirika. Ni mahali panapowakaribisha wote, kama vile msalaba unavyoonyesha, ambapo kila mtu anakaribishwa.”

— António Amorim, mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Kati huko Lisbon, Ureno, akizungumzia maadhimisho ya miaka mia moja ya kanisa hilo. Sabato, tarehe 23 Novemba, ilijaa sherehe za kuwepo kwa kanisa hilo pamoja na usanifu wake. Kanisa hili lilijengwa mwaka 1924 na lilibuniwa na msanifu majengo maarufu Porfírio Pardal Monteiro. Ni alama ya kihistoria na usanifu majengo katika mji mkuu wa Ureno. Vilevile, Huduma ya Posta ya Kitaifa ilizindua kadi ya posta ya kumbukumbu kuashiria tukio hili, ambalo linaadhimisha historia na matokeo ya jengo la kanisa la Waadventista la Sabato huko Lisbon.

“Hii ni hatua kubwa ya kuendelea kutoa huduma kwa wasioona nchini Kanada, na ni rasilimali nzuri kwa makanisa kushiriki na wale wenye changamoto za kuona katika jamii zao. Ushirikiano wetu wa miaka mitatu utasaidia kubadilisha mandhari ya huduma ambazo makanisa yetu yanaweza kutoa kwa jamii zao.”

— Paul Llewellyn, mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Kanada, akizungumzia mkataba mpya wa miaka mitatu na Christian Record Services. Ushirikiano huu, utakaoanza mwaka 2025 hadi 2027, utaimarisha ubora wa maisha kwa watu wengi nchini Kanada. Mkataba huu unahakikisha kwamba wanachama wataendelea kupokea rasilimali muhimu bila gharama za ziada. Hii ni pamoja na upatikanaji wa programu tumishi ya maktaba ya mtandaoni, Mwongozo wa Kujifunza Biblia kwa Watu Wazima na usajili wa magazeti ya Christian Record Services.

Idadi ya watu waliokutana uso kwa uso kwa ajili ya tamasha la tatu la filamu lililofanyika Caracas, Venezuela, mnamo Novemba 30. Gala ya UVOFILMS 2024 ilijumuisha mada inayohusiana na imani ya Kikristo, “Familia.” Kwa jumla, uzinduzi wa filamu 17 ulionyeshwa katika makundi manne: masimulizi ya kubuni, video fupi, dokumentari, na rekodi ya sauti. Katika miezi mitatu kabla ya tukio hili, zaidi ya wazalishaji 20 walishiriki katika warsha na kupokea mwongozo kutoka kwa majaji na wageni wengine, ikiwa ni pamoja na wale ambao hawakufika katika uteuzi wa mwisho.

Idadi ya wanamuziki vijana kutoka Kanisa la Chuo cha Kimataifa cha Asia-Pasifiki nchini Thailand waliamua kutumia mapumziko yao mafupi ya sikukuu ya mwisho wa mwaka kusafiri hadi Hong Kong na Macao, mojawapo ya maeneo yenye gharama kubwa zaidi ulimwenguni. Kupitia maombi, imani na mipango, kundi hili liliweza kushiriki upendo wao kwa ajili ya Yesu na kubadilishana thamani za kitamaduni kupitia muziki katika makanisa na shule za Waadventista kutoka Desemba 13 hadi 17. Kundi hili lilifanya maonyesho ya muziki yaliyogusa mandhari ya furaha, matumaini na shukrani.

Mpango huu unaleta afueni kwa jamii zilizo hatarini. 

Habari ya ADRA Haiti na Divisheni ya Amerika-Kati

Katika kukabiliana na mgogoro wa chakula unaozidi kuongezeka katika Caracol, eneo la kaskazini-mashariki mwa Haiti, Shirika la Maendeleo na Misaada la Waadventista (ADRA) nchini humo hivi karibuni liligawa mamia ya pakiti za chakula muhimu katika Shule ya Taifa ya Caracol. Mradi huu unalenga kupunguza mateso makali yanayozikumba familia zilizo hatarini zaidi katika eneo hilo.

 

 

MGOGORO UNAOKUA

Katika eneo la Trou-du-Nord, Idara ya Kaskazini-Mashariki mwa Haiti, Caracol inakabiliwa na mgogoro mkali wa chakula unaozidishwa na hali ya usalama inayozorota nchini humo. Hali hii imewaacha watu wengi wakiwa na uhitaji mkubwa wa msaada wa haraka, viongozi wa ADRA Haiti walisema. Timu ya dharura ya ADRA Haiti ilijipanga haraka kuzindua Mpango wa Dharura wa Msaada wa Chakula na Fedha (EFACH), kwa kushirikiana na Hazina ya Nafaka ya Kanada (Canadian Foodgrains Bank) na ADRA Kanada, mwezi uliopita.

 

“Kufuatia taarifa za hivi karibuni zinazoonyesha ukali wa mgogoro huu wa chakula, tulielewa haraka umuhimu wa kuingilia kati huko Caracol,” alisema Myrlaine Jean Pierre, mkurugenzi wa ADRA Haiti. “Hatutahangaika kutekeleza mradi huu kwa kushirikiana na wabia wenzetu ili kupunguza mateso ya watu hawa waliokumbwa na janga kubwa.”

 

Kuanzia Desemba 2024 hadi Februari 2025, mradi utasambaza msaada wa chakula kwa takribani watu 8,560 kutoka kaya 1,070 katika awamu tatu, alisema. Kila pakiti ya chakula, iliyogawiwa katika Shule ya Taifa ya Caracol tarehe 16 Desemba, ilijumuisha mfuko wa mchele wenye kilo 25 (paundi 55), mfuko wa maharagwe wenye kilo 12.5 (paundi 27.5), mfuko wa mahindi wenye kilo 12.5, pakiti za tambi 24, sukari ya kilo 2.5 (paundi 5.5), na lita 5.7 (takribani galoni 1.5) za mafuta ya kupikia. Vilevile, kila mpokeaji alipokea uhamisho wa fedha wa dola za Kimarekani 30 ili kusaidia zaidi mahitaji yao ya haraka.

 

 

KUSAIDIA JAMII ZILIZO HATARINI

Kwa wakazi wengi wa Caracol, misaada hii ilikuwapo kama kimbilio katikati ya msimu wa likizo wenye changamoto. Anita, mkazi mwenye miaka 80 wa kijiji hicho, alielezea faraja yake: “Ni Mungu mwenyewe anayetuzuru katika kipindi hiki kigumu. Shukrani kwa msaada huu, sina hofu tena ya mwisho wa mwaka huu.”

 

Ugawaji wa chakula pia unaangazia tatizo kubwa la uhaba wa chakula linalokumba karibu nusu ya idadi ya watu wa Haiti. Kulingana na taarifa ya hivi karibuni ya Viashiria vya Bei za Walaji (Consumer Price Index [CPI]) kutoka Uratibu wa Usalama wa Chakula wa Taifa (National Food Security Coordination [CNSA]), Shirika la Chakula na Kilimo (Food and Agriculture Organization [FAO]) na Mpango wa Chakula wa Ulimwenguni (World Food Program [WFP]), asilimia 48 ya Wahaiti wanakutana na uhaba mkubwa wa chakula. Makundi yaliyo hatarini, ikiwa ni pamoja na watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, wazee na watu wenye mahitaji maalum, ndio wanakutana na athari kubwa za mgogoro unaoendelea.

 

 

JUKUMU LA ADRA KATIKA HUDUMA ZA UBINADAMU

Kadiri Haiti inavyoendelea kukutana na hali ya kisiasa isiyotabirika na shida za kiuchumi, msaada huu wa dharura unaonyesha kujitolea kwa ADRA katika kutoa msaada muhimu wakati wa mahitaji, alisema Jean Pierre. Kwa kuchukua hatua za haraka kukutana na mahitaji ya haraka ya wale wanaosumbuliwa zaidi, ADRA Haiti inachukua jukumu muhimu katika kupunguza mzigo wa uhaba wa chakula na kufanya kazi kuelekea mustakabali wenye matumaini kwa watu wa Caracol, alieleza.

 

“Msaada huu wa wakati mwafaka unaotolewa na ADRA unaakisi kujitolea kwetu katika kupunguza mateso ya watu hawa walio katika hali ngumu na kufanya kazi kwa ajili ya mustakabali bora,” alisema.

Wamishonari wa kwanza kufika nchini waliwasili Bougainville mwaka 1924. 

Reeves Papaol, Adventist Record na Adventist World

Kuanzia Desemba 18 hadi 31, 2024, zaidi ya watu 4,000, wakiwemo viongozi wa kanisa, maafisa wa serikali na waumini kutoka Papua New Guinea (PNG) yote na Visiwa vya Solomon, walikusanyika kuadhimisha sherehe za miaka 100 ya Utume wa Waadventista wa Sabato Bougainville. Kanisa la Waadventista wa Sabato katika eneo hilo liliadhimisha miaka 100 ya imani, huduma na mchango kwa jamii. Ingawa Bougainville ni sehemu ya Papua New Guinea, kijiografia ni sehemu ya fungu-visiwa vya Solomon.

 

Washiriki wa sherehe walijumuisha kutoka mtoto wa miezi 4 hadi bibi mwenye umri wa miaka 94, wote wakihamasishwa na kaulimbiu “Tukiadhimisha Miaka 100 ya Kisa cha Mungu katika Bougainville.”

 

Sherehe hizi zilifanyika katika maeneo matatu ya kihistoria, yakiwemo Lavelai, ambako wamishonari wa kwanza waliwasili mwaka 1924, Kastorita, ambako wamishonari walifika kwa mashua na kwa miguu mwaka 1927, na Rumba, Arawa, ambako ofisi ya misheni ilianzishwa mwaka 1929. Kila eneo lilikuwa na ibada za kutabaruku, uzinduzi wa makumbusho, siku tatu za uamsho, masimulizi ya kihistoria kutoka kwa wawakilishi wa familia za waanzilishi, na maonyesho ya kitamaduni, yakiwemo maigizo ya ujio wa wamishonari. Katika maeneo yote, zaidi ya watu 200 walibatizwa.

 

 

UONGOZI NA NJOZI

Viongozi wa serikali na kanisa walihudhuria sherehe hizo na kushiriki ujumbe wa motisha na njozi kwa siku zijazo. Miongoni mwao alikuwa James Marape, waziri mkuu wa Papua New Guinea. Alielezea uhusiano wake binafsi na urithi wa Utume wa Waadventista.

 

Alisema, “Kama isingekuwa wamishonari wa awali wa Bougainville walioleta utume huu hadi Tari mwaka 1955, nisingekuwa mtu au kiongozi niliye leo.” Akitafakari athari za mabadiliko ya maisha ya utume huu, alieleza kuwa baba yake, Mchungaji John Marape, alinufaika moja kwa moja kwa kazi ya Utume wa Waadventista.

 

Waziri mkuu alisisitiza, “Makanisa yote makuu nchini PNG yanapaswa kuendelea kuifikia jamii, vijiji na watu kwa ujumla ili kuendeleza amani, elimu, afya na kuishi maisha yenye uwiano. Hii ndiyo kazi halisi ya utume wa makanisa.”

 

Peter Tsiamalili, Jr., waziri wa polisi na mwakilishi wa Bougainville, alieleza jinsi Kanisa la Waadventista wa Sabato limeimarisha mshikamano na ukuaji wa kiroho, akitambua mchango wake mkubwa kwa jamii.

 

Francisca Semoso, mwakilishi wa Kaskazini mwa Bougainville, alisisitiza umuhimu wa wanawake na watoto katika kazi ya umishonari, akisema, “Malezi huanzia nyumbani, watoto wetu ndio jamii tunayoijenga kwa siku zijazo.”

 

Timothy Masiu, waziri wa mawasiliano na mwakilishi wa Kusini mwa Bougainville, alitoa wito wa uwajibikaji katika uongozi wa kanisa, akiwahimiza wachungaji kuongoza katika kuhamasisha amani na wema katika jamii.

 

Kutoka kwa kanisa, Malachi Yani, mwenyekiti wa Union Misheni ya Papua New Guinea, aliwatia moyo wakazi wa Bougainville kuongeza sauti zao na kujitwika jukumu la safari yao ya kiroho. Vilevile, Danny Philip, mkurugenzi wa mkakati wa uanafunzi wa Divisheni ya Pasifiki Kusini, alihimiza Kanisa la Waadventista wa Sabato katika ukanda wa Pasifiki kuongoza mabadiliko ya kweli katika maeneo yote wanayohudumu, hasa Bougainville.

 

Hafla hiyo pia ilifunua malengo makubwa, yakiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Waadventista ya Green Valley huko Buin kwa wanafunzi wa madarasa ya 7-10, pamoja na ukarabati na uhamishaji wa umiliki wa vituo vya afya katika Kastorita, Wisai, na Darupute, miongoni mwa vingine.

 

 

MATOKEO YA KIROHO NA JAMII

Sherehe ya miaka 100 iliadhimisha hali ya kiroho ya kanisa na mchango wake wa kudumu kwa jamii, viongozi wa kanisa wa kanda walieleza. “Kanisa limethibitisha tena kujitolea kwake kuhudumia Bougainville na maeneo mengine, kuhakikisha kuwa urithi wa imani na huduma unaendelea kwa vizazi vijavyo,” walisema.

Mpango huo umeunganisha huduma ya matibabu pamoja na ustawi wa kiroho katika hospitali binafsi. 

Cristin Serrano, Habari ya Union ya Kolombia Kaskazini na Divisheni ya Amerika–Kati

Kituo kipya kilichozinduliwa kinatoa msaada wa kihisia na kiroho kwa wagonjwa na familia zao katika hospitali binafsi huko Bucaramanga, Kolombia, shukrani kwa juhudi za Kanisa la Waadventista wa Sabato katika eneo hilo.

 

Kituo hiki, ambacho kimezinduliwa katika Hospitali ya Internacional de Colombia, kilifunguliwa rasmi wakati wa hafla iliyohudhuriwa na wafanyakazi wa hospitali na viongozi wa kanisa. Eneo hili lina duka la vitabu likiwa na machapisho ya Chama cha Uchapishaji cha Divisheni ya Amerika–Kati (IADPA), kona ya chakula bora inayohamasisha tabia chanya, pamoja na sehemu inayotoa rasilimali nyingine na bidhaa za sanaa kwa watu wazima na watoto.

 

Kituo hiki, kinachoitwa Letras de Vida (Barua za Uzima), kinahudumu kama kituo cha mvuto kwa msaada wa Konferensi ya Mashariki mwa Kolombia. Lengo lake ni kuhamasisha afya kupitia maarifa ya Mungu, hatua muhimu katika huduma ya hospitali kwa kuunganisha siyo tu matibabu ya kitabibu bali pia msaada wa kihisia na kiroho, kulingana na viongozi wa kanisa mahalia.

 

Jonathan Cáceres Prada, Mwadventista wa Sabato na mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya Internacional de Colombia, ndiye mwenye njozi nyuma ya mpango huo. Anaamini kuwa nafasi hii itatoa faraja kwa wale wanaopitia nyakati ngumu hospitalini hapo.

 

 

MNARA WA MATUMAINI KWA WOTE

Kituo hiki pia kinatoa huduma ya pekee ya kukopesha vitabu kwa mfumo wa gari la vitabu (bookmobile), ambacho husambaza vitabu moja kwa moja hadi vyumbani mwa wagonjwa. Kwa zaidi ya vitabu 100 vinavyopatikana, mkusanyiko huu unashughulikia mada kama vile maendeleo binafsi, maisha ya kiroho, uimara wa familia na afya. Wagonjwa wanaweza kuomba vitabu kupitia tovuti rasmi ya kituo hicho, ambako watapokea huduma maalum kupitia kipengele cha mazungumzo mtandaoni.

 

“Kwa mwongozo wa Mungu, tunaanza sura mpya. Letras de Vida ni mnara wa taa utakaowaongoza watu wengi bila shaka,” alisema Cáceres wakati wa uzinduzi wa kituo hicho mnamo Desemba 6, 2024. “Asanteni nyote kwa kuwa sehemu ya njozi hii ambayo sasa imekuwa halisi.”

 

Kituo hiki kimepokea msaada mkubwa kutoka katika Konferensi ya Mashariki mwa Kolombia, inayoratibu huduma za kimishonari za kujitolea ndani na kimataifa kupitia mpango wake wa Shule ya Utume, imekuwa sehemu ya juhudi hizi. Kama sehemu ya ushirikiano huu, kituo hiki pia kinatoa msaada wa kuzuia kujiua na huandaa miradi ya kijamii inayoendeshwa na wanaojitolea, huku kikialika ushiriki kutoka kwa jamii yote ya hospitali.

 

Elie Henry, mwenyekiti wa Divisheni ya Amerika-Kati, aliwapongeza viongozi wa hospitali na kanisa kwa juhudi zao za kushughulikia mahitaji ya wagonjwa, familia zao, wageni na wafanyakazi wa hospitali. “Tunamsifu Mungu kwa nafasi hii maalum, ambayo itatoa fursa za kuungana na wale wanaougua na wanaohitaji uponyaji na tumaini,” alisema.

 

 

MATOKEO NJE YA HOSPITALI

Uzinduzi wa Letras de Vida ulipata umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari vya eneo hilo, ukionyesha matokeo chanya ya mpango huo. “Miradi kama hii inaimarisha utume wa Waadventista wa Huduma kwa jamii, kuleta tumaini na ustawi zaidi ya waumini wa kanisa,” walisema viongozi wa kanisa.

 

Cáceres aliongeza, “Kuwa na fursa ya kusambaza vitabu vilivyojawa tumaini kwa wale wanaovihitaji zaidi, kuwapa mwongozo na mwelekeo wa kurejeshwa, ni baraka kubwa, na haya yote yamewezekana kwa neema ya Mungu.”

 

Letras de Vida inatarajiwa siyo tu kuboresha ubora wa maisha kwa wagonjwa na familia zao, bali pia kuleta hali ya utu katika mazingira ya hospitali kwa kutoa nafasi ya faraja na tafakari. Kituo hiki kiko wazi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.

Kupitia kujitolea, Ellen Lopes anatafuta njia za kuwahudumia watu nje ya mipaka. 

Cristina Levano, Divisheni ya Amerika Kusini na Adventist World

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Ellen Lopes alijikuta akihitaji kufanya uamuzi utakaobaini maisha yake. Alikuwa ameota kuwa mmishonari, lakini hakuwa na uhakika wa jinsi ya kuanza safari hiyo. 

 

Wakati wa mpango wa ibada ulioitwa “Mawio 40 Pamoja na Mungu,” Ellen alianza kuomba kwa bidii kwa ajili ya mwongozo. “Kila ombi lilionekana kuwa kama mazungumzo na Mungu, nilipomwomba anionyeshe hatua inayofuata,” alikumbuka.

 

Jibu lilikuja kupitia fursa ya kusoma katika Taasisi ya Afya ya Wildwood, chuo cha kimishonari nchini Marekani. Huko, Ellen aligundua ulimwengu wa kazi ya utume wa matibabu na akajitosa katika mada ambazo zingebadilisha mtazamo wake wa maisha, kama vile kuishi maisha yenye afya na kula kwa njia bora. “Ilikuwa kana kwamba Mungu amefungua mlango na kusema, ‘Hii ndiyo njia’. Nilijua ingebadili maisha yangu milele,” alisema.

 

 

KUSUDI KUU

Baada ya uzoefu huu wa kipekee, Ellen alirejea Brazil na kuamua kusomea taaluma ya utangazaji katika Chuo Kikuu cha Waadventista wa Sabato cha Brazil (UNASP), akichanganya shauku yake ya mawasiliano na tamaa ya kuhudumu. “Niliona jinsi mawasiliano yalivyoweza kuwa chombo chenye nguvu kwa ajili ya utume. Nilitaka kutumia kile nilichojifunza ili kusaidia kuleta tumaini kwa watu,” alieleza.

 

Akiwa na diploma mkononi, alijiunga na mradi wake wa kwanza mkubwa wa kimishonari nchini Peru. Kwa muda wa miezi sita, Ellen alifanya kazi katika jamii zilizotengwa, akitumia mbinu mbalimbali za mawasiliano kusaidia juhudi za ndani. “Kila siku ilikuwa safari ya kujifunza. Niliiona furaha ya watu walipofikiwa, na hilo liliishibisha nafsi yangu. Hapo ndipo nilithibitisha kuwa kuhudumu ndiko kulikoyapa maisha yangu maana,” alisema.

 

Alirejea Brazil kwa sababu za kifamilia, lakini Ellen hakusahau kuhusu huduma ya utume. Alianza kufanya kazi kama meneja wa masoko katika Shule ya Waadventista ya Central Brazil (zamani ikiitwa IABC) huko Goiás, ambako alipata fursa nyingi za kuhudumu. Ingawa alifikiri kwamba angekaa kwa muda mfupi, shauku yake ya utume katika jamii yake ilimzuia kuondoka.

 

Tangu hapo, Ellen na mume wake, ambaye ni daktari wa meno, wametoa muda wao wa likizo fupi kwa ajili ya miradi ya muda mfupi. “Kila mwaka tunajihusisha katika angalau miradi miwili, yaweza kuwa mahali maalum, kitaifa au hata kimataifa. Huduma ni namna yetu ya kuliishi kusudi la Mungu kwa ajili ya maisha yetu,” alisema.

 

 

UTUME ULIOONGOZWA NA NJOZI 

Miongoni mwa uzoefu mwingi ambao huduma ya kujitolea ulimpatia, Ellen anapenda kukumbuka huduma yake huko Guinea-Bissau, Magharibi mwa Afrika, ambako kwa takribani mwezi mmoja mume wake alifanya huduma za meno zaidi ya 200, wakati yeye akijitolea katika mawasiliano na kusaidia mradi. “Ilifurahisha kuona namna mambo madogo yanavyoweza kubadilisha maisha. Shukrani katika macho ya watu ni kitu ambacho sitaweza kusahau,” alisema.

 

Leo Ellen hutazama nyuma kwa shukrani na kutazama mbele kwa matumaini. Kila mradi, kila uzoefu na kila changamoto inaimarisha hakika yake kwamba utume si tu kazi bali ni mtindo wa maisha. “Maisha huleta maana ikiwa tu tutajiweka tayari kwa Mungu ili kutumika pale anapotuita,” alisema. “Hilo ndilo huchangamsha moyo wangu na kunipatia nguvu ya kuendelea.”

Imani na matendo, ujumbe na utume 

NA JEROME SKINNER

Wakati wa kipindi cha maswali na majibu cha majadiliano katika jopo kuhusu msamaha, mwanamume mwenye sauti inayolia aliuliza, “Unawezaje kupatana pamoja na mtu aliyeua familia yako yote mbele yako?” Swali hili la kutisha liliibua mada muhimu ya moyo. Mtu anawezaje kusamehe na kupatanishwa mbele ya mwovu huyo?

 

Yapo matarajio katika uzoefu wa binadamu wa kupokea rehema na msamaha wa Mungu, wakati, kwa muda huo huo, kunaweza kuwa na ukimya wa kutoa neema ile ile anapokosewa, hususan ikiwa kosa linaonekana kuwa kubwa na lisilo na huruma. Huu mgogoro wa fumbo kati ya msamaha na haki ya Mungu ndiyo kiini cha injili. Kwa kuwa Mungu ndiye, ambaye kwa upande mmoja ni mwingi wa rehema, akituonyesha neema Yake nyingi isiyopimika sisi ambao tulikuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu (Efe. 2:4-8) na wakati huo huo, Yeye ndiye atakaye mwajibisha kila mtu kwa mambo ambayo wameyatenda maishani, pamoja na makosa yasiyotubiwa (Mhu. 12:14; 2 Kor. 5:10). Kwa neema Yake, katika kushughulika na watoto Wake, Mungu daima hutenda kwa haki na uadilifu (Zab. 33:5; 89:14). Kama watoto Wake, watu wa Mungu wanapaswa kujifunza kutoka kwa Mungu jinsi ya kupokea na kuonyesha rehema kwa namna inayoendana na uzoefu wao na Bwana (Zab. 18:25; 97:10).

 

Kwa Wakristo, msalaba ndiyo mahali ambapo ni chanzo kikuu cha msamaha na kanuni ya milele ya haki ya Mungu vinakutana. Kutoka moyoni mwa Mungu, swali ambalo kwa mtazamo wa kibinadamu halina jibu, kama lilivyojadiliwa hapo juu, linapata majibu ya kiteolojia pamoja na mwaliko wa kubadili moyo, ili kuruhusu msamaha na haki ya Mungu kushika nafasi yake ipasavyo katika upatanisho (Zab. 85).

 

 

TABIA YA MUNGU, MSAMAHA NA HAKI

Biblia inatambua uzito wa msamaha kwa kuwasilisha mtazamo mpana unaojumuisha vipengele vya kosa, kimwili, kihisia na kiroho (Zab. 38:1-14) vinavyohitaji (1) msamaha, (2) suluhisho linaloshughulikia kosa, na (3) matokeo yanayolenga upatanisho (Zab. 51). Biblia inafanya hivyo kwa kutumia maneno na taswira mbalimbali zinazoonyesha dhambi (Mwa. 18:20; 1 Yoh. 3:4), madeni (Mt. 6:12; Kol. 2:14), au makosa (Mwa. 50:17; Law. 16:16; Rum. 5:14) yakisamehewa (Mt. 6:12), kuondolewa (Kut. 32:32), kusafishwa (Zab. 51:1), kusitiriwa (Zab. 32:1), kukombolewa (Zab. 69:18; Ufu. 5:9), kufanyiwa upatanisho (Law. 4:20), kusuluhishwa (Mwa. 32:20), kupitwa (Kut. 12:13), na kurejeshwa (Law. 5:15; 2 Kor. 13:9, 11). Maandiko yanasisitiza msamaha wa Mungu na wa wanadamu, ambayo yana mchakato na malengo tofauti lakini yanayounganika (2 Kor. 2:5-11).

 

Msamaha wa Mungu hautegemei sifa au ustahili wa mwenye kosa au aliyekosewa. Msamaha Wake unategemea tu tabia Yake ya upendo, haki, neema na rehema (Kut. 34:6, 7; Dan. 9:18; Mal. 3:6). Kwa kuwa tabia ya Mungu ndiyo msingi wa tendo la msamaha, msamaha hupatikana ndani ya kuwepo Kwake kunakodumu na si kwa kujitenga. Kwa hivyo, wanadamu hawawezi kuibua mioyo yenye kusamehe au kutoa msamaha wa kweli unaoweza kuleta ukombozi bila msukumo wa neema ya Mungu (Kol. 3:13). Ni kutoka kwa Mungu kwamba msamaha huonyeshwa na kupokelewa (Zab. 130:4).

 

Aidha, si kwamba tu msamaha wa Mungu haupatikani kwa kustahili, bali pia ghadhabu ya Mungu dhidi ya dhambi na wenye dhambi ni haki (Rum. 1:18; 5:9-11). Hili linazua swali la haki. Ikiwa wanadamu waliopotoka hawastahili rehema bali ghadhabu, basi sifa kuu ya msamaha inahusiana na haki ya Mungu. Je, Mungu anawezaje kudumisha uaminifu Wake kwa haki na uadilifu Wake katikati ya upotovu na uasi wa wanadamu, huku akionyesha rehema kwa mwenye kosa na faraja kwa waliodhuriwa? (linganisha Zab. 9:12, 13; 10:12; 22:24.)

 

Msalabani, ghadhabu ya Mungu dhidi ya dhambi na rehema ya Mungu kwa wenye dhambi hukutana, na haki ya Mungu inaridhishwa huku ikikusudia kuokoa (Efe. 2:16). Adhabu ya Mungu inahitajika kutokana na kosa lililotendwa. Kwa muumini, kosa hupokea haki yake kupitia dhabihu ya Kristo (Rum. 8:1-4). Kwa njia hii, Mungu anaweza kuwa mwenye haki katika kushikilia kiwango Chake cha mwenye haki kamili na mwenye kuwahesabia haki wenye dhambi ambao hawastahili, lakini wanafaidika milele na neema na rehema Yake (Rum. 3:21-31; Efe. 2:1-10). Kwa namna hii, tendo la kusamehe wengine kwa unyenyekevu na maombi hutambua kuwa ghadhabu ya Mungu imeshughulikiwa kupitia kile ambacho Kristo alifanya msalabani, na hatimaye kupitia huduma Yake ya upatanishi kama Kuhani wetu Mkuu (Rum. 5:9-11; Ufu. 15:1). Hili haliondoi maumivu anayopitia mtu, lakini linatoa uhuru kutoka katika roho ya kisasi na uchungu inayotoka kwa Shetani. Kwa mtazamo wa kibinadamu, hatuwezi kupunguza haki kwa namna inayoweza kuleta fidia ya ndani au ya milele inayoleta amani (Taz. Kol. 1:20). Hivyo basi, msamaha unajumuisha athari za mahusiano kati ya watu pamoja na jinsi Mungu anavyotekeleza haki ya kurejesha kabla ya kuleta haki ya adhabu.

 

 

MSAMAHA, HAKI NA FIDIA

Kupitia kifo cha Yesu kwa niaba yetu na neema ya Mungu, msamaha wa kibinadamu humpa mtu aliyekosewa uhuru moyoni, kwa kuelewa kwamba malipo ya deni linalotokana na kosa hilo kutoka kwa mkosaji yanabaki mikononi mwa Mungu. Wakati mwingine maumivu, athari za muda mrefu, au matokeo ya milele huwa makubwa kiasi kwamba hakuna fidia ya kibinadamu inayoweza kuleta haki kamili katika jambo hilo. Ingawa matumaini yanaweza kuwa kwamba mkosaji atatambua kosa na kukiri na kutubia dhambi, msamaha hauwezi kutegemea kitendo cha mkosaji (Mt. 5:38-42; Rum. 12:17). Pamoja na kusema hayo, ni muhimu kutambua kwamba Mungu anajali kuhusu maumivu na uchungu anaopitia kila mtoto Wake. Anataka watoto Wake waishi wakijua kwamba hawapaswi kuwa na moyo wa kulipiza kisasi, kwa kuwa lengo kuu la Mungu ni kukomboa na kurejesha kile kilichovunjika (Rum. 12:19; 1 Tim. 2:4). Hata hivyo, kilio cha moyo kinaweza kuwa kikubwa zaidi pale ambapo mkosaji anaonekana kufanikiwa licha ya kutenda dhambi bila kuwajibishwa, jambo ambalo linaweza kuwa lenye kuhuzunisha sana (Zab. 94:3). Mtunga Zaburi anawahimiza waaminifu wasifadhaike kwa sababu ya watenda maovu, kwa kuwa hatimaye watakabili dhambi zao ikiwa hawatazitubu (Zab. 37:4, 5; Rum. 12:19).

 

Kutoa msamaha pia kunaweza kuwa jambo gumu kwa sababu ukubwa wa kosa unaweza kuwa mdogo au mkubwa sana, na ingawa uzito na athari zake zinaweza kutofautiana, bado mwito wa kusamehe bila masharti unatolewa katika hali zote hizi (Mt. 18:21, 22).

 

Hili pia linazua maswali kuhusu haki. Katika Maandiko, Mungu alianzisha mfumo wa upatanisho ulioshughulikia makosa kwa kuzingatia nia ya mkosaji, ikiwa ni kwa bahati mbaya, kwa kutojali, au kwa makusudi (Law. 4:20). Mfumo huu ulijumuisha muda wa kutambua kosa (Law. 4:13; Mdo. 17:30). Mtu mwenye hekima, Sulemani, anatambua kwamba, “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya” (Mhu. 8:11).Kwa hakika, waovu wanapotenda mabaya dhidi ya wenye haki, mara nyingi hufanya hivyo kwa uasi, bila kujali matokeo au maumivu waliyosababisha (Zab. 10:6, 11, 13; Isa. 26:10; Rum. 2:4). Kwa kawaida, waovu hutenda uovu (Dan. 12:10). Lakini maumivu na uchungu unaweza kuwa mkali zaidi pale ambapo kosa limetendwa na muumini mwenzako au mpendwa wako (Zab. 41:9; 55:12-14). Ingawa inaweza kuonekana na kuhisiwa tofauti, katika hali zote mbili kosa husababisha tatizo moja na hitaji la upatanisho, ambalo linaweza kujumuisha kitendo cha kurekebisha madhara yaliyosababishwa au kosa lililotendwa (Kut. 22:1; Luka 19:1-10).

 

Tatizo linalosababishwa na kosa na hitaji lake la kushughulikiwa linapaswa kuonekana kama jambo linalohitaji haki. Wakati haki inapozingatiwa, msamaha si suala la kustahili au kutostahili. Makosa yanapotendwa na au dhidi ya wenye haki, mara nyingi wanamwomba Mungu aingilie kati kwa haki Yake (Zab. 7:3-11; 35:24; 43:1; Ufu. 15:3; 19:1, 2). Haki haijumuishi tu kuwajibika kwa makosa bali pia fursa ya fidia na ukombozi hata mbele ya uovu mkubwa (2 Fal. 21:1-18; 2 Nya. 33:10-13).

 

Aidha, mtume Paulo anasema wazi kwamba msamaha ulitolewa kwa waumini wakati bado wakiwa wakosaji dhidi ya Mungu (Rum. 5:8). Kwa hivyo, haki hufanya msamaha kuwa wa lazima na wenye kuwezekana kwa sababu kile ambacho Mungu anawaomba waliokosewa ni kuonyesha neema ile ile waliyopewa kupitia matendo Yake ya haki. Mungu huwapa ushauri huu wale wanaotaka kuwa kama Yeye (Kut. 34:9; Mt. 6:14, 15; Luka 7:44-48; Mt. 5:44-48). Mungu anapotoa msamaha, haandiki makosa katika kumbukumbu za makosa au kuyahifadhi katika akili ili kuyatumia dhidi ya wale waliokwisha kusamehewa (Zab. 130:3; Mika 7:18-20; 1 Kor. 13:5). Badala yake, damu ya Yesu hufuta kumbukumbu ya kosa, akilibeba juu Yake mwenyewe, akitoa dawa ya uponyaji, na kufanya kazi ya kurejesha kile kilichovunjika. Lengo la haki ya Mungu katika mchakato wa msamaha ni upatanisho (2 Kor. 5:17-6:1). Lengo hili ni la msingi katika kutembea na Mungu kiasi kwamba anatuamuru kutafuta upatanisho kabla ya kutoa ibada yetu Kwake (Mt. 5:23-25).

 

Wakati akielezea kuondolewa kwa kosa lisilofaa kwa njia hii, kuondolewa kwa kosa hakukubali tabia hiyo wala hakupendekezi idhini kwa kosa lenyewe.2 Kwa hakika, mtu mwenye hekima anaendelea kusema: “Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake” (Mhu. 8:12). Haki ya Mungu huenda isiwe ya haraka, lakini ni ya hakika. Namna uzoefu unavyopatikana unategemea namna mkosaji anavyohusiana na huduma ya haki ya Mungu. Maarifa ya Mungu hujua namna, lini na kwa kiasi gani alete haki katika mchakato wa msamaha. Kucheleweshwa kwa adhabu si ushahidi wa Mungu kutojali, bali kumekusudiwa kuchochea toba na kutubu ambako Yeye hufanyia kazi, ambayo ni ishara ya haki (Luka 18:1-8; Mdo. 5:30-32).

KUOMBA KWA AJILI YA HAKI

Msimamo wa kudumu wa moyo wa maombi humsaidia mwombaji “uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.” (Zab. 34:14). Kwa kuomba kwa ajili ya haki, tunamwaachia Mungu mchakato wa ukombozi, fidia na suluhu. Maombi yanampatia Mungu fursa kamili ya kuingia mioyoni mwetu kwa njia zinazowezesha upatanisho mbele ya uovu mkubwa. Hii ndiyo haki ya Mungu kupitia injili ya Yesu Kristo inavyofanya kazi. Kazi Yake ya kubadilisha inaweza kubadilisha wauaji kuwa wamishonari (Gal. 1:11-24) na wakosoaji kuwa waumini (Yn. 3; 19:38-42). Na pale msalabani, upendo wa Mungu, ulioonyeshwa katika msamaha na haki ambayo Mungu pekee angechanganya, ulimgeuza mwasi kuwa mtu aliyekombolewa (Luka 23:32-43).3 

 

Vivyo hivyo, tunapojisalimisha kwa Yesu, haki Yake iliyoonyeshwa pale Kalvari inapanua kutakasa dhamiri zetu kutoka kwa matendo ya mauti ya dhambi, ambayo ni pamoja na hamu yetu ya kulipiza kisasi au ukimya wetu wa kusamehe. Mwishowe, Yesu alijitoa kwa ajili yetu ili kutuwezesha kwa nguvu kutafuta kwa bidii kufanya haki, kupenda neema na kutembea kwa unyenyekevu pamoja Naye (Tito 2:14; Mika 6:8).

1 Nukuu za Biblia zimetolewa kwa ruhusa kutoka Swahili Union Version Bible, toleo la 1952. Haki zote zimehifadhiwa. 

 

2 J. David Stark, “Forgiveness,” Lexham Theological Wordbook (Bellingham, Wash.: Lexham Press, 2014).

 

3 Tazama Ellen G. White, The Desire of Ages (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1898, 1940), kur. 750, 751.

Jerome Skinner ni profesa mwenza wa Agano la Kale na teolojia katika Seminari ya Teolojia ya Waadventista wa Sabato, Chuo Kikuu cha Andrews, Berrien Springs, Michigan.

NA HOWARD WILLIAMS

Bibi yangu mzaa baba, Fern (Hurd) Williams, alikulia katika familia yenye watoto wengi ambapo alikuwa mmoja wa ndugu 12. Kama ilivyokuwa kawaida wakati huo, familia zilikuwa kubwa na mapato yalikuwa madogo. Baba yake, Ray Hurd, alifanya kazi yoyote aliyoipata ili kuweka chakula mezani. Wakati wa kisa hiki walikuwa wakiishi Saint Helena, California. Takribani robo ya maili (mita 400) kutoka kwenye nyumba yao aliishi mwanamke mzee mzuri aitwaye Ellen White.

 

Sasa, Dada White alikuwa na desturi ya kuchukua kigari cha farasi ili kupata hewa safi na mwangaza wa jua kila alasiri. Hii pia ilimpatia nafasi ya kupita na kuwaona watu aliowajua na kuwajali. Alikuwa na wasiwasi maalum kwa familia ya Hurd kutokana na ukubwa wa familia yao na kiwango cha mapato. Mara kadhaa alimwajiri babu Ray kufanya kazi za kukata miti katika shamba lake la matunda na kufanya kazi zingine za kawaida katika nyumba yake. Mara nyingi alijitokeza kutembelea kuona jinsi walivyokuwa wanaendelea. Bibi yangu alikuwa mtoto mdogo wakati huo, lakini baadaye maishani alizungumza kuhusu kumbukumbu nzuri za kutembelewa na Dada White.

 

 

MNUFAISHWA

Tukaendelea mbele kwa miongo kadhaa. Vita Kuu vya Pili vya Dunia vilikamilika, na ujenzi mkubwa ulianza kutokea nchini Marekani. Mifumo ya kutengeneza mbao ilijitokeza kila mahali katika Kaskazini Magharibi mwa Pasifiki, na kuleta ajira nyingi. Angalau ndugu wawili wa bibi yangu wakawa madereva wa malori, wakibeba mbao kutoka kwenye viwanda vya mbao kaskazini mwa California kwenda kila mahali ambapo zilihitajika. 

 

Mmoja wa ndugu zake, mdogo zaidi, alingia kwenye duka la magari la malori huko Santa Rosa, California, akitaka kununua lori la kubebea mbao. Mahitaji wakati huo yalikuwa makubwa. Mmiliki wa duka alikubali kumuuzia lori kwa kumfadhili kupitia biashara yao. Kila kitu kilikwenda vizuri kwa muda, kisha mahitaji ya mbao yakapungua. Fedha zilianza kuwa ngumu, akaanza kuwa na wasiwasi kama angeweza kufuatilia malipo ya lori lake. Akiwa na dhamira nzuri na akijaribu kufanya jambo sahihi, aliamua kwenda kwenye duka la malori na kumjulisha mmiliki kwamba ikiwa angeshingwa kulipa malipo yote, angemlipa mmiliki kipindi kazi itakapoongezeka tena. 

 

Baada ya kushirikiana na mmiliki kuhusu hali yake, mtu huyo alionekana kuchukua jambo hilo kwa utulivu na kusema kwa urahisi, “Bwana Hurd, usijali kuhusu chochote! Nitasimamia hilo.” 

 

Ndani ya majuma machache, barua ilifika posta kutoka kwenye duka la malori. Aliifungua na kuangalia hati mbele yake kwa mshangao! Pale, kwenye ukurasa wa mbele wa hati halisi ya lori lake, ilisema “MALIPO YAMEKAMILIKA.” Mapema alivyoweza, alirudi kwenye duka la malori ili kutatua kosa lililoonekena wazi.

 

Baada ya kumjulisha mmiliki sababu ya kutembelea kwake, mtu huyo aliegemea nyuma kwenye kiti chake na kusema; “Bwana Hurd, nahitaji kukusimulia kisa.”

AMANA 

“Nilipokuwa mtoto mdogo, nilishi si mbali na mahali familia yako ilipoishi. Kwa kweli, niliijua familia yako. Wakati ulifika,” aliendelea, “wakati mmoja baada ya mwingine, kila mwanafamilia alipougua, hadi nilipobakia mimi peke yangu ambaye bado ningeweza kufanya kitu chochote, na hata mimi nilianza kujihisi vibaya. Nilikuwa nikifanya kila nililoweza kuitunza famila yangu, lakini kama mtoto mdogo, sikuweza kujua nini cha kufanya ili kuwahudumia na kuwarejesha katika afya nzuri. Wakati huo muhimu, ambapo maisha ya familia yetu yote yalikuwa hatarini, palikuwa na mtu aliyegonga mlango, nilipoulifungua, alikuwepo mzee mwanamke aliyeitwa Bi. White aliye simama pale na alitaka kujua jinsi familia yetu ilivyokuwa.”

 

“Baada ya kuingia na kutathmini hali yetu,” alisema, “alijitolea kwa ahadi kwamba angekwenda kuchukua mahitaji na kurudi tena. Alirudi haraka na hakutoka kando yetu mpaka kila mmoja wetu aliporudisha afya yake. Alikuwa mwanamke malaika.”

 

Mmiliki wa duka aliendelea, “Nimefanikiwa kifedha na kwa muda mrefu sasa, nimepata dhima ya kwamba ninapaswa kufanya jambo fulani, kwa mtu fulani, ili kulipa zawadi kubwa aliyotupatia huyo mwanamke. Familia yetu nzima, bila shaka, ilidai maisha yetu kwake. Sidhani kama yeyote kwetu angekuwa hai leo ikiwa asingefika wakati sahihi kutuokoa. Nilijua kuwa yeye alikuwa Mwadventista wa Sabato, pia najua kuwa wewe ni Mwadventista wa Sabato, hivyo wazo lilijitokeza kwangu, Nani bora kupewa msaada kuliko mtu kutoka katika imani yake? Hivyo, hapana, hakukuwa na kosa kwenye hati ya lori lako. Mkopo wako umelipwa kabisa, na naweza kulala kwa amani, nikijua kwamba mwishowe niliweza kulipa ile zawadi tuliyoipokea zamani!”

 

Babu yangu alirudi nyumbani siku hiyo akimshukuru Mungu na akiwa na shukrani nyingi kwamba siyo tu Bi. White alionyesha kanuni za uponyaji za Mungu ambavyo hufanya kazi, bali alionyesha, kwa vitendo, kwamba aliishi kile alichohubiri, kwa upendo kwa ajili ya wengine na kwa kufuata kanuni za Mungu za afya.

Howard Williams, mmishonari aliyestaafu na mchungaji aliyehudumu Bolivia, Ufilipino na Alaska na Ldaho, anaishi Oregon kati, Marekani.

Mungu anajibu maombi

NA TED N. C. WILSON

Ulikuwa ni mpango wa uthubutu, lakini mtu alipaswa kuufikia mji huo wenye watu zaidi ya 8,000. Karibia mji wote ulikuwa na watu wasio Wakristo, kwani asilimia 99 ya wakazi wake walifuata dini kuu isiyo ya Kikristo.

 

Kwa miaka mingi, kulikuwa na majaribio kadhaa ya kuwafikia kwa ajili ya ujumbe wa malaika watatu, lakini mji huu, ulioko kwenye pwani ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania, ulionekana kuwa mgumu kupenya kwa ujumbe wa injili.

 

Hata hivyo, hili halikuwazuia kundi dogo la vijana kutoka makanisa ya Waadventista wa Sabato katika jiji lililo umbali fulani kuandaa mpango wa kuthubutu kufanya mkutano wa kiinjilisti katika mji huo.

 

 

JITIHADA YENYE HATARI

Kwa kawaida, maandalizi ya mkutano wa uinjilisti huhusisha mipango mingi, ikiwemo maelezo mengi na mipangilio ya vifaa, lakini vijana hawa waliandaa mkutano huo kwa njia kuu ya maombi. Wakijua kuwa kazi hii ilikuwa nyeti na hatari, waliamua kutumia majuma mawili katika maombi ya dhati, wakimsihi Mungu aingilie kati.

 

Kwa muujiza, siku chache baadaye walipata kibali kutoka kwa serikali ya mji huo cha kufanya mikutano ya kidini. Habari zilisambaa haraka, na baadhi ya wakazi wa mji huo walikasirishwa na mpango huo.

 

Wakijua kuwa wao ni vijana na hawakuwa na uzoefu mkubwa, na kwamba hii ilikuwa kazi yenye hatari kubwa, Waadventista hawa vijana walikutana kila alfajiri saa 11:00 asubuhi ufukweni kuwaombea wakazi wa mji huo, mikutano yao, na ulinzi wa Mungu.

 

 

UKUTA WA MOTO

Asubuhi moja, bila wao kujua, baadhi ya vijana wa mji huo walitumwa na viongozi wa eneo hilo kwenda kuwaua Waadventista waliokuwa wakifanya maombi ufukweni. Lakini Mungu aliyasikia maombi ya vijana hawa. Walipokaribia kuwashambulia, waliona ukuta wa moto ukiwazunguka Waadventista hao! Wakiwa wameshtushwa, hawakuthubutu kushambulia, badala yake walikimbia!

 

Waadventista hao waliendelea kuomba na kuanza mikutano yao. Lakini wazee wa mji huo walidhamiria kuwazuia. Walituma vijana wao kwenda kuiba vifaa na samani zilizotumiwa katika mkutano. Lakini walipofika kuiba, walimwona mtu mrefu sana, akiwa amevaa vazi jeupe na akiwa na upanga unaong’aa, akizunguka vifaa hivyo. Kwa mara nyingine, mpango wao mwovu ulishindikana.

 

Waadventista waliendelea kuomba kwa bidii na kuendesha mikutano yao. Usiku mmoja, wakati mkutano ukiendelea, wazee wawili waliovaa mavazi ya kitamaduni walipita katikati ya umati wakielekea mbele, ambako kijana mmoja wa Waadventista alikuwa akihubiri. Lakini kabla hawajafika mbele, ghafla walianza kukimbia na kuruka huku wakilia, “Tunateketea! Tunateketea!” na walikimbia. Baadaye, watu hawa walieleza jinsi walivyoona ukuta wa moto ukimzunguka mhubiri kijana, hivyo wakashindwa kumshambulia.

 

Baada ya njama zao zote kushindikana, wale waliopinga mikutano hiyo walitaka kujua ni aina gani ya “uchawi” Waadventista walikuwa wakitumia kujilinda. Vijana hao waliwaeleza kwa furaha kwamba hakukuwa na “uchawi”, bali wanamtumikia Mungu wa mbinguni aliye hai, ambaye huwasikia wanapomwomba kila siku na kwamba walikuwa chini ya ulinzi wa malaika wa Mungu.

 

Habari za miujiza hii zilipoenea hadi miji ya jirani, mwandishi mmoja wa habari alichapisha kisa hiki katika Msema Kweli, gazeti linalosambazwa nchi nzima.

 

Mwisho wa mkutano, watu 50 walibatizwa. Ingawa kazi katika eneo hilo bado ni changamoto, sasa yapo makanisa matatu yaliyopangwa rasmi katika mji huo, yakiwa na jumla ya waumini takribani 200. Baadhi ya vijana Waadventista waligeuka kuwa wainjilisti walei na wawili kati yao sasa ni wachungaji.

MAOMBI NI UFUNGUO

Marafiki, tunao uhakika kwamba, “Maombi ni ufunguo mkononi mwa imani ili kufungua ghala la mbinguni, ambamo zimehifadhiwa rasilimali zisizo na mipaka za Uweza wa Mungu.”1

 

Hapa ndipo nguvu ya kweli ilipo! Tunaweza kupanga kwa bidii programu za Ushiriki wa Kila Mshiriki Ulimwenguni (Global Total Member Involvement [TMI]), lakini bila kumwomba Bwana kwa dhati ili kubariki mipango hiyo na kutupatia mipango mikubwa zaidi, hatutafanikiwa sana.

 

Maombi ni ya muhimu sana, yanazidi kuwa hitaji la lazima kadiri ulimwengu unavyozidi kuporomoka. Bila maombi, tutawezaje kuwaleta kwa Kristo watu walio na shughuli nyingi, waliokengeushwa na hata wanaoudhiwa ulimwenguni na kushiriki pamoja nao ujumbe adhimu wa malaika watatu? Roho Mtakatifu anahitaji kuwavuta tunapomwomba Bwana kwa bidii ili atende kazi kupitia juhudi zetu ndogo. Kila uhusiano binafsi tunaotengeneza, ambalo ndilo lengo kuu la TMI, lazima ufunikwe kwa maombi.

 

 

KIELELEZO CHETU

Yesu Ndiye kielelezo chetu. Katika kitabu kizuri cha Thoughts From the Mount of Blessing, tunasoma jinsi wanafunzi “waliona jinsi alivyotumia muda mwingi katika upweke akiomba kwa Baba Yake. Siku Zake zilikuwa katika huduma kwa umati uliomzunguka, akifunua madanganyo ya hila za marabi, na kazi hii isiyo na kikomo mara nyingi ilimchosha hata mama Yake, ndugu Zake na hata wanafunzi Wake walihofia kwamba maisha Yake yangepotea. Lakini aliporudi kutoka katika saa za maombi ambazo zilihitimisha siku yenye uchovu, waliona utulivu usoni Mwake na hali ya kuburudika iliyotawala kuwepo Kwake.”2

 

Kisha, zingatia hili: “Ni kutoka katika saa zilizotumiwa na Mungu ndipo alipotoka, asubuhi kwa asubuhi, kuwaletea wanadamu nuru ya mbinguni. Wanafunzi walikuja kuhusisha saa Zake za maombi na nguvu ya maneno Yake na matendo Yake.”3

 

Je, ungependa uweza wa Mungu katika maisha yako ili kuzifikia roho kwa ajili Yake? Unapatikana kwa kuomba. Ninakutia moyo, pamoja na nafsi yangu, kutumia muda zaidi katika maombi, tukimwomba Bwana atupatie hekima, mwongozo na ufanisi tunapoendelea na Ushiriki wa Kila Mshiriki Ulimwenguni —kuufikia ulimwengu kwa ajili Yake!

1 Ellen G. White, Steps to Christ (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1956), kur. 94, 95. 

 

2 Ellen G. White, Thoughts From the Mount of Blessing (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1956), uk. 102. 

 

3 Ibid., kur. 102, 103. 

Ted N.C. Wilson ni mwenyekiti wa Konferensi Kuu ya Waadventista wa Sabato. Makala za nyongeza na maoni zinapatikana katika X (awali Twitter): @pastortedwilson na katika Facebook: @Pastor Ted Wilson.

Kile ambacho msamaha halisi unataka 

NA ELLEN G. WHITE

Barua hii iliandikwa na Ellen G. White kwa Kaka na Dada Mills.—Wahariri.

Natumai hamtadhani kuwa sina nia ya kweli kwenu, ninayo. Bwana ana nia nanyi. Ikiwa mtatembea na kutenda kwa ushauri wa Mungu, mtajitahidi kwa kila njia kuwa na umoja na ndugu zenu. Si wote walioko kanisani wanatembea katika nuru ya Neno la Mungu na wanajiingiza katika hatari kubwa ya majina yao kufutwa katika kitabu cha uzima. Lakini Mungu ashukuriwe kwamba ninyi si wachukuaji wa dhambi zao. Yupo Mkombozi mmoja tu wa familia ya binadamu. Kristo amebeba dhambi zetu. Amechukua huzuni zetu. “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5).

 

Jukumu lako sasa ni kutakasa nafsi yako mbele za Mungu na kuwaacha wengine wafanye vivyo hivyo. Chochote kile ambacho wengine wamekifuata, wewe unayo kesi yako mwenyewe ya kuishughulikia. Unalo Neno la Mungu, lililo wazi na lenye utofauti. Fuata Neno hili. Asili ya kibinadamu mara nyingi ni ngumu kudhibiti, na wale ambao hawafuati kwa makini Neno la Mungu wako katika hatari. Adui anapata faida juu yao. Ukaidi wa asili ya binadamu mara nyingi ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo katika maisha ya kiungu. Unayo tabia ngumu sana ya kuishinda, lakini Mungu atakusaidia.

 

 

KUTOA KILA KIKWAZO

Hakuna wakati wala mahali ambapo ni sahihi kusema, Sitamsamehe ndugu yangu, na sitaishi na kufanya kazi kwa kushirikia naye. Kwa kufanya hivi, wakala wa kibinadamu anajiweka kinyume na mafundisho yaliyo wazi ya Kristo. 

 

Tafadhali takasa nafsi yako, kwa kufuata Neno kwa umakini, haidhuru njia yoyote ile inayoendeshwa na mtu mwingine yeyote. Tunayo nafsi ya kuishughulikia, na inatupasa kuwa waaminifu kwa nafsi zetu wenyewe, vinginevyo, mwelekeo wetu wa asili na urithi wa makosa utapata nafasi ya kuongoza. Wakati mtu anapokosea, hatupaswi kuharibu nafsi zetu wenyewe, bali tumngoje Bwana. Ikiwa ndugu yako anakufanyia uonevu kwa kutokujua, kisha akakushikia mkono wa ushirika, akisema, “Ikiwa nimekosea na kukuumiza au nimekuhukumu isivyo, nisamehe,” na wewe unajitenga naye na kukataa kumsamehe, umekwenda mbali na Mshauri Mkuu, na unahitajika wewe mwenyewe kutubu na kusamehewa.

 

Umepitia nyakati za majaribu makali, na Bwana anafahamu madhara yaliyotokea. Lugha za uharibifu hazina idadi. Hawajui mambo wanayodai. Wanapita kwenye ardhi ambayo itawapasa wapite tena wakati kila kesi itakapozungumziwa mbele za Mungu, wakati wa hukumu utakapofika na vitabu vitakapofunguliwa na kila mtu atahukumiwa kulingana na mambo yaliyoandikwa katika vitabu, iwe ni mema au maovu. Kisha, wale ambao maneno yao sasa yanaumiza na kujeruhi, lazima wajibu kwa kila kauli waliyosema na kubeba matokeo ya maneno waliyosema ili kujeruhi na kuumiza nafsi za urithi wa Bwana. Yapo mambo mengi ambayo sasa hayaonekani katika nuru sahihi, ambayo katika siku hiyo yatakuwa wazi.

 

 

MSAMAHA NI UAMUZI 

Lakini swali la msamaha halihitaji tafsiri kwani ni wazi. Ikiwa ndugu akifanya kosa, msamehe ikiwa atakuomba msamaha. Ikiwa si mnyenyekevu vya kutosha kuomba, msamehe kwa moyo wako na uoneshe msamaha wako kwa neno na tendo.

 

Kisha uzito wa dhambi yake hautakuwa kwa namna yoyote juu yako. “ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe” (tazama Gal. 6:1). Wakati atakutolea mkono na kusema, “Nisamehe,” hupaswi kugeuka na kukataa kumsamehe, kwa sababu unaweza kufikiria kwamba hajishushi vya kutosha na hajui anachosema. Huna haki ya kumhukumu kwa sababu huwezi kusoma moyo wake. Neno la Mungu linasema, Ikiwa atatubu, msamehe. “Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe” (Luka 17:4). Na haitupasi kusamehe tu mara saba, bali sabini mara saba. Kama vile Mungu anavyotusamehe, ndivyo tunavyopaswa kumsamehe mwingine. Hivyo tunahamasisha toba na kukiri.

 

 

MSAMAHA WA KWELI HAUNA MASHARTI

Haupaswi kusema, “Nitakapoona umebadilika, ndipo nitakusamehe.” Huu siyo mpango wa Mungu. Hii ni kulingana na ushawishi wa asili ya kibinadamu badala ya ushawishi wa Mungu. Kutokujali na ugumu wa moyo havipaswi kukubaliwa, kwani si mfano wa Kristo. Kwa kuonyesha kwamba hujali roho ya ndugu yako na hutaki ushirika naye, unamuumiza ndugu yako na kumwekea mfano mbaya.

 

Ndugu yangu, umekosea na unahitaji kuja kwa moyo uliolainika kwa ndugu yako. Kuwa mshiriki wa kanisa kwako siyo kitu kikubwa. Kitu kikubwa ni kutakasa kutoka moyoni kila kitu kitakachopunguza athari yako kwa wema katika kanisa na ulimwenguni. Unayo kazi ya kufanya ili kujitahidi kuingia katika mlango mwembamba. Ikiwa wengine wanaotangaza ukweli wanatumia kipaji chao cha kusema kuripoti mambo yanayoumiza roho yako, wanafanya kazi inayomfurahisha adui.

 

Ipo haja ya ulimi kuguswa na makaa ya moto ya mreteni. Mungu hapendezwi na aina hii ya mazungumzo kanisani. Ikiwa kila mtu angehifadhi maneno yake ili kutoa faraja, kutia moyo na kubariki, kungekuwa na huruma zaidi, ambayo ni upendo, na kuiinua kweli zaidi. Ikiwa wanaume na wanawake wangeacha kuwa wachochezi, wakichochea ugomvi, kungekuwa na onyesho zuri zaidi katika uzoefu wao wa Kikristo. Wakati masengenyo yanapoenea, hakuna uhitaji wa dhambi.

Waadventista wa Sabato wanaamini kwamba Ellen G. White (1827-1915) alitumia kipawa cha unabii cha kibiblia kwa zaidi ya miaka 70 ya huduma ya hadhara. Kipengele hiki kimechukuliwa kutoka katika barua ya Ellen G. White namba 23, mwaka 1901, katika Letters and Manuscripts, vol. 16, uk. 25.

Mungu anapokuwa kiini 

NA HEATHER KRICK

Mume wangu na mimi tulikuwa tumebadilisha madereva, na nilikuwa nimekaa kwa utulivu nikiendesha gari tulipoelekea njia kuu, tukiwa na hamu ya kurudi nyumbani baada ya safari ndefu nchini. Ghafla, bila kutarajia, lori kubwa-tela lilijitokeza kwa kasi kwenye taa yangu ya pembeni, taa yake ya rangi ya machungwa ikiwaka kwa namna ya kutisha huku likielekea moja kwa moja kwenye njia yangu kana kwamba mimi sikuonekana. Nilikuwa nimeshachelewa kufunga breki.

 

Nilijikuta nikienda pembeni, kwa hofu, nikavuta gurudumu la gari kidogo zaidi. Sasa mzunguko wa kati wa kinga ulikuwa unaonekana kwa hatari mbele yangu. Nikijitahidi kurekebisha, na tukarudi kwa haraka kuelekea kwenye lori lililokuwa linakaribia. Sehemu ya abiria ya sedan yetu ya Toyota Camry ambapo mume wangu alikuwa amekaa iligonga upande wa chuma wa tela ya lori. Tukiwa hatujadhibiti, tuliendelea kupoteza mwelekeo kupitia barabarani tena, hatimaye tukasimama ghafla tulipogongana na kinga hiyo ya kati.

 

Yote haya yalitokea ndani ya muda unaoweza kusoma kisa hiki. Vipande vya glasi vilikuwa vimetawanyika ndani ya gari, na upande wa abiria na upande wa nyuma-kulia wa gari ulikuwa umevunjika na kubonyea, lakini tulikuwa hai! Tulipokuwa tukikaa pale kwa mshtuko, mume wangu aligeuka kuangalia nyuma kuwatazama vijana wetu wawili. Kwa ajabu, sisi sote tulikuwa hatuna majeraha na afisa wa polisi ambaye alitusaidia alikubaliana kwamba “tulikuwa wenye bahati” kutokuwa na majeraha. Bila shaka tulijua kuwa malaika wa Mungu walitutunza. Licha ya mshtuko, tulimshukuru Mungu kwa hiari. Kwetu ilikuwa ni wakati wa ibada. 

 

Wahusika wengi wa Biblia, wakiwa wanadamu kama sisi, walikuwa na uzoefu sawa na wetu, ambao ulileta hali ya ibada katika hali mbalimbali. Hebu tuangalie baadhi yao.

 

 

NYAKATI ZA IBADA KATIKA BIBLIA 

Ibrahimu alikuwa amemteua mtumishi wake mwaminifu Eliezeri kutekeleza kazi muhimu: kumtafutia mke Isaka. Eliezeri hakuweza kujizuia kujiuliza kama Bwana angeruhusu safari yake kwenda Nahori iwe na mafanikio. Aliposubiri karibu na kisima, alipanga na kuomba. Ishara ya kwamba alikuwa msichana sahihi? Angeteka maji kwa ajili yake na pia atachota maji kwa ajili ya ngamia wake.

 

Mapema alimwona msichana mmoja ambaye alimvutia, alimwomba maji. Rebeka mara moja alitimiza ishara hiyo na pia alimualika nyumbani kwa baba yake. Jibu la Eliezeri? “Yule mtu akainama akamsujudu BWANA” (Mwanzo 24:26). Kabla ya kukubali, kabla ya kwenda nyumbani, kabla ya kula, kabla ya kufanya jambo lingine lolote, alitumia dakika moja kumrudia Mungu, ambaye alijibu maombi yake wazi kabisa.

 

Mcha Mungu Ayubu alikuwa na siku ngumu sana. Mjumbe asiyetarajiwa alijitokeza, akisema kwamba Waseba walikuwa wamechukua ng’ombe na punda wa Ayubu na kuwaua watumishi wake. Kabla mjumbe huyo hajamaliza kusema, mtumishi mwingine alikuja akasema kwamba moto kutoka mbinguni ulikuwa umewaunguza kondoo na watumishi. Mtumishi mwingine alifika wakati huo na kutangaza kwamba ngamia wake walikuwa wametekwa na Wakaldai. Ayubu alikuwa na mshtuko, lakini pigo kubwa lilikuja mwishowe.

 

Watoto wote wa Ayubu walikuwa nyumbani kwa ndugu mkubwa wakiwa na sherehe wakati upepo (labda dhoruba) ulipoharibu nyumba, bila kuacha masalia. Hii ilikuwa habari ya kushangaza, lakini cha kushangaza, Biblia inarekodi majibu ya ajabu ya Ayubu kama ifuatavyo: “Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuangua chini, na kusujudia” (Ayubu 1:20). Akikumbwa na maafa zaidi ya yale ambayo mtu anaweza kufikiria kutokea katika siku moja, ikiwa ni pamoja kupoteza watoto wake wote, Ayubu alirarua mavazi yake, akanyoa kichwa chake, na, ingawa alikuwa na huzuni, kwa urahisi alimgeukia Mungu wake na kumwabudu.

 

Wakati Gideon mwenye hofu alisikia mtu akisimulia ndoto kuhusu Gideon kushinda vita, alijua kwamba Mungu alikuwa na suluhisho na angeshinda vita alivyoviogopa. Aliona jinsi Mungu alivyokuwa mwaminifu na uoga wake ukageuka kuwa hofu na ibada (Waamuzi 7:15).

Wakati alipoitembelea Misri, Musa aliwaonyesha watumwa wa Waisraeli namna fimbo yake ingekuwa nyoka na walistaajabia na kushukuru. Wakitambua sasa kwamba Mungu wao alikuwa amewakumbuka na kuona maisha yao yenye shida, waliinamisha vichwa vyao na kumsujudia (Kutoka 4:31).

 

Kisha alikuwepo Eli. Hana alikuja kumwacha Samweli mdogo katika hema ya kukutania. Kuhani Mkuu Eli aliguswa na dhabihu kubwa ya mama huyu mtii katika kumwachia mtoto wake. Akilinganisha mtindo wa malezi ya Hana na malezi yake ya kibinafsi, alijihisi aibu na heshima, na akaanguka mbele za Bwana na kumwabudu.*

 

Walipokuwa kwenye mashua kwenye bahari ya Galilaya, wakiwa wamezungukwa na giza la asubuhi, wanafunzi waliona kivuli juu ya maji na wakaanza kuogopa. Lakini kisha walisikia sauti ya Yesu na kuona sura Yake na walijua msaada ulikuwa njiani. Petro alifurahia sana kutoka kwenye mashua inayosukwasukwa baharini na kufika kwa Yesu.

 

Kadiri Petro alivyomwangalia Yesu, aliona muujiza—alitembea juu ya maji! Lakini mara alipoondoa macho yake kutoka kwa Yesu na kutazama mawimbi, alianza kuzama. Akiwa amekosa tumaini, alilia kwa sauti, “Niokoe!” Yesu bila kuchelewa alimfikia na kumwinua. Hatimaye walikuwa kwenye mashua pamoja.

 

Kutazama muujiza kulifuta hofu kubwa iliyowatesa hata wavuvi walioshinda bahari waliofanyika kuwa wanafunzi. Baada ya Petro kutembea juu ya maji ili kumfikia Yesu, na upepo kukoma, wale waliotazama wangeweza kusema tu, “Hakika wewe u Mwana wa Mungu” (Mathayo 14:33). Mungu alikuwa amewavuta na sasa walimwabudu.

 

 

NYAKATI MUHIMU SANA

Hizi zilikuwa ni nyakati muhimu sana ambazo zilipelekea ibada. Waisraeli walimwona Mungu, kupitia Musa, akigeuza fimbo kuwa nyoka. Wanafunzi walimwona Yesu akitembea juu ya maji. Eli aliona uaminifu wa Hana kwa Mungu. Eliezeri aliona jibu la ajabu kwa maombi yake. Na Ayubu alitembea kwa imani kwa sababu alijua na kumtumaini Mungu licha ya kuwekwa kwenye mavumbi kwa ugonjwa, maombolezo na mafadhaiko.

 

Ninapoendesha gari karibu na mahali pa ajali yetu ya gari, nakumbuka ule wakati muhimu sana ambapo Mungu alitulinda. Na, wakati hali zisizotarajiwa za furaha au majaribu zinatokea, na zitatokea, kwani hakuna anayeziepuka, visa vya wahusika hawa wa Biblia vinanichochea pia kukumbatia hizi nyakati muhimu sana ambazo zinamleta Mungu mbele yangu kwa uwazi.

*Tazama Ellen G. White, Patriarchs and Prophets (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1890, 1908), uk. 571.

Heather Krick, mzawa wa Afrika Kusini, anaishi California na ni mke mwenye furaha wa mume wake mchungaji, Bill. 

Kujenga Msingi wa Umilele 

NA BETH THOMAS

Katika ulimwengu wa leo unaobadilika kila wakati, umuhimu wa msingi imara kwa mioyo na akili za vijana hauwezi kupuuzwa. Kanisa la Waadventista limeweka Machi 22, 2025, kama siku ya kuonyesha umuhimu wa elimu ya Kikristo. Elimu ya Kikristo inatoa njia ya kipekee na yenye maana kubwa katika kujifunza, ikijitofautisha na shule za umma. Imejengwa juu ya imani, maadili na mtazamo wa Kikristo, na inawezesha wanafunzi kufanikiwa kitaaluma na kuishi maisha yenye kusudi na uadilifu.

 

Moja ya faida kuu ya elimu ya Kikristo ni msisitizo wa kuunganisha imani na kila kipengele cha kujifunza. Katika shule za umma mara nyingi hutumia mtaala wa kidunia, unaolenga katika kutofungamana na upande wowote kuhusu dini. Ingawa hii inahudumia watu wa jamii mbalimbali, inaacha nafasi ndogo kwa wanafunzi kuchunguza jinsi imani na elimu zinavyoweza kuungana. Hata hivyo, shule za Kikristo hufungamanisha kanuni za kibiblia katika kila somo—kuanzia sayansi, historia, hadi fasihi. Hii inawezesha wanafunzi kuona ulimwengu kupitia lensi ya ukweli wa kibiblia, ikiwasaidia kukuza uelewa wa kina wa kusudi lao na utambulisho wao katika Kristo.

 

Tofauti kuu ya elimu ya Kikristo ni msisitizo wake katika kujenga tabia. Shule za umma zinaweza kuangazia mafanikio ya kitaaluma na ustadi wa kijamii, lakini shule za Kikristo zinakwenda mbali zaidi kwa kulinda na kukuza ukuaji wa kiroho na maadili ya wanafunzi. Walimu katika shule za Kikristo mara nyingi huhudumu kama washauri na kuonyesha mfano wa tabia ya Kikristo, wakiwaongoza wanafunzi katika safari yao na Mungu. Kupitia maombi ya kila siku, madarasa ya Biblia, na majadiliano kuhusu maamuzi ya kimaadili, wanafunzi wanapata fursa ya kuchagua kilicho bora.

 

Elimu ya Kikristo inatoa mazingira salama na yenye msaada ambapo wanafunzi wanaweza kustawi na kukua kiroho. Wakati mwingine, shinikizo la utamaduni wa kidunia, ushawishi wa rika na wakati mwingine, misongamano darasani inaweza kufanya iwe vigumu kwa wanafunzi kushikilia imani yao katika mazingira ya shule za umma. Shule za Kikristo, kwa upande mwingine, hujenga jamii yenye mshikamano na maadili yaliyopo. Wanafunzi huzungukwa na marafiki na walimu wanaoshiriki imani zao, na hii inajenga mazingira yenye upendo na msaada kwa ukuaji wao wa kiroho.

 

Aidha, elimu ya Kikristo pia inawatayarisha wanafunzi kuwa nuru na chumvi katika ulimwengu. Lengo si tu kulinda vijana dhidi ya ushawishi wa kidunia, bali pia kuwapatia ufahamu wa kukabiliana na ulimwengu kwa njia inayoleta maana. Wanafunzi wanajifunza kufikiri kwa kina, kutetea imani yao, na kukabili changamoto za maisha kwa mtazamo ambao Kristo Ndiye kiini. Hii ni muhimu kwa Wakristo wanaoitwa kuwa mabalozi wa Kristo katika jamii zao na maeneo yao ya kazi.

Shule za Kikristo pia zinaweza kuwa njia ya uinjilisti, zikifungua milango ya kushiriki imani hata nje ya jamii ya Waadventista. Familia nyingi zisizo za Waadventista huchagua elimu ya Kikristo kwa sababu ya maadili ya kiroho na mazingira rafiki. Hii hutengeneza fursa pekee ya kushiriki injili kwa urahisi na kwa njia yenye matokea mazuri. Kupitia mafundisho ya kibiblia ya kila siku na kushiriki katika shughuli za kiroho, wanafunzi wasio Waadventista mara nyingi hukutana na upendo wa Yesu kwa njia zinazoleta mabadiliko. Uzoefu huu unaweza kupanda mbegu za imani ambazo hukua baada ya muda wao wa kuwa shuleni.

 

Katika enzi ambayo ukweli halisi mara nyingi unapuuzwa na maadili ya kibiblia yanazidi kuwekwa pembeni, shule za Kikristo hutoa kimbilio mahali ambapo Neno la Mungu linabaki kuwa mamlaka ya mwisho. Zinawawezesha wanafunzi kusimama imara katika imani zao na kukabiliana na changamoto za maisha ya kisasa kwa ujasiri na neema.

 

Hatimaye, elimu ya Kikristo ni zaidi ya mafanikio ya kitaaluma; inahusu kuunda mioyo na akili kwa ajili ya umilele. Kuweka imani, tabia na mtazamo wa kibiblia kuwa kipaumbele kunawawezesha vijana kuuishi wito wao kama wafuasi wa Kristo. Kwa familia za Kikristo zinazotafuta elimu inayoendana na maadili yao na kuimarisha imani yao, uwekezaji katika elimu ya Kikristo ni wa thamani na muhimu kweli.

Beth Thomas ni mhariri msaidizi wa Adventist World.

Maisha na Urithi wa Malcolm Abbott 

NA LESTER DEVINE

Toleo la awali la muhtasari huu wa kihistoria lilichapishwa kwenye tovuti ya Ensaikopidia ya Waadventista wa Sabato, encyclopedia.adventist.org. Toleo hili limetoholewa kwa ajili ya maudhui na mahususi.

 

Malcolm Abbott alikuwa msimamizi wa Eneo la Utume la Waadventista wa Sabato huko New Guinea wakati alipochukuliwa kama mfungwa wa kiraia wakati wa Vita Kuu vya Pili vya Dunia huko Rabaul, New Guinea, na baadaye kupoteza maisha yake akiwa na umri wa miaka 33.

 

 

MAISHA YA AWALI

Malcolm alizaliwa katika familia ya Waadventista huko Waverly, kitongoji cha Sydney, New South Wales, Australia, mnamo Januari 12, 1909.

 

Muhtasari wa maisha yake katika Nyaraka za Waadventista unatupatia maelezo zaidi kuhusu elimu yake. “Baada ya kusoma katika shule ya Gordon, alijiunga na Shule ya Sekondari ya North Sydney, ambapo alipata heshima sana kwa tabia njema na umahiri wake katika michezo. Alipopendekezwa, akiwa na umri wa miaka kumi na sita, ahamishwe kwenda Chuo cha Umishonari cha Australasian, mkuu wa shule (ambaye pia alikuwa mwalimu wa mama yake Mac) alisita kumruhusu kuondoka.”1

 

Malcolm alihitimu kozi ya biashara ya miaka mitatu kutoka chuo cha Australasian Missionary na akakubali nafasi ya kazi kama karani katika kampuni ya Sanitarium Health Food. Pia alifanya kazi katika ofisi ya Union Konferensi ya Australasian, na baadaye aliajiriwa kama mhasibu na msimamizi wa nidhamu katika chuo cha New Zealand Missionary.

 

Akiwa New Zealand, Malcolm alifunga ndoa na Una Frances (“Fran”) Spengel. Fran alikuwa muuguzi aliyehitimu kutoka Santariamu ya Sydney. Fran alizaliwa huko Boonah, Queensland, mwaka 1906. Familia yake ilihamia Avondale ili watoto wao waweze kuhudhuria masomo katika chuo cha Australasian Missionary, ambapo walinunua nyumba iliyokuwa ikimilikiwa hapo awali na W. C. White mkabala na Sunnyside, makazi ya Ellen G. White.

 

Malcolm alitumia miaka mitatu akifanya kazi ya elimu katika chuo cha New Zealand Missionary, kisha akafanya kazi za ukarani katika taasisi mbalimbali za kanisa kabla ya kuwekewa mikono mnamo Septemba 1939. Katika mwezi huo huo, alichaguliwa kuwa msimamizi wa Eneo la Utume la New Guinea.

 

 

MSIBA WAKATI WA VITA

“Baada ya kuhudumu kwa uaminifu katika nafasi hii kwa muda wa miaka mitatu, likizo ya familia ya Abbott ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1941. Kwa kujua kwamba Mchungaji na Bi. Tutty pia walistahili likizo wakati huo huo, Mchungaji Abbott alisema kwamba yeye na dada Abbott wangeahirisha likizo yao kwa miezi michache ili eneo la utume lisibaki bila watendakazi. Kama angechukua likizo yake kwa wakati, angekuwa Australia wakati wa uvamizi mbaya wa New Guinea.”2

 

Mnamo Desemba 1941, familia za wamishonari wa Waadventista wa Sabato waliokuwa Papua New Guinea walihamishwa hadi Australia kwa usalama. Ndani ya miezi saba, jeshi la wanamaji la Japani lilikuwa limevuta nyuma jeshi la Australia na kuchukua mji wa Rabaul kwenye kisiwa cha New Britain, na kuanzisha kituo cha kijeshi kwa ajili ya mashambulizi zaidi kwenye Visiwa vya Solomon na Papua New Guinea.

 

Malcolm alibaki Papua New Guinea, mahali ambapo alikuwa karibu na eneo lililovamiwa na jeshi la Japani, na punde alikamatwa na majeshi ya uvamizi.

 

Mnamo Juni 22, 1942, Malcolm pamoja na wanaume wengine 1,052 walipakiwa ndani ya Meli ya gereza Montevideo Maru kusafirishwa kuelekea Kisiwa cha Hainan. Kwenye meli hiyo, walikuwapo askari wapatao 845 na raia 208. Tovuti ya Nyaraka za Taifa la Australia inaeleza hatima ya askari wa Australia katika eneo la East New Britain kabla ya shambulio la Wajapani: 

 

“Kati ya askari wa jeshi la Australia 1,396 waliokuwa Rabaul kabla ya shambulio, 160 waliuawa kusini mwa mji huo huko Tol, takribani 400 waliweza kutoroka na kufika Australia, huku waliobaki wakichukuliwa kama wafungwa wa vita (POWs). Baada ya uvamizi, raia wengi walikusanyika karibu na Rabaul, ambapo jeshi la Wajapani liliweka kambi ya wafungwa wa kiraia na kijeshi.

 

“Mnamo Juni na Julai 1942, mamlaka ya wanamaji wa Japani ilifanya majaribio mawili ya kuwahamisha wafungwa hawa hadi Japani. Kikundi cha kwanza, kilichojumuisha maafisa wapatao 60 wa Australia na wanawake 18, wakiwemo wauguzi wa jeshi, kilifika salama. Kikundi cha pili, ambacho kihistoria kinadhaniwa kujumuisha POWs wapatao 845 na wafungwa wa kiraia 208, kiliondoka tarehe 22 Juni kuelekea kisiwa cha Hainan kwa kutumia meli ya Montevideo Maru, meli ya mizigo iliyochukuliwa na jeshi la wanamaji la Japani. Meli hiyo haikuwa na alama ya kubeba wafungwa wa vita (POWs). Mnamo Julai 1, meli hiyo ilishambuliwa kwa topido na kuzamishwa na manowari ya USS Sturgeon karibu na kisiwa cha Luzon, Ufilipino, na kusababisha vifo vya wafungwa wote waliokuwa ndani. Tukio hili la Montevideo Maru linatajwa kuwa janga kubwa zaidi la baharini katika historia ya Australia, iwe wakati wa amani au vita.”3

 

Kwa miezi mingi, familia za watu hawa hawakujua kilichowapata. Baada ya kumalizika kwa vita, rekodi za Japani, zikiwemo orodha za majina ya wafungwa waliokuwa ndani ya Montevideo Maru, zilipotafsiriwa, waziri wa masuala ya nje wa Jumuiya ya Madola ya Australia aliwataarifu familia kuhusu majina ya waliokuwa ndani ya meli hiyo wakati iliposhambuliwa. Malcolm Abbott aliorodheshwa kama mfungwa namba 145.

 

Wakati wa ibada ya kumbukumbu iliyofanyika katika kanisa la Wahroonga mnamo Novemba 10, 1946, ili kutoa heshima kwa Waadventista wale waliopoteza maisha yao wakiwa wafungwa wa vita, maneno ya heshima maalum yalitolewa kwa kumkumbuka Malcolm Abbott na uaminifu wake:

 

“Uaminifu wake katika kazi, upendo wake kwa watendakazi wenzake, shauku yake kwa ustawi wa wenyeji wa New Guinea ilimfanya abaki karibu na eneo la uvamizi, ambapo aliangamia pamoja na Waustralia wenzake wapatao elfu moja na mia moja, tunasikitika sana kwa kuwapoteza wote hawa.”4

 

Mnamo Julai 1, 2012, mnara wa kumbukumbu ulisimikwa huko Canberra kwa heshima ya waliopoteza maisha yao katika janga hilo. Mnara huo ulizinduliwa rasmi na Gavana Mkuu wa Australia, mbele ya watu zaidi ya 800, wakiwakilisha familia za waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha.

 

 

KAZI YA FRAN NA MAISHA YA BAADAYE

Baada ya kuhamishwa kwa Fran kutoka Papua New Guinea, akimwacha mume wake ambaye hakumwona tena, alifanya kazi katika Hospitali ya Waadventista ya Sydney hadi alipostaafu mwaka 1971. Katika miaka yake ya baadaye alikuwa mshauri wa bweni la wanawake. Kwa kuwa hakuwa na watoto wake wa kuwazaa, aliwalea wanafunzi ambao ndio familia yake. Alifurahia kuwatembelea wanafunzi, mara nyingi akiriki pamoja nao uzoefu wake. Fran alifariki mwaka 1993.

Lester Devine, Ed.D., ametumia zaidi ya miongo mitatu katika uongozi wa elimu wa kanisa katika divisheni mbili za Kanisa la Waadventista wa Sabato ulimwenguni, Divisheni ya Amerika Kaskazini (1969 - 1982) na Divisheni ya Kusini mwa Pasifiki (1982 – 2005). Baada ya miaka 40 ya huduma ya kidini, alihitimisha safari yake ya utumishi kama mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Ellen G. White/Kituo cha Utafiti cha Waadventista katika Chuo Kikuu cha Avondale (Avondale University College), Australia.

Swali hili limeletwa na baadhi ya watu wanaoamini kwamba, kwa ujumla, kanisa si la kiroho jinsi linavyopaswa kuwa, na kwa hiyo, ndani yake Mungu analo kundi la waumini waaminifu ambao wanaunda masalia wa kweli. Kujibu mtazamo huu, nitatetea kwamba msingi wake ni kutokuelewa asili na jukumu la masalia wa nyakati za mwisho.

 

 

MASALIA WA NYAKATI ZA MWISHO KAMA MWISHO

Katika Biblia, Mungu daima amewahifadhi masalia kupitia ambaye Yeye hutimiza mipango Yake kwa wanadamu. Lakini pia tunapata kile kinachoweza kuita mtindo wa ukuaji na uasi. Kikundi kidogo, masalia, huongezeka na kuwa kundi kubwa ambalo, kwa sababu ya kutotii kwao kwa kudumu kwa Mungu, linakataliwa Naye. Kwa neema, Mungu huwahifadhi masalia wadogo na mchakato mzima huanza upya. Unabii wa kiapokaliptiki (mambo ya nyakati za mwisho) huvunja mzunguko huu potofu kwa kutangaza ushindi wa mwisho wa masalia wa nyakati za mwisho wa Mungu. Katika Ufunuo, watu wa Mungu waliobaki wanashambuliwa kutoka nje na kutishiwa kutoweka, lakini Mungu na Mwana-Kondoo wanawahifadhi (Ufu. 13:16-14:1). Ulimwengu wote unadanganywa na kuongozwa kwenye uasi na ukanaji wa imani, lakini si masalia (Ufu. 13:8). Ndiyo, masalia watakua kwa kuwaita watu wa Mungu ambao bado wako Babeli watoke humo, lakini kundi hilo kubwa litasalia kuwa waaminifu kwa Kristo na litashinda (Ufu. 17:14).

 

 

MASALIA NI WA KIHISTORIA NA WANAONEKANA WAZI

Pendekezo la kwamba wapo masalia ndani ya masalia linamaanisha kwamba masalia wa kweli hawaonekani. Hili huenda kinyume na picha ya ufunuo wa masalia wa Mungu katika nyakati za mwisho kama kitu kamili kinachoonekana, yaani, kuweza kuonekana na kutambuliwa na wengine. Ni wa kihistoria kwa sababu ilitokea baada ya kutimizwa kwa unabii wa siku 120 mnamo mwaka 1798 (Ufu. 12:14. 17). Udhihirisho wake unahakikishwa na ukweli kwamba Biblia inatoa sifa kadhaa zinazowatambulisha masalia na kuwafanya watambulike. Kwa mfano, masalia wanazishika amri za Mungu (aya ya 17); wameweka imani yao kwa Yesu kama Mwokozi (Ufu. 14:12); Roho ya unabii imedhihirishwa miongoni mwao (Ufu. 12:17; linganisha na Ufu. 19:10); wanao muhuri wa Mungu na wa Mwana-Kondoo juu yao (Ufu. 14:1); na wanadumu katika kujitoa kwao kwa Yesu hata mwisho (aya ya 12). Udhihirisho wa masalia ni wa lazima kwa sababu wanakusudia kutimiza utume wao. Ili wale wanaotoka Babeli wajiunge nao, watu wa Mungu wa masalia wa nyakati za mwisho lazima wawe kundi maalum la waumini.

 

 

MASALIA NA UKWELI

Moja ya sifa muhimu zaidi za masalia ni kwamba wanao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa wanadamu ambao unapaswa kutangazwa waziwazi (Ufu. 14:6-10). Ufunuo hauashirii kwamba masalia watajitenga na ujumbe huo kwa tendo la uasi na ukanaji wa imani. Kinyume chake, watautangaza kwa ulimwengu mzima kama maandalizi ya ujio wa Kristo (aya ya 6-20). Changamoto ambayo masalia watakabiliana nayo inatoka nje, lakini pia upo uwezekano kwamba baadhi yao hawataishi kulingana na kweli waliyoaminiwa. Hawakatai kweli waliyoipokea, lakini baadhi yao wanaweza kupoa kiroho na Bwana atawaondoa miongoni mwa masalia Wake wa nyakati za mwisho (Ufu. 3:15, 16). Hii inaonyesha kwamba masalia wenyewe hawatashindwa na uasi ambao utamfanya Bwana kuinua masalia kutoka ndani ya masalia.

Ángel Manuel Rodríguez, Th.D., ni mstaafu baada ya kuhudumu kama mchungaji, profesa na mwanateolojia.

Njia kuelekea afya na uzima 

Rasilimali za afya za kanisa letu zinasisitiza shukrani. Je, ni kweli inaathiri afya yangu?

Shukrani, ambayo ni kutambua na kuthamini mambo chanya katika maisha, si hisia tu bali ni chombo chenye nguvu cha kuboresha afya ya kiakili na kimwili.

 

Utafiti umeonyesha kuwa shukrani ina athari kubwa kwa afya ya akili kwa kubadilisha mtazamo kutoka kwa mawazo hasi hadi mtazamo wenye matumaini zaidi. Tafiti zinaonyesha kuwa watu wanaotoa shukrani mara kwa mara hupata viwango vya chini vya sonona na wasiwasi, jambo linalowasaidia kukabiliana vyema na msongo wa mawazo na changamoto za maisha.

 

Shukrani pia inahusiana na uimara wa kihisia. Watu wanaotoa shukrani wanao uwezo mkubwa wa kupata maana ya maisha na kudumisha tumaini. Pia, shukrani huimarisha mahusiano na kupunguza hisia za upweke, kwani mahusiano chanya ni muhimu kwa ustawi wa kihisia. Aidha, shukrani huongeza kujihisi mwenye thamani. Kujikita katika kile tulichonacho badala ya kile tunachokosa husaidia kupunguza athari mbaya za kujiona duni, jambo ambalo mara nyingi linachochewa na kulinganisha, matokeo ya mitandao ya kijamii.

 

Shukrani ina faida dhahiri kwa afya ya mwili. Mojawapo ya njia kuu ni kupitia kupunguza msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo sugu umehusishwa na magonjwa mbalimbali ya mwili, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo na udhaifu wa kinga ya mwili. Kushukuru husaidia kupunguza viwango vya homoni za msongo kama vile kortisoli, na hivyo kusaidia kuboresha afya kwa ujumla. 

 

Kuboreka kwa usingizi ni faida nyingine muhimu. Watu wanaotoa shukrani huwa na usingizi bora na muda wake. Kukumbuka baraka zetu na kutoa shukrani kabla ya kulala kunaweza kusaidia akili kutulia, na hivyo kuimarisha usingizi tulivu. Shukrani pia imeonyeshwa kuhimiza tabia bora za maisha ya afya. Watu wanaokuza tabia ya kushukuru wanao uwezekano mkubwa wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kula vyakula vyenye lishe na kushiriki katika hatua za kujikinga kiafya, jambo linalochangia matokeo bora ya afya ya muda mrefu.

 

Pia, shukrani inahusiana na kupungua kwa dalili za magonjwa sugu. Kwa mfano, watu wenye shinikizo la damu wamepata udhibiti mzuri wa shinikizo lao baada ya kufanya mazoea ya kushukuru mara kwa mara. Vilevile, wale wanaoishi na maumivu sugu wameripoti maumivu kidogo na ufanisi mkubwa wa mwili wanapoelekeza mawazo yao kwenye mambo wanayoshukuru katika maisha yao.

 

 

KUKUZA SHUKRANI

Faida za shukrani zinaweza kupatikana kupitia mazoea rahisi na makusudi. Mafunzo ya Biblia kwa maombi na tafakari vinaweza kutusaidia kutambua na kufurahia baraka zetu, bila kujali hali tulizonazo.

 

Kuhifadhi jarida la shukrani na kuorodhesha baraka tunazoshukuru kwa kila siku ni njia yenye nguvu ya kukuza tabia hii. Kuandika barua za shukrani au kutoa shukrani kwa maneno pia huongeza hisia ya shukrani.

 

Shukrani ni msingi wa ustawi wa kiakili na kimwili na hutoa njia ya maisha yenye kuridhisha na yenye usawa. Tunashukuru kwamba Mungu alithibitisha baraka hii kupitia ujumbe wa afya ulioaminiwa kwa kanisa hili miaka 150 iliyopita: 

 

“Hakuna kitu kinachochangia zaidi katika kukuza afya ya mwili na roho kuliko roho ya shukrani na sifa. Ni jukumu la lazima kupinga mawazo na hisia za huzuni na kutoridhika—kama ilivyo jukumu kuomba. Ikiwa tunakwenda mbinguni, tunawezaje kwenda kama kundi la wafiwa, tukiugua na kulalamika tunapoelekea hadi nyumbani kwa Baba yetu?”*

* Ellen G. White, The Ministry of Healing (Mountain View, Calif: Pacific Press Pub. Assn., 1905). uk. 251.

Zeno L. Charles-Marcel, daktari bingwa aliyeidhinishwa na bodi, ni mkurugenzi wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu. Peter N. Landless, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa nyuklia na moyo na mkurugenzi mstaafu wa Huduma za Afya za Waadventista wa Konferensi Kuu, pia ni daktari bingwa aliyeidhinishwa na bodi.

Mganga wa jadi 

“Marta, ni kitu gani cha kwanza unataka kufanya ukifika mbinguni?” 

 

Marta alikuwa tayari amefikiria swali hilo hata kabla sijaliuliza! Badala ya kuniangalia na kujibu, Marta aliinua macho yake juu, mbali zaidi ya kilele cha mti mrefu wa korosho, kana kwamba alikuwa akiangalia mawingu yakisafiri angani juu ya mbingu ya Msumbiji. Kisha akatabasamu, akainama mbele na akaanza kuzungumza kwa bidii kwa lugha yake ya Changana.

 

Marta alikuwa ameketi juu ya kitambaa cha capulana chenye rangi angavu, akifanya kazi na wanawake wengine wa kijijini kutoa maganda ya mavuno ya karanga za msimu. Ilikuwa kama sherehe, kila mwanamke akisimulia hadithi za ajabu za familia, na kila mtu akicheka kwa furaha kwa kipeo cha hadithi inayojulikana na wote. Nilialikwa kujiunga na wanawake hao kwa sababu mke wangu, Brenda, alikuwa ameniita ili kumsikiliza Marta akisimulia tena moja ya hadithi zake anazozipenda zaidi.

 

 

NDOTO

Miaka mingi iliyopita, kulingana na kisa, Marta, ambaye alikuwa curandeira (mganga wa jadi) wa kijiji, alimpata Yesu moyoni mwake na kuwa evangelista (mwinjilisti) wa kijiji.

 

Yote yalianza kupitia ndoto, moja ya ndoto nyingi ambazo Marta alikuwa akipata alipokuwa akifanya kazi na mizimu kama mganga wa jadi, akitafuta dawa sahihi za matatizo ya jirani zake. Dawa zake zilifanya kazi na watu walimlipa vizuri. Mizimu ilikuwa imempatia maisha mazuri, mazuri kiasi kwamba Marta alikuwa hata ameanza kuweka akiba ya kununua lori. Kumiliki lori dogo la mizigo (pickup) kungemfanya awe mtu muhimu zaidi kijijini! Alijua lilikuwa wazo la kipuuzi, hasa kwa kuwa hakukuwa hata na barabara ya kufika kijijini kwake. Kulikuwepo na njia pana ya ng’ombe tu.

 

Kisha ndoto ikaja.

 

“Marta, Marta.” Sauti kubwa ilimwita kwa jina lake na kumwamuru atoke nje ya kibanda chake. Marta alijifunua kutoka chini ya blanketi, akafungua mlango kidogo, na kuchungulia nje. Hapo, mbele ya kibanda chake, karibu na mahali pake pa moto, palikuwa na Toyota pickup mpya kabisa, nyeupe, yenye milango minne na magurudumu ya nne kwa nne!

 

Marta alikimbia hadi kwenye gari hilo, akaligusa kuhakikisha kama ni halisi, kisha akalizunguka lote, akiipapasa rangi yake nyeupe inayong’aa, akiangalia taa, vibao vya mbele na nyuma, vioo na nembo zake. Kwa tahadhari, kana kwamba aliogopa kama hayo si ya kweli, akaushika mlango wa dereva. Ulifunguka! Ndani, funguo zilikuwa zikining’inia kwenye swichi ya kuwashia gari!

 

Ndani ya muda mfupi, alikuwa tayari ameketi kwenye kiti cha dereva, akihisi mtikisiko wa injini yenye nguvu ya gari lake jipya. Akaanza kuendesha gari kuzunguka kijiji, akijaribu kutowaamsha majirani zake. Kisha, ghafla, akavuta usukani na kuanza kupaa juu, juu zaidi ya miti ya mikorosho, juu ya miti ya maembe, kupitia mawingu, kupitia nyota, moja kwa moja hadi kwenye kuta za mawe za mji mkubwa wa mbinguni. Juu sana, mbali na kijiji chake kidogo cha Mucapane, Msumbiji. 

 

Aliangalia kama kuna mtu aliyekuwa akimwangalia. Alipotazama tena kupitia kioo cha mbele cha gari, aliona akiendesha kwa kasi kuelekea lango la mji mkubwa wa mawe, mji wa kutisha uliokuwa umening’inia angani katikati ya nyota!

 

Marta aligeuza usukani na kuelekea kwenye lango kuu la mji huo, lakini lilikuwa limefungwa. Akatoka nje ya gari lake na kuanza kupiga mlango akiomba aingie, lakini kila kitu kilikuwa kimya. Alipaza sauti kwa nguvu, kiasi kwamba kila mtu aliyekuwa ndani angesikia, lakini bado lango lilibakia limefungwa kwa ajili ya curandeira huyo kutoka Mucapane.

 

 

UKWELI KUHUSU MJI HUO

Marta alishtuka kutoka usingizini, akipiga kelele na akiwa anatiririkwa jasho ndani ya kibanda chake.

 

Marta akalala kimya kwa muda mrefu. Alikuwa amezoea mizimu kumpa ndoto za ajabu na za kutatanisha, lakini ndoto hii ilikuwa tofauti. Safari hii, ndoto hiyo ilionekana kuwa na tumaini! Alijua kwamba alihitaji kupata njia ya kurudi tena kwenye ule mji wa mbinguni, lakini hakuwa na wazo lolote la jinsi ya kufika huko au kufungua mlango. Kwa hivyo, Marta, curandeira ambaye alikuwa amezoea kuwasaidia wengine kupata majibu ya matatizo yao, akaanza kumwomba kila mtu msaada. Lakini hakuna mtu aliyekuwa na habari yoyote kuhusu mji mkubwa wa mawe ulio angani!

 

Kisha, alasiri moja, mtu fulani akataja kuwa kuna mkulima huko Machumbutane ambaye huenda anajua ukweli kuhusu mji huo wa angani. Hilo lilitosha kwa Marta. Mara moja, “mganga wa roho,” curandeira wa kijiji, akaweka chakula kwenye kikapu na kuanza safari ya kutembea kwenye njia ya vumbi kuelekea vibanda vya mbali vya Machumbutane. “Nikifanikiwa tu kupata ufunguo wa mji huo, itatosha”, Alijisemea huku akitembea.

 

Alipofika, alikuta kikundi cha watu waliokuwa wakisoma Biblia ya Kikristo, wakimwomba Mungu kwa jina la Yesu, wakiabudu siku ya Jumamosi, na wakipanga kuungana na Mwokozi wao katika ule mji mkubwa wa mbinguni.

 

Marta akawasikiliza, akasoma pamoja na rafiki zake wapya na akampenda Yesu.

 

 

KURUDI NYUMBANI

Marta aliporudi nyumbani, ndoto ile ikajirudia tena. Safari hii, alikuwa tayari sauti ilipomwita jina lake.

 

“Marta! Marta!”

 

Akakimbilia nje, akajirusha ndani ya Toyota pickup yake nyeupe, na akaendesha kwa kasi, akipaa juu ya miti ya mikorosho na maembe hadi kufika tena kwenye ule Mji Mkubwa wa Mawe ulio angani!

 

Usiku huu, lango lilikuwa wazi, lakini lilikuwa limezuiliwa na jitu kubwa lenye “mabega mapana, mikono iliyokunjwa kifuani na uso uliokunjamana.” Maneno yake yalikuwa wazi kabisa.

 

“Lazima uache maisha yako ya zamani ya kuwa curandeira, uteketeze vifaa vyote vya uganga wako, na uwafundishe majirani zako habari za Yesu na mji Wake wa mbinguni.”

 

Marta akageuza gari, akabonyeza kichapuzi na kurudi moja kwa moja nyumbani Mucapane. Akaingia kwa haraka ndani ya kibanda chake, akakusanya “vifaa vyote vya uganga” alivyokuwa navyo, na akavipeleka kwenye sehemu ya moto. Akachochea moto na kutupa ndani hirizi, mifupa na sanamu zake pendwa. Hata alichoma fedha zote alizokuwa amehifadhi kwa ajili ya kununua gari, aliziteketeza ndani ya moto huo.

 

Ni fedha chafu, Marta akawaza na wala sihitaji gari kufika mbinguni.

 

Kishindo cha moto ule kilisikika kijiji kizima na kila mtu akatoka nje kushuhudia tukio hilo la ajabu. Asubuhi hiyo, Marta akaanzisha mikutano ya Yesu katika kijiji cha Mucapane, Msumbiji. Walikutana pembeni ya mahali pake pa moto, chini ya mkorosho mrefu kijijini, wakijifunza pamoja kurasa chache za Biblia na kupanga safari yao ya kuelekea mbinguni.

 

“Marta, ni kitu gani cha kwanza unataka kufanya ukifika mbinguni?”

 

“Hebu nikuambie ninachotaka kufanya nikifika nyumbani mbinguni,” Marta alinyanyua uso wake kwa furaha kutoka kwenye kazi ya kubambua karanga. “Ninataka kutembea kwa muda mrefu na Yesu. Ninataka kuushika mkono Wake. Ninataka kuisikiliza sauti Yake. Ninataka kumtazama machoni. Nataka kumwambia, ‘Asante kwa kunipenda mimi, curandeira, hadi kunifanya kuwa evangelista!’”

 

Marta alipomaliza kusimulia kisa chake, wanawake waliokuwa wakibambua karanga waliijaza Mucapane kwa kelele na furaha za Hosana! Hosana!

Dick Duerksen, Mchungaji na msimuliaji, anaishi Portland, Oregon, Marekani.

Safari ya Farasi 

Furaha, mafundisho, na ulinzi wa Mungu 

NA MAYRI CLARKE 

Safari ya farasi. Sauti ya maneno hayo yalisisimua mwili wangu! Kwa kuwa rafiki zangu wengi kutoka kanisani walikuwa na farasi, tulipanga shughuli zinazohusiana na farasi mara kwa mara kama inavyowezekana. Safari hii nilifurahi sana kuwa na farasi wangu, Lightning, kwa ajili ya safari hii. Alikuwa na rangi ya kahawia iliyokolea, na alikuwa na manyoya ya kustarehesha marefu ya dhahabu katika shingo na mkia wake, pamoja na haiba ya ujasiri. Alikuwa anafurahisha kupanda, lakini pia alikuwa na ukaidi. Mara nyingi alikataa kusimama licha ya kuvuta hatamu kwa nguvu zote; alionekana kusahau kuwa nilipaswa kuwa na udhibiti.Natumaini safari hii atanisikiliza, nilijiwazia.

 

Furaha yetu ilitanda hewani, ikachanganyika na harufu ya farasi na vifaa vya ngozi. Dada yangu Naomi, rafiki yangu John, dada yake Kaylee1 na wengine wote pia walikuwa na farasi wao wa safari. Hamasa ilizidi kuongezeka tulipokuwa tukijiandaa kwa shauku na safari yetu ya farasi. Baada ya kuwafungia farasi matandiko na kupakia chakula kwenye mikoba yetu kwa ajili ya chakula cha mchana, tulikusanyika kuomba kuwepo na ulinzi wa Mungu. Hata hivyo ilikuwa ni mpaka baadaye siku hiyo ndipo tulipotambua umuhimu wa maombi yetu.

 

Tulipanda farasi kwa maili kadhaa katika barabara ya lami, tukifuata njia ndani ya msitu. Nilifurahia mandhari ya asili tulipopita maeneo mapya kwangu. Nyasi mbichi za kijani zilichanganyika na mashamba makavu, ili kutofautisha na anga la bluu angavu. Jua kali liliimulika ngozi yangu, likiangaza miili ya farasi wenye jasho. Kila tulipokutana na sehemu nzuri ya barabara ya udongo, tulikimbia kwa kasi na uhuru, tukifurahia upepo uliopishana na pumzi zetu zenye furaha. Ilikuwa burudani ya ajabu!

 

Baadaye kidogo, tulipokuwa tukisonga kwenye njia yenye mizunguko, Kaylee, aliyekuwa akimwendesha farasi wa kaka yake aitwaye Justin, na mimi tulianza kujiuliza kwa sauti: “Ni farasi gani mwenye kasi zaidi: Lightning au Justin?” Justin alikuwa mrefu na mwembamba, kana kwamba aliumbwa kwa ajili ya mbio na kuruka vizuizi. Lightning, akiwa karibu mkono2 mmoja kwa ufupi kuliko Justin, alikamilisha tofauti hiyo ya kimo kwa ujasiri na kiburi. “Naam, kuna njia moja tu ya kujua.” Tuligeukiana kwa macho yenye shauku na tukasema, “Tushindane mbio!”

 

Kwa kuwa tulikuwa kwenye njia pana ya kutosha kwa farasi wawili, katikati ya msitu, tulidhani ilikuwa ndefu vya kutosha kwa mbio. “Tayari, jiandae, nenda!” Tulianza kwa kasi, tukiwaacha wengine nyuma kwenye wingu la vumbi. Kelele za kwato za farasi zilivuma, Adrenalini ilikuwa inangezeka, matawi ya miti yalionekana kushangilia tulipopita kwa kasi. Farasi walihisi furaha hiyo. Ilikuwa mbio ya kukaribiana sana: Lightning anaongoza; hapana, Justin anaenda mbele moja kwa moja; lakini subiri, Lightning anazidi kuongeza kasi; na sasa . . . Oh, hapana!

 

SIMAMA! Kaylee na mimi tulikuwa tumejikita sana kwenye mbio hadi tukasahau kabisa barabara ya lami iliyokuwa ikikaribia kwa kasi. Kwato zinazokimbia kwa kasi na lami havichangamani! Kwa haraka nikamtazama Kaylee, nikaona miguu yake ikinyooka kwenye tandiko huku akitumia nguvu zake zote za mikono kuvuta hatamu za ngozi kwa nguvu, akitumaini kumzuia farasi wake mwenye ari, lakini haikufanikiwa. Justin alidhani ilikuwa tu pendekezo. 

 

Lightning naye alidhani hivyo kwa sababu alikataa kusimama na kumruhusu Justin amshinde. Tulikuwa na sekunde chache tu za kuzuia farasi wetu waliokuwa wakikimbia kabla ya kufika kwenye barabara hatari ya lami. Nilipoona sehemu ndogo ya nyasi kando ya barabara, nilifanya uamuzi wa haraka wa kugeuka kwa kasi kushoto, nikivuta hatamu kwa nguvu kadiri nilivyoweza, kwa wasiwasi nikitumaini kwamba Lightning angeelekea huko badala ya barabarani. Aliteleza kidogo kwenye lami, kwato zake zikigusa lami kwa muda mfupi, lakini alijimudu haraka na kusimama juu ya nyasi. Nilishukuru alipoachana na ukaidi wake wa kawaida wakati wa dharura yetu. 

 

Alikuwa rahisi kumzuia kuliko Justin. Nilishusha pumzi kwa shime, lakini tena nikashikilia pumzi yangu nikimwaangalia Kaylee akifanya jitihada zake zote kubaki kwenye tandiko wakati Justin aliyekuwa akiteleza na kuteleza kwenye lami, karibu aanguke, na akajikwaruza mguu wake wa nyuma kwenye lami. Hatimaye alijimudu na kuvuka upande mwingine wa barabara. Loo! Tulikuwa salama. Wakati tulipochukua sekunde chache kupumzika na kusubiri wengine katika kikundi chetu wafike, tuliona damu kwenye mmoja wa miguu ya nyuma ya Justin kutokana na kuteleza kwake barabarani. 

 

Kaylee alihofia jinsi kaka yake atakavyopokea jeraha la farasi wake na kwa tukio letu la hatari lisilo la busara. Lakini kilichotokea baada ya hapo kilitufanya tusahau hayo kwa muda kuhusu hilo. Sekunde chache baada ya kutoka barabarani, lori kubwa la huduma za umma lilipita kwa kasi. Kaylee na mimi tulitazamana kwa mshangao, tukitambua ghafula kwamba kama tungechelewa sekunde chache tu, mambo yangeweza kuwa tofauti. Tulipokuwa tukirudi nyumbani, nilifikiria jinsi tulivyokuwa karibu na mwisho mbaya, nikiwa na shukrani kwa ulinzi na wakati mwafaka wa ajabu wa Mungu. Niliamua pia kuwa mwangalifu zaidi ikiwa nitawahi kushiriki mbio kwenye barabara nisiyoifahamu tena.

 

 “Malaika wa BWANA” kwa hakika “hufanya kituo, akiwazungukia wamchao, na kuwaokoa” (Zab. 34:7).

1 Majina yamebadilishwa.

 

“Mkono” ni neno la kipimo cha urefu wa farasi kutoka ardhini hadi mabegani mwake. “Mkono” mmoja ni sawasawa na inchi 4 (sentimita 10). 

Mayri Clarke anaandika kutoka Chattanooga, Tennessee, Marekani.

Mchapishaji
Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review
Justin Kim

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa
Hong, Myung Kwan

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World 
Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun, Dong Jin Lyu

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review
Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani
Enno Müller, Beth Thomas, Jonathan Walter 



Wahariri waliopo Seoul Korea


Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali
Gabriel Begle

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi
Daniel Bruneau

Meneja wa Shughuli
Merle Poirier

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri
Marvene Thorpe-Baptiste

Wahariri/Washauri wengine
E. Edward Zinke

Meneja wa Fedha
Kimberly Brown

Mratibu wa Usambazaji
Sharon Tennyson

Bodi ya Utawala
Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong, Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Tae Seung Kim; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

Maelekezo ya Usanifu na Muundo
Types & Symbols

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:
Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

Tafsiri
Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

Msomaji wa prufu
Lilian Mweresa

Usanifu wa toleo la Kiswahili
Daniella Ingram, Ashleigh Morton, Teya Esterhuizen, Digital Publications

Uchapishaji wa Kidijitali
Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu
Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott
/Types & Symbols

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org Tovuti: www.adventistworld.org

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

Vol. 21, Na. 3

swipe down
powered by
SEND-IT.ME

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Please wait ...