

ENDELEA KUPOKEA ADVENTIST WORLD KISWAHILI
Tunawathamini na kuwatambua wote waliojisajili na tuna taarifa mpya na za kusisimua kuhusu jinsi mnaweza kuendelea kusoma na kupata Adventist World.
KULIPATA KWENYE WHATSAPP
Kwa sababu ya umaarufu wa kulipata jarida hilo kwenye WhatsApp, tunahamia kwenye mfumo mpya wa kutangaza ambao utatuwezesha kuwasiliana nanyi mara kwa mara. Bonyeza kiungo kilicho hapo chini kujiunga na chaneli ya WhatsApp Broadcast ambapo tutakujulisha toleo jipya linapokuwepo.


KULIPATA KWENYE TOVUTI

Lipate jarida hilo kwenye tovuti yetu, kwa kukibonyeza kiungo kilicho hapo chini:

Tovuti hiyo vilevile inabeba Adventist World kwa lugha anuwai.
KULIPATA KWENYE FACEBOOK
Kiungo cha toleo la hivi karibuni la Adventist World huwekwa kwenye Ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi. Kwa “Liking” ukurasa huu utapokea taarifa zetu mpya na kuweza kututumia jumbe ukiwa na majibu yoyote.

HIFADHI MAKTABA YA JARIDA LA KISWAHILI KWENYE SIMU YAKO AU KOMPYUTA
Tumetengeneza maktaba ya kidijitali ya majarida yote ya Adventist World. Ili kulipata kusanyo hili kwa urahisi kwenye simu yako, fuata hatua zilizo hapo chini:
Bonyeza kiungo kilicho hapo chini ili kuipata maktaba.

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.
AU

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.
Kwa maoni yoyote au majibu, tafadhali jiskie huru kututumia barua pepe kwenye kwambokaj@ecd.adventist.org. Tunapenda kusikia kutoka kwako na tunatazamia uhusiano mzuri na wasomaji wetu wa Adventist World-Kiswahili.
Asante sana na Mungu awabariki,
Timu ya Adventist World-Kiswahili













Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa kwambokaj@ecd.adventist.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.
Picha ya jalada: Brett Meliti


Kitovu cha Kanisa
Na Justin Kim
Daima kanisa limekuwa na makusudi ya kiulimwengu. Kilichobadilika katika karne hii ni kwamba kusudi hilo limetambuliwa. Lakini, ni wapi katika kanisa hili la kiulimwengu, ni kitovu cha Ukristo? Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara na Amerikca kusini zimeona ukuaji ambao haujawahi kushuhudiwa. Shughuli ya utume inaendelea na idadi kubwa ya watu wanaishi Mashariki ya Kati, bara Hindi na Asia. Utajiri wa kanisa na rasilimali za kimkakati za utume zipo Amerika Kaskazini, Ulaya, na baadhi ya sehemu za Pasifiki ya Kusini.
Utafiti mmoja umeonyesha ramani ya kitovu cha takwimu cha Ukristo kiulimwengu kati ya 33-2100 B.K. Kila sehemu ya takwimu inawakilisha mahali ambapo nusu ya Wakristo wote wanaishi kaskazini na nusu kusini yake, pamoja na nusu ya mashariki na nusu magharibi. Baada ya Pentekoste, kanisa lilijikita Yerusalemu, lakini Ukristo kwa ujumla ulikua kaskazini-magharibi kuelekea Ulaya. Wakati wa mabaraza ya kanisa la awali, kituo cha takwimu kilikuwa Asia Ndogo, au Uturuki ya leo. Matengenezo ya miaka ya 1500 yaliona ukuaji zaidi kuelekea Ulaya, wakati enzi ya wamishionari ya karne ya 18 na 19 ilisogeza kanisa magharibi. Ukuaji katika karne ya ishirini ulionekana barani Afrika na Amerika Kusini na kusababisha ukuaji wa kusini magharibi katika miaka ya 1970. Leo tunaona makadirio yakiendelea kuelekea kusini, na pia mashariki kuelekea Asia, yaani, China na India, nchi mbili zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani.
Shughuli ya umishionari ilikuwa “kutoka magharibi kwenda kwingine,” lakini sasa ni “kutoka kila mahali hadi kila mahali.” Utume sasa umekuwa kazi ya kiulimwengu. Kihispania ni lugha inayoongezeka ya waumini na nyingine zikiinuka kama vile Kichina sanifu, Kihindi, na Kiswahili. Brazili ni nchi yenye idadi kubwa ya Waadventista wa Sabato. Nchi kama Mexico, Zaire-Kongo, Ufilipino, Ethiopia na Uganda zinatazamiwa kuwa nchi kumi bora za Ukristo.
Je,leo kitovu cha Ukristo ulimwenguni ki wapi? Kwa vile kaskazini, kusini, magharibi na mashariki ni miundo ya kijiografia kwenye sayari ya mduara, kituo hicho si cha kijiografia, si cha kitaifa, si cha kiutamaduni, wala kitaasisi. Kitovu ni pale Kristo anapofanya kazi katika moyo, akili, na mwili; kitovu ni pale Mwadventista ye yote anapoishi na kuwasilisha injili kutoka kila mahali hadi kila mahali; kitovu ni Kristo (Kol. 1:15—19).
Kwa vile kanisa limethibitisha ukweli wa kuwa la kiulimwengu, sasa tunafunga chapisho la Adventist World na kujiunga na mkondo wa kimataifa ambao lilipamba moto na urithi wa miaka 175 wa Adventist Review. Toleo linalofuata litaendelea na kazi yake ya kuwatia moyo Waadventista kote ulimwenguni na kumuweka Yesu kuwa kitovu cha imani yetu, kanisa letu na utume wetu.

* Sun Young Chung and Todd M. Johnson, “Tracking Global Christianity’s Statistical Centre of gravity, AD 33-2100,” International Review of Mission 95 (2004): 167.


Picha: Jim Botha
Eglan Brooks, Mwenyekiti wa Union Konferensi ya Uingereza, afungua Mkutano wa Kilele wa Ulinzi. Zaidi ya washiriki 130 walikusanyika Februari 21-27, katika Chuo cha Elimu ya Juu cha Newbold ili kujadili, kujifunza, na kutafakari kuhusu masuala ya ulinzi ndani ya kanisa.


"Ishara rahisi lakini muhimu, kama vile simu, ziara, au mazungumzo, vinaweza kuleta mabadiliko, kutoa tabasamu na kuunda uhusiano wa upendo na ukaribu."
— Giovanni Benini, mkurugenzi wa Casa Mia, nyumba ya kustaafu huko Forli, Italia, kuhusu mpango mpya unaoitwa “Waweza kumuasili Babu.” Mpango huo mpya ni sehemu ya utume wa kituo hicho, kwani unalenga kupambana na upweke wa wazee na kuwapa raia fursa ya kugundua tena maana ya jamii. Benini na wafanyakazi wake wamejitolea ili kuboresha maisha ya wakazi wao, ili kuunda mazingira ya familia ambapo kila mtu anaweza kujisikia yuko nyumbani.

Zaidi ya 1,800
Idadi ya watu waliohudumu wakati wa maonyesho ya bure ya afya katika kitongoji nje ya Asunción, mji mkuu wa Paraguay. Maonyesho hayo yalitoa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na dawa za familia kwa watu wazima na watoto, magonjwa ya moyo, magonjwa ya wanawake, mfumo wa mkojo, saikolojia na magonjwa ya macho, pamoja na miwani inayoagizwa na daktari bila malipo. Watu pia walikuwa na nafasi ya uchunguzi wa ultrasound, ECGs, na upakwaji wa dawa kwa jinsi ilivyohitajika. Tukio hili lilikuwa matokeo ya ushirikiano kati ya Asunción Adventist Sanitarium na AdventHealth.



Je, Yesu atarudi hali ningali hai?
Washiriki wa Kanisa letu kote Ulimwenguni waliulizwa ikiwa wanaamini kuwa Yesu angerudi hali wangali hai au la.


Punguzo la Asilimia 20
Idadi ya mbinu za kupunguza gharama zilizofundishwa wakati wa mafunzo ya afya na mtindo wa maisha katika Mkutano wa North New South Wales, Australia, wakati wa darasa la mapishi kwa bajeti ya kumudu. Washiriki walijifunza jinsi ya kuandaa milo sahili, yenye afya nyumbani. Kwa kuweka kipaumbele katika vikundi vya chakula kama vile mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, na kunde, wawasilishaji walishiriki jinsi gharama za mboga zinavyoweza kupunguzwa kwa asilimia 20. Wakiongozwa na waelimishaji wa afya na mtindo wa maisha Margot Marshall na Kym Fowler, na mtaalamu wa lishe na daktari wa mtindo wa maisha Kaysie Vokurka, mafunzo ya FoodSAVE yalipinga dhana kwamba ulaji bora ni ghali.



“Nimefurahia mafundisho! Mungu atukuzwe, nawashukuru waandaaji na timu yote. Tumejifunza mambo mengi mapya tunayoweza kuyatumia katika Idara ya Wanawake. Nawashukuru kwa nyakati nzuri tulizokuwa nazo pamoja.”
—Zlatka Ivanova, kutoka Nova Zagora, Bulgaria, mshiriki wa mafunzo ya Idara ya Wanawake, yaliyofanyika katika Kituo cha Afya huko Banya, Bulgaria, juu ya uzoefu wa tukio hilo. Mafundisho yaligusia mawanda mapana ya mada, ikiwa ni pamoja na historia na falsafa ya idara ya wanawake, wanawake katika Biblia, uongozi wa Yesu wa mfano. Washiriki pia walijadili huduma katika makundi madogo, harakati za kanisa dhidi ya unyanyasaji na ugunduzi wa karama za roho.

Tunashuhudia jambo la kutisha la kupoteza waumini baada tu ya kubatizwa, na wengi wanaosalia kanisani hawafanyi kitu chochote, wanakuwa tu wapasha mabenchi. Mkutano huu . . . umekusudiwa kutuandaa sisi sote kuwa wafanya-wanafunzi wenye ufanisi wanaohusika kikamilifu katika utume wa kanisa.”
—Munaji Musa, mkurugenzi wa uinjilisti kwenye Union Konferensi ya Kaskazini mwa Nigeria. Tukio hili lilishughulikia changamoto kali zinazozuia ufanisi wa ufanyaji wanafunzi na kuwabakisha waumini kanisani.

Zaidi ya Millioni 3
Idadi ya nakala za Living With Hope, kitabu cha umishonari mwaka huu, kilichoandikwa na Marcello Niek na Bruno Raso, ambazo zilitolewa na kusambazwa na vijana huko Mexico. Usambazaji wa vitabu ulikuwa mojawapo ya mipango kadhaa ambayo vijana waliifanya ili kuunga mkono katika Siku ya Vijana Duniani mnamo Machi 15. Kikundi cha Pathfinder huko Huixtla, Chiapas, kilikutana na rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum Pardo, na walishiriki naye kitabu na wakaweza kupiga naye picha.




Ripoti ya Mweka Hazina wa GC inaangazia kuongezeka kwa lengo la dhamira licha ya tete ya juu.

Marcos Paseggi, Adventist World
Huku kukiwa na “kutokuwa na uhakika wa juu zaidi wa sera ya kiuchumi,” maofisa wa fedha wa Konferensi Kuu (GC) wa Kanisa la Waadventista wa Sabato walisema wanamshukuru Mungu kwa kile walichokiita kuingilia kati Kwake katika masuala ya kifedha ya kanisa. “Tunamsifu Bwana kwa nafasi nzuri ya kifedha kwa kanisa, ukizingatia hali ya ulimwengu kiuchumi,” alisema mwekahazina wa GC Paul H. Douglas kwenye Mkutano wa Spring wa 2025 wa kanisa huko Silver Spring, Maryland, Aprili 8.
Douglas aliripoti kuwa GC ilimaliza mwaka wa fedha ikiwa na takriban dola za Marekani milioni 338 katika mali halisi, asilimia 94 ikiwa ni fedha taslimu na uwekezaji. “Tumekuwa mawakili waaminifu wa rasilimali ambazo Mungu ametoa kuendeleza kazi ya ufalme Wake,” alisema. Wakati huo huo, alisisitiza kwamba uwezo wa kifedha wa GC “sio kwa sababu ya mafanikio yetu wenyewe—ni kusudi la Mungu la kimbingu kutupatia kile tunachohitaji ili kufanya kazi Yake.”
UKUAJI WA MABADILIKO
Kwa 2024 GC ilipokea takriban dola milioni 4 zaidi ya ile sehemu yake ya zaka ya takriban dola milioni 82 ambazo zilipangwa katika bajeti, Douglas aliripoti. Zaka, hata hivyo, zilionyesha mwelekeo usio sawa tangu 2019 ambao unaweza kuhusishwa na utekelezaji wa makubaliano ya uwiano wa zaka kati ya maeneo ya makanisa ya ulimwengu, ambayo hupunguza vyema mchango wa Divisheni ya Amerika Kaskazini (NAD) kwa bajeti ya jumla, aliripoti. Pia, mwaka wa 2024 uimarishwaji wa kiasi kikubwa kwa dola ya Marekani dhidi ya fedha za kigeni ulisababisha kiasi kidogo cha zaka kilichopokelewa kutoka kwa baadhi ya nchi duniani.
Matoleo yamezidi tena yale yaliyokuwa yamepangwa. Douglas alieleza kwamba kuna mabadiliko yanayokua katika mpangilio wa matoleo ya zaka ya michango. Zaka ilitoka kwa kuchangia asilimia 58 kwenye bajeti ya 2020 hadi asilimia 45 tu mnamo 2024. “Mabadiliko yanayoongezeka ya matoleo yanayozidi zaka yanapendekeza kwamba kupendezwa na utume wa kanisa kiulimwengu kunatawaliwa katika mioyo na akili za washiriki wa kanisa letu,” Douglas alisema. “Bila shaka, kutakuwa na ushawishi wa kutafakari juu ya kazi ya kanisa mahalia ambayo itakuwa yenye ufanisi zaidi kwa sababu ya uangalifu wenye kusudi unaotolewa kwa kazi ya ulimwenguni pote.” Kile tunachokiona hapa kuhusu matoleo ni ndoto,” alisema mkurugenzi wa uwakili wa GC Marcos Bomfim baada ya kukaribia moja ya vipaza sauti. “Inaleta furaha, na nadhani tunaweza kukua zaidi.”
BADO MUNGU ANATAWALA
Mungu ameendelea kulibariki kanisa Lake kupitia uaminifu wa washiriki wetu ili tuweze kuendeleza utume wetu wa kuufikia ulimwengu kwa ajili ya Kristo, Douglas alisisitiza.
Pesa za utume zilizopigiwa kura kugawanywa zimetumika na zitatumika katika kusaidia mipango ya utume inayosimamiwa katika kanisa mahalia na makanisa ya divisheni zote ulimwengu. Kwa mwaka wa 2025, dola milioni 6.7 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya kanisa mahalia, aliripoti.
Alifunga kwa kusisitiza imani yake na timu yake katika uongozi wa Mungu. “Licha ya changamoto zote tunazokabiliana nazo duniani kote . . . kazi ya kanisa inasonga mbele,” Douglas alisema. “Ingawa neno 'kutokuwa na uhakika' linaelezea hali ya sasa ya kiuchumi, tunatambua katika nyumba hii kwamba Mungu bado anatawala.”



Mhariri Mwadventista anachungua nguvu ibadilishayo ya usimuliaji wa kisa cha kweli.

Marcos Paseggi, Adventist World
“Kisa binafsi kilichojawa na Nguvu ya injili kina nguvu inayokaribia kutoshindwa” alisema Jarrod Stackelroth wakati wa Mkutano wa Kidijitali wa Uanafunzi huko Gold Coast, Queensland, Australia, mnamo Machi, 15, 2025. Stackelroth, mhariri mkuu wa Adventist Record na Signs of the Times katika Divisheni ya Pasifiki Kusini, alijadili jinsi uwezo wa kusimulia hadithi ya kweli—pamoja na hadithi yako ya kibinafsi—inavyoweza kuwa na uwezo wa kuunganisha, kuwawezesha, na kusaidia kubadilisha wengine.
KUPENYA KATIKA KELELE ZA KIDIJITALI
Kuhusiana na hilo, Stackelroth alisisitiza kwamba “hadithi za kweli zina uwezo wa kupenya katika kelele za kidijitali na kufikia mioyo. . . . AI, kwa namna itakavyokuwa, haitaweza kamwe kusimulia kisa chako binafsi.”
Alieleza kuwa AI inaweza kutoa hoja za kuvutia sana, kukuza muhtasari wa mazungumzo, na kukusaidia katika kazi yako. “Lakini haiwezi kuelezea ushuhuda wako wa binafsi,” alisema.
NGUVU YA HADITHI
Katika muktadha huu ujumbe wa ukweli ni muhimu sana, Stackelroth alisema. Na hadithi binafsi zina uwezo wa kukuza ukweli. Kulingana na yeye na wataalam katika uwanja huo, hadithi zinaweza kusaidia kuunda uhusiano wenye mguso ambao unaweza kuongoza katika kufikia uhusiano wa kudumu. Zinaweza pia kusaidia kuongeza uwazi, ambao hujenga imani na uaminifu. Hatimaye, hadithi zinaweza kutusaidia kujihusisha kwa uhalisi ili kujenga mahusiano yenye maana.
Stackelroth pia alisisitiza kuwa kushiriki hadithi binafsi na uzoefu hubeba uzito wenye mguso ambao unaweza kusaidia kufikia kuwa na uhusiano wa kudumu. Hadithi huvunja vizuizi na kujenga madaraja, zikionyesha jinsi Mungu anavyofanya kazi kwa watu na katika ulimwengu.
“Huenda watu walioko jirani na wewe wasielewe maoni au imani yako, lakini hawawezi kupingana na kisa chako binafsi . . . na jinsi Mungu anavyofanya kazi maishani mwako,” alisema. “Na unaposhiriki na wengine kushindwa kwako, unaposhiriki dhiki zako, unammulika Mungu, sio wewe mwenyewe.” Ni kama kusema, “Mimi ni takataka; Sina cha kutoa, isipokuwa kile ambacho Mungu amenipa ili nikupatie wewe.”
VISA VIPONYAVYO NA KUBADILISHA
Kusikiliza visa binafsi kunaweza kubadilisha maisha yetu na namna tunavyoiishi imani yetu, alisema Stackelroth. Kwa sababu Stackelroth alivutiwa na nguvu ya visa viponyavyo, alifanya utafiti juu ya masimulizi ya kiwewe, hususani kwa askari wastaafu wanaoteseka kwa ugonjwa wa msongo baada ya kufikwa na kiwewe (PTSD). “Kueleza kisa chako hukusaidia kupona; kinawasaidie wengine pia kupona,” alisema. Ndio maana ninavutiwa sana na visa.”
Ufunguo hata hivyo ni kufanya vile ilivyo sahihi” kwa unyenyekevu, Stackelroth alisisitiza akinukuu 2 Wakorintho 11:30: “Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.” Yote yanahusiana tu na kujinyenyekeza na kuonyesha upole, alisema. Wakati uo huo lazima uwe mwerevu kwa kujua ni wakati na mahali gani unapoweza kuelezea kisa chako. Na uguswe na kuwa na huruma unapofanya hivyo, aliongeza Stackelroth.
“Ninakutia moyo utafute njia za kutumia uhalisia ili kupunguza ukosefu wa uaminifu uliopo katika jamii leo. Na labda unaweza kuwa mtu ambaye humfanya mtu mwingine [aseme], ‘Nataka kile alichonacho. Ninaona kwamba kuna kitu tofauti, na ninakitaka,’” alisema.



Mtandao mpya ulioanzishwa utakuwa na lengo la kimishonari, wanasema.

Daniel Kluska, Union Konferensi ya Poland, na Adventist World
Mnamo Machi 29, huko Podkowa Leśna, Poland, viongozi mahalia wa kanisa na maofisa wa vyombo vya habari waliendesha ibada ya shukurani ili kusherehekea uanzishaji wa taasisi mpya ya umishonari: Hope Media Poland.
Tadeusz Niewolik, mkurugenzi mpya aliyeteuliwa, aliainisha hali ya upekee wa kukusanyika huko: kwa kusudi sahili la kumwabudu Mungu pamoja, na pia kukumbuka historia nzuri ya taasisi za umishenari za kanisa zilizopita huko Poland. Ibada ilifuatiwa na nyimbo za shukrani, mlo wa pamoja, na mkusanyiko wa mchana ambapo wafanyakazi walishiriki ushuhuda wao.
TAASISI MPYA
Kwa miezi kadhaa Union Konferensi ya Poland imekuwa katika mchakato wa kubadilisha taasisi zilizopo kuwa moja iliyo mpya iitwayo Hope Media Poland. Ibada ya shukrani ilionyesha shukrani kwa utendaji wa zamani wa taasisi za kimishonari za kanisa huko Poland na uzinduzi wa shirika jipya.
Waumini wa kanisa la Waadventista huko Podkowa Leśna walihudhuria, pamoja na wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi na waliokuwa wafanyakazi wa taasisi za kanisa zinazofanyiwa mabadiliko. Niewolik alionyesha shukrani kwa waliohudhuria na kuwatia moyo kuzingatia kwa sala na kuelekeza mawazo yao kwenye uongozi wa Mungu “katika miaka iliyopita na siku zijazo.”
USOMAJI WA PEKEE WA BIBLIA
Badala ya makundi ya kawaida ya majadiliano na kujifunza Biblia, Peter Bylina, katibu wa PUC, alialikwa kutoa muhtasari wa kujifunza lesoni kwa kawaida. Alifanya hivyo kwa njia ya ushairi, akionyesha wazo la msingi—kwamba sheria ya Mungu kiini chake ni upendo kwa Muumbaji na kwa jirani zetu. Alionyesha wazi kwamba pasipo kuwa na uhusiano binafsi na Mungu, hatuwezi kuitimiza kabisa amri ya upendo.
Jambo muhimu kwenye huduma hiyo lilikuwa ni uwasilishaji wa filamu zinazosimulia hadithi za taasisi nne zilizopita za kimishonari, ambazo shughuli zao sasa zinahamishiwa kwenye Hope Media Poland.
SHIRIKA MWAVULI
Taasisi mpya itaunganisha taasisi kadhaa, ikijumuisha nyumba ya uchapishaji, ambayo ilifunguliwa mnamo Mwaka 1921 huko Bydgoszcz. Filamu iliyoonyeshwa iliangazia wajibu wake katika kuwaunganisha waumini na ufanikishaji wa uinjilisti nchini Poland, pamoja na matatizo ya kipindi cha vita na enzi ya Ukomunisti. Wazungumzaji baada ya uwasilishaji walijumuisha Miroslaw Harasim, mkurugenzi wa Nyumba ya Uchapishaji ya Poland, na mhariri mkuu wa shirika hilo Andrzej Siciński.
Video nyingine ilimtaja Emanuel Beret, mwanzilishi wa Correspondence Bible School, ambayo iko Warsaw, Podkowa Leśna, na Bielsko-Biała na anashughulika na makumi ya maelfu ya waandishi wa Biblia. Pia wanatoa kozi kuhusu mfadhaiko, msongo, na afya ya kimhemko, alisema Lucyna Kurz, mmoja wa wafanyakazi wa shule.
Filamu ya mwisho ilitolewa kwa taasisi ndogo zaidi ya zote zilizowasilishwa—“Sauti ya Matumaini [Voice of Hope].” Ilianza shughuli zake takriban miaka 50 iliyopita. Voice of Hope ilisaidia wasikilizaji wa radio wakati wa zama za ukomunisti kupata maudhui ya Biblia bila udhibiti wa kila mahali. Ushirikiano na Adventist World Radio umeiwezesha Voice of Hope kukua kitaaluma.
Baadaye katika ibada hiyo Niewolik alieleza kwamba Kanisa la Waadventista nchini Poland kwa sasa linahamisha shughuli za uchapishaji, vyombo vya habari, na mafunzo ya taasisi zake zilizopo za kimishenari kwenda Hope Media Poland. “Kanisa linatarajia kupata fursa mpya za kueneza injili kwa njia ya machapisho, vipindi vya redio na televisheni, na miradi mingine ya mtandaoni,” alisema.



Paper Love Ministry imewafikia maelfu nchini Ufilipino na kwingineko

Edward Rodriguez, Divisheni ya Kusini mwa Asia-Pasifiki
Katika ulimwengu unaotawaliwa na ujumbe wa papo hapo na miitikio ya muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii, idara moja huko Cavite, Ufilipino, inaendelea kuwavutia watu wengi—kadi moja iliyotengenezwa kwa mikono kwa wakati mmoja.
Paper Love Ministry, kikundi kidogo lakini chenye shauku cha wasanifu wa Kiadventista, kimejitolea kuunda kadi za salamu zilizotengenezwa kwa mikono ambazo huleta faraja, hutia moyo na hamasa kwa watu binafsi wanaohitaji. Wakitumia nyenzo sahili za sanaa—karatasi, kalamu, vibandiko, mihuri, na upendo—watu hawa wajitoleao hugeuza kurasa zilizo wazi kuwa vikumbusho vya kutoka moyoni vya kuwapo kwa Mungu na huruma ya kibinadamu. Kile kilichoanza kama kitendo chema cha fadhili kimekua na kuwa harakati ya maana ambayo inabadilisha maisha katika nafasi tofauti—kutoka vyumba vya hospitali hadi njia za ndege.
“Mnamo 2017 nilianza kufanya kazi ya dhati: kuunda kadi zilizotengenezwa kwa mikono ili kuwapa wageni,” alieleza Joy Tagolgol, mwanzilishi wa huduma hiyo. “Lilikuwa tendo rahisi lakini lenye nguvu na la fadhili, lililoeneza furaha kwa wale niliokutana nao. Tulisonga mbele kwa haraka hadi 2024; na tendo hili dogo limechanua na kuwa utamaduni mzuri unaoshirikishwa kwa marafiki. Kwa pamoja tunatengeneza kadi za wafanyakazi wa ndege, kwani kazi yetu mara nyingi hutupeleka angani.”
Tagolgol na rafiki zake mara nyingi huwapa kadi wahudumu wa ndege wakati wa safari zao. Miitikio, alisema, imekuwa mikubwa.
“Wahudumu wengi wa ndege, waliguswa na tendo letu lenye mguso mkubwa, wanaonyesha shukrani zao kwa tabasamu la kutoka moyoni na wengine hata kumwaga machozi ya shangwe.” Katika kazi zao za kuchosha, mara nyingi malalamiko hufunika thamani yao na kufanya kadi zetu zilete mguso mkubwa sana,” akaongeza. Mungu atukuzwe kwa kutubariki kwa uvumbuzi na mikono ili kuendeleza huduma hii, tukipeleka nuru na upendo kwa wahudumu wa kwenye ndege tunaokutana nao.”
JAMBO LA KUSHIKIKA KATIKA ULIMWENGU WA KIDIJITALI
Paper Love Ministry inasimama kama kipingamizi cha hali isiyo ya kawaida ya mawasiliano ya kidijitali. Ingawa teknolojia huwezesha ubadilishanaji wa haraka, asili binafsi ya ujumbe ulioandikwa kwa mkono hutoa jambo la kina zaidi. Utafiti unaendelea kudokeza kwamba yaliyoandikwa kwa mkono huibua mwitikio mkubwa zaidi wa kihisia kuliko ujumbe wa kidijitali. Vile vile, makala iliripoti kwamba asilimia 70 ya watu wazima wanaona kupokea kadi za karatasi kuwa na maana zaidi kuliko njia mbadala za dijitali.
Kadi zilizoandaliwa na Paper Love Ministry mara nyingi huwa na aya za Biblia na maneno ya kufariji, zikiruhusu watu wanaojitolea kushiriki kwa uzuri tumaini na upendo wa Kristo kwa njia ambazo ni za heshima na za kweli.
ZAIDI YA SANAA—NI HUDUMA
Mawanda ya huduma hii huenda mbali zaidi ya kwenye ndege. Watu wa kujitolea hupanga warsha mahalia na kushirikiana na vikundi vya kijamii ili kuwafundisha wengine jinsi ya kutengeneza kadi kama njia ya kuwafikia wengine. Iwe imetumwa kwa wagonjwa, washiriki wa kanisa, au wageni, kila kiumbe kinabeba ujumbe wa neema.
Tangu mwanzo wake mdogo mnamo mwaka 2017 hata kufikia ukuaji wake mwaka 2024, Paper Love Ministry inaonyesha kwamba matendo sahili ya fadhili, yanayokita mizizi katika sala na kusudi, yanaweza kuacha athari ya kudumu.
Huduma hii inatukumbusha kuwa sio lazima upaze sauti ili kusikika,” alisema mmoja wa wachapishaji wa kwenye mitandao ya kijamii. “Unahitaji tu kuwa mkweli.”
Tagolgol alisisitiza kwamba “katika kila kadi iliyofungwa utepe na aya ya Maandiko yenye wino, Paper Love Ministry inatuma ujumbe tulivu lakini wenye nguvu: unaonekana, unapendwa, na kuna tumaini.”


Injili na ujumbe wa onyo
NA THOMAS R. SHEPHERD
Ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12 ni kitovu cha utume wa kanisa letu na umekuwa tangu mwanzo. Waadventista wa awali waliona katika mahubiri haya yenye nguvu utume wao kwa ulimwengu katika maandalizi kwa ajili ya ujio wa hivi karibuni wa Bwana na Mwokozi wetu. Lakini kama unausoma ujumbe huu wenye sehemu tatu kwa mara ya kwanza, unaweza kushangaa jinsi unavyoendana na maisha katika karne ya ishirini na moja. Je, ujumbe huu wenye sehemu tatu una maana gani kwetu leo na ni kwa jinsi gani tunaweza kushiriki na wengine maana yake kwa jirani zetu?
MPANGILIO
Ujumbe wa malaika watatu unaonekana katika njozi kuu ya Ufunuo 12-14.1 Katika njozi hii kuu mada kuu za Ufunuo zinafikia upeo wake—wema dhidi ya uovu, utii dhidi ya uasi, ibada ya kweli dhidi ya ibada ya uongo. Ufunuo 12 huanza na picha ya kuhuzunisha ya mwanamke (watu wa Mungu waaminifu) wakikimbizwa na joka kubwa jekundu (shetani na vibaraka wake wa duniani, Ufu. 12). Vita vinaanzia mbinguni kwa Mikaeli na Malaika Zake wakimshinda yule joka na kumtupa chini duniani. Lakini joka anamkimbiza mwanamke nyikani na kwenda kufanya vita na wazao wake waliosalia (watu wa Mungu katika siku za mwisho).
Ufunuo 13 huongeza mkazo kwa kuzungumzia juu ya wanyama wawili (mamlaka za mwisho za mateso), mmoja toka baharini, mwingine toka katika nchi, ambao wanaendeleza mateso ya watu wa Mungu. Inaonekana kana kwamba wema utashindwa na uovu kushinda, wakati malaika watatu wanapotokeza uwandani (Ufu. 14), wakitangaza ujumbe wa wokovu na ujumbe wa uangamivu. Baada ya kazi yao kuisha yuaja Mwana wa Adamu katika mawingu ya mbinguni, akitimiza kile ambacho malaika watatu wamekihubiri. Kwa hiyo, kwa nini tunao ujumbe huu wa malaika watatu katika hatua hii ya Ufunuo?
UJUMBE WA INJILI
Ujumbe wa malaika wa kwanza unasomeka kama ifuatavyo katika Ufunuo 14:6, 7:
“Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa. Akasema kwa sauti kuu, ‘Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.’ ”2
Ujumbe wa malaika huyu unaitwa “Injili ya Milele,” lakini hauonekani hivyo kwa wasomaji wengi. Hakuna kutajwa kwa neema, imani, tumaini, upendo, msamaha, wokovu wala msalaba. Inawezekanaje ujumbe huu uitwe injili wakati hauna maneno ambayo tunayahusisha kabisa na ujumbe wa Wokovu wa Agano Jipya? Tatizo liko katika dhana yetu ya jinsi ya kuelezea ujumbe wa injili. Tumezoea ufafanuzi wa Paulo wa haki kwa imani, upatanisho na Baba kupitia kwa Bwana Yesu na kisa cha msalaba kama kinavyoelezwa katika vitabu vya Injili.
Lakini njia nyingine ambayo kwayo ujumbe wa injili unaelezwa inatoka kwa Yesu Mwenyewe. Katika Marko 1:14, 15 tunakutana na ujumbe wa Yesu punde tu baada ya ubatizo Wake. “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, ‘Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.’ ” Hapa ujumbe mnyofu wa injili ya Yesu una sehemu kuu tatu: utimilifu wa unabii wa Biblia (hapa utimizwaji wa ujio wa Masihi uliotajwa hapo kabla katika Danieli 9:24—27), ahadi ya Agano (ufalme wa Mungu umekaribia) na mwito kwa ajili ya uanafunzi (tubuni na kuiamini Injili).3
Tunaviona vidokezo vivyo hivyo vitatu katika ujumbe wa malaika wa kwanza: utimilizwaji wa unabii wa Biblia (hapa saa ya hukumu kama ilivyotabiriwa katika Danieli 7—8), ahadi ya Agano (kupokelewa kwa ufalme na watu wa Mungu katika hukumu [angalia Dan. 7:22]) na mwito kwa ajili ya uanafunzi (mcheni, mtukuzeni na kumwabudu Mungu kama ilivyo kitovu katika ujumbe wa hukumu na Mungu kama Mwumbaji).4 Kwa hiyo, ujumbe wa malaika wa kwanza huenda sambamba na kuhubiri kwa Yesu. Yesu alihubiri ufalme wa Mungu wakati wa uanzishwaji wa kanisa la Agano Jipya; Ufunuo hutangaza utimilizwaji wa ufalme wakati wa ufungwaji wa historia ya dunia.
Wakati mahubiri ya Yesu yalitoa mwito wa uanafunzi katika mandhari ya ulimwengu wa Kimediterania wa siku Zake, ujumbe wa malaika wa kwanza unatoa mwito wa uanafunzi katika mandhari ya pambano la nyakati za mwisho kati ya wema na uovu. Mcheni Mungu, sio wanyama. Mtukuzeni Mungu, sio wanadamu wala mamlaka za uovu. Mwabuduni Mungu pekee, sio mnyama wala sanamu yake. Kwa hiyo ujumbe wa malaika wa kwanza kwa kweli ni ujumbe wa Injili katika mandhari ya siku za mwisho za historia ya dunia. Lakini je, vipi kuhusu ujumbe wa malaika yule wa pili na wa tatu?

KWA NINI LUGHA HIYO YA KUTISHA?
Katika nuru ya ujumbe wa Yesu tunaweza kuona kwamba malaika wa kwanza anahubiri Injili katika mandhari ya wakati wa mwisho. Lakini ujumbe wa malaika wa pili na wa tatu—anguko la Babeli na ghadhabu ya Mungu juu ya waabudu wa uongo—huonekana kwa wengi kuwa haupatani na upendo wa Mungu wote kwa watu wote. Inawezekanaje kwa Mungu anayeelezea upendo Wake mkuu katika Yohana 3:16 (“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”) awe Mungu huyo huyo ambaye anaahidi kuharibiwa kwa wanaomwabudu mnyama katika Ufunuo 14? Lugha ni ngumu katika Ufunuo 14:9—11: “Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo. Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.”
Je, haya yote yanamaanisha nini?
MNYAMA: SANAMU NA ALAMA YAKE
Mnyama alielezewa katika ujumbe wa malaika yule wa tatu ni mnyama kutoka baharini wa Ufunuo 13. Kujifunza kwa umakini sura ya 13 kunaonyesha kwamba mnyama kutoka baharini ni mamlaka ya mpinga-Kristo ambayo inaudanganya ulimwengu, akiwapotosha watu kutoka katika ibada ya Mungu wa kweli. Zaidi ya hayo, mnyama kutoka baharini na mshirika wake, mnyama kutoka nchi kavu (mpinga-Roho Mtakatifu katika teolojia ya Ufunuo), hutishia kumtesa na kumwua mtu awaye yote ambaye hatamwabudu mnyama kutoka baharini.5 Hii dhana ya ibada ni kiini cha pambano katika Ufunuo. Pande mbili zimefunuliwa: wamwabuduo mnyama dhidi ya wanaomwabudu Mungu.
Sanamu ya mnyama ni ukumbusho wa sanamu kuu ya dhahabu ya Nebukadnezza katika Danieli 3. Pale kila mtu aliamuriwa kuiabudu sanamu iwakilishayo mamlaka ya Nebukadneza na mtazamo wa ulimwengu vinginevyo ukabiliane na mateso ya kufisha katika tanuru liwakalo moto. Vijana watatu mashujaa waliikataa amri ya mfalme na kisha kimiujiza walishinda moto wa tanuru kwa uweza wa Mungu. Kwa hiyo, sanamu ya mnyama katika Ufunuo 13 huwakilisha mamlaka na mtazamo wa kiulimwengu wa mamlaka ya mpinga Kristo na washirika wake katika kumwasi Mungu. Ni ama ukubaliane na mamlaka hii au ukabiliane na mauti.
Alama ya mnyama ni ishara ya kutii matakwa ya mnyama wa baharini. Kwa vile Ufunuo ni kitabu cha ishara, hatufai kuichukulia alama hiyo kama aina ya chale iliyochanjwa kwa mtu, bali inaashiria kuwa mtu huyo amekubaliana na matakwa ya mnyama huyo iwe ni kwa moyo wake wote (alama kwenye paji la uso) au hata kwa vitendo vya nje (alama ya mkono).
MVINYO WA GHADHABU YA MUNGU
Tunarudi kwenye ile lugha ngumu katika Ufunuo 14:9—11. Tunaweza kuliuliza swali kwa namna tofauti kidogo. Ni kwa nini Mungu awatishe wanaomwabudu mnyama kwa moto na kiberiti? Kuna ubaya gani kumwabudu mnyama? Ni kanuni ya asili yetu kwamba tunabadilika kuwa kama kile tunachokienzi. Wapenzi wa wacheza sinema maarufu au wana michezo maridadi huvaa kama wao, kuzungumza kama wao, hata kuwaigiza. Katika hali ya juu tunabadilika kuwa kama kile tunachokiabudu. Ukimwabudu mnyama, utaanza kufikiri na kutenda kama mnyama.
Kwa sababu mnyama ni mpinga Kristo, unaanza kutenda kwa namna tofauti na vile anavyotenda Yesu. Kile anachokipenda Yesu wewe unakichukia. Pale anapoonyesha huruma kwa waliotwezwa, unaonyesha kutojali kwa wale wanaoteseka. Pale Yesu alipo mwadilifu, mwaminifu, anapojawa na wema na ukweli, unakuwa mtovu wa uadilifu, unakosa uaminifu, ukijawa na uovu, chuki na udanganyifu. Ni jambo la hatari sana kumwabudu mnyama na sanamu yake. Kwa kweli, uovu wote, makosa ya jinai, vita, matusi, uongo na chuki tunavyoviona ulimwenguni ni dalili tu za ukweli wa tatizo la kudumu—ibada ya uongo, na kuabudu sanamu. Ibada ya uongo huleta maadili ya uongo (kuwatendea vibaya watu).
Sasa je, ni kwa nini Mungu ashughulikie haya yote kwa mvinyo wa ghadhabu Yake? Fikiria kuwa unashuhudia kitendo cha unyanyasaji wa hali ya juu na udhalimu mkubwa. Je, haupaswi kushughulikiwa? Kuacha unyanyasaji na dhuluma bila kushughulikiwa, hiyo yenyewe itakuwa ni dhuluma.
Mungu hataruhusu unyanyasaji wa mpinga Kristo kuendelea katika dunia yetu. Kama vile daktari wa upasuaji, ataikatilia mbali saratani inayouangamiza ulimwengu wetu. Dhambi ndiyo saratani hiyo. Ujumbe wa malaika wa kwanza huelekeza kwenye suluhisho ambalo Mungu anatoa kwa ulimwengu wenye ugonjwa wa dhambi—kurudi kwa Mungu. Kita maisha yako kwa Yesu ili uweze kupata furaha ya kweli, thamani ya maadili ya kweli, maana ya kweli, ibada ya kweli na kuwatendea wengine kwa huruma. Vinginevyo, saratani ya dhambi itayala maisha yako na kuharibu mahusiano yako. Liko hivyo na wala halihitaji mjadala.

MALAIKA WENGINE
Kiukweli kuna zaidi ya malaika watatu katika Ufunuo 14. Watatu zaidi wanatokeza katika nusu ya mwisho wa sura hii. Jambo kuu katika sura hii na la kitabu ni Ufunuo 14:14.6 “Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali.” Huu ni ujio wa pili wa Yesu Kristo katika mawingu ya utukufu ili kuwaokoa watu Wake. Ambapo mpaka sasa katika ufunuo kumekuwa na kuhamia katika patakatifu pa Mungu pa mbinguni, lakini kutoka hapa na kuendelea harakati ni kuelekea nje. Ufunuo 14:15 inasema, “Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa.’ ” Kwa ishara, mundu katika mkono wa Yesu ni mundu wa wokovu anapovuna nafaka za dunia zilizoiva. Nafaka imeokolewa, imetunzwa ghalani, hivyo mavuno haya ni ishara ya wokovu. Matukio haya yanafanana na ujumbe wa injili wa wokovu wa malaika wa kwanza.
Katika sehemu inayobaki ya Ufunuo 14 malaika wengine wawili wanahusika katika ishara ya uvunaji wa zabibu za dunia. Zabibu zinakamuliwa zinapovunwa na kutiririsha kitu cha rangi ya damu—ishara ya laana, kuangamizwa kwa waovu. Malaika hawa wawili wanaendana na ujumbe wa malaika wa pili na wa tatu, ambao huhubiri ujumbe kinyume na ujumbe wa wokovu unaoletwa na malaika wa kwanza.
HITIMISHO
Ufunuo 14:6-12 hutoa ujumbe wa onyo kwa dunia kabla tu ya Yesu Kristo kurudi, ujumbe wa wokovu na uharibifu, mwito kwa ajili ya uanafunzi ili kumrudia Mungu au ukabiliane na matokeo halisi ya uangamivu wa milele, sio kwa sababu Mungu ni mbaya na asiyejihusisha nasi, bali ni kwa sababu ibada ya uongo itaharibu maisha yako na Mungu hataruhusu uovu, chuki, maumivu na huzuni kuendelea.
Ufunuo 14:14-20 hutuonyesha utimilizwaji wa ujumbe huo wa onyo katika fungu la 6—12. Mavuno ya aina mbili yanakuja, mavuno ya wokovu na mavuno ya uangamivu. Mungu anakutaka wewe na mimi, majirani zetu, miji yetu na nchi zetu kupokea maonyo na kuokolewa. Huu ndio utume wetu mkuu tupaswao kushiriki na ulimwengu wote.

1 Wasomi wana mawazo mbalimbali kuhusu muundo na kiini cha kitabu cha Ufunuo. G. K. Beale ana mjadala mrefu kuhusu muundo huo katika maoni yake, na mojawapo ya miundo anayoipendelea ni maono saba yenye utangulizi na hitimisho. Tazama: G. K. Beale, The Book of Revelation, NIGTC (Grand Rapids, Mich.: Eerdmans, 1999), uk. 108-151. Tazama pia Ranko Stefanovic, Revelation of Jesus Christ, toleo la pili (Berrien Springs, Mich.: Andrews University Press, 2009), kur. 24-50. Stefanovic anapendelea muundo wa kisanaa wa ulinganifu ukiwa na maono ya sura za 12-13 katikati. Mimi binafsi napendelea sura za 12-14 kama maono ya kiini, huku ugeuzo mkuu ukiwa katika Ufunuo 14:14, panapotokea mabadiliko ya kuelekea kutoka katika patakatifu pa mbinguni baada ya hatua hiyo.
2 Isipokuwa imetajwa vinginevyo, nukuu za Maandiko zimetolewa katika Swahili Union Version Bible. Zimetumika kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa.
3 Danieli 9:24-27 inaelezea kuja kwa Masihi na inaonyesha kipindi cha muda kuanzia “kutolewa kwa amri ya kuirudisha na kuijenga tena Yerusalemu.” Amri ya mwisho ya kuijenga tena Yerusalemu ilitolewa mwaka 457 K.K. Katika unabii huu, kuja kwa Masihi kungetokea baada ya majuma 69 ya kinabii, au miaka 483 halisi, ambayo inaifikia mwaka 27 B.K., kipindi kilekile ambacho Kristo alibatizwa, akatiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, na kuanza huduma Yake (tazama Marko 1:9-11; Matendo 10:38).
4 Danieli 7 inaonyesha hukumu ya Mungu juu ya nguvu za kidunia zilizo ovu. Danieli 8 inaonyesha utakaso wa mahali patakatifu pa mbinguni sambamba na kipindi chake cha kutokea, yaani unabii wa jioni na asubuhi 2,300. Kwa kuzingatia kwamba mwanzo wa kipindi hicho umewekwa na Danieli 9—yaani kuja kwa Masihi—basi mwanzo wa hukumu unaifikia mwaka 1844.
5 Mnyama wa baharini katika historia ni Rumi katika awamu yake ya Kikristo, na mnyama wa nchi ni Marekani, inayofanya kazi kwa ushirikiano na mnyama wa baharini. Tazama C. Mervyn Maxwell, God Cares (Boise, Idaho: Pacific Press Pub. Assn., 1985), gombo la 2, kur. 324-349.
6 Ufunuo inaanza na maono ya Yesu akitembea kati ya vinara vya taa katika patakatifu pa mbinguni (Ufu. 1:12, 13). Maono yanapoendelea, kuna mwendo wa kuelekea ndani katika patakatifu pa mbinguni, na kilele chake ni Ufunuo 11:19, ambapo inaonekana Sanduku la Agano katika patakatifu pa patakatifu. Kuanzia Ufunuo 14:15 na kuendelea, mwendo ni kutoka nje ya patakatifu pa patakatifu, ukionyesha hukumu.

Thomas R. Shepherd, Ph.D., Dr. P.H., ni profesa mkuu wa utafiti katika Seminari ya Teolojia ya Waadventista kwenye Chuo Kikuu cha Andrews, Berrien Springs, Michigan, na mchungaji katika Konferensi ya Michigan.


Mpango wa Mungu usiotarajiwa wa kunitumia
NA VICKI FUNK
Uzoefu wangu katika huduma ya gerezani ulianza mwaka 2017 nilipokuwa nimesoma makala ya Mradi Steps to Christ juu ya mwanamke aliyetuma kadi kwa watu binafsi waliokuwa chini ya ulinzi. Nilijiwazia mwenyewe, ninaweza kufanya hivyo! Kizuizi kikubwa kilikuwa ni kupata orodha ya watu wa kuwatumia kadi hizo. Niliwasiliana na gereza mahalia, lililoko maili chache tu kutoka kanisani kwetu. Nimekuwa nikilipita gereza hilo nilipokuwa nikienda shuleni na kanisani tangu mwaka 1969, bila kuwafikiria kwa kina watu waliokuwa nyuma ya kuta hizo ndefu. Roho Mtakatifu alinisukuma, kwa hiyo nilipiga simu gerezani.
Nilizungumza na chapleni ambaye aliniambia mara moja nimpelekee pendekezo la kile ambacho ningependa kufanya. Nilimwambia nahitaji tu orodha ya watu ambao ningeweza kuwatumia kadi. Aliniambia nimtumie pendekezo kwa barua pepe. Baada ya kukata simu, nikiwa nimechanganyikiwa kwa kiasi fulani na ombi hili, nilianza kuwasiliana na watu wengine ili kupata mawazo mbalimbali. Nilielekezwa kwa mtu kutoka Three Angels Broadcasting Network (3ABN). Mtu huyo alinipa anwani ya shirika liitwalo Christmas Behind Bars. Sikuwa nalifahamu shirika hilo, lakini nilimpigia simu mkurugenzi, Lemuel Vega, ili kuona vile atakavyonisaidia. Sikuwa najua jinsi ambavyo amekuwa akijihusisha na huduma ya magereza. Huduma yao ilikuwa ya muhimu sana kwa huduma yetu changa ya kuwafikia wafungwa.
BARAKA ZISIZOTARAJIWA
Niliweka miadi na chapleni mkuu wa Kituo cha Stateville Correction Center huko Illinois, Marekani, ili kujadili jinsi ya kushiriki injili na watu waliofungwa huko. Huu ulikuwa mkutano mzuri sana, ukionyesha jinsi Mungu anavyofungua milango kwa kazi Yake kusonga mbele.
Kabla ya mkutano, nilimtumia chapleni orodha ya mambo ambayo ningependa kuwafanyia wafungwa na alikubaliana na takribani kila kitu: (1) Kwa njia ya huduma Christmas Behind Bars, tunampatia kila mfungwa mfuko ambao unakuwa na vitu kama kitabu Steps to Christ, masomo ya Biblia tangamano bure na vyakula; (2) tunatoa vitabu, vitafunwa, karatasi, penseli na vitu vingine; (3) moja kwa moja tunawaandikia wafungwa kadi za siku ya kuzaliwa na krisimasi, n.k. chapleni aliniuliza kuwa ni wafungwa wangapi ningependa kuwaandikia na kwa sababu zipi, nilisema 500. (Lazima alikuwa ni Roho Mtakatifu aliyeniongoza, maana kwa kweli, sijui kile nilichokuwa nakiwaza.)
Pia nilimwuliza chapleni ikiwa tunaweza kuendesha huduma za kidini kwa wafungwa. Alisema hajawahi kuwa nayo, lakini alilifanyia kazi ombi langu: “ninakutaka utuletee mafundisho ya Biblia kutoka kwenye kitabu cha Danieli na Ufunuo kuanzia mwezi Juni au Agosti.” (Mimi? Ningesema nini kingine? Ndio!) Nilipokuwa nikiondoka gerezani siku ile, imani yangu ilihamasika sana, kuona jinsi Bwana alivyofungua mlango ili kuwahudumia watu hawa.

Kanisa langu lilikuwa ndio tu limemaliza semina ya hadhara juu ya Danieli na Ufunuo na mchungaji alikuwa ameniomba mimi kushiriki katika kuongoza mtiririko wa mafundisho haya. Kumbe sikujua kuwa nilikuwa naandaliwa kufundisha mtiririko huu wa masomo katika Gereza la Stateville. Mungu alikuwa akiniandaa na sikuwa nalijua hilo.
Mwishoni mwa msimu wa vuli, nilianza Masomo yangu ya Biblia juu ya Danieli na Ufunuo pamoja na wanaume 30 hivi. Kadiri muda ulivyopita, niliona kwamba wanaume fulani wangeondoka, na wengine wangekuja. Kabla ya mtiririko wa masomo kuisha, nilitoa seti zaidi ya 100 za mafunzo ya Biblia, magazeti, vitabu, na vifaa vingine. Wafungwa hao waliniuliza maswali kuhusiana na mafundisho, mafungu ya Biblia na imani yangu. Niliendelea kufundisha huko Stateville, nikishughulika na vitabu vingine vya Biblia, kama vile Ezekieli na Warumi, hadi UVIKO-19 ulipotokea.
Hata wakati wa UVIKO-19, washiriki wa kanisa walituma zaidi ya kadi 300 na vifaa vya kidini. Orodha yangu ya watu binafsi imeongezeka hadi zaidi ya watu 550. Tunaendelea kuwafahamisha wanaume hawa kuwa hawajasahaulika na kwamba Mungu anawapenda. Hatutumii kadi tu bali pia tunatuma machapisho na kadi ili waombe Mafundisho ya Biblia angalau mara moja kwa mwaka.
Mungu anaigusa mioyo ya wanaume hawa. Wengi wameomba masomo ya Biblia, Biblia yenyewe, vifaa vya kidini bila malipo, na shauku ya kubatizwa katika Kanisa la Waadventista wa Sabato. Ninapokea barua za kila juma zinazoonyesha shukrani na wakati mwingine ikijumuisha zaka na matoleo kwa ajili ya kanisa.
Kamwe sikuwahi kufikiri kwamba ningekuwa mtu ambaye Mungu angenitumia ili kuwafikia wale walio nyuma ya kuta za gereza, lakini amekuwa akiniandaa kwa ajili ya huduma hii na wala sikuwa najua hivyo.

Vicki Funk ni mratibu wa kuwafikia wengine kanisani kwake huko Joliet, Illinois, Marekani. Kisa hiki kilichapishwa hapo awali katika toleo la Agosti 2023 la Lake Union Herald.


Sasa ndio wakati wake
NA TED N. C WILSON
Akiwa uhamishoni kwenye ufukwe wa huko Patmo, mtume Yohana alijikuta akiwa na wakati mwingi wa kutafakari juu ya miongo yenye matukio mengi ambayo yalikuwa yamefanya safari yake kuwa vile ilivyo. Zaidi ya miaka 60 ilikuwa imepita tangu alipomwona mara ya mwisho Mwokozi wake mpendwa akipaa mawinguni kwa ahadi ya kurudi tena. Yerusalemu iliharibiwa, wafuasi wa Yesu wakatawanyika kote, na kati ya wale wanafunzi 12 wa kwanza, yeye pekee ndiye aliyebaki. Lakini akiikumbuka ahadi ya Yesu, “tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mt. 28:20), alikuwa na amani.
Ghafla ukimya wa tafakari ya Yohana ulivunjwa na sauti kuu nyuma yake, kama ya tarumbeta, ilisikika: “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho” na “Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba” (Ufu. 1:8, 11).
Akigeuka kwa haraka, mwanafunzi mpendwa alimwona Yesu Kristo Mwenyewe, akisimama mbele yake katika utukufu Wake wote. Kazi ya Yohana ilikuwa bado haijaisha. Yesu alikuja ili kumpatia kile ambacho kingekuwa kazi maalum:
“Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo” (aya ya 19).
Ulikuwa ndio mwanzo wa “Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi” (aya ya 1).
Kupitia huu ufunuo wa pekee, Yesu alifunua, kwa lugha ya ishara, historia ya baadaye ya kanisa Lake katika zama zote hata mwisho wa wakati. Na huu ufunuo wa Mungu unaonyesha sio tu historia ya baadaye bali unaonyesha pia ujumbe muhimu mno kwa ajili yetu leo, ikiwa ni pamoja na ujumbe wa malaika watatu.
MWITO KUU
Ufunuo 14:6 – 12 huwasilisha huu ujumbe wa wakati wa mwisho kama mwito mkuu ili kumwabudu Mungu kuwa ni muumbaji wetu, na kutambua kuwa hukumu imekwisha anza, kutambua anguko la Babeli na kwa makusudi kuikataa alama ya mnyama.
Mungu ameutoa huu ujumbe wa haraka kwa watu Wake masalio wa wakati wa mwisho ili kuufikisha kwa ulimwengu wote kabla Yesu hajarudi. Ni fursa ya namna gani kuwa sehemu ya watu wa Mungu wa siku ya mwisho wakitangaza ujio wa hivi karibuni wa Yesu Kristo—sisi sio tu kanisa; tu watu wenye ujumbe kwenye utume.
Kutoka kwenye kalamu yenye uvuvio tunasoma, “Kwa namna ya pekee Waadventista wa Sabato wamewekwa ulimwenguni kuwa walinzi na kuwa nuru ya ulimwengu. Wamekabidhiwa onyo la mwisho kwa ulimwengu unaoangamia. Juu yao inang’aa nuru kuu kutoka kwenye Neno la Mungu. Wamepewa kazi yenye umuhimu mkubwa mno—utangazaji wa ujumbe wa malaika wa kwanza, wa pili na wa tatu. Hakuna kazi nyingine yenye umuhimu mkubwa wa namna hiyo. Hawapaswi kuruhusu kitu chochote kuteka usikivu wao. Ukweli muhimu zaidi kuwahi kutolewa kwa wanadamu tumepewa ili kuutangaza kwa ulimwengu. Utangazaji wa ukweli huu unapaswa kuwa kazi yetu. Ulimwengu unapaswa kuonywa na watu wa Mungu wanalazimika kuwa wakweli kwenye amana iliyokabidhiwa kwao.”1
UMEITWA
Kaka na dada zangu, Mungu anakualika kuwa sehemu ya mwito Wake wa mwisho kwa ulimwengu. Je, Utamuitikia na kusema, “Ndio, Bwana, Ninakwenda”?
Huenda wewe ukawa kama mwanamke wa Brazili ambaye hadi sasa, kwa msaada wa Mungu, amewavuta zaidi ya watu 80 kwa Bwana. Pale aliposikia kuhusu harakati za “ninakwenda” aliuliza, “Hii Nitakwenda inamaanisha nini?—Nimeshakwenda!” Bado anakwenda.
Hata kama bado hujamwambia Bwana, “Nitakwenda,” bado hujachelewa. Bwana Yesu anakuita—unahitajika uufikie ulimwengu kwa ajili Yake.
Uvuvio unatuambia kwamba “kazi ya Mungu katika dunia hii haiwezi kwisha bali mpaka pale wanaume na wanawake kujumuisha washiriki wetu kujitokeza kazini na kuunganisha juhudi zao pamoja na zile za wachungaji na maofisa wa kanisa.”2
TMI ULIMWENGUNI
Hii ndiyo maana ya Uhusikaji wa Washiriki Wote Ulimwenguni (TMI)—kila mtu, kila mahali, anashiriki ujumbe wetu kwa ulimwengu tuliopewa na Mungu. Unaitwa, umechaguliwa na Mungu Mwenyewe, ili kuwafikia wengine kwa ajili Yake.
Hili linafanyikaje? Kwanza, lazima tuombe kwa bidii ili kujaza na Roho Mtakatifu. Yesu aliahidi, “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13). Na kabla tu ya kuangikwa msalabani alitoa ahadi hii: “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohana 14:26).
Tunapokuwa tukidai ahadi hizi tunaweza kuwafikia wengine kwa ajili ya Yesu, tukionyesha huruma, kuwasaidia wanaoteseka na kufundisha haki.3 Ongea na jirani na rafiki zako, waombee na kuomba pamoja nao, waambie kile ambacho Yesu amekufanyia, waalike katika mikutano kanisani mwako, toa mafundisho ya Biblia na kuwa mchapakazi katika kuwafikia wengine kanisani mwako.

USHUHUDIAJI ENDELEVU
Hizi ni baadhi tu ya njia ambazo kwazo unaweza kutumika katika TMI Ulimwenguni. Kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita familia moja ilipata njia ya pekee ya kumtia moyo mtoto wao ili kuwa kielelezo hai cha Uhusikaji Mkamilifu wa Kila mshiriki.
Binti yao mdogo alizaliwa punde tu uinjilisti wa TMI uliposhika kasi katika nchi yao ya Burundi. Ulikuwa ni wakati wa taharuki, watu wa Burundi walipowaambia majirani, marafiki, ndugu na hata wageni juu ya Yesu. Watu walikuwa wakikutana katika makundi madogo ili kujifunza Biblia. Kisha walikutanika katika mikutano mikubwa ya uinjilisti, ambapo watu wengi walibatizwa.
Wenzi hawa walifurahia kushuhudia uinjilisti wa TMI na walitaka familia yao iwe endelevu katika ushuhudiaji. Binti yao alipozaliwa, wakachagua jina bora kwa ajili yake kuwa TMI. Kadiri binti huyo mdogo alivyokua, TMI ikawa zaidi ya jina lake—ikawa mtindo wa maisha yake. Alipokuwa na umri wa miaka minne tu, alianza kuimba ili kuwafikia wengine kwa ajili ya Yesu. Leo hii ana miaka 6 na kwa njia ya uimbaji wake tayari ameigusa mioyo ya watu wengi.
Marafiki, hata kama majina yenu sio “TMI,” bado mnaweza kuwa sehemu ya Uhusikaji Mkamilifu wa Kila Mshiriki! Yesu anakuja hivi karibuni. Sasa ndio wakati wa kujihusisha. Sasa ndio wakati wa kuitikia mwito wa Mungu, ukisema, “Ndio Bwana, Nitakwenda! Nitume mimi.”

1 Ellen G. White, Testimonies for the Church (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1948), vol. 9, uk. 19.
2 Ibid., uk. 117.
3 See Ellen G. White, Welfare Ministry (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1952), uk. 250.

Ted N. C. Wilson ni Mwenyekiti wa Konferensi Kuu ya Waadventista wa Sabato. Makala nyingine na vitabu vya maelezo zaidi vinapatikana katika X (awali Twitter):@pastortedwilson na kwenye Facebook: @Pastor Ted Wilson.


NA MERLE POIRIER
Unashikilia mkononi mwako jarida la mwisho la Adventist World. Hebu litafakari jambo hilo kidogo. Hata kama nilijua kuwa siku hii itakuja, ni vigumu kwangu kuandika, hebu jisomee. Mimi, kati ya wafanyakazi wote katika ofisi ya Adventist Review, ndiye pekee niliyefanya kazi na Adventist Worldwakati wa kuanzishwa kwake na kuendelea sasa hadi siku yake ya mwisho. Chapisho lingefikisha miaka 20 mwaka huu, kwa hivyo elewa huzuni yangu katika wakati huu.
Hivi karibuni nilihudhuria ibada ya kumbukumbu ya rafiki yangu. Mume wake alitoa hotuba ya maombolezo, akieleza kwa hisia maisha yao waliyoshiriki pamoja, akisisitiza machungu ya kumpoteza mpendwa wake. Ni kawaida kuhisi huzuni kwa kuondokewa na mtu wa aina hiyo. Hata hivyo, kanisa langu la nyumbani liliungua chini ya mwaka mmoja uliopita, na nimeshangazwa na huzuni inayokuja na kupoteza jengo. Na sasa, mimi pamoja na wenzangu, tunakabiliwa na kupoteza chapisho letu. Tena napata hii hisia ya huzuni isiyo ya kawaida.
MWANZONI
Wazo la Adventist World lilitambulishwa na Mwenyekiti wa zamani wa Konferensi Kuu, Jan Paulsen. Ilikuwa ni wakati ambapo kulikuwa na upungufu wa rasilimali za Waadventista katika sehemu fulani za dunia. Mahali ambapo kuna ombwe, kitu au mtu ataingilia kati ili kuziba pengo, kulikuwa na wasiwasi kwamba uelewa wa teolojia ya Waadventista ilikuwa ikiharibiwa. Suluhisho lilikuwa ni kuwa na chapisho ambalo lingezunguka ulimwengu wa Waadventista na kuwaunganisha washiriki katika ukweli, habari, vipengele, na hadithi. Ingawa hili halikuwa wazo geni katika historia ya Adventist Review, huo ndio ulikuwa upeo wake. Jan Paulsen aliliweka miguuni pa William (Bill) G. Johnsson, ambaye wakati huo alikuwa mhariri wa Adventist Review.
Bill Johnsson alisisimka na kujawa na shauku lakini kwa haraka alizidiwa. Tayari alikuwa akiongoza Adventist Review, na ulikuwa mwaka wa Mkutano Mkuu wa Konferensi Kuu uliohusisha saa za maelezo na maandalizi. Siku moja alipokuwa na huzuni isiyo ya kawaida, nilijitolea kuingilia kati na kusaidia. Hivyo ndivyo ulivyokuwa mwanzo wangu na Adventist World ulivyokuwa mwanzoni kabisa ukijumuisha kuonyesha mfano kwa jambo la kwanza na mtenda kazi mwenzangu Kim Maran ili “Kuuza” wazo kwa wenye viti wa divisheni mbalimbali. Sasa ukiangalia nyuma takribani miaka 20 iliyopita naamini watu wanne mahsusi wanaweza kutambuliwa kwa Adventist World ilipofika leo.
WALIOLETA MABADILIKO

Bill Knott, wakati huo akiwa mhariri mwenza, aliingia kati ili pia kumsaidia Johnsson katika mikutano, kufanya kazi na nyumba za uchapishaji, kupata zabuni, na kuunda mpango wa usambazaji—ambalo pengine lilikuwa changamoto kubwa kuliko zote. Tulijua jinsi ya kuunda gazeti, kuhariri, kubuni na kulichapisha, lakini unawezaje kuliwasilisha kote ulimwenguni ambako hakuna mfumo wa kulipokea? Kwa mfano, eneo moja lilitumia baiskeli kama usafiri mahsusi. Mwito wa utume na kueneza injili ni mkubwa mpaka pale utakapotambua kwamba mwendesha baiskeli hakuwa akichukua nakala chache, lakini mamia! Bila uvumilivu, majadiliano na uelewa wa Bill, Adventist World lisingeweza kuwa na mwanzo mzuri lililoupata.

Roy Adams akawa mlinzi na mlezi wa kwanza wa Adventist World. Mhariri makini, wa kina, na mwangalifu, Roy alihakikisha kwamba Adventist World lilikuwa na usawa wa kimataifa katika upeo wake, tena si jambo rahisi kwa mfanyakazi ambaye wakati huo alikuwa na upeo wa mkubwa wa Amerika Kaskazini. Roy alizikusanya karatasi hizo mpya pamoja. Aliomba ramani ya ulimwengu iletwe na kuwekewa pini katika maeneo ambayo hadithi au habari zilishirikishwa ndani ya chapisho. Ilikuwa picha ya mara moja ya jinsi tulivyouhudumia ulimwengu. Ambapo kulikuwa hakuna usawa au pengo, Roy alihakikisha hadithi zinapatikana kutoka eneo hilo. Anaweza kupewa sifa kwa kuleta usawa, kutopendelea, na ufahamu katika kugundua jinsi ya kuwafikia washiriki wote.

Claude Richli aliingia mnamo mwaka 2007 wakati Bill Knott akiwa ndiye mhariri. Moja ya malengo ya Bill lilikuwa ni kuwafanya wafanya kazi kuwa wa mataifa yote. Bila shaka, Claude alichangia kwa kuwa alifanya kazi katika divisheni nyingine kadhaa na kuzungumza angalau lugha tano. Lakini muhimu zaidi ilikuwa nguvu ambayo Claude aliileta kwa timu yetu. Alikuwa mtaalam mzuri wa hesabu, kiasi kwamba wakati alipoletwa katika timu ya wafanyakazi mambo yote kuhusu idadi ya maneno yalileta mtazamo mpya. Alikuwa mwenye ushawishi, aliyejawa na mawazo mazuri na kuona fursa kwenye Adventist World ambayo ilikaribia kufikiwa. Ustadi wa Claude pamoja na uangalifu wa Roy ulikuwa karibu kupeleka chapisho hilo sehemu ambazo bado hazijaonekana—kiuhalisi.
Nilikuwa nikisimamia usambazaji, ambao ulikuwa kurasa za karatasi zenye kolamu zinazoonyesha majina ya nchi, anwani, wasimamizi na zaidi. Claude alisafiri kote ulimwenguni kwa mtindo wa haraka, na nilizoea kumtania nikisema mahali ambapo watu wengi walikusanya zawadi, Claude alikusanya nchi na lugha mbalimbali. Wakati Claude alipokuwa ofisini kwetu, alikusanya idadi ya lugha kutoka 4 hadi 21! Tulileta timu ya watafsiri, ambao pia nilikuwa msimamizi wao. Lugha za kwanza zilizojadiliwa zilikuwa Kihispania, Kifaransa, na Kireno. Ingawa hii ilionekana kuwa sawa, haikuwa hivyo. Claude alikabiliana na changamoto kana kwamba Kifaransa, Kihispania, na Kireno zilikubalika ulimwenguni pote. Nimefanya kazi na watafsiri wale wale wa asili kwa takriban miaka 18, wote wamejitolea kwa dhati katika jukumu hili la kufanya chapisho kupatikana kwa kila mshiriki duniani kote.
Ni Claude ambaye aligundua masuala ya usambazaji alipokuwa akitembelea maeneo mbalimbali. Claude ndiye aliyewasaidia wale waliokuwa wameshindwa kujua jinsi ya kupokea au kuyagawanya magazeti. Claude ndiye aliyetayarisha chapisho la kila robo mwaka liitwalo Adventist World Digest kwa ajili ya wale ambao hawakuweza kumudu kuchapisha gazeti kamili la kila mwezi. Claude ndiye aliyegundua kuwa barani Afrika gazeti hilo lilienda mbali zaidi ya yale yaliyokusudiwa. Divisheni za Afrika zilikuwa mojawapo ya wapokezi wenye shauku kubwa wa Adventist World, wakilipatia umuhimu mkubwa sana. Likiwa limekusudiwa kwa ajili ya washiriki, walilipeleka kila mahali. Mtu angeenda kumwona Daktari, gereji, hotelini, au maeneo mengine ambapo sio kwa Waadventista wa Sabato na kukuta magazeti mengi ya Adventist World. Wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya mikutano ya uinjilisti na kujifunzia Biblia. Hivi karibuni tumejifunza kupitia barua kuwa Adventist World limegusa maisha ya wafungwa walioomba kupewa Biblia na mafundisho ya Biblia.

Mwisho lakini sio kwa muhimu, ni Gerald Klingbeil. Sitamsemea kwa undani kwa sababu unaweza kujisomea mwenyewe katika ukurasa wa 21, lakini alipofika mnamo mwaka 2009, alikuwa mlinzi mwingine wa Adventist World. Tukiwa ofisini mara nyingi tunamsikia akisema kuwa gazeti hili ni “mwanangu.” Baba wa wasichana watatu, aliongeza wa nne kwa gazeti hili. Alileta umaizi mpya sio tu kwa sababu ni mzaliwa wa ujerumani, bali pia kwa kuwa amewahi kuishi kote ulimwenguni akileta utajiri wa uzoefu wa ulimwengu. Aliwafundisha wafanya kazi kuwa na mtazamo wa kiulimwengu na sio tu Kiingereza. Alileta hamasa ya kuwasaidia waandishi kufikisha sauti zao kanisani akipanua idadi ya waandishi wetu kwenye nchi nyingi tofauti. Hususani alijitahidi kutafuta njia za kusaidia kuleta uelewa muhimu wa kibiblia ikijumuisha kuimarisha uelewa Imani za Msingi za Waadventista. Wakati wa Gerald, Adventist World lilipata kufahamika sana. Likawa kama vile ambavyo Jan Paulson alivyotamani—chombo unganishi kilichotambuliwa na washiriki wa kanisa kote ulimwenguni.

KWAHERI YA MOYO
Labda sasa unaweza kuelewa kwa nini ninaweza kuwa na huzuni tunapokaribia mwisho. Lakini wakati mtu anapokuwa ni mtu wa imani na mfuasi wa Mungu, wakati nyakati zinaweza kuwa za kukatisha tamaa, hatuwezi kukaa hapo kwa muda mrefu, kwa sababu tunajua ni nani anayeongoza. Safari ya Adventist World inaweza kuendelea, lakini tayari lilikwishafanya jambo ambalo hakuna chapisho lingine katika historia yetu limetimiza—kuanzisha njia ya ulimwenguni pote. Sasa mbio hizo zitachukuliwa na uchapishaji wake dada wa, Adventist Review. Ambapo Adventist Review kwa kiasi kikubwa limezuiliwa Amerika Kaskazini, sasa litahudumia ulimwengu kwa njia ile ile ya Adventist World. Watu walioanzisha Adventist World hawakufanya kazi bure. Walisaidia tu kufanya mwelekeo wa nuru uwe wazi zaidi.
Kwaheri rafiki yangu wa uchapishaji. Imekuwa ni fursa nzuri kuwa na kiti cha mstari wa mbele kukuona ukiunganisha zaidi ya Waadventista milioni 21 duniani kote.

Merle Poirier ni meneja wa uendeshaji wa Adventist Review na Adventist World.


Safari ya Uhariri ya Adventist World
Na Gerald A. Klingbeil,
Mwito wa kujiunga na timu ya uhariri ya Adventist Review Ministries ulikuja kama kitu cha kushtua mnamo mwaka 2006. Ndio tu tulikuwa tumehama kutoka Marekani Kusini kwenda Asia na nilifurahia kazi yangu kama profesa wa Biblia ya Kiebrania na mkuu wa kitivo kwenye seminari katika Taasisi ya Kimataifa ya Waadventista ya Masomo ya Juu huko Manila, Ufilipino. Tulikataa kwa lugha nzuri—huu haukuwa wakati mwafaka.
Miaka miwili baadaye mwito ulikuja tena—na wakati huu tuliukubali, ijapokuwa kwa kusitasita. Wengi wa marafiki zangu katika tasnia ya elimu hawakuelewa. Kwa nini niache kufundisha darasani niende kuhariri magazeti mawili maarufu? Lilikuwa ni swali zuri mno na niligundua kuwa nilihitaji kuwa sehemu ya mazungumzo ambayo yalienda mbali zaidi ya darasani au wakati fulani—kutenganisha minara miwili ya tasnia ya elimu. Adventist World, kitoto kipya mjengoni, kilitoa fursa hiyo.
Mkondo wa kujifunza ulikuwa na mteremko mkali na mwendo ulikuwa wa kuchosha. Nilifurahia kufanya kazi na timu nzuri na kama mhariri mkuu wa kwanza ambaye lugha yake ya asili haikuwa Kiingereza moja ya vipaumbele vyangu ilikuwa ni kuandaa waandishi wapya vijana, wa kimataifa zaidi ambao uelewa wao, ndoto, shauku na mawazo yao vingekuwa baraka kwa gazeti linalochapwa katika lugha karibu dazeni mbili zikifikia mabara yote. Adventist World ilikuwa ni hatua makini ya kanisa la Waadventista ulimwenguni kwenda zaidi ya mizizi yake ya Marekani na kulikumbatia kanisa huko Afrika, Marekani Kati na Kusini, Asia, Ulaya, na eneo la Pasifiki.
Niliongoza usanifu mkubwa wa jarida mwaka wa 2018, ambao ulijumuisha sio tu mwonekano wa kisasa zaidi bali pia ulihusisha uamuzi makini wa kuzingatia zaidi idadi kubwa ya vijana washiriki wa kanisa la Waadventista. Tulijumuisha kwa mara ya kwanza safu ya kila mwezi iliyoandikwa na vijana kutoka kote ulimwenguni (“Sauti za Milenia”), pamoja na kipengele kilichoandikwa na kilichoundwa kwa ajili ya watoto (Imani Inayokua). Pia tulitambua kwamba tamaduni nyingi ulimwenguni huhusiana vyema na hadithi na tulifurahi kujumuisha hadithi ya kila mwezi ya msimulizi wa hadithi Dick Duerksen (Naweza Kukusimulia Kisa?).
Makala zetu kuhusu masomo ya Biblia au Imani za Msingi hazikuhusisha wasomi tu, bali pia wengine ambao walifurahia kufikiri kibiblia. Kwa kutiwa moyo na timu yetu, wachangiaji wetu walianza kututumia makala katika lugha nyingine kando na Kiingereza—na tulilipa kwa furaha tafsiri hizi.
Sehemu ya majukumu yangu ilihusisha pia kusafiri hadi kwenye kona nyingi za Kanisa la Waadventista kuzungumza kwenye mikutano ya wachungaji, kwenye makongamano ya kitaaluma, juma la maombi ya chuo kikuu au mikusanyiko mingine ya kanisa. Ushirika wangu katika Kamati ya Utafiti wa Kibiblia wa Konferensi Kuu ulitoa fursa nzuri za kuunganishwa na masomo ya Waadventista na pia nilifurahia safari zangu za Afrika Magharibi kama sehemu ya Kamati yao ya Utafiti wa Kibiblia. Safari hizi zote zilitoa fursa ya kuajiri waandishi na kuweka sikio langu kwenye msingi wa fikra za Waadventista kote ulimwenguni.
Mzunguko wa uzalishaji wa kila mwezi ulikuwa na shughuli nyingi sana na kwa sababu ya changamoto changamani za utayarishaji wa jarida katika maeneo tofauti na katika lugha tofauti kulihitaji mpangaji mkuu wa vifaa. Tulifurahi kuwa na Merle Poirier kuchukua jukumu hilo.
Zaidi ya kuwa na muda mchache wa kufanya kazi na wakati mwingine matatizo ya kifedha ya kusaidia kuendesha shughuli za kimataifa nilibahatika kuona kanisa likikomaa na kukua zaidi ya asili yake ya Amerika Kaskazini. Adventist World alikuwa mtoto wa umri wake ambapo ushirikiano na muunganiko vilikuwa sehemu ya mtandao mkubwa ulioleta ulimwengu karibu zaidi. Mitindo hii imegeuzwa katika maeneo mengi, na tutafanya vyema kama kanisa kutilia shaka ugawaji wa kikanda na kujifikiria wenyewe kitaifa. Kisa cha Adventist World ni ukumbusho wa wakati ufaao kwamba mwili wa Yesu ni wa kimataifa, umeunganishwa, unajali mshikamano, na kukumbatia makundi yote ya umri.

Gerald A. Klingbeil, D.Litt. alihudumu kutoka 2009 hadi 2023 kama mhariri msaidizi wa kile kilichojulikana kama Adventist Review Ministries. Akiwa mzaliwa wa Ujerumani, mnamo 2023, alirudi Ujerumani na kwa sasa anahudumu kama CFO wa Konferensi ya Hanseatic.


Kuanzisha kwa makusudi
NA BOYAN LEVTEROV
Ninalipenda kanisa langu! Kuwa Mwadventista kunasisimua kwa sababu imani yetu imekitwa kwenye injili ya Yesu na tarajio la ujio Wake wa hivi karibuni. Lakini, katika miaka yangu 26 ya uzoefu wa uchungaji, nimeshuhudia kwamba msisimko wetu juu ya ujio wa mara ya pili wa Yesu mara nyingi hutuletea shauku ya kujifunza kwa kina unabii wa Biblia kuliko shauku ya kushuhudia kwa ulimwengu tumaini la kuja kwa Yesu hivi karibuni. Moja ya changamoto kubwa sana katika huduma yangu ya kichungaji imekuwa kuwahamasisha washiriki kubadilika kutoka kuwa waabudu wa siku moja kwa juma na kuwa wanafunzi ambao wanawashirikisha wengine ujumbe wa injili kila siku.
Kazi ya kuhubiri injili kwa ulimwengu ni kiini cha uwepo wetu. Katika hubiri Lake la hatima ya mambo yote, Yesu alifunua kwamba mwisho utakuja sio pale tutakapoelewa ishara zote, bali pale ujumbe huu wa injili (utakapohubiriwa ulimwenguni kote” (Mt. 24:14). Vilevile, katika maneno Yake ya mwisho kwa wanafunzi, Yesu alituonya tusijisumbue na “wakati na saa,” bali tuwe mashahidi huko “Yerusalem, Uyahudi, Samaria na mwisho wa nchi” (Matendo 1:8).
ZAIDI YA CHEO
Nilipokuwa nikiwatia moyo washiriki wangu kuishi maisha ya utume, ghafla niligundua kuwa tuliuona utume wetu kuwa wa kwenye kusanyiko letu tu. Tunajaribu kuweka mkazo katika majengo makubwa na mipango ya ibada. Matendo 1:8 inatukumbusha kwamba mwito wa Mungu ni mkubwa mno, kwa namna hiyo. Ni kwenda ng’ambo hata kufika “Uyahudi, Samaria na mwisho wa nchi.”
Tumechangia katika msisitizo wetu wa ubinafsi kwa kupuuzia kuweka msisitizo mpana wa agizo la uinjilisti. Wakati tunayo mipango ya mafanikio ya uinjilisti kila mwaka na washiriki wetu kujitolea kuwafikia wengine kila siku, tumepuuza kabisa kupanua utume wetu hata kufikia maeneo mapya. Roho Mtakatifu atuongoze ili tupanue utume wetu zaidi yetu sisi wenyewe. Vuguvugu la Uadventista la awali halikuwa juu ya kukuza makanisa mahalia. Ilikuwa ni kufanya wanafunzi, vuguvugu la kuanzisha makanisa kila mahali. Zamani kabla hatujawa na idara rasmi ya utume kitaasisi, wachungaji na wanafunzi wapya walitumwa kama wainjilisti kwenye jamii mpya, miji, nchi na hata mabara.
James White aliandika kwa upana juu ya hitaji la kuanzisha makanisa mapya. Kwa Mfano, mnamo mwaka 1862, aliandika: “hakuna njia nyingine kwa mhubiri kuweza kujithibitisha kama kuingia katika maeneo mapya. Huko anaweza kuona matunda ya kazi yake, kwa kufanya hivyo anaonyesha kwa nduguze kwamba ametumwa na Bwana.”1
Ellen White pia alilipatia kanisa changamoto ya kuwa na mtazamo mpana wa umishenari. Injili inapaswa kuhubiriwa katika nchi na miji yote. . . . makanisa yanapaswa kupangwa, na mipango iliyowekwa kwa ajili ya kazi itimizwe na washiriki wa kanisa jipya lililopangwa.”2 “Lazima makanisa mapya yapangwe, na washiriki wapya kusimikwa. Wakati huu kunapaswa kuwa na wawakilishi katika kila mji na katika kila eneo la mbali duniani.”3 “Eneo baada ya eneo linapaswa kutembelewa, makanisa yanapaswa kuinuliwa moja hadi lingine.”4 Wengi wa waumini wa makanisa makubwa hawafanyi kitu chochote kinachoonekana. Wanaweza kukamilisha kazi njema, badala ya kujikusanya pamoja, ikiwa wangetawanyika katika maeneo ambayo hayajafikiwa na ukweli bado. . . . Wengi wa waumini wanakufa kiroho kwa kushindwa kuifanya kazi hii. Wanakuwa wagonjwa na wasiojiweza.”5
James na Ellen White waliyatia changamoto makanisa mahalia kukuza viongozi ambao wangehudumia mahitaji ya kanisa mahalia wakati mchungaji (na wengine waliojisikia kuitwa) wangekuwa huru kwenda na kufanyia uinjilisti maeneo mapya. Hii ilifanana na kile kilichofanywa na kanisa la mitume. Roho aliwaambia wazee wa kanisa la Antiokia kuwatuma Paulo na Barnaba, wazee wao wakuu, kwenye utume wakati wao walipokuwa wakilitunza kanisa (Matendo 13:1-3).
Roho hiyo ya utume iliendelezwa na kanisa la Waadventista kote hata kufikia miaka ya mwanzo ya 1990, kabla ya kuanza kubadilika taratibu kwa kile tunachokiona kwenye makanisa mengi leo. Mnamo mwaka 1912, Mwenyekiti wa Konferensi Kuu, A. G. Daniells, aliandika onyo kwa makanisa ambayo yalitaka kuwa na wachungaji kwa ajili tu ya kutunza na kuhudumia mahitaji ya waumini waliobatizwa. Daniells aliogopa kupoteza utamaduni wa kazi ya kuwafikia wengine. Kama alivyoeleza:
Hatujawaweka watumishi wetu kwenye makanisa kuwa wachungaji kwa kiasi kikubwa. Katika baadhi ya makanisa makubwa tumechagua wachungaji, lakini kama desturi, tumejiweka tayari kwa ajili ya huduma maeneo ya mbali, kazi ya uinjilisti na kaka na dada zetu wamejitolea kusimamia ibada makanisani kwao na kuendeleza kazi makanisani kwao bila wachungaji hao. Na ninatumaini kuwa hili halitakoma kuwa utaratibu wa kanuni ya utendaji wa kanisa hili; maana pale tunapokoma kuendeleza kazi ya utume wetu na kuanza kutulia makanisani mwetu, kukaa nao na kufanya kile wanachokifikiri na kuwaombea na kazi yao ipaswayo kufanywa, basi makanisa yetu yataanza kudhoofika na kupoteza uzima na utendaji wao na kupooza na kudumaa na kazi yetu itakuwa mapumzikoni.6
KUASILI MTAZAMO WA UKUAJI
Mnamo mwaka 2006, nilikubali mwito wa kuwa mwanzilishi wa makanisa wa wakati wote katika Konferensi ya Texas. Nilikuwa sehemu ya vuguvugu la umishenari lililoanzishwa na Kanisa la Waadventista wa Sabato Richardson, likiwa na mchungaji mwenye kuupenda umishenari sana na timu ya wazee iliyopenda ushuhudiaji. Kwa kushirikiana kwa zaidi ya miaka 20, kanisa la Richardson na makanisa yake “mapya” yalianzisha makanisa mapya 14 yenye zaidi ya jumla ya washiriki 3,000.
Leo, zaidi ya nusu ya jumla ya idadi ya makanisa ya Waadventista katika Amerika Kaskazini yamepanda au kupungua, wakati konferensi na makanisa ambayo yameasili upandaji makanisa kama sehemu ya mkakati wao wa kuwafikia wengine yanakua na kuongezeka. Ili kuwa tena vuguvugu la kimishenari, makanisa ya Waadventista lazima yajitolee katika kuzidisha wanafunzi, kukuza viongozi, na kuangalia ng’ambo zaidi ya kanisa lao la “Yerusalemu” kwa kujumuisha upangaji wa kanisa kama sehemu ya maono yao ya uinjilisti.
Hebu fikiri pamoja nami kwamba kanisa lako liliamua kuanzisha kanisa moja jipya kila baada ya miaka 10. Kisha, kila kanisa lililoanzishwa hivi karibuni linajitolea kufanya vivyo hivyo. Kufikia mwaka 2055, unaweza kuwa na makanisa mapya 16 ya Waadventista katika maeneo 16 mapya! Sasa fikiria kuwa humusi moja ya mikutano 168,000 ya Waadventista walijitolea vivyo hivyo.7 Tungeweza kufanya idadi ya makanisa ya Waadventista kuwa maradufu kwa miaka 30 tu. Je, uko tayari kurudi kwenye kiini chako cha kiutume na umishenari wa Kiadventista na kwenda ng’ambo zaidi ya “Yerusalemu” yako?
“Habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote . . . ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mt. 24:14).

1 James White, “Go Ye Into All the World and Preach the Gospel,” Review and Herald, Apr. 15, 1862, uk. 156.
2 Ellen G. White, Evangelism (Washington, DC: Review and Herlad Pub. Assn., 1946), uk. 19.
3 Ellen G. White, Testimonies for the Church (Mountain View, Calif.: Pacific Press Press Pub. Assn., 1948), vol. 6, uk. 24.
4 Ibid., vol. 7, uk. 20.
5 Ibid., vol. 8, uk. 244.
6 A.G. Daniells, “The Church and Ministry: An Outline of Lesson No. 5,” Pacific Union Recorder, Apr. 4, 1912, uk. 1.
7 Takwimu za Kanisa la Waadventista Ulimwenguni, 2021, zilizotolewa kwenye https://www.adventist.org/statistics/.

Boyan Levterov, D.Min., ni mchungaji mwanzilishi wa makanisa wa Konferensi ya Potomac, ambaye kwa sasa anatumikia Kanisa la Renewal huko Rockville, Maryland, Marekani.


Kidogo-Kidogo
NA MARION PEPPERS
Miaka michache iliyopita, nilishawishika kuanzisha kikundi cha afya kanisani kwangu huko Albuquerque, New Mexico. Kadiri nilivyoanza kujifunza zaidi juu ya lishe, nilikatishwa tamaa na kuonekana kutohitajika kanisani kwangu. Nakumbuka kufikiri kwamba, Kanisa linahitaji kujua kuhusu hili! Ilinigusa kwamba kanisa letu lilipewa ujumbe wa afya, lakini ilionekana kana kwamba hakuna mtu aliyekuwa akifuata kanuni hizi za kuokoa maisha. Nilitamani mtu ajitokeze na kuanzisha idara ya afya. Kisha nikagundua kwamba naweza kuwa mtu huyo! Ninaweza nisijue kila kitu, lakini nilikuwa tayari na uwezo, na hilo ndilo pekee ambalo Mungu analihitaji.
Niliogopa sana kuanza; sikujua nianzie wapi wala nifanye nini, kwa hiyo niliuliza kanisa letu waniambie kile walichotaka. Niliunda karatasi ya utafiti ili kubainisha mahitaji ya afya ya washiriki na ni aina gani ya ushauri wa kiafya waliuona ni bora kwa kanisa letu mahalia. Kulikuwa na mwitikio mkubwa kwa darasa la upishi wa vyakula vya mimea, kwa hivyo hilo lilikuwa jambo la kwanza tulilofanya.

Nilianza na wasilisho kuhusu lishe inayotokana na mimea, na tukajifunza jinsi ya kupika sahani kadhaa za vyakula vya afya ikiwa ni pamoja na mkate wa mahindi na tambi zilizopigwa na boga na karanga ya kusaga. Baada ya mkutano huu, nilianza kufundisha mtiririko wa sheria nane za afya zinazohusu kanuni za afya za mtu binafsi, zikifuatiwa na kushiriki kwa pamoja chakula chenye lishe.
Lengo langu kwenye kundi hili lilikuwa kuwatia moyo watu kutunza “mahekalu” ambayo Mungu alitupatia ili tuwe tayari na kuweza kufanya kazi Yake. Ingawa darasa lilikuwa dogo, athari yake ilikuwa ya halisi. Washiriki kadhaa wa kanisa walianza kufanya mabadiliko katika mtindo wao wa maisha, wakitekeleza yale waliyojifunza na kupata faida kubwa kwa kufanya hivyo. Kile kilichoanza kama huduma ndogo kimekuwa fursa endelevu ya kuwahudumia wengine kupitia afya na elimu.
Ikiwa haujazingatia, nakuhimiza uanzishe huduma yako ya afya katika mji wako! Tunahitaji kushiriki ujumbe wa afya kwa ulimwengu, lakini tunawezaje kufanya hivyo ikiwa kanisa letu wenyewe halijui lolote kuhusu hilo? Sio lazima uwe na sifa au uwezo fulani. Hata mimi sikuwa na cho chote. Mungu yuko tayari kumtumia ye yote! Ikiwa una maswali na wasiwasi, muulize Mungu. Yuko tayari zaidi kusikia maombi na wasiwasi wako.

Naiyah Van Why alisomea masuala ya lishe na elimu-lishe katika Chuo Kikuu cha New Mexico. Kwa sasa anafanya kazi katika Chuo cha Castle Valley karibu na Moab, Utah, Marekani.




Waefeso 1:10 ni sehemu ya kifungu kirefu kinachojumuisha aya 3-14, kilichojawa na umaizi wa kiteolojia. Ndani ya kifungu hicho, aya ya 10 inafanya muhtasari wa ujumbe mkuu wa Paulo kwa Waefeso.
MPANGO WA MUNGU.
Paulo anakusudia kuonyesha mbele ya Waefeso mpango wa Mungu wa kuunganishwa tena kwa kila kitu katika Kristo. Ulimwengu, chini ya nguvu za Kristo kama matokeo ya kafara Yake, unaelekea kwenye lengo hili muhimu zaidi la Mungu. Kimsingi, Paulo anatoa maono ya siku zijazo za ulimwengu kutoka kwa Muumba Mwenyewe. Maono haya ya wakati ujao yanadokeza kwamba ulimwengu uliumbwa awali “katika Kristo” (Kol. 1:16), lakini kuna kitu kilienda vibaya na haupo tena kikamilifu ndani ya Kristo. Uingiaji wa dhambi uliigawanya, na kuifanya iwe muhimu kurejesha vitu vyote kwenye umoja katika Kristo. Ukuu wa mpango wa Mungu unazidi sana maslahi yetu ya binafsi.
Sisi tu sehemu ya kitu fulani kikubwa kuliko sisi ambacho hufika kwenye sehemu za ndani kabisa za ulimwengu. Paulo anatupatia changamoto kuondoa mkazo wetu kutoka kwa ulimwengu tunaoujua na kutazama kwa imani wakati ujao wa ulimwengu uliounganishwa katika Kristo. Hakika, maono haya ya mpango wa Mungu kwa ulimwengu hutupatia njozi ya wakati ujao kuwa ni zaidi ya yale ambayo nguvu nyingine zozote za kiroho au za kibinadamu zingeweza kufikia.
UHUSIKAJI WA UUNGU
Kile ambacho Mungu anatupatia ni cha muhimu mno kiasi kwamba Baba (Efe. 1:3), Mwana (f. 3) na Roho Mtakatifu (f. 13), wanahusika pamoja katika matokeo yake. Kwa hakika, mpango huo uliundwa moyoni mwa Mungu muda mrefu kabla ya uumbaji wa ulimwengu. Inaitwa “siri ya mapenzi Yake [Mungu}” kwamba kwa wakati mwafaka alitambulishwa kwetu na Bwana Yesu (f. 9—11). Yeye ni chombo cha Mungu ambapo kupitia Yeye Baba “aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;” “alituchagua katika Yeye [Kristo] kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu” (f. 3, 4) na katika Yeye tunao ukombozi wetu (f. 7). Ukombozi huu utafikia ulimwengu wote. Baada ya ulimwengu kumrudia Mungu katika utimilifu wa ukombozi, utaimba tena sifa kwa utukufu wa Mungu (mstari 14). Kwa Paulo, taswira hii ya siku za usoni si jambo la kufikirika la uongo au udanganyifu ulioundwa na wanadamu wasio na tumaini. Linatimizwa katika historia ya mwanadamu, si kama tokeo la asili la maendeleo ya mwanadamu, bali kama tokeo la utendaji wa Mungu.
UKWELI WA SASA
Kulingana na Paulo, tunashuhudia mwanzo wa utekelezaji wa mpango wa Mungu kwa ajili ya ulimwengu katika uwepo wa kanisa ulimwenguni. Kuwepo kwa kanisa ni hatua ya kwanza ya Mungu katika kutekeleza mpango Wake wa kuunganisha ulimwengu katika Kristo. Tayari imeshaanzishwa kwenye sayari hii ndogo kupitia katika kazi ya wokovu ya Kristo ambaye, kupitia kazi ya Roho, amekuwa akiwashawishi wanadamu kuweka imani yao katika Kristo ili kuunganishwa ndani Yake (f. 11—13). Waumini kama hao sasa wako ndani ya Kristo na hatakoma hadi kazi Yake ijumuishe ulimwengu wote. Kusudi la Mungu lilifikia kwanza Wayahudi ambao, kulingana na Paulo, walikuwa ndio “walitangulia kuwa na tumaini kwa Kristo” (f. 12), walifuatiwa na Wamataifa ambao, “baada ya kusikiliza ujumbe wa ukweli, injili ya wokovu wenu . . . mliamini pia” (f. 13). Naam, kuunganishwa kwa ulimwengu katika Kristo kumeanzishwa na sisi tayari ni sehemu yake. Sisi, waumini, ni ushahidi wa kimaksudi wa tukio hili la ulimwengu.

*Nukuu za Biblia zimetolewa katika Swahili Union Version Bible. Haki zote zimehifadhiwa.

Ángel Manuel Rodríguez, Th.D., amestaafu baada ya kutumika kama mchungaji, profesa na mwanateolojia.


Nguvu ya mazoezi kwa Mwili na Akili
Ninaelewa kuwa lishe bora inaweza kukuza afya ya akili na mwili. Je, mazoezi ya kila siku ni muhimu kwa ajili ya afya ya kimwili na kiakili?
Umeuliza swali zuri na la muhimu mno. Kuna mijadala mingi na hata mifarakano kuhusu chakula na lishe, ambayo ni muhimu sana. Miongoni mwa sababu nyingi zinazosababisha maisha marefu na afya ya utambuzi, mazoezi ni njia moja bora zaidi ya kuongeza maisha na kupunguza hatari ya kupungua kwa utambuzi. Utafiti unaonyesha mara kwa mara kuwa mazoezi ya mwili ya kila siku huboresha afya ya moyo na mishipa, huongeza utendaji wa ubongo, na hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa magonjwa ya mfumo wa neva kama vile Alzheimers na shida ya akili.
MAZOEZI NA KUISHI MIAKA MINGI
Mazoezi yanahusiana moja kwa moja na kuongezeka kwa muda wa kuishi kwa kupunguza hatari ya magonjwa sugu, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, kisukari, na saratani—sababu zinazoongoza za vifo duniani kote. Ubora wa moyo na mishipa una jukumu muhimu katika kuishi maisha marefu. Tafiti zimeonyesha kuwa utimamu wa juu wa mfumo wa moyo na mishipa ulihusishwa sana na kupunguza hatari ya vifo, bila kujali umri. mazoezi ya mwili ya kila siku hupunguza mwako uchungu, huboresha utendaji wa kinga, na huongeza ufanisi wa mitochondria, ambayo yote huchangia maisha marefu, yenye afya.
Kwa kuongezea, mazoezi ni mrekebishaji mwenye nguvu wa afya ya umeng’enyaji. Yanaongeza utendaji wa insulini, hupunguza shinikizo la damu, na yanakuza profaili zenye afya, hupunguza hatari ya ugonjwa wa kimetaboli na ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2—yote mawili yanahusishwa sana na kufupishwa kwa maisha. Mazoezi ya upinzani husaidia kudumisha ukubwa wa misuli na uzito wa mfupa, sababu muhimu katika kuzuia udhaifu na kupungua kwa umri.
MAZOEZI NA AFYA YA AKILI
Faida za kufanya mazoezi zinaenda mbali zaidi ya afya ya mwili hata kufikia afya ya akili. Tafiti zinaonyesha kuwa mazoezi ya mwili ya kila siku huongeza neuroplasticity—uwezo wa ubongo kuunda mizunguko mipya na miunganisho ya ndani—na uongezekaji wa viwango kwa sababu ya neurotrophic(BDNF), protini muhimu kwa ajili ya kujifunza na kumbukumbu. Mazoezi pia hukuza neurogenesis,haswa katika hippocampus, eneo la ubongo muhimu kwa ajili ya uchakataji wa kumbukumbu.
Mazoezi huboresha mtiririko wa damu kwenye ubongo, kupunguza hatari ya shida ya akili ya mishipa inayotokana na kuharibika kwa usambazaji wa damu kwa ubongo. Mazoezi ya Aerobic, kama vile kutembea, kukimbia, au kuendesha baiskeli, yamehusishwa na kiwango kikubwa cha hippocampalna kupungua polepole kwa ubongo unaohusiana na umri. Watu walio na viwango vya juu vya mazoezi ya mwili wana hatari ndogo sana ya kupungua kwa utambuzi kwa wakati.
Mazoezi pia hupunguza uvimbe sugu na msongo wa uwekaji oksijeni, vitu viwili vikuu vinavyochangia kuzorota kwa mfumo wa neva. Kwa kupunguza uchochezi wa utaratibu na kuimarisha ulinzi wa antioxidant, mazoezi hulinda neurons (seli za neva) kutokana na uharibifu unaohusishwa na magonjwa yadhoofishayo, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa Alzheimer na shida nyingine ya akili.
NI MAZOEZI KIASI GANI HUHITAJIKA?
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza angalau dakika 150 – 300 za mazoezi ya aerobic ya nguvu ya wastani au dakika 75-150 za mazoezi ya nguvu kwa juma, yakijumuishwa na mazoezi ya mafunzo ya nguvu angalau mara mbili kwa juma. Hata ongezeko kidogo la viwango vya shughuli—kama vile matembezi ya haraka ya kila siku—kunaweza kuleta manufaa makubwa kiafya.
HITIMISHO
Wakati chakula bora, kupumzika (usingizi) na uhusiano wa kijamii ni muhimu kwa ajili ya afya na kuishi maisha marefu, mazoezi hubaki kuwa kiungo kikuu kati ya kuongeza maisha na uhifadhi wa utendaji wa akili. Uwezo wake wa kupunguza hatari ya magonjwa sugu, kuimarisha ustahimilivu wa ubongo, na kukuza uhai kwa ujumla huifanya kuwa msingi wa mtindo wowote wa maisha unaozingatia haja ya kuishi maisha marefu. Mazoezi ya mwili ya kila siku sio tu uwekezaji katika afya ya mwili—ni nguzo ya msingi ya maisha marefu, yenye afya nzuri ya akili (3 Yohana 2).

Zeno L. Charles-Marcel, mkufunzi wa magonjwa ya ndani aliyeidhinishwa na bodi, ni mkurugenzi wa Huduma ya Afya ya Waadventista katika Konferensi Kuu.
Peter N. Landless, mtaalamu wa magonjwa ya moyo aliyeidhinishwa na bodi na mkurugenzi mstaafu wa Huduma ya Afya ya Waadventista ya Konferensi Kuu, ni mkufunzi pia.


Kisa chetu kinaanza mapema mnamo miaka ya 1960.
“Kijana, droo yako ya fedha taslim inapungukiwa na senti 45. Hiyo ni zaidi ya senti 45 unazopaswa kuwa nazo kwenye droo yako mwishoni mwa kazi leo.”
Nikatazama chini kwa mara nyingine tena kwenye hesabu zangu. Bosi wangu, Bw. Britt, msimamizi wa fedha wa hospitali, alikuwa sahihi. Nilikuwa nimejaribu kufanya hesabu zangu ziwe sawa kwa senti, lakini nilikuwa mchanga na sikuwa mkamilifu kama Bw. Britt alivyonihitaji kuwa.
“Richard, Ngoja nikusimulie hadithi.”
Bw. Britt aliniambia niketi chiti kwenye kiti cha keshia, pale ambako nilikuwa nafanyia kazi. Niliketi, akili yangu ikijaribu kukumbuka akaunti za wagonjwa niliowahudumia siku hiyo. Imewezekanaje mimi kupungukiwa na senti zote 45?
“Hapo zamani za kale,” Bw. Britt alianza, “zamani sana mwaka 1928, kulikuwa na keshia kijana aliyejulikana kama E. E. Martin, na meneja mtoa pesa alikuwa Bw. Harley Rice. Kijana Bw. Martin aliketi katika kiti hiki-hiki unachokikalia katika ofisi hii na siku hiyo alishangaa kwa nini droo yake ilidaiwa senti 45. Alifanya kazi siku nzima. Mmoja wa wagonjwa, mwanaume ajulikanaye kama Bw. Henry Porter, alikuwa amejaribu kulipa sehemu ya deni lake kwa kuponi ya zamani badala ya kulipa kwa pesa taslim au kwa cheki.”
“Bw. Porter alikuwa amewasiliana na hospitali yetu, ambayo ilikuwa inajulikana kama Paradise Valley Sanitarium huko zamani, kwa sababu alikuwa ameshikwa na baridi kali na aliamini kwamba akipata tiba ya maji kwa siku kadhaa inaweza kusaidia. Tulituma gari ili kumchukua kutoka hotelini kwake, the Del Coronado. Tulimpa kimoja cha vyumba vyetu vizuri, kilichokuwa na maji kila wakati na choo, na alikaa pale kwa takribani juma zima. Alifurahia sana, kwa sababu mkewe alijiunga naye siku chache za mwisho.”
“Bw. Britt,” niliingilia kati, “huyu bwana Porter lazima alikuwa na bili kubwa!”
“Uko sawa kijana. Bwana Porter aliposimama pale pale ili kuondoka, mtunza fedha, Bw. Martin, alimpa jarida lililoandikwa kwa mkono la gharama anayodaiwa. Bwana Porter aliiangalia na kuandika hundi kwa ajili ya kila kitu isipokuwa gharama yake kubwa ya matumizi ya simu. Kwa hiyo, alitoa kitabu cha kuponi na kuchana kuponi za kutosha kulipa bili hiyo. Kisha akakabidhi hiyo hundi na kuponi kwa Bwana Matin, ambaye alikuwa hajawahi kuona kuponi za zamani hapo awali.”
“Sijawahi kuona kitu kama hicho pia, Bw. Britt. Pengine ningesema nitarudi na kuja mara moja kukuona.”
“Na hivyo ndivyo alivyofanya Bwana Martin! Alichukua kuponi hizo, akamtabasamia Bw. Porter, kumwomba kwanza akubaliane na mtunza fedha, Harley Rice.”
“Ilikuwaje Bwana Martin kupata deni kwa akaunti hiyo kwa senti 45?”
“Usinitangulie,” alicheka Bw. Britt.
“Sawa. Je, kuponi zilikuwa nzuri?”
“Vizuri sana. Harley Rice alilipigia simu tawi la San Diego la kampuni ya simu na kuomba kuzungumza na meneja. Meneja alipokuja kwenye simu, Harley alimwambia kuhusu kuponi za Bw. Porter na kumuuliza ni nini.”
“Vitabu hivyo vya kuponi hutolewa kwa wenye hisa wetu wakubwa na washiriki wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya simu,” meneja huyo alisema. “Tafadhali zipokee kama pesa taslimu.”
“Lo! Bw. Porter lazima alikuwa mtu muhimu sana!”
“Naam, hakuna mtu hapa aliyelifikiria sana jambo hilo, lakini jioni hiyo alipokuwa akitoa hesabu, Bw. Martin aligundua droo yake ilikuwa na punguzo la senti 45—kwenye hazina—kama ulivyo leo. Harley Rice alichunguza hesabu hizo na kugundua kwamba tulikuwa tumepiga sehemu ya bili ya Bw. Porter kimakosa, na kwamba tulikuwa na deni lake la senti 45.”
“Senti arobaini na tano si jambo kubwa sana. Walifanya nini kuhusu hilo?”
“Ilikuwa jambo kubwa kwa Harley Rice. Alirekebisha akaunti haraka na kutuma barua ya kuomba msamaha, ya Februari 10, 1928, pamoja na hundi ya senti 45 kwa Bw. Henry Porter katika Hoteli ya Del Coronado.”
“Bw. Porter alifikiria nini kuhusu hilo?”
“Siku mbili baadaye Harley Rice alipokea barua kutoka kwa Bw. Porter. Ndani yake kulikuwa na hundi hiyo, iliyoidhinishwa kurudi kwenye Paradise Valley Sanitarium, ikiwa na barua ya kushukuru kwa uaminifu wa Bw. Rice.”
“Bwana Britt, uliniambia hadithi hiyo ili kunifanya nijisikie vizuri kuhusu senti 45 ninazopungukiwa kwenye droo yangu?”
“Hapana, Dick. Nilikuambia hadithi hiyo ili kila wakati ukumbuke kuwa mwangalifu na mkarimu, na kuhakikisha kuwa kazi yako inafanywa kwa usahihi na kwa uzuri.”
“Inaonekana kwangu kama vile kuna la ziada kwenye hadithi hii.”
“Hakika! Mnamo Aprili 16, 1928, Bw. Harley Rice, msimamizi wetu wa fedha, alipokea barua nyingine iliyoandikwa kwa mkono kutoka kwa Bw. Porter, hii ikiwa na alama ya posta kutoka Denver, Colorado. Hivi ndivyo ilivyosema:
‘Tafadhali unaweza kunipa anwani ya meneja wa mashirika yako mbalimbali, kwa kuwa ningependa kuwasiliana naye kuhusu kuanzisha taasisi kama hiyo huko Denver.’ ”
“Je, alifanya kweli?”
“Usitangulie hadithi yangu!”
“Samahani, Bw. Britt.”
“Bwana Rice alituma barua hiyo kwa baba yake mwenyewe, Mzee M. L. Rice, ambaye alikuwa katibu mwenza wa Idara ya Matibabu ya Konferensi Kuu huko Washington, D.C. Kisha akasahau kuhusu hilo. Harley wala baba yake hawakuamini kabisa kile Bw. Porter alikuwa akikisema kuhusu kutaka kuanzisha hospitali mpya. Lakini mipango ya safari ya Mzee Rice ilijumuisha mapumziko ya saa nne katika kituo cha treni cha Denver, kwa hiyo alimtumia Bw. Porter barua ya kukubali kukutana naye.”
“‘Inashangaza,’ Mzee Rice alimwambia mwanawe Harley, ‘kwamba mtu huyu angezungumza kuhusu kuwa na hospitali huko Denver. Najiuliza kama anajua kwamba tuna Sanitariamu bora mno maili chache tu kutoka Boulder, Colorado.’ Kwa hiyo Mzee Rice aliamua kumwambia Bw. Porter kuhusu Boulder Sanitarium, na akapanda treni.”

Bw. Porter alipopata barua alicheka, akigundua kwamba sio Harley wala baba yake aliyeamini kuwa mtu huyu alikuwa amedhamiria.
“Hiyo ilibadilika haraka wakati Bw. Porter alipokutana na Mzee Rice kwenye kituo cha gari moshi. Alimweka mgeni wake kwenye gari kubwa la farasi na dereva aliyevaa sare na kumpeleka kuzunguka Denver, akimuonyesha majengo yote ambayo familia ya Porter walikuwa wanamiliki.”
“Safari ilijumuisha vituo viwili muhimu sana. Cha kwanza kilikuwa katika jengo la Benki ya Kitaifa ya Denver, ambapo Bw. Porter alikuwa mwenyekiti. Cha pili kilikuwa ni kwenye ekari 40 za mashambani kwenye ukingo wa mji.”
“Eneo hili litakuwa ndio mahali pa hospitali yako mpya, Mzee Rice. Nimeamua kukupa $330,000 kwa ajili ya hospitali mpya. Hiyo itagharamia ardhi, majengo, na vifaa. Hapa, ngoja nikutembeze hadi mahali ambapo utaweza kuwa na shamba dogo la kuwapatia wageni mboga.’”
“Mzee Rice alilemewa kabisa, alistaajabu, na kujawa na shauku wakati huo huo.”
“ ‘Nitasaidia katika uanzishaji wote,’ alisema Bw. Porter, ‘lakini itabidi uiendeshe hospitali peke yako. Najua unaweza kufanya hivyo, kwa sababu namjua kijana wako Harley na wafanyakazi wengine katika Paradise Valley. Ninatumaini kwamba utaiendesha hospitali hii kwa uaminifu, haki, na kwa uzuri. Ninaweza kukuamini kwa afya yangu na mali yangu.’ ”
“Hayo yote ni kwa sababu ya hundi ya senti 45!”
Hapana kijana mdogo. Bw. Porter alitoa zaidi ya dola milioni 3 kwenye hospitali kwa sababu alijifunza kwamba anaweza kutuamini kwa ajili ya afya na mali yake.
Sasa Bw. Britt alitabasamu na kuniambia, “nenda katafute senti zako 45.”

Dick Duerksen, mchungaji na msimuliaji wa hadithi, anaishi Portland, Oregon, Marekani.


Mungu Njiani
Msaada wakati tusioutegemea
NA DAVID ROSS

Magari. Yako kila mahali! Tunayaona mengi sana kiasi kwamba tunayachukuliwa kuwa ya kawaida. Magari ni vitu bora sana kuwa navyo. Tunayatumia kwenda kufanya manunuzi ya chakula, hospitalini, au kanisani. Tunayatumia kwenda majumbani kuwasalimu ndugu na marafiki. Lakini mara nyingi tunayafikiria tu pale yanapoharibika au pale kunapokuwa na ajali na watu kupoteza maisha—au kuokolewa.
Je, umewahi kusikia au kupata ajali ambapo mtu fulani alipona kimiujiza? Dada yangu alinihadithia kisa cha wakati aliposhindwa kuliongoza gari lake kwenye barabara yenye barafu. Gari lake lilipoteleza kuelekea kwenye mteremko mkali, alichofanya ni kuomba tu. Kisha gari lake likasimama nchi chache ukingoni mwa mteremko huo. Mungu alimuokoa.
Kisa changu mwenyewe kilitokea miaka kadhaa iliyopita. Nilikuwa nikiendesha katika barabara kushuka mlimani. Nilipokaribia kwenye kona, nilikanyaga breki ili kupunguza mwendo. Barabara ilikuwa imelowa baada ya mvua kunyesha na matairi yakashindwa kutulia. Niliteleza huku na huku na kisha kugonga lori lililokuwa linapanda mlima. Gari langu liliharibika kabisa lakini sikuumia hata kidogo. Nilidhani kuwa nina bahati sana wakati ule lakini baadaye niligundua kuwa ilikuwa ni Mungu aliyeniokoa.
Sio kwamba Mungu anakuwa nasi tu nyakati za kutisha. Yuko pamoja nasi kila wakati.
Miaka mingi iliyopita, nilikuwa nikirudi nyumbani toka safarini na niliona mtu amesimama barabarani akiomba lifti. Muomba lifti husafiri bure kwa kupewa lifti na magari yapitayo barabarani, kawaida anasimama barabarani na kuashiria kwa dereva kuwa muhitaji. Nilisimama na kumwuliza kuwa alikuwa anaenda wapi. Alitaka lifti kwenda katika Jiji la New York! Sikuweza kumfikisha huko bali nilimshusha salama huko Syracuse, New York.
Sasa gari nililokuwa nikiliendesha lilikuwa na tatizo. Geji isomayo kiasi cha mafuta ilikuwa imeharibika, nilikuwa tu nikikadiria kuwa ni wakati gani niongeze mafuta. Nilipokuwa nikiendelea kuelekea nyumbani, niliona bango liloonyesha kuwa barabara ya kuchepukia kwenda nyumbani ilikuwa ni maili 10. Nitafika tu salama, nilifikiri. Lakini nikiwa nimebakisha maili 2 tu kufika pale, gari lilitetereka na kusimama. Sikuwa na uchaguzi mwingine zaidi ya kutembea hadi pale pa kuchepukia. Lakini punde tu kabla sijaanza kutembea nikaona gari likisimama kando yangu. Huyo mtu mwema alinipeleka kwenye kituo cha mafuta na baada ya kujaza chombo changu alinirudisha mpaka kwenye gari langu na kusubiri ili kuhakikisha kuwa kila kitu kilikuwa sawa.
Ninajua kuwa matukio haya mawili yalihusiana. Mungu alinielekeza kumsaidia mtu aliye mhitaji na kisha Mungu akatuma mtu ili kunisaidia wakati nilipokuwa mhitaji.
Miaka mitatu iliyopita, mke wangu na mimi tulikuwa tukiendesha nje ya mji tulipopiga kona kali na kutumbukia shimoni. Tulihangaika sana kutoka lakini tulishindwa. Mtu mmoja aliye mwema alikuja kutoka nyumba ya jirani ili kutusaidia, lakini hata kwa msaada wake, hatukufanikiwa. Kile tulicholazimika kufanya ni kuita gari la kutuvuta. Kisha, kwa mshangao gari hilo lilifika! Tulikuwa hata bado hatujapiga simu kuliita! Yule dereva alituvuta kwa urahisi kutoka shimoni. Nilipomwuliza kuwa itatugharimu shilingi ngapi alijibu, ilikuwa ni “utendaji wake wa tendo jema kwa siku.”
Hivi karibuni, nilikuwa nikiendesha gari kwenda nyumbani wakati tairi langu lilipotoka ghafla. Nikasogea pembeni ili kulibadilisha. Ilikuwa wakati wa baridi, theluji na baridi kali. Sikuwa na glavu, na iliniwia vigumu kufungua boliti zilizoshikilia tairi. Ghafla gari fulani lilikuja nyuma yangu. Wanaume wawili walitoka nje, wakachunguza hali hiyo, na katika muda usiozidi dakika moja walikuwa wamebadilisha tairi. Nilipouliza jinsi ningeweza kuwalipa, walijibu, “Utalipa huko mbele,” wakimaanisha kamsaidia mtu mwingine aliye na uhitaji.
Wakati fulani tunaweza kujaribiwa kuwa matatizo yetu ni madogo sana kwa Mungu kuingilia kati. Watu wazima wanafikiri, huu sio ugonjwa mkubwa, wakati tunapaswa kununua au kutengeneza hili au hoja ya familia. Mungu ana mambo bora ya kuhangaikia kuliko masuala yangu madogo. Watoto wanaweza kufikiri, Mungu hapendezwi na matatizo yangu madogo shuleni au pamoja na kaka au dada yangu. Lakini Yesu anatukumbusha kwamba, “Hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote” (Luka 12:7). Mungu anajali kila hali maishani mwetu.
Katika kila hali yangu, Mungu alimtuma mtu fulani kuja kunisaidia. Mungu yuko hivyo. Hatuachi wala kututelekeza. Yuko pamoja nasi daima katika hali zote. Bila kujali kama tatizo ni kubwa au dogo, tunaweza kumtumainia Bwana daima.

David Ross ni mstaafu na anaishi huko Belleville, Ontario, Kanada. Ni mzee wa kanisa katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Belleville.


Mchapishaji
Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.
Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review
Justin Kim
Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa
Hong, Myung Kwan
Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World
Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun, Dong Jin Lyu
Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review
Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott
Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani
Enno Müller, Beth Thomas, Jonathan Walter
Wahariri waliopo Seoul Korea
Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun
Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali
Gabriel Begle
Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi
Daniel Bruneau
Meneja wa Shughuli
Merle Poirier
Mratibu wa Tathmini ya Uhariri
Marvene Thorpe-Baptiste
Wahariri/Washauri wengine
E. Edward Zinke
Meneja wa Fedha
Kimberly Brown
Mratibu wa Usambazaji
Sharon Tennyson
Bodi ya Utawala
Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong, Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Tae Seung Kim; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson
Maelekezo ya Usanifu na Muundo
Types & Symbols
Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:
Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote, Yohannes Olana
Tafsiri
Ufunuo Publishing House, Southern Tanzania Union Mission.
Msomaji wa prufu
Lilian Mweresa
Usanifu wa toleo la Kiswahili
Daniella Ingram, Ashleigh Morton, Digital Publications
Uchapishaji wa Kidijitali
Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)
Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu
Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott
/Types & Symbols
Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638
Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org Tovuti: www.adventistworld.org
Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.
Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.
Vol. 21, Na. 6

