ENDELEA KUPOKEA ADVENTIST WORLD KISWAHILI

Tunawathamini na kuwatambua wote waliojisajili na tuna taarifa mpya na za kusisimua kuhusu jinsi mnaweza kuendelea kusoma na kupata Adventist World.

KULIPATA KWENYE WHATSAPP

Kwa sababu ya umaarufu wa kulipata jarida hilo kwenye WhatsApp, tunahamia kwenye mfumo mpya wa kutangaza ambao utatuwezesha kuwasiliana nanyi mara kwa mara. Bonyeza kiungo kilicho hapo chini kujiunga na chaneli ya WhatsApp Broadcast ambapo tutakujulisha toleo jipya linapokuwepo.

KULIPATA KWENYE TOVUTI

Lipate jarida hilo kwenye tovuti yetu, kwa kukibonyeza kiungo kilicho hapo chini:

Tovuti hiyo vilevile inabeba Adventist World kwa lugha anuwai.

KULIPATA KWENYE FACEBOOK

Kiungo cha toleo la hivi karibuni la Adventist World huwekwa kwenye Ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi. Kwa “Liking” ukurasa huu utapokea taarifa zetu mpya na kuweza kututumia jumbe ukiwa na majibu yoyote.

HIFADHI MAKTABA YA JARIDA LA KISWAHILI KWENYE SIMU YAKO AU KOMPYUTA

Tumetengeneza maktaba ya kidijitali ya majarida yote ya Adventist World. Ili kulipata kusanyo hili kwa urahisi kwenye simu yako, fuata hatua zilizo hapo chini:

 

Bonyeza kiungo kilicho hapo chini ili kuipata maktaba.

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 

AU

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 


Kwa maoni yoyote au majibu, tafadhali jiskie huru kututumia barua pepe kwenye kwambokaj@ecd.adventist.org. Tunapenda kusikia kutoka kwako na tunatazamia uhusiano mzuri na wasomaji wetu wa Adventist World-Kiswahili.

Asante sana na Mungu awabariki,
Timu ya Adventist World-Kiswahili

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa kwambokaj@ecd.adventist.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

Picha ya jalada: Wilhelm Gunkel

Makanisa Machafu na yenye Fujo 

Na Justin Kim

Kilimo siyo taaluma yangu, hivyo nakifikiria kipindi cha mavuno kuwa ni kipindi cha kuvutia ambacho mashamba ya nafaka yanaenea hadi upeo wa macho na ambapo nyuzi zao za dhahabu hukutana na anga la vuli. Ngano ikiwa inatikiswa na upepo, wavunaji huimba kwa sauti na kwa midundo ya kike na ya kiume, wakiratibu mwendo wao wa kuvuna na mapigo ya wimbo. Marobota ya nyasi huruka huku na huko kati ya marundo ya matunda na mbogamboga. Watoto na watu wazima hufanya kazi kwa pamoja wakifurikwa na msisimko. Wanyama hushangilia kwamba mavuno yatawasaidia kustahimili majira ya baridi kali.

 

Maandiko hayatii chumvi sana. Mithali 14:4 inasema, “Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe; bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi.” Ng’ombe ni wanyama wenye nguvu kwenye kilimo, kifasihi ikiwakilisha nguvu na uzalishaji. Wanaweza kubeba mizigo mikubwa na kutoa nguvu ya msuli inayoweza kuhitajika kwa kazi mbalimbali. Lakini pamoja na mnyama huyu kuwa adhimu pia kuna sehemu za ubaya wa ufugaji. Kwa maneno mengine matokeo makubwa yanatokana na njia zenye machafuko.

 

Inapokuja kwa uinjilisti, mavuno ya roho, Mungu anahusisha binadamu. Na ndani ya binadamu kuna machafuko mengi. Kama madimbwi yanavyohitaji kujazwa kila wakati, tunahitaji huduma ya kudumu, kujazwa na matengenezo. Kama vile mabanda na madimbwi yanavyotakiwa kusafishwa udongo wao, tunahitaji utakaso, kuoshwa na matengenezo. Kuna harufu mbaya, madoa na aibu. Hii haitokani na kazi ya Shetani bali ni kawaida kutoka kwa binadamu mwenye asili ya dhambi: udhaifu, mafadhaiko, kutokuelewana, wivu, unyonge, ukaidi, kasoro za kitabia, vichocheo vya kisaikolojia, kukata tamaa, kukosa subira na fadhaa. Lakini ndani ya Hekima ya ajabu ya Mungu, Yeye huona tu ahadi kubwa na nguvu ndani ya ng’ombe, Yeye pia hudumu hadi mwisho katika mabanda na madimbwi yetu.

 

Wengi wanayo mitazamo sawa ya kuvutia kuhusu kanisa na maisha ya kiroho, wakidhani kuwa mambo yote ya kidini ni makamilifu na yenye upendo, bila kufadhaika, kushindwa au vizuizi. Tunategemea maelewano kamili kati ya watendakazi wa Mungu yenye matokeo kamili. Lakini tunaona kwamba makumi ya Wachungaji huacha huduma kila mwezi, mamia ya washiriki huacha ushirika kila mwaka, na maelfu ya waumini huacha imani katika kila kizazi. Ni sahihi Mithali kutotia chumvi. 

 

Hata hivyo, lengo si kwa ng’ombe wala hori. Lengo ni kwenye mavuno. Ukitazama mavuno, uchafu una thamani zaidi. Kama unaweza kuona, nguvu ya mavuno, inaweza kushinda mchungaji yeyote aliyevunjika moyo, mshiriki mwenye chuki, au muumini aliyepoteza imani. Kwa maana hatufanyi kazi kwa ajili ya sasa hivi bali kwa tumaini la mavuno. Licha ya machafuko tunayopitia, macho yetu na yatazame “kuongezeka” kwa mavuno kwa ajili ya Bwana.

Picha: Marcos Paseggi

Wanafunzi wa Pinehill Adventist Academy huko Champhai, Mizoram, India, wamewapokea viongozi wa kanisa la Waadventista wa Sabato wa eneo hilo na viongozi wa Maranatha Volunteers International kwa zawadi ya jadi ya kabila la Mizo. Viongozi wa kanisa, wafadhili, na wanaojitolea wameungana kujenga shule mpya ambayo inatarajiwa kuongeza maradufu ya idadi ya wanafunzi ya sasa 350-karibu na mipaka ya Myanmar.

“Nilikuwa nimewaona wataalamu wengine na wataalamu wa lishe hapo awali, lakini walionekana tu kutaka niondoke haraka. Hapa, ilikuwa mara ya kwanza kuhisi kusikilizwa na yale waliyosema yalikuwa na maana. Nilijua ningeweza kujaribu.” 

— Bob (jina limebadilishwa kwa ajili ya kulinda utambulisho), mkazi wa eneo la vijijini katika New South Wales, Australia, akizungumzia Kituo cha Tiba ya Mtindo wa Maisha cha ELIA. Kituo hiki, ambacho kiko katika Hospitali ya Waadventista ya Sydney, hivi karibuni kimepanua huduma zake kwa watu wanaoishi katika maeneo ya vijijini. Kituo hiki kinatoa miadi ya binafsi pamoja na programu za kliniki za majuma 12, ikiwa ni pamoja na Mpango wa ELIA wa Kliniki ya Kisukari wa Majuma 12 na Mpango wa ELIA wa Kliniki ya Saratani ya Matiti wa Majuma 12.

“Leo ni siku muhimu kwa ajili ya kanisa letu. Tunapojitahidi kuwajumuisha wanawake katika jamii kwenye miradi yetu, tumeshirikiana na serikali yetu ya mitaa ili kuwajali wanawake hawa kwa kuwapatia wataalamu wetu, watendakazi wetu, na rasilimali zetu (zinazotoa) msaada maalum wa kiroho.” 

— Celia Olivo, kiongozi wa huduma za wanawake katika Eneo la Utume la Ecuador Kusini, kuhusu mradi wa “Florezca” au Flourish (Sitawi). Mradi huu ulifanyika wakati wa Siku ya Kupinga Ukatili, inayoadhimishwa kila Novemba 25. Mpango huu ulitoa mafunzo ya kuwaimarisha wanawake katika masuala ya kiroho, kujipenda na njia bora za kusimamia hisia zao.

Kutafakari Maisha ya Yesu

Washiriki wa kanisa waliulizwa ni mara ngapi wanatafakari na kufikiria kuhusu maisha ya Yesu.

“Kazi ya umishonari inaleta baraka kubwa zaidi kwa wamishonari wenyewe na pia inawajalia vijana neema katika eneo la utume. Natumaini huduma hii itaendelea kuwanufaisha vijana Waadventista wa Korea na pia kutoa fursa ya wokovu kwa vijana wa Taiwan.” 

— Kim GwangSung, mchungaji mwandamizi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Sanmin, akizungumzia Huduma ya Umishonari kwa Vyuo Vikuu vya Umma(Public Campus Ministry [PCM]) katika kanisa lake la nyumbani. Mwaka 2024, huduma hii ya vijana ilizaa ubatizo wa waumini wawili. Kupitia kujitolea na ushiriki wa kizazi kipya, kanisa linazidi kuwa hai na lenye mtazamo wa siku za usoni. Utume wa PCM wa Kanisa la Sanmin hauishii tu kwenye matukio kama ubatizo, bali unakuwa msingi wa ukuaji endelevu wa kiroho.

“Tunashukuru sana kwa ukarimu ambao Sanitarium imeonyesha katika miaka minne iliyopita, pamoja na shauku yao inayoendelea kwa ajili ya utume wetu. Msaada wao wa kudumu umetuwezesha kuwapatia jamii tunazohudumia kifungua kinywa chenye afya, hasa wakati familia nyingi zaidi zinapokabiliwa na changamoto ya kupata chakula cha kutosha.” 

— Gavin Findlay, afisa mkuu mtendaji wa New Zealand Food Network [NZFN], akizungumzia ushirikiano na Sanitarium, kampuni ya chakula chenye afya ya Waadventista wa Sabato. Kupitia ushirikiano huu, vituo viwili vya usambazaji vya NZFN hupokea, kupanga, na kuhifadhi chakula kilichotolewa, ambacho baadaye husambazwa kwenye vituo 65 vilivyosajiliwa vya usambazaji wa chakula. Mahitaji ya huduma hizi yameongezeka kuliko hapo awali. Ripoti ya 2024 ilionyesha kuwa zaidi ya kaya moja kati ya tano zenye watoto chini ya miaka 15 katika eneo hilo ziliripoti kuwa “chakula huisha mara kwa mara au wakati mwingine,” idadi iliyoongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2022.

Zaidi ya 120

Idadi ya watu waliokusanyika Novemba 6-10 kwa ajili ya Mkutano wa Kituo cha Mahusiano kati ya Waadventista na Wayahudi (JCAR) wa 2024 katika Kituo cha Mafunzo cha Waadventista cha Araçoiaba da Serra, São Paulo, Brazili. Tukio hilo lilitoa mihadhara mikuu, mafunzo na hamasa kwa mawakili Waadventista kutoka Ajentina, Australia, Brazili, Uingereza, Ufaransa, Israeli, New Zealand, Ukraine na Marekani wanaounga mkono juhudi za kujenga madaraja kati ya imani hizi mbili. Pia lililenga kuhamasisha kubadilishana uzoefu na kuwatia moyo viongozi wa jamii za Waadventista wanaotafuta kuanzisha uhusiano na jumuiya ya Kiyahudi katika maeneo yao husika.

Zaidi ya 19,000

Mnamo 2024, Divisheni ya Asia-Pasifiki Kusini iliwezesha timu 1,744 za Sauti ya Vijana (Voice of Youth [VOY]) na kuhamasisha vijana 50,616 kumshuhudia Yesu katika jamii zao. Juhudi hizi zilipelekea watu 19,240 kubatizwa katika nchi za Ufilipino, Indonesia, Singapore, Vietnam, Laos, Myanmar, Malaysia, Timor-Leste na Thailand. Mpango huu wa vijana ulioanzishwa mwaka 2021 umeendelea kukua na kufikia matokeo makubwa ya kiroho mnamo mwaka 2024. VOY ni mpango wa ushuhudiaji unaolenga kuwawezesha vijana kushiriki ujumbe wa malaika watatu katika jamii zao. Unawapatia vijana fursa, mafunzo na rasilimali za kushiriki injili kwa njia zinazofaa kwa mazingira yao. Mpango huu hauwabadili tu wale wanaosikia injili, bali pia unawaimarisha kiroho vijana wanaoongoza juhudi hizi.

Mpango wa ADRA wa ‘Keeping Girls Safe’ (Kuwaweka Wasichana Salama) umekuwa ukiendelea kwa miaka ishirini. 

Tracey Bridcutt, Adventist Record

Mpango wa Maendeleo na Misaada wa Waadventista (ADRA) unaoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wasichana walio hatarini unaendelea kuwapa ulinzi dhidi ya hatari ya usafirishaji haramu wa binadamu nchini Thailand.

 

Mpango wa Kuwaweka Wasichana Salama umekuwa mwangaza wa matumaini kwa miongo miwili, ukitoa usalama, elimu na ahadi ya maisha bora kwa wasichana walio hatarini kusafirishwa kwa madhumuni haramu.

 

Mpango huu katika hali yake ya sasa ulianzishwa chini ya uongozi wa Greg Young, ambaye sasa ni mkurugenzi wa ADRA Kanda ya Pasifiki Kusini. Wakati huo, alikuwa mkurugenzi wa ADRA Thailand. Hapo awali, mpango huu ulikuwa ukiendeshwa kutoka kwenye jengo lililokodishwa, lakini sasa unatekelezwa kutoka kwenye kituo cha hifadhi kilichopo Chiang Rai, ambacho kimefadhiliwa na kujengwa na ADRA Norway.

 

“Tulipoanza, ilikadiriwa kuwa kulikuwa na takribani makahaba 800,000 walio chini ya umri wa miaka 18 nchini Thailand, huku 200,000 kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 12,” Young alieleza. “Wengi wao walitoka katika jamii za walio wachache kutoka maeneo ya milimani, ambao hawakuwa na kipato.

 

“Watu walikuwa wakiwatembelea familia zao wakiahidi 'fursa' kwa wasichana hawa kuja mijini kufanya kazi kama wahudumu wa mkahawa, wasaidizi wa nyumbani, au wauguzi wa watoto. Lakini ukweli ni kwamba wengi wao waliishia katika sekta ya biashara ya ngono, kwa hivyo tuliona kuwa hili lilikuwa tatizo kubwa.”

 

Afisa wa ufuatiliaji na tathmini wa ADRA Thailand, Arthur Leung, alisema kuwa mpango huo unawahudumia wasichana kuanzia umri wa miaka mitano hadi 18. “Wasichana hawa bado hawajasafirishwa, lakini wako katika hatari kubwa ya kutumbukia katika hali hiyo,” alisema.

 

Wasichana hawa hutambuliwa kupitia taarifa kutoka kwa walimu wa shule na Idara ya Maendeleo ya Kijamii ya serikali ya Thailand. Kwa wavulana walioko katika hatari sawa, ADRA inashirikiana na makazi mengine ili kuhakikisha wanapata msaada wanaohitaji.

 

Mwaka huu, wasichana 19 wamepokelewa katika kituo cha hifadhi, huku watano kati yao wakifanikiwa kurudi katika familia zao baada ya hali zao nyumbani kuboreshwa. Kituo hiki kinao uwezo wa kuhifadhi wasichana 30. Wasichana walioko hapo huchangia katika maisha ya pamoja kwa kushiriki majukumu kama kupika chakula chao na kusafisha kituo kwa zamu.

 

Mpango huu unashughulikia moja ya sababu kuu zinazowaweka watoto katika hatari: changamoto za kifedha. “Mbali na hifadhi, tunatoa pia ufadhili wa masomo kwa watoto ili kuweza kusaidia familia zao,” Leung alisema. “Usafirishaji haramu wa binadamu mara nyingi hutokea kutokana na shinikizo la kifedha.”

 

“Ni bora zaidi watoto kubakia na familia zao,” aliongeza. “Iwapo kila kitu kitakwenda vizuri, hakuna mtoto anayepaswa kuwa hapa. Lakini mradi upo uhitaji, tutaendelea kutoa msaada.”

 

Mpango huu haujikiti tu kwenye hifadhi, bali pia kwenye kuwafikia jamii na kutoa elimu. Hii inajumuisha mafunzo mashuleni kuhusu usalama wa mtandaoni na mbinu za kukabiliana na hatari zinazowakabili watoto walio hatarini.

 

Athari za muda mrefu za mpango huu ni kubwa, ambapo wakazi wa zamani wa hifadhi hii wameendelea na masomo ya juu na hata kupata taaluma mbalimbali. Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 17, ambaye ameishi katika kituo hicho kwa miaka 10, alielezea shukrani zake kupitia mkalimani: “Kila kitu hapa ni cha kufurahiwa.” Anao mpango wa kusomea uhasibu baada ya kuondoka kwenye hifadhi.

 

Wakati wa mikutano ya mwisho wa mwaka ya Divisheni ya Pasifiki Kusini ya Kanisa la Waadventista iliyofanyika Chiang Mai, Thailand, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji (Division Executive Committee [DEC]) walipata fursa ya kutembelea hifadhi hii na kujifunza zaidi kuhusu shughuli zake.

 

Terry Kessaris, mjumbe wa DEC kutoka Australia Magharibi, alisema kuwa kutembelea hifadhi hiyo lilikuwa “somo kubwa kwangu. . . . Niliguswa sana, siyo tu na hali ya wasichana hawa, bali pia na upendo, uangalizi na usalama wanaopokea.”

Mkutano wachunguza njia za kuongeza watafsiri wa lugha za alama. 

Thais Suarez, Divisheni ya Amerika Kusini na Adventist World

Katika jitihada za kupanga na kuifikia jamii ya wasio na uwezo wa kusikia huko Peru, Kanisa la Waadventista wa Sabato katika Union Misheni ya Peru Kaskazini (NPUM) hivi karibuni waliandaa mkutano wa kwanza wa Huduma ya wasio na uwezo wa kusikia ya Waadventista (Adventist Deaf Ministry [ADM]) katika eneo hilo.

 

Tukio hilo katika eneo la Chuo Kikuu cha Peruvian Union huko Ñaña, Peru, lilipewa kichwa cha “Mikono Inayobadilisha” na liliongozwa na Edison Choque, mkurugenzi wa Huduma ya Mahitaji Maalum ya Waadventista (APM) katika NPUM. Liliwakutanisha viongozi wa eneo la utume, waumini waaminifu na watu wasio na uwezo wa kusikia ambao tayari ni washiriki wa Kanisa la Waadventista au wanaolitambua.

 

Mkutano huo ulilenga kuwafundisha washiriki juu ya uanzishaji wa vikundi vipya vya ADM katika maeneo mbalimbali. Washiriki walijifunza kuhusu uinjilisti, mtindo wa maisha wa Kiadventista, tafsiri ya Lugha ya Alama ya Peru (PSL) na misingi ya kuanzisha huduma hii katika maeneo yao. Aidha, viongozi walisisitiza umuhimu wa kuwa pamoja na uelewa wa utamaduni wa wasio na uwezo wa kusikia, wakijadili changamoto za mawasiliano wanazokumbana nazo na umuhimu wa utume huu.

 

 

UKUAJI WA HUDUMA

Kwa zaidi ya miaka miwili ya kazi kwa ajili ya wasio na uwezo wa kusikia, ADM katika Chuo Kikuu cha Peruvian Union iliwatia moyo washiriki wa mkutano huo, waandaaji walisema. Mkurugenzi wake, Hillary Jaimes, alisisitiza hitaji la kujifunza lugha ya alama kama ishara ya upendo kwa wengine na kuwa pamoja kwa hakika. “Watu wengi wasio na uwezo wa kusikia nchini Peru wanaishi katika hali ya upweke kutokana na changamoto za mawasiliano. ADM ni utume wa muhimu wa kuwaunganisha na kanisa na kuwapatia nafasi ya kujua ukweli,” alisisitiza.

 

Matokeo ya mkutano huu wa kwanza yalionekana miongoni mwa washiriki, waliodadisi umuhimu wa huduma kwa wasio na uwezo wa kusikia na haja ya kuipanua zaidi. Viongozi wa kanisa wa kanda hiyo walisema wanatarajia kuanzisha vikundi vipya vya ADM katika miji mingine ya Peru, ikiwemo Chiclayo, Trujillo, Chimbote, Tarapoto na Lima kufikia mwaka 2025. Katika miji hiyo, viongozi tayari wamewatambua watu wasio na uwezo wa kusikia wanaovutiwa kujiunga na Kanisa la Waadventista.

 

 

KUKABILIANA NA CHANGAMOTO

Kwa sasa, Peru inawatambua watafsiri wa PSL waliothibitishwa wasiozidi 100, huku nchi ikiwa na takribani raia 500,000 wasio na uwezo wa kusikia. Upungufu huu ni changamoto kubwa kwa upanuzi wa vikundi vya ADM. Hata hivyo, viongozi walisema kwamba kujitolea kwa waliohudhuria tukio hilo linaloandaliwa na Waadventista ni hatua muhimu kuelekea kuwa pamoja na upatikanaji wa huduma.

 

Tukio hilo halikuwatia moyo tu washiriki, viongozi wa kanisa wa kanda walisema, bali pia lilionyesha umuhimu wa kuwafundisha wakalimani zaidi na kuimarisha vikundi vya ADM kote nchini. “Kanisa la Waadventista linawahimiza washiriki wote kuwa sehemu ya utume huu, likileta tumaini na ujumbe wa Mungu kwa jamii ya wasio na uwezo wa kusikia nchini Peru,” walisema.

 

 

KUHUSU HUDUMA YA MAHITAJI MAALUM YA WAADVENTISTA (APM)

APM inatetea utambuzi wa utu na heshima ya kila mtu, ikilenga kusaidia watu kugundua vipawa vyao visivyojulikana licha ya unyanyapaa unaohusiana na ulemavu au upungufu. Inathibitisha kwamba kila mtu anacho kipawa, anahitajika, na ni wa thamani; kwamba watu huenda pale wanapokaribishwa lakini hubakia pale wanapothaminiwa; na kwamba thamani ya mtu inatokana na Uumbaji, si kwa kile anachoweza au asichoweza kufanya.

 

Huduma hizi zinajumuisha makundi saba maalum ya watu, wakiwemo wasio na uwezo wa kusikia, wasio na uwezo wa kuona, wenye ulemavu wa mwili na wale walio na changamoto za afya ya akili. Pia inajumuisha yatima na watoto walio katika mazingira magumu, waliopoteza wenza wao wa ndoa na wale wanaowatunza wengine.

Watendakazi, viongozi, na washiriki wakumbuka safari ya taasisi hiyo. 

Libna Stevens, Habari za Divisheni ya Kati ya Amerika

Waadventista wa Sabato hivi karibuni walisherehekea nusu karne ya huduma ya kujitolea na huduma ya afya kupitia Hospitali ya Waadventista ya Valley of Angels (HAVA) iliyoko Valle de Ángeles, Honduras.

 

Tukio hilo la siku mbili, lililofanyika Novemba 15-16, iliwaleta pamoja watendakazi wa zamani na wa sasa, wakurugenzi, viongozi wa kanisa na washiriki ili kuangalia safari ya ajabu ya hospitali hii kutoka kuwa kliniki ya matibabu ya kawaida hadi kuwa nguzo ya huduma za afya katika kanda hiyo.

 

“Hili limekuwa ni jambo la kipekee kushirikiana na waanzilishi wetu, watekelezaji wa zamani, viongozi wa kanisa na wajumbe wa bodi ya hospitali, wote ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine mafanikio ambayo Hospitali ya Waadventista ya Valley of Angels inayo leo,” alisema mkurugenzi wa HAVA, Reynaldo Canales.

 

Ikiwa na watendakazi 60 ambao ni madaktari na zaidi ya watendakazi 120 wanaosaidia, HAVA ina vyumba vitatu vya upasuaji, huduma za mionzi, tiba ya mwili, maabara, meno na ushauri wa kitabibu, pamoja na huduma za muda mrefu kwa wagonjwa walio wazee.

 

 

MAONO ZAIDI YA MIPAKA

Sehemu ya sherehe za kumbukumbu iliheshimu urithi wa marehemu Robert S. Folkenberg, mwenyekiti wa zamani wa Misheni ya Waadventista ya Honduras, ambaye aliona huduma ya matibabu kwa ajili ya eneo hili katika miaka ya mwanzoni mwa 1970. Baada ya kuruka juu ya bonde la Valle de Ángeles, Folkenberg alionyesha eneo ambalo hospitali ingejengwa baadaye. Shukrani kwa michango ya kimataifa na kujitolea kwa wahandisi, matabibu wamishonari, na viongozi wa kanisa mahalia, kliniki ilifunguliwa rasmi milango yake Novemba 1974.

 

Folkenberg, ambaye baadaye alihudumu kama mwenyekiti wa Konferensi Kuu ya Kanisa katika miaka ya 1990, alikumbukwa kwa upendo wakati wa sherehe. Mwanawe, Robert Folkenberg Jr., mwenyekiti wa Konferensi ya Kusini Mashariki mwa New England nchini Marekani alisafiri kutoka Marekani kushiriki sherehe.

 

 

MATOKEO YA KIROHO NA MATIBABU

Wakati wa ujumbe wake siku ya Sabato, Folkenberg Jr. alishiriki ujumbe na waumini, akiweka mfano wa kuvutia kutoka kwenye kisa cha kibiblia cha Elisha, ambaye alizungukwa na maadui lakini alibaki akizingatia uongozi wa Mungu. “Palikuwapo na changamoto nyingi katika kujenga hospitali hii, lakini miaka hamsini baadaye, tupo hapa na malaika wa Mungu wameitunza na kuilinda,” alisema. “Kama vile Mungu alivyotuongoza zamani, ataendelea kutusaidia kukabiliana na maisha yajayo.”

 

Kwa madaktari Frank na Janet McNeal, ambao walifika Honduras mwaka 1974 kama madaktari wa kwanza wa kimishonari wa tiba, uzoefu huo ulikuwa na athari kubwa katika maisha yao. Janet McNeal alishiriki safari ya familia yao na uzoefu wao. “Kama mume wangu, ambaye alifariki, angekuwa hapa, angefurahi sana kuona jinsi hospitali ilivyokua,” alisema.

 

 

KUJITOA WAKFU NA HUDUMA

Kwa David Velazquez, mtendakazi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika HAVA, akiwa na uzoefu wa miaka 38 katika idara ya maabara, hospitali inayo mahali maalum moyoni mwake. “Nakumbuka wakati ardhi ya hospitali ikinunuliwa. Ilikuwa ni taasisi ya kwanza ya huduma za afya nchini Honduras kutoa tiba ya mwili na uchunguzi wa ultrasound,” alisema Velazquez.

 

Albert Handal, daktari wa kwanza wa HAVA Mhondurani, alikumbuka miaka yake ya mwanzo katika hospitali. “Nilimkuta mke wangu, Darlene, hapa HAVA. Tumekuwa na wanandoa kwa miaka 46 sasa,” alisema.

 

Matthew Davis alikumbuka kumbukumbu nzuri za miaka yake ya mwanzo Valle de Ángeles, akihudhuria sherehe hii kwa niaba ya wazazi wake, Tom na Pauline Davis, ambao walihudumu HAVA kutoka 1981 hadi 1984. “Kuona kazi nzuri inayofanyika hapa leo kunaujaza moyo wangu furaha,” alisema.

Zaidi ya wawakilishi 100 wa Waadventista wanakutana nchini Bulgaria kwa mara ya kwanza kihistoria. 

David Neal, Divisheni ya Ng’ambo ya Ulaya na Adventist World

Katika tukio la kihistoria kwa ajili ya Waadventista, zaidi ya wawakilishi 100 kutoka nchi 23 walikutana huko Plovdiv, Bulgaria, Novemba 26-28 katika Mkutano wa kwanza wa Utume wa Waadventista na Utamaduni wa Orthodox.

 

Tukio hili lilikuwa ni juhudi za kushirikiana kati ya makanisa kadhaa ya kanda na lengo lake lilikuwa kuchunguza jukumu na ufanisi wa utume wa Waadventista katika muktadha wa tamaduni za Orthodox. Ingawa mkutano huo ulijumuisha makala za kitaaluma, mfululizo wa “Kuwa Mwadventista Katika Nchi Yangu” pia ulitoa msingi wa mapendekezo ya kimkakati.

 

Je, ni tamaduni zipi za kipekee katika utamaduni wa Orthodox? Waadventista wanapaswa kuelewa nini kuhusu Orthodox ya Mashariki katika muktadha wa utume wao? Je, mkusanyiko kutoka nchi mbalimbali unaweza kuwa jukwaa la kukuza rasilimali, utafiti na mawazo ya vitendo kwa ajili ya kuanzisha vikundi vipya katika maeneo haya? Mkutano ulijaribu kujibu maswali haya na mengine yanayohusiana.

 

 

KANUNI ZA MSINGI

Akikaribisha washiriki nchini Bulgaria, Milen Georgiev, mwenyekiti wa Bulgaria Union Konferensi alishiriki baadhi ya kanuni zenye kuleta uhusiano wenye maana na Wakristo wa Orthodox. Alipendekeza kuwaona wengine kuwa bora kuliko sisi wenyewe; kuuishi ukweli kwanza katika maisha yetu kabla ya kuuhubiri kwa wengine; na kumtukuza Yesu – si madhehebu yetu wala sisi wenyewe.

 

Mwenyekiti wa Konferensi ya Latvia, Imants Ģipslis, alisisitiza hitaji la kuheshimu imani yao na utambulisho wao wa kitaifa. “Usiwatarajie kuacha kanisa lao [mara hiyo hiyo], lakini toa mwaliko wa kufanya mazungumzo kuhusu uzoefu wao binafsi na Mungu,” alisema.

 

 

KUTOKA ORTHODOX HADI MWADVENTISTA

Laurențiu Nistor, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Adventus Cernica, Romania, alishiriki changamoto za kipekee anazokutana nazo Mkristo wa Orthodox anapokuwa Mwadventista wa Sabato. Kama alivyosema mmoja wa washiriki wapya, “Napenda imani yangu [ya Uadventista] mpya. . . . Lakini naendelea kwenda katika kanisa kuu la dayosisi . . . ili nijiweke kabisa katika kuwapo na Mungu. Napata kwamba katika ibada ya Waadventista, kuna kiwango kidogo sana cha muziki na maombi kuliko kiasi kinachohitajika kwa roho yangu.”

 

Akijibu, Igor Mitrović kutoka Serbia aliuliza, “Je, Uadventista ni wa kuvutia vya kutosha katika upande wa uzuri? Hakuna uzuri wa kumvutia Mtu wa Orthodox katika ibada ya Waadventista.”

 

Cristian Dumitrescu, pia kutoka Chuo Kikuu cha Adventus Cernica, alielezea changamoto hii kwa kusema, “Ukweli hauonyeshwi tu kupitia njia ya kiakili, bali pia kupitia njia ya kihisia.”

 

Katika wakati wa mkutano, uzinduzi wa kitabu cha 2025, Adventism Meets Eastern Orthodoxy: Historical, Theological, and Missiological Bridges, ulialika jamii ya Waadventista kukabiliana na changamoto za kitamaduni na kiteolojia katika kushirikiana na imani ya Orthodox ya Mashariki. Wachangiaji ishirini katika kitabu hiki ni wataalamu wanaohusiana na dini na tamaduni za Orthodox.

 

 

MAPENDEKEZO YA KIMKAKATI

Viongozi waliweka mapendekezo matatu ya msingi: (1) kuunda uelewa mkubwa ndani ya kanisa wa namna utume wa Waadventista unavyoweza kuungana na dini ya Orthodox na tamaduni; (2) kufikiria miradi ya majaribio katika eneo; na (3) kuunda kundi la kimataifa la ushauri ili kuongoza mapendekezo mawili ya kwanza.

 

“Kitu cha muhimu zaidi ambacho mtu anapaswa kukipatia kipaumbele wakati wa kuwasiliana na mwakilishi wa kundi lolote la Orthodox ni mfano wa utakatifu wa Kikristo,” alisema Eugene Zaitsev, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Divisheni ya Ulaya-Asia. “Mara nyingi maisha ya Kikristo halisi ndiyo yanatoa hubiri lenye mguso zaidi na hoja yenye usadikisho zaidi wa ukweli wa kibiblia. 

Barua ya mwisho ya Ellen White 

Moja ya barua zenye kutia moyo zaidi kutoka kwa Ellen White pia inatambulika kama barua yake ya mwisho inayofahamika, iliyoandikwa mnamo Juni 14, 1914. Ujumbe wake wa tumaini na uhakika ulisomwa kwa mara ya kwanza hadharani mwaka 1916 katika mikutano ya union huko Amerika Kaskazini. Kisha ulichapishwa katika vijitabu mbalimbali kabla ya kupatikana rasmi mnamo mwaka 1923 kama sura ya mwisho katika Testimonies to Ministers and Gospel Workers, kwa kichwa “Maisha ya Ushindi.” 

 

Jambo la kipekee ni kwamba barua hii inaelekezwa kwa “Dada Yangu Mpendwa,” bila kutaja jina. Ingawa mtu huyu alikuwa akijulikana kwa Ellen White na wafanyakazi wake katika ofisi wakati barua hiyo ilitumwa (na bila shaka kwa miaka kadhaa baadaye), utambulisho wa mpokeaji wa awali umekuwa fumbo kwa muda mrefu. Hata hivyo, kutokana na utafiti wa hivi karibuni, sasa tunafahamu jina lake na kisa chake.

 

Martha Andrea Creeper na dada yake pacha, Emma, walizaliwa huko Bristol, Uingereza, mnamo Juni 5, 1883, kwa wazazi Richard na Martha Augusta Creeper. Mama yao, aliyekuwa Mjerumani, alikutana na kuolewa na baba yao, mfanyabiashara wa mvinyo, alipokuwa akiendelea na mafunzo ya kufundisha Kifaransa na Kiingereza nchini Uingereza. Cha kusikitisha, Bw. Creeper alipitia hali ya kufilisika kutokana na vitendo vya rafiki yake na akiwa katika hali hiyo ya msongo wa mawazo, alijikuta katika hospitali ya wagonjwa wa akili ambako alifariki mwaka 1888.

 

Mama yao Martha, akiwa mjane, aliwatunza mabinti wake sita wadogo waliokuwa na umri kati ya miaka 2 na 8, pamoja na mtoto wa kambo wa miaka 18 kutoka katika ndoa ya kwanza ya Bw. Creeper. Cha kusikitisha, kijana huyo aliondoka nyumbani kwa siri na familia ilishindwa kumpata. Aliporudi Ujerumani, Bi. Creeper aliweza kuwakimu binti zake kwa kufundisha Kiingereza. Kwa bahati njema, alikutana na Waadventista wa Sabato waliomsaidia, na mwaka 1890 alijiunga na kanisa la Altona-Hamburg.

 

Punde wanafamilia walianza kupata ajira katika tawi jipya la uchapaji lililofunguliwa huko Hamburg. Bi. Creeper pia alihudumu kama mkuu wa idara ya uuguzi katika Santariamu ya Friedensau na alisaidia nyumba ya uchapaji katika miradi ya tafsiri, ikiwemo ile ya Testimonies for the Church, The Great Controversy, na The Desire of Ages, kazi aliyoifurahia sana.

NGUVU YA KUTIWA MOYO

Kila mmoja wa mabinti wa familia alijitolea katika kazi ya kanisa—isipokuwa wa mwisho, aliyefariki kwa ugonjwa wa dondakoo akiwa na umri wa miaka 5. Binti mkubwa aliolewa na Mzee Waldemar Ehlers, ambaye aliacha kazi katika nyumba ya uchapaji ya Hamburg ili kufundisha nchini Brazili. Binti mwingine aliolewa na kaka yake Waldemar, Johannes, ambaye alikuwa mmishonari mwanzilishi huko Tanzania (wakati ule ikiitwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani). Mabinti wengine walihudumu katika taasisi za kanisa, mmoja katika taasisi ya uchapaji na mwingine ya tiba.

 

Martha—aliyepokea barua ya mwisho kutoka kwa Ellen White—alibatizwa mwaka 1896 akiwa na umri wa miaka 13. Miaka mitatu baadaye, alianza kufanya kazi katika idara ya uhariri ya nyumba ya uchapaji ya Ujerumani, na kipaji chake dhahiri cha kuandika mashairi na vitabu vya watoto kilimfanya kuwa mhariri wa gazeti la watoto Unser Kleiner Freund (Rafiki Yetu Mdogo) mwaka 1909.

 

Hata hivyo, licha ya mchango wake wa thamani kwa washiriki wa kanisa wanaozungumza Kijerumani, Martha alianza kuhisi kutostahili mbele za Mungu, hali ambayo iliathiri akili na huduma yake. Mzee Guy Dail, rafiki wa muda mrefu wa familia na Katibu wa Divisheni ya Ulaya, alimwelezea kijana wa Ellen White, W. C. White, wasiwasi wake kuhusu Martha:

 

Sasa ni mwenye wasiwasi mwingi na mara nyingi hudhani kuwa yeye ni mwenye dhambi mkubwa kiasi kwamba Bwana amemkataa na hawezi tena kumruhusu afanye kazi katika kazi Yake kwa sababu hastahili. . . . Anaogopa sana kuhusu wakati wa taabu na kuhisi kana kwamba Bwana atamtupa mbali. . . . Kulingana na alichoniambia, inaonekana yupo katika hali ya kukata tamaa kwa sababu ya hatia ya dhambi—ingawa anasema ameungama dhambi zake na anaamini kuwa amesamehewa. Hata hivyo, anaonekana kwamba hawezi kujikabidhi kabisa mikononi mwa Yesu, akijua kuwa atamtunza.1

 

Mzee Dail alionyesha tumaini kwamba iwapo Ellen White angemwandikia Martha maneno machache ya kutia moyo, huenda yangempatia faraja na amani aliyohitaji.

 

Mara tu baada ya kupokea barua ya Dail, kulikuwa na mwitikio wa haraka. Ndani ya siku chache, Mzee White alimwandikia Dail, “Leo ninaweza kukutumia ujumbe kutoka kwa Mama [Ellen White] kwa Bi. Creeper. Ninakutumia nakala mbili. Moja ikiwa na ujumbe mfupi kutoka kwangu ukisema, ‘Mama ananiagiza nikuambie kuwa katika maandishi yake, amechagua haya, kama jambo muhimu kwa ukamilifu wa uzoefu wako wa Kikristo.’ Sehemu ya mwisho ya kauli hii ni maneno ambayo Mama aliyatumia aliponikabidhi maandishi hayo.”

 

Kisha akaongeza maneno haya: Msihi ageuze macho yake kutoka kwenye maandishi hayo hadi kwenye Biblia, na asome ujumbe wenye tumaini na faraja ulioandikwa humo, akizingatia kuwa haya yameandikwa kwa ajili yake na Yeye anayewajua na kuwapenda watoto Wake wote.”

 

Ujumbe wa Ellen White ulikuwa ni upi, katika barua yake ya inayofahamika kuwa ya mwisho? Barua nzima inaweza kusomwa katika kurasa 13-15 za toleo hili. Miongoni mwa vifungu vizuri zaidi katika barua hiyo ni maneno haya ya uhakikisho:

 

“Usizungumzie kutostahili kwako na mapungufu yako. Wakati unahisi kana kwamba huzuni inakufunika, mtazame Yesu na useme, Yu hai ili kuniombea.”

 

Ni haki yako kumtumainia Yesu kwa wokovu wako, kwa namna iliyo kamili, yenye uhakika, na yenye heshima kuu; kusema, “Ananipenda, ananikubali; nitamtegemea, kwa maana aliyatoa maisha Yake kwa ajili yangu.

 

“Neema ni sifa inayotolewa kwa wanadamu wasiostahili. Hatukuwa tumeitafuta, bali ilitumwa kututafuta. Mungu anafurahia kuwapa neema wale wote wanaoihitaji, si kwa sababu tunastahili, bali kwa sababu hatustahili. Hali yetu ya uhitaji ndiyo sifa inayotupatia uhakika kwamba tutapokea zawadi hii.”2

 

Mwitikio wa Martha ulikuwaje kwa barua hii ya dhati? Ikiwa alimjibu kwa kumwandikia Ellen White, hakuna jibu lililohifadhiwa, lakini tunajua kwamba aliendelea kumtumikia Mungu kwa uaminifu katika nyumba ya uchapaji ya Ujerumani hadi alipostaafu mwaka wa 1949 baada ya miaka 50 ya huduma. “Shangazi Martha,” kama alivyofahamika kwa upendo miongoni mwa watendakazi wenzake, alifariki mwaka 1976 akiwa na umri wa miaka 93,lakini ujumbe alioupokea kutoka ng’ambo ya Bahari ya Atlantiki unaendelea kututia matumaini na uhakikisho hadi leo.

1 Guy Dail kwa W. C. White, Mei 21, 1914. Historia ya familia ya awali ilikusanywa kutoka Dail to White, August 23, 1912.
 

2 Ellen G. White, “My Dear Sister,” barua ya pili, 1914 (Juni 14), imechapwa katika Testimonies to Ministers and Gospel Workers (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1923), kur. 516-520
 

3 Obituary, Martha Creeper, Advent-Echo, vol. 75, no. 21 (Novemba 1, 1976): 17. Courtesy of Bernd Müller and Markus Kutzschbach.

Tim Poirier ni makamu mkurugenzi na mhifadhi nyaraka wa Ellen G. White Estate, Inc.

NA ELLEN G. WHITE

St. Helena, California, Juni 14, 1914

 

Dada yangu mpendwa,

Bwana amenipatia ujumbe kwa ajili yako—na si kwa ajili yako tu, bali pia kwa nafsi zingine ambazo zinatatizwa na mashaka na hofu kuhusu kukubaliwa kwao na Bwana Yesu Kristo. Neno Lake kwako ni: “Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu” (Isa. 43:1). Unatamani kumpendeza Bwana, na unaweza kufanya hivyo kwa kuamini ahadi Zake. Anangoja kukupeleka katika bandari ya uzoefu wa neema, naye anakusihi, “Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu” (Zab. 46:10). Umepita katika kipindi cha msukosuko, lakini Yesu anakuambia: “Njoni kwangu, . . . nami nitawapumzisha” (Mt. 11:28). Furaha ya Kristo moyoni ina thamani isiyolinganishwa. “Ndipo walipofurahi” (Zab. 107:30), kwa sababu wanapewa nafasi ya kupumzika katika mikono ya upendo wa milele.

Ondoa mashaka yako kwa Baba yetu wa mbinguni. Badala ya kuzungumza juu ya mashaka yako, jikomboe nayo kwa nguvu za Yesu na ruhusu nuru kuangaza moyoni mwako kwa kuonyesha imani na tumaini kwa Mungu kwa sauti yako. Najua kuwa Bwana yuko karibu sana na wewe ili akupatie ushindi, ninakuambia: Jipe moyo, uwe na nguvu, jiondoe kutoka katika giza la kutokuamini. Mashaka yatavamia mawazo yako, kwa sababu Shetani anajaribu kukushikilia mateka kwa mamlaka yake katili; lakini mkabili kwa nguvu anazokupatia Yesu na ushinde mwelekeo wa kudhihirisha kutokuamini katika Mwokozi.

 

Usizungumzie kutostahili kwako na mapungufu yako. Wakati unapohisi kana kwamba huzuni inakufunika, mtazame Yesu na useme: “maana yu hai sikuzote ili aniombee” (Ebr. 7:25). Sahau mambo ya nyuma na amini ahadi: “Nasi tutakuja kwake” na “kufanya makao kwake” (Yn. 14:23).

 

Mungu anangoja kukupa baraka ya msamaha, ya ondoleo la uovu na ya zawadi ya haki kwa wale wote watakaoamini katika upendo Wake na kupokea wokovu Anaoutoa. Kristo yuko tayari kumwambia mwenye dhambi atubuye: “Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi” (Zek. 3:4). Damu ya Yesu Kristo ni ombi lenye nguvu linalozungumza kwa niaba ya wenye dhambi. Damu hii “hutusafisha na udhalimu wote” (1 Yohana 1:9).

 

Ni haki yako kumtumainia Yesu kwa wokovu wako, kwa namna iliyo kamili, yenye uhakika, na yenye heshima kuu; kusema, “Ananipenda, ananikubali; nitamtegemea, kwa maana aliyatoa maisha Yake ili kuniokoa.” Hakuna kitu kinachoweza kuondoa mashaka kama kukutana na tabia ya Kristo. Anatangaza: “Ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe” (Yn. 6:37); yaani, hakuna uwezekano wowote wa kumkataa, kwa kuwa Nimeahidi kumpokea. Mshike Kristo kwa neno Lake, na acha midomo yako itangaze kuwa umepata ushindi.

 

Je, Yesu ni wa kweli? Je, anamaanisha kile anachosema? Jibu kwa uhakika Ndiyo, kila neno. Ikiwa umeliamini hili, basi kwa imani dai kila ahadi aliyoitoa na upokee baraka; kwa maana kukubaliwa huku kwa imani huleta uzima rohoni. Unaweza kuamini kwamba Yesu ni mwaminifu kwako, hata kama unajiona kuwa mdhaifu zaidi na usiyestahili kati ya watoto Wake. Unapoamini, huzuni yako yote, mashaka yako yote, hurudishwa kwa mdanganyifu mkuu aliyeyaanzisha. Unaweza kuwa baraka kubwa ikiwa utamfuata Mungu kwa neno Lake. Kwa imani iliyo hai inakupasa kumwamini Yeye, hata kama utahisi msukumo mkubwa wa kusema maneno ya kutokuamini.

 

Amani huja kwa kutegemea uweza wa kiungu. Kadiri nafsi inavyoamua kutenda kulingana na nuru inayotolewa, Roho Mtakatifu huwapa nuru zaidi na nguvu. Neema ya Roho hutolewa ili kushirikiana na uamuzi wa nafsi; lakini si mbadala wa matumizi binafsi ya imani. Mafanikio katika maisha ya Kikristo yanategemea kupokea na kutumia nuru ambayo Mungu ameitoa. Si wingi wa nuru na ushahidi unaoufanya moyo kuwa huru katika Kristo; bali ni kuinuka kwa nguvu za nafsi, nia ya dhati na bidii ya moyo, ili kulia kwa dhati: “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9:24).

Ninafurahia matarajio mazuri ya wakati ujao, nawe pia unaweza kufurahia. Kuwa na moyo wa furaha na umsifu Bwana kwa fadhili Zake. Yale usiyoweza kuyaelewa, mkabidhi Yeye. Anakupenda na kukuhurumia kwa kila udhaifu wako. “Aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo” (Efe. 1:3). Isingeridhisha moyo wa Mungu asiye na kikomo kuwapa wale wanaompenda Mwana Wake baraka ndogo kuliko anayompa Mwanawe.

 

Shetani anatafuta kuvuruga mawazo yetu kutoka kwa Msaidizi mkuu, akitaka kutufanya tutafakari juu ya hali yetu duni ya kiroho. Ingawa Yesu anaona hatia ya maisha yetu ya zamani, anatoa msamaha; nasi hatupaswi kumfedhehesha kwa kutilia shaka upendo Wake. Hisia za hatia lazima ziwekwe chini ya msalaba, la sivyo zitaathiri chanzo cha uhai wetu. Shetani anapokuletea vitisho vyake, jiepushe navyo na utulize moyo wako kwa ahadi za Mungu. Wingu linaweza kuwa jeusi kwa lenyewe, lakini linapojazwa na nuru ya mbinguni, hugeuka kuwa mwangaza wa dhahabu, kwa kuwa utukufu wa Mungu unakaa juu yake.

 

Watoto wa Mungu hawapaswi kutawaliwa na hisia na mihemko. Wanapoyumba kati ya tumaini na hofu, moyo wa Kristo unaumia; kwa kuwa amewapatia ushahidi wa wazi wa upendo Wake. Anawataka wawe imara, wenye nguvu na wenye msimamo katika imani takatifu. Anawataka wafanye kazi aliyowapa; ndipo mioyo yao itakuwa mikononi Mwake kama vinubi vitakatifu, ambavyo kila sauti yake itatoa sifa na shukrani kwa Yeye aliyetumwa na Mungu kuondoa dhambi za ulimwengu.

 

Upendo wa Kristo kwa watoto Wake ni mwema kama ulivyo na nguvu. Ni wenye nguvu kuliko mauti; kwa maana alikufa ili kununua wokovu wetu na kutufanya tuwe wamoja Naye, kiroho na milele. Upendo Wake ni wenye nguvu kiasi kwamba unadhibiti uwezo Wake wote na kutumia hazina kubwa za mbinguni ili kuwatendea wema watu Wake. Haubadiliki kamwe—ni ule ule jana, leo na hata milele. Ingawa dhambi imekuwepo kwa vizazi vingi, ikijaribu kupinga upendo huu na kuuzuia kuwafikia wanadamu, bado unatiririka kwa wingi kwa wale ambao Kristo alikufa kwa ajili yao.

 

Mungu anawapenda malaika wasio na dhambi, wanaotenda huduma Yake na kutii amri Zake zote; lakini hawapewi neema, kwa kuwa hawakuwahi kuihitaji—hawakuwahi kutenda dhambi. Neema ni sifa inayotolewa kwa wanadamu wasiostahili. Hatukuwa tumeitafuta, bali ilitumwa kututafuta. Mungu anafurahia kuwapa neema wale wote wanaoihitaji, si kwa sababu tunastahili, bali kwa sababu hatustahili. Hali yetu ya uhitaji ndiyo sifa inayotupatia uhakika kwamba tutapokea zawadi hii.

 

Haipaswi kuwa vigumu kukumbuka kwamba Bwana anatamani uweke mizigo yako na mashaka yako miguuni Pake na uache hapo. Mwendee ukisema, “Bwana, mizigo yangu ni mizito mno kwangu kubeba. Je, utanibebea?” Naye atajibu, “Nitakubebea. Kwa fadhili za milele nitakurehemu. Nitachukua dhambi zako na nitakupa amani. Usiendelee tena kujiwazia vibaya; kwa kuwa nimekununua kwa damu Yangu Mwenyewe. Wewe ni wangu. Nitautia nguvu moyo wako ulio dhaifu. Nitaondoa majuto yako ya dhambi.”

 

“Mimi, naam, Mimi ndimi,” Bwana aliweka wazi, “niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitakumbuka dhambi zako. Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” (Isa. 43:25, 26). “Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, Bwana, nasema haki; nanena mambo ya adili” (Isa. 45:19). “Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine” (Isa. 45: 22). Itikia mwito wa rehema ya Mungu, dada yangu na useme, “Nitamtegemea Bwana, na kufarijiwa. Nitamshukuru Bwana; kwa kuwa hasira Yake imegeuzwa mbali. Nitafurahi katika Mungu, anayenipa ushindi.”

Barua hii (Letter 2, 1914) imechapishwa kwa ukamilifu wake katika Testimonies to Ministers and Gospel Workers, kur. 516-520.

Amri za Mungu na imani ya Yesu 

NA TED N. C. WILSON

Sisi ni familia ya thamani ya Waadventista wa Sabato, inayokua kwa kasi, tukifikia zaidi ya waumini milioni 23, kwa utukufu wa Mungu na kwa uweza Wake. Ni dhahiri kwa watu wengi kwamba tunaishi katika nyakati zisizo za kawaida, huku ulimwengu ukivunjika kimwili, kijamii, kiuchumi, kisiasa, na kiroho.

 

Tunapoelekea mwisho wa ulimwengu na ujio wa Yesu ulio karibu, Mungu anatuita kama vuguvugu Lake la Marejeo kuwa waaminifu Kwake na ujumbe Wake wa siku za mwisho kuliko wakati wowote. Yesu anatuhimiza, “… Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima” (Ufu. 2:10). Yapo mashinikizo kutoka kila upande ya kutupotosha kutoka kwenye uaminifu wetu, lakini Mungu anatutaka tumtazame Yeye na Neno Lake kikamilifu.

 

 

WATU WA MUNGU WA SIKU ZA MWISHO

Kitabu cha Ufunuo kinawatambulisha watu wa Mungu wa siku za mwisho kama “wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu” (Ufunuo 12:17). Na Ufunuo 19:10 inatuambia: “Ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.” Ni upendeleo mkubwa kupokea maelekezo, ushauri na wazo zuri kutoka kwa Mungu kupitia Ellen G. White kama sehemu ya Roho ya Unabii. Simama imara katika Neno Takatifu la Mungu na kwa maagizo Yake katika maandiko ya Ellen White yaliyo Roho ya Unabii.

 

Kama sehemu ya ujumbe wenye nguvu wa malaika watatu uliopo katika Ufunuo 14:6-12, tunasikia mwito wa kuwa waaminifu tena katika aya ya 12, inayowatambulisha watu wa Mungu: “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.”

 

Kweli hii ya kina kuhusu uaminifu kwa Mungu, Neno Lake, na amri Zake inaakisiwa vyema katika Kumbukumbu la Torati 7:9: “Basi ujue ya kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kuzishika amri zake, hata vizazi elfu.”

 

 

MATABAKA MAKUU MAWILI

Katika kitabu cha ajabu Pambano Kuu, tunasoma, “Katika shindano hili ulimwengu wote wa Wakristo utagawanyika katika matabaka mawili makubwa—wale wanaozishika amri za Mungu na imani ya Yesu kwa upande mmoja, na wale wanaomwabudu mnayama na sanamu yake na kupokea chapa ya mnyama. Hata kama kanisa na serikali wataunganisha nguvu zao kuwalazimisha ‘wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa’ (Ufunuo 13:16), wapokee ‘chapa ya mnyama,’ hata hivyo watu wa Mungu hawataipokea [Ufunuo 15:2, 3].”¹

 

Kristo ndiye kiini cha uaminifu wetu kwa Neno Lake, amri Zake na ujumbe wa malaika watatu. Ni haki Yake iliyoko ndani ya kila kitu tunachoweza kutimiza kupitia Yeye. 

 

Ellen White aliandika, “wakati mwingine tutakuwa katika mashaka makubwa na tusijue cha kufanya. Lakini nyakati hizo ni fursa yetu kuchukua Biblia na kusoma ujumbe aliotupatia; kisha tupige magoti na kuomba msaada Wake. Mara kwa mara, ametoa ushahidi kuwa Yeye ni Mungu anayesikia maombi na anayejibu. Hutimiza ahadi Zake kwa kiwango kikubwa zaidi ya tunavyotarajia kupokea msaada.”²

 

Kama watu wa Mungu wa siku za mwisho wanaitwa kuwa waaminifu kwa kuamini na kutangaza Neno Lake, tuwe watu wenye bidii na waaminifu wenye maombi, tukitegemea nguvu na neema ya Yesu Kristo pekee. Tunaambiwa: “Ushindi mkuu zaidi kwa ajili ya kazi ya Mungu haupatikani kwa mabishano yenye kazi kubwa, kuwepo kwa vifaa vingi, ushawishi mpana, au wingi wa rasilimali; hupatikana katika chumba cha maombi pamoja na Mungu, ambapo watu wenye imani ya dhati, wanaosumbuka wanashikilia mkono wenye nguvu.”³

 

 

YEYE NI MWAMINIFU

Katika 1 Wathesalonike 5:24, tunakumbushwa juu ya uaminifu wa Mungu katika kutunza uaminifu wetu Kwake: “Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.” Yuda anatuhimiza katika aya ya 3 “kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.” Wapo mashujaa wengi wa Biblia waliokuwa waaminifu, na Mungu anatuita tuwe waaminifu kama wao—watu kama Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Yusufu, Yokebedi, Musa, Esta, Eliya, Hana, Samweli, Daudi, Abigaeli, Petro, Paulo, Dorkasi, Yohana na wengi zaidi.

 

Katika kipindi hiki cha ajabu katika historia ya dunia, tunaitwa kuwa waaminifu katika Neno la Mungu. Tunaambiwa waziwazi: “Mungu ametoa ushahidi wa kutosha kwa msingi wa imani kwa yeyote atakayetaka kuamini. Katika siku za mwisho dunia itakuwa karibu kukosa imani ya kweli. Kwa hila kabisa, Neno la Mungu litachukuliwa kuwa lisilotumainiwa, huku hoja za kibinadamu zikikubaliwa, hata kama zinapingana na ukweli wa wazi wa Maandiko.”⁴

 

Marafiki zangu, tunaishi katika siku hizo hasa. Neno la Mungu linapuuzwa, linadharauliwa na linapotoshwa ili kuakisi mawazo ya kibinadamu badala ya kile Biblia inachosema kwa hakika. Hili linaonekana wazi zaidi katika kile ambacho Mungu anakitaja kuwa dhambi katika aina zake nyingi, ikiwemo ukweli wa kibiblia kuhusu ujinsia wa binadamu. Tunaitwa kuwa waaminifu kwa Mungu na kwa Neno Lake.

 

Tunapoelekea kwenye pambano la mwisho dhidi ya Shetani na dhambi, Mungu anatuita kuwa waaminifu Kwake, kwa Neno Lake, kwa ujumbe wa Marejeo na kwa tangazo la ujumbe wa malaika watatu ambao unalenga haki ya Kristo na amri Zake kumi nzuri, zinazoonyesha kuwa tabia Yake imejengwa juu ya upendo Wake wa milele kwa kila mmoja wetu.

WOTE WAMEITWA

Kila mtu anayo nafasi katika kazi ya Mungu na ameitwa kuwa mwaminifu katika kutangaza ujumbe Wake wa siku za mwisho. Tunaambiwa, “Hatuna wakati, wala maneno ya kupoteza katika mabishano. . . . Kuna haja ya nguvu iliyotakaswa. Majeshi ya mbinguni yako tayari kusonga mbele, na yuko wapi wakala wa kibinadamu wa kushirikiana na Mungu?”⁵

 

Kisa cha maisha yetu binafsi na ushuhuda wetu kinapaswa kushirikiwa na ulimwengu tunaposhuhudia kwa uaminifu juu ya Yesu na uweza Wake wa kuokoa. Tunapomtegemea Yeye, atatupatia uwezo ya kuwa waaminifu kwa sababu Yeye ndiye kila kitu kwetu. Kuwa mwaminifu kwa amri Zake kumi kwa uweza Wake si uhalalishaji wa matendo, bali ni kusisitiza haki Yake ya kutufanya kuwa wenye haki na kututakasa, kwa kuwa Yesu Kristo ndiye utoshelevu wetu.

 

Je, uko tayari kuwa sehemu ya Mpango wa Ushiriki wa Kila Mshiriki Ulimwenguni (TMI) katika kushiriki ujumbe wa Mungu ulimwenguni? Je, uko tayari kuitikia ombi la Kristo—“Ni nani basi aliye mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?” (Mathayo 24:45). Umeteuliwa kwa ajili ya utume na umeitwa kuwa mwaminifu. Songa mbele na useme, “Ndiyo Bwana, nitakwenda.” Mungu akubariki unapoendelea kuwa mwaminifu Kwake. Maranatha!

1 Ellen G. White, Pambano Kuu (Mountain View, Calif: Pacific Press Pub. Assn., 1911), uk. 372.

 

2 Ellen G. White, katika Pacific Union Recorder, Desemba 26, 1912.

 

3 Ellen G. White, Gospel Workers (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1915), uk. 259.

 

4 Ellen G. White, Spiritual Gifts (Battle Creek, Mich.:  Seventh-day Adventist Pub. Assn., 1864), vol. 3, uk. 94. 

 

5 Ellen G. White, Testimonies to Southern Africa (Cape Town, S.A.: South African Union Conference of Seventh-day Adventists, 1977), uk. 44.

Ted N.C. Wilson ni mwenyekiti wa Konferensi Kuu ya Waadventista wa Sabato. Makala za nyongeza na maoni zinapatikana katika X (awali Twitter): @pastortedwilson na katika Facebook: @Pastor Ted Wilson.

NA ROY E. GRAF

Tangu siku za awali, waasisi wa Waadventista walielewa umuhimu wa fundisho la Biblia kuhusu patakatifu pa mbinguni kama sehemu kuu inayounda mfumo wao wa imani. Kwa maneno ya Ellen G. White, somo la patakatifu lilikuwa “lilifungua mfumo kamili wa ukweli, ulioshikamana na kuafikiana.”¹

 

Kwa hivyo, Ellen White na waasisi wengine Waadventista walitambua kuwa fundisho la patakatifu lina maana muhimu sana kwa utume wa kanisa, ambao unahusisha kutangaza kweli ya sasa kuhusu patakatifu pa mbinguni kama ilivyoangaziwa katika ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12.

 

Kwa sababu walitambua umuhimu wa ujumbe huu kwa utume wa kanisa, waasisi waliweka mkazo mkubwa katika mafundisho ya kweli kwa wale waliotaka kuwa washiriki wa kanisa. Hili lilihusisha msisitizo maalum juu ya somo la patakatifu, hukumu ya upelelezi na maandalizi ya ujio wa Kristo mara ya pili.²

 

Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita, Waadventista wengine wamepunguza umakini wao kuhusu nafasi ya patakatifu kama kipengele cha msingi kinachoathiri uelewa wetu wa utume na kutuongoza katika utendaji wetu. Wengine wameiga mbinu za utume zinazolenga zaidi kuwafanya watu wamkubali Kristo mwanzoni mwa safari yao ya Kikristo, huku wakipuuzia ukuaji wa kiroho na uanafunzi. Mbinu kama hii mara nyingi haizingatii umuhimu wa watu kufanya uamuzi wa dhati kuhusu mafundisho ya Biblia na mtindo wa maisha.³ Hali hii imesababisha baadhi ya waumini wapya kutokuwa na mizizi imara katika imani ya Waadventista, hivyo kuwa wepesi kuiacha baadaye na pia, kusababisha changamoto mbalimbali katika maisha ya kanisa.

 

 

KUELEKEA KUUELEWA UTUME KWA MTAZAMO WA PATAKATIFU

Je, uelewa wa kibiblia na Waadventista kuhusu patakatifu unawezaje kusaidia kubadilisha hali hii?

 

Kama ilivyotajwa, waasisi wa Waadventista walijenga mafundisho yao kuzunguka fundisho la patakatifu. Ninaamini kwamba uelewa na utendaji wa sasa wa Waadventista kuhusu utume unapaswa pia kujengwa katika mtazamo huu. Patakatifu ni kiini cha ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12, ambapo malaika wa kwanza anatangaza kuwa saa ya hukumu imewadia. Waadventista kihistoria wamechukulia ujumbe huu kama kiini cha mahubiri yao. Kwa hiyo, patakatifu panawezaje kuunda uelewa na utendaji wa utume?

 

Katika sehemu ifuatayo, ningependa kuangazia vipengele vinne: (1) patakatifu hueleza uelewa wa Kibiblia kuhusu wokovu ambao ndiyo msingi wa utume na uanafunzi, (2) patakatifu hueleza maudhui ya ujumbe unaopaswa kutangazwa, (3) patakatifu hueleza mtazamo wa kanisa kama jamii ya kiagano, kikuhani na ya kimishonari ambayo waongofu wapya hujiunga nayo, (4) patakatifu hueleza matukio ya mwisho yanayoongoza utume wa wakati huu.

Patakatifu Huunda Uelewa wa Kibiblia Kuhusu Wokovu

 

Mbinu inayotumika katika utume inahusiana kwa ukaribu na jinsi wokovu unavyoeleweka. Katika Biblia, uelewa wa wokovu umejengwa juu ya kile ninachokiita mfumo wa uhusiano wa patakatifu. Patakatifu siyo tu jengo halisi lililoko mbinguni. Mungu anahusiana na ulimwengu kupitia mfumo huu mgumu, ambapo anakaa pamoja na viumbe Wake, anapokea ibada yao na kutekeleza mpango wa wokovu hadi utakapokamilika.

 

Katika mfumo huu, patakatifu panaeleza na kudhihirisha uelewa wa Kibiblia kuhusu wokovu. Wokovu unahitaji mchakato wa upatanisho, yaani, mchakato ambao Mungu hutafuta kuwapatanisha wanadamu walioanguka na Yeye na kuondoa tatizo la dhambi (2 Kor. 5:19-21; Ufu. 21:4-5). Kutokana na mtazamo huu, upatanisho siyo tu kile Kristo alichofanya msalabani. Unajumuisha mpango mzima wa kiungu wa kuangamiza dhambi.

 

Katika ngazi ya mtu binafsi, utekelezaji wa mpango huu wa wokovu pia ni mchakato, si tukio la mara moja kama wengine wanavyodhani. Mchakato huu unahusisha, pamoja na mambo mengine, haki na utakaso. Haki si kitu kingine bali msamaha wa Mungu (Rum. 4:6-8), ambao unahitajika kila siku, kila wakati mtu anapotenda dhambi (1 Yoh. 2:1; 1:9). Msamaha huu hupatikana kupitia huduma ya maombezi inayoendelea ya Kristo katika patakatifu pa mbinguni (Marko 11:24-26; Yn. 14:13). Haki hii inamwezesha muumini kukuza maisha ya utakatifu kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliyemtumwa na Kristo kutoka patakatifu pa mbinguni kama mwakilishi Wake (Ufu. 5:6). Bila haki hakuna utakaso wa kweli (Rum. 6 na 8). Lakini bila utakaso, hakuna haki pia (Kol. 1:21-23).

 

Mtazamo huu wa Kibiblia kuhusu wokovu kama mchakato ambao, kwa nuru ya patakatifu, hujumuisha kwa pamoja kupokea msamaha wa Mungu kila mara na kukua katika utakatifu, humaanisha kwamba utume wa uanafunzi pia unapaswa kuwa mchakato. Uanafunzi unapaswa kuwa mchakato (Kol. 2:6). Si sawa kulenga tu kuwawezesha watu kumpokea Kristo na kubatizwa, bali waumini wapya wanapaswa kufundishwa kabla na baada ya ubatizo pia. Kama ambavyo upo mchakato wa kabla ya msamaha unaojumuisha utambuzi wa dhambi, toba na ungamo (Zab. 51:4; Luka 18:13; Matendo 2:38; 3:19; Zab. 32:5) na mchakato wa baadaye wa kukua katika utakatifu na mtindo wa maisha ya Kikristo (Rum. 6:22), uanafunzi unapaswa kujumuisha maandalizi ya kabla na baada ya ubatizo ili kusaidia mchakato huo.

Shughuli za Patakatifu Zinaunda Maudhui ya Ujumbe

 

Kuelewa ujumbe wa kibiblia kuhusu wokovu ni jambo la msingi katika kuwafikia watu ambao hawajaufahamu ujumbe huo. Shughuli za Kristo katika patakatifu pa mbinguni zinaeleza mpango wa wokovu. Kwa hivyo, kazi ya Kristo ni mada kuu katika Agano Jipya (tazama, kwa mfano, Matendo 5:31; Rum. 8:34; Ebr. 7:25; 8:1; 1 Tim. 2:5; 1 Yn. 2:1; Ufu. 5:7-8). Kwa hiyo, shughuli za Kristo katika patakatifu sasa zinapaswa kuunda maudhui ya ujumbe wa watu masalia wa leo (kama ilivyoelezwa katika Ufu. 14:6-12).

 

Ikiwa Kristo anaendelea kuwaombea waumini katika hukumu ya upelelezi kabla ya ujio Wake, basi somo hilo linapaswa kuwa sehemu muhimu ya ujumbe wa Waadventista. Kwa hivyo, utume wa Waadventista leo hauwezi kueleweka kwa kuzingatia tu Agizo Kuu katika Mathayo 28:18-20. Unapaswa pia kueleweka kwa kuzingatia Ufunuo 14:6-12, ambapo ujumbe wa malaika watatu unawakilisha kweli ya sasa kwa wakati huu.⁴

 

Hii inamaanisha kuwa utimilifu wa utume na mchakato wa uanafunzi lazima ujumuishwe na maandalizi thabiti ya mafundisho kwa waumini wapya, ili kila mmoja aweze kuelewa ujumbe wa patakatifu na hukumu na kufanya uamuzi wa makusudi na wa vitendo kuuhusu. Katika patakatifu pa mbinguni, Mungu hushughulikia nia za wanadamu ambazo zinapaswa kufanya maamuzi yenye maarifa, si kwa msingi wa hisia za ghafla au msisimko wa kihisia wa muda mfupi. Si jambo la kushangaza, basi, kwamba Agano Jipya linaangazia sana haja ya kufundisha mafundisho na umuhimu wa Neno katika mchakato huo (1 Tim. 4:13, 16; 6:3; 2 Tim. 3:15-16; 4:2-3; Tito 1:9; 2:1, 7).

Patakatifu Huunda Mtazamo wa Kanisa

 

Wale wanaokubali ujumbe wa injili wanakuwa sehemu ya kanisa. Kanisa ni hekalu la kiroho, jumuiya inayoundwa na wakazi wa kiroho wa patakatifu pa mbinguni (1 Kor. 3:16; Ufu. 11:1; 21:3) ambao wameingia katika agano pamoja na Mungu kwa kujitoa wao wenyewe kuitii sheria Yake ya upendo (Yer. 31:31-33; Ufu. 12:17; 14:12).

 

Washiriki wa kanisa ni sehemu ya jumuiya ya kikuhani na kimishonari, taifa takatifu, ambalo jukumu lake ni “kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1 Pet. 2:9; tazama Kut. 19:6).5 Kupitia tangazo hilo, katika nafasi yao kama makuhani wa kimishonari, wanawaleta wengine kwa Kristo, kuhani mkuu wa patakatifu pa mbinguni (Ebr. 8:1–2), ambaye kwa Yeye wanapokea nguvu ya kuishi maisha matakatifu kwa kutii masharti ya agano. Masalio ya watu wa wakati wa mwisho wanatambuliwa kwa sifa hii (Ufu. 12:17; 14:12).

 

Waumini tayari, kwa namna fulani, ni raia wa Yerusalemu mpya na waabudu wa patakatifu pake kwa imani (Gal. 4:26; Efe. 2:18-19; Fil. 3:20; Ebr. 11:10, 16; 12:22; 13:14), ambako Kristo anawakilisha na ni mtangulizi wao (Ebr. 6:20). Katika dunia mpya, waumini wataishi katika Yerusalemu mpya, inayojulikana kama “hema ya Mungu,” ambamo Mungu na Mwana-Kondoo wataendelea kupokea ibada milele (Ufu. 21:3; 22:3).

 

Katika muktadha huu, ubatizo ni ishara ya kukubali masharti ya agano na kuingia katika jumuiya ya kiagano, kikuhani na kimishonari, kama vile tohara ilivyokuwa ishara ya agano katika Agano la Kale (Kol. 2:11-12) kwamba mtu alikuwa sehemu ya jumuiya ya kikuhani na kimishonari ya Israeli (Kut. 19:5-6). Kwa hivyo, unapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Yule anayebatizwa anaonyesha hadharani kwamba anataka kuwa mshiriki wa jumuiya, anakubali masharti ya agano yaliyowekwa katika amri (Rum. 6:1-6), na anatamani kuwa kuhani mmishonari kama sehemu ya ukuhani wa waumini wote (1 Pet. 2:9). Sabato, kwa upande wake, ni ishara ya kudumu na kuendelea katika, na uaminifu kwa, masharti ya agano (Kut. 31:17; Ufu. 14:6-7). Hii inamaanisha kuwa yeyote anayekubali ubatizo lazima afundishwe ipasavyo kuhusu ahadi anayotoa kwa kushiriki katika tendo hilo.

Patakatifu Huunda Matukio ya Unabii Yanayoongoza Utume

 

Hatimaye, shughuli za patakatifu zinaathiri matukio ya unabii yanayoongoza utume wa Waadventista. Shughuli za patakatifu zinahusiana na ujio wa kwanza wa Kristo (Dan. 9:24–27; Gal. 4:4) na pia zinahusiana na ujio Wake wa mara ya pili (Dan. 7:13–14; Mt. 25:31). Utume wa wakati wa mwisho wa kanisa la masalio (Ufu. 12:17) ni kushirikiana katika maandalizi ya watu kwa ajili ya ujio wa Kristo (Ufu. 14:6–12). Mungu analikusanya kanisa ndani ya Kristo—kichwa chake (Efe. 1:22–23) na kuhani wake mkuu (Ebr. 8:2)—wale wote wanaokubali kuwa sehemu ya jumuiya ya agano na kushiriki katika ukuhani Wake wa kimishonari ulimwenguni katika nyakati za mwisho (Ufu. 1:6; 5:10). Kwa upande wao, wale wanaojiunga na jumuiya ya agano huweka nadhiri ya kuwa washiriki wa kimishonari popote pale Mungu anapowaamuru, “mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza” (2 Pet. 3:12, msisitizo umeongezwa). Kwa kushirikiana na nguvu za kiungu, watu wa Mungu wanapaswa kufanya sehemu yao ili kuendeleza kazi ya mwisho ya kuhubiri injili (Mt. 24:14) huku Kristo akihitimisha huduma Yake katika patakatifu pa mbinguni (Ebr. 9:28). Kwa njia hii, shughuli za patakatifu zinatoa mfumo wa matukio ya mwisho na kuongoza utume wa masalio wa mwisho ndani ya mfumo huo.

HITIMISHO

Patakatifu huelezea mafundisho na utume wa Waadventista katika historia. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, baadhi ya watu wameweka msisitizo mkubwa katika uzoefu wa awali wa waliofanywa kuwa wanafunzi, huku maandalizi yao ya mafundisho na mtindo wa maisha wa Kikristo yakipuuzwa. Hali hii inabeba hatari kubwa ya kanisa kupoteza utambulisho wake na kufifisha ujumbe wake wa kipekee kwa ulimwengu. Zamani, mafundisho ya patakatifu yalikuza utambuzi “kuwa mkono wa Mungu uliongoza vuguvugu kuu la marejeo” na pia yalifunua “wajibu wa sasa kwa kuonyesha nafasi na kazi ya watu Wake.”6 Ni wakati wa kuruhusu mafundisho ya patakatifu kurekebisha upya uelewa wa Waadventista kuhusu ujumbe wao na utume wao.

1 Ellen G. White, Pambano Kuu (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1911), uk. 351.

 

2 Tazama P. Gerard Damsteegt, Foundations of the Seventh-day Adventist Message and Mission (Grand Rapids, Mich.: Eerdmans, 1977), kur. 295-296.

 

3 Tazama Russell Burrill, Radical Disciples for Revolutionary Churches (Fallbrook, Calif.: Hart Research Center, 1996), kur. viii-ix.

 

4 Tazama, baadhi ya sifa, Burrill, Radical Disciples, 75-81.

 

5 Nukuu za Maandiko zimetolewa katika Swahili Union Version Bible. Haki zote zimehifadhiwa.

 

6 E. G. White.

Roy E. Graf ni profesa wa teolojia ya kimaudhui (systematic theology) katika Chuo Kikuu cha Waadventista River Plate na mhariri mwenza wa DavarLogos.

Kisa cha Sharath Babu Nakka 

NA PRATAP GOPALA RAO 

“Ni bora kuwasha mshumaa kuliko kulaani giza.” Kwa Sharath Babu Nakka, hii siyo tu istiari nzuri bali ni kanuni inayoongoza maisha yake ya ajabu.

 

Sharath Babu Nakka, profesa wa teolojia na utume katika Chuo Kikuu cha Waadventista wa Sabato cha Spicer, Pune, India, ameishi katika ulimwengu wa giza kamili kwa miaka hamsini na tano iliyopita, lakini hali hiyo haijamzuia wala kumpokonya shauku yake ya maisha. Badala yake, anaanza kila siku mpya kwa matumaini safi na furaha, huku tabasamu lake liking’aa usoni mwake. Bila shaka, yeye ni mmoja wa Wakristo wenye furaha na mtazamo chanya zaidi utakaowahi kukutana nao.

 

Katika ziara yangu ya hivi karibuni nchini India, nilimwona akitoka nje ya nyumba, akivuta hewa safi ya asubuhi na kutamka kwa furaha, “Ee, ni siku nzuri!” Ingawa hana uwezo wa kuona, anaona kwa uwazi zaidi kuliko wengi wetu wenye macho lakini tunashindwa kuthamini uzuri wa mazingira yanayotuzunguka. Zaburi 118:24 inafupisha mtazamo wake juu ya maisha: “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.” Siku hii. Si kesho. Siyo siku nyingine au wakati wa baadaye ambapo maisha yatakuwa mazuri na kamili tena. Bali ni leo, hata katikati ya changamoto na huzuni za maisha. Kwa Sharath Babu, furaha haiamuliwi na hali, bali inatokana na ahadi zisizoshindwa na uaminifu wa Mungu.

 

 

ILITOKEA GHAFLA

Sharath Babu alizaliwa na kukulia katika kijiji cha mbali cha Srirangapatnam, katika jimbo la Andhra Pradesh, kusini mwa India. Akiwa amezingirwa na mashamba ya mpunga yenye kijani kibichi na mitende ya nazi iliyochanuka, kijiji chenyewe kilikuwa na nyumba chache za matope zilizo na mapaa ya nyasi na barabara nyembamba za vumbi. Ni wachache, ikiwa wapo, waliokuwa na umeme au maji ya bomba.

 

Wengine wanaweza kujiuliza ni jambo gani jema lingeweza kutokea mahali kama hapo. Lakini kijana huyu alikuwa mwenye maono, na ndoto yake ya kuwa mwalimu wa shule ya sekondari wakati fulani ingempeleka katika shule ya bweni ya Waadventista wa Sabato huko Narsapur, umbali wa takribani kilomita 80 (maili 50) kutoka kijijini kwake. Huko alikuwa bora katika masomo. Aliyafurahia maisha, alipenda shule na alionyesha dalili za kuwa na mustakabali mzuri. Halafu, ghafla, ikatokea.

 

Bila onyo lolote, alishindwa kuona kabisa kwa macho yote mawili. Ghafla, aliingia katika ulimwengu wa giza lisilo na mwisho ambalo hajawahi kupona.

 

Akiwa ndiye mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne—na mvulana pekee—wa Subhakara Rao Nakka, mchungaji wa Kiadventista wa kijijini, na mke wake Kamalarathnam, Sharath Babu alikuwa fahari ya wazazi wake na tegemeo lao katika uzee wao (katika utamaduni wa Kihindi, mtoto wa kiume ana maana kubwa). “Nilikuwa na umri wa miaka 10 tu wakati huo, lakini bado nakumbuka kila kilichotokea siku ile,” anakumbuka. Anakumbuka hasa jinsi alivyowageukia wazazi wake waliokuwa wakihuzunika na akawasihi, “Tafadhali msilie. Mungu atanitunza.”

 

Madaktari wa kijiji walishindwa kuelewa kilichotokea na wakawashauri wampeleke Hospitali ya Kikristo ya Chuo cha Tiba huko Vellore, umbali wa kilomita 650 (takribani maili 400). Huko, baadhi ya madaktari bingwa wapasuaji wa macho nchini walimfanyia upasuaji Sharath Babu, huku baba yake akiwa nje ya chumba cha upasuaji, akiomba na kumlilia Mungu kwa ajili ya muujiza. Lakini ibilisi pia alikuwa pale, akimdhihaki: “Wewe si mchungaji, mtu wa maombi? Dini yako inakufaa nini sasa? Yuko wapi Mungu wako unapomhitaji? Unawezaje kuvumilia kuona mwanao akiwa kipofu, akihukumiwa kuishi maisha ya kuombaomba barabarani au katika vituo vya treni kijijini kwenu? Afadhali ungemuua na kufa pamoja naye.” Baba yake hakuhitaji kukumbushwa kuhusu hali duni ya wasioona, hasa katika sehemu kama India. Taifa hili lina idadi kubwa zaidi ya watu wasioona ulimwenguni. Wapo kila mahali, wakiomba sarafu chache au kipande cha mkate ili kujaza matumbo yao matupu.

 

Baba yake baadaye alikiri kwamba siku hiyo nusura ajitoe uhai, anakumbuka Sharath Babu. Lakini kwa mpango wa Mungu, alisikia sauti zingine siku hiyo—sauti tamu na za kupendeza zikija kutoka ukumbi wa mbali, ambako watendakazi na wagonjwa katika hospitali hiyo ya Kikristo walikuwa wakikusanyika kila asubuhi na jioni kuimba na kuomba pamoja. Walikuwa wakiimba kwa lugha ya Kitamil, lakini aliweza kufuatilia baadhi ya maneno: “Katika nyakati za majaribu na matatizo yako, Mungu atakuvusha salama.” Akitiwa moyo kutokana na ujumbe wa wimbo huo na imani isiyotetereka ya mwanawe kwa Mungu, baba yake alianza kuamini tena.

 

“Mpeleke nyumbani,” madaktari walisema. “Hakuna tunaloweza kufanya kurejesha uwezo wa kuona wa mwanao. Neva yake ya macho imeharibika kabisa; hili ni tukio baya zaidi kuwahi kushuhudiwa. Ni muujiza kwamba bado yuko hai.” Ndoto za utotoni za Sharath Babu, zilizokuwa zinaanza kuchanua, zilipokonywa kikatili. Kilichokuwa mbele yake ni jangwa la kukata tamaa na hali isiyo na tumaini.

MUNGU ALIFUNGUA NJIA

Sharath Babu alikaa nyumbani kwa miaka miwili iliyofuata, akiwa amezama katika ulimwengu uliokuwa na giza kuliko usiku wa siku elfu moja. Ingawa hakuwa na msaada wowote wa kibinadamu, hakukosa tumaini. Imani yake kwa Mungu ilikuwa thabiti. Na Mungu hakumwacha. Kwa mkono wa uongozi wa Mungu, alifikishwa kwenye shule ya Kikristo ya wasioona, haikuwa mbali sana na nyumbani. Shule hiyo ilikuwa ikiendeshwa na kundi la Kipentekoste. Kwa miaka mitano iliyofuata, shule hiyo ikawa nyumbani kwake. Huko alijifunza kusoma na kuandika kwa herufi za maandishi ya nukta nundu na kupata ujuzi wa msingi wa maisha.

 

Alipomaliza darasa la saba, tayari alikuwa na umri wa miaka kumi na nane. Lakini kwa sababu alikuwa mwanafunzi mzuri, aliruhusiwa kuruka madarasa mawili na kuingia moja kwa moja darasa la kumi. Mwaka huo, alifanya mtihani wa kitaifa wa cheti cha shule ya sekondari (kabla ya chuo) na kufaulu.

 

Chuo cha Spicer Memorial (sasa Chuo Kikuu cha Waadventista wa Sabato cha Spicer), chuo pekee cha Kiadventista nchini India wakati huo, kilikuwa ndicho kituo kilichofuata cha Sharath Babu. Kilikuwa umbali wa takribani kilomita 1,000 (zaidi ya maili 600) kutoka nyumbani na katika mazingira tofauti kabisa ya kitamaduni. Kujifunza kuishi bwenini hakukuwa rahisi. Alimtegemea kabisa mtu wa kumshika mkono na kumwongoza kutoka sehemu moja hadi nyingine—darasani, kanisani, maktaba, au kantini. Uongozi wa chuo ulimteua mwanafunzi wa mwaka wa mwisho kumsaidia kusoma masomo yake na kumwandalia kazi za nyumbani. Darasani, alitegemea kinasa sauti kurekodi mihadhara. Kufikia mwaka wa tatu, alikuwa amejua maandishi ya nukta nundu vya kutosha kuendelea sambamba na walimu wake. Punde madokezo yake ya mihadhara yalikuwa yamekamilika kiasi kwamba wanafunzi wenzake walimwendea wakitaka msaada wa masomo.

 

Kwa kuwa hakuwa na shughuli nyingi za nje ya darasa wala vivutio vya kumkatiza, alijikita kikamilifu kwenye masomo yake. Akiandikisha alama 19 kwa muhula na kuhudhuria vipindi vyote vya majira ya joto, Sharath Babu aliweza kukamilisha shahada ya kwanza ya dini katika muda wa miaka mitatu na nusu. Lakini hakuna mtu aliyekuwa tayari kumpa kazi. Hivyo, aliamua kuendelea na masomo ya uzamili katika chuo kikuu cha umma kilicho karibu. Lakini Mungu alikuwa na mipango mingine kwa ajili ya maisha yake. Katika mwaka huo huo, Chuo Kikuu cha Andrews kilianzisha shahada ya uzamili katika dini, ambayo ilitolewa kikamilifu katika kampasi ya Spicer. Sharath Babu alikuwa miongoni mwa wahitimu wa kwanza wa Spicer waliopata nafasi ya kujiunga na programu hiyo. Alimaliza masomo yake mnamo mwaka 1985, kwa kuandika kazi yake ya uzamili yenye kichwa: “Dhana ya Wokovu Katika Uhindu.” Kwa mara nyingine tena, hakupata kazi. Lakini, pasipo yeye kujua, Mungu alikuwa akifanya kazi kwa siri.

 

Juni 21, 1990, ni tarehe ambayo Sharath Babu hataweza kuisahau kamwe. Alisikia jina lake likitangazwa kupitia mfumo wa sauti wa chuo. Alipaswa kufika katika ofisi ya mkuu wa chuo. Alijua hilo lingeweza kumaanisha jambo moja tu—tatizo! Lakini hofu yake ilitoweka haraka. “Najua Mungu anao mpango kwa ajili ya maisha yako, Sharath Babu, lakini sijui ni upi,” alisema mkuu wa chuo, M.E. Cherian. “Wakati tukisubiri, ningependa kukupa kazi. Tumepoteza walimu kadhaa mwaka huu, na tunahitaji kujaza nafasi hizo. Kuanzia kesho, utakuwa ukifundisha katika Idara ya Dini.” Leo, miaka 34 baadaye, bado anafundisha hapo, na anafurahia kila dakika. Matukio ya mwisho, Danieli na Ufunuo, historia ya kanisa, fundisho la Sabato na Uhindu ni baadhi ya kozi anazopenda kufundisha.

 

 

MIUJIZA ILIYOONGEZEKA

Kulikuwa na tukio lingine lililobadilisha maisha ambalo lilitokea siku hiyo hiyo, Juni 21, 1990. Sharath Babu bado alikuwa katika hali ya kutoamini alipokuwa akitoka katika ofisi ya mkuu wa chuo—hakuwa ameomba kazi hiyo. Akiwa anamsubiri nje, dada yake Jeevana, ambaye wakati huo alikuwa akiishi katika bweni la wanawake na akichukua shahada ya uzamili katika Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Pune. “Subiri mpaka usikie kile ambacho ninataka kukusimulia, anna [maana yake kaka mkubwa],” alisema kwa furaha isiyoweza kufichika. “Nimepata mkazi mwenza chumbani.”

 

“Jina lake ni Sumathi.” Jeevana aliendelea. Alifiwa na wazazi wake akiwa msichana mdogo, lakini kupitia msaada wa kifedha wa Christian Children’s Fund na upendo wa wanandoa wa Kihindi, K.S.D. Charles na mkewe Seleina, aliweza kumaliza masomo yake ya sekondari na sasa anasomea uchumi wa nyumbani (home economics).” Kisha akatoa maneno ambayo yangebadilisha maisha ya Sharath Babu milele: “Sumathi amekuwa akikuangalia kwa muda; na anakupenda, anna.” Aliendelea dada yake, Jeevana. “Ikiwa mama na baba wako tayari kumpokea, anataka kuolewa nawe.”

 

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwamba mnamo Juni 21, 1991, mwaka mmoja kamili baadaye, Sharath Babu na Sumathi Kisku walifunga ndoa katika kijiji chake cha asili cha Srirangapatnam. Kwa siku kumi mfululizo kabla ya harusi, mvua kubwa za monsuni zilikuwa zimegeuza kijiji na maeneo yake ya jirani kuwa tope lisilopitika. Haikuwezekana kubadilisha tarehe ya harusi au kupanga mahali pengine. Kisha kwa muujiza (hakika ilikuwa ni mkono wa Mungu), siku moja kabla ya harusi, mvua ilisimama, na jua likawaka sana, likikausha njia za matope na kuziruhusu kupitika tena. Wageni wa kwanza kufika kwenye harusi walilazimika kuvuka maji yaliyowafikia magotini na kubeba miavuli—kwa sababu mvua bado ilikuwa inanyesha kwa nguvu katika miji na vijiji vya jirani. Srirangapatnam pekee ndiyo ilikuwa sehemu kavu kwa maili nyingi pande zote.

 

Wanandoa wapya walijenga maisha yao katika kampasi ya Chuo cha Spicer, ambako Sharath Babu alirejea kufundisha. Sumathi alifanya kazi katika ofisi ya mahudhurio na baadaye katika kituo cha Ellen G. White. Hatimaye, binti yao mpendwa, Seleina, alikuja kukamilisha familia yao ya watu watatu.

NDOTO ILIYOTIMIA NA MAONO YA BAADAYE

Mnamo mwaka 2007, kwa msaada na kutia moyo kwa mke wake, Sharath Babu alizindua huduma ya kimataifa. Ilianza na mkutano wa injili wa siku 21 jijini London, ambao ulipelekea watu 9 kubatizwa. Huo ulikuwa mwanzo wa safari nyingi zaidi kuelekea visiwa vya Uingereza. Mialiko ilianza kumiminika kutoka sehemu zingine za mbali: Monze, Zambia; Manado, Indonesia; Kisii, Kenya; Minneapolis, Minnesota, Marekani.

 

Janga la UVIKO-19 lilikuwa kizuizi cha muda, lakini tangu wakati huo, mialiko imeendelea kuongezeka; na sasa, akiwa na umri wa miaka 64, Sharath Babu hajaonyesha dalili zozote za kupunguza kasi. Kila mwaka, wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka na likizo za majira ya joto, yeye huwachukua wanafunzi na kuzunguka kote nchini akifanya mikutano ya uamsho—jambo ambalo amekuwa akilifanya tangu enzi za shahada yake ya kwanza. Zaidi ya hayo, kwa miaka kumi, kila Jumatatu, ameendelea kuonekana kwenye Good News Television Channel, iliyoko Hyderabad, India. Miaka mitatu iliyopita, Path to Salvation (kituo kingine kisicho cha Waadventista) kilimwalika kufanya kipindi cha kila siku juu ya unabii na matukio ya siku za mwisho. Pia, anaendelea kuwa mtangazaji wa mara kwa mara katika Hope India, tawi la Hope Channel International.

 

“Ndoto yangu ilikuwa kuwa mwalimu wa shule ya sekondari,” anasema Sharath Babu. “Leo mimi ni profesa wa chuo na seminari, nikifundisha wachungaji na walimu wa baadaye. Nilikuwa na umri wa miaka kumi wakati shetani alimdhihaki baba yangu kwamba nitakuwa ombaomba kipofu mitaani India. Miaka hamsini na mitano baadaye, bado ninaishi katika ulimwengu wa giza nene, lakini Mungu amenitumia kuangaza nuru ya utukufu na neema Yake katika sehemu zenye giza zaidi duniani. Kwake Yeye iwe heshima yote, na sifa zote.”

 

Nilipomuuliza chanzo cha nguvu zake na mtazamo wake mzuri wa maisha, alijibu haraka: “Ahadi nyingi zilizomo katika Biblia, hasa tumaini la kurejea kwa Kristo hivi karibuni, zinanisaidia kuweka mambo katika mtazamo sahihi. Mateso yangu ni ya muda mfupi tu; lakini maisha yatashika mkondo wake tena siku moja.”

 

Kwa furaha kubwa, anatazamia siku hiyo ambapo macho yake yatapata kuona tena—sio mashamba ya mpunga kijijini kwake, wala mitende ya nazi inayopigwa na upepo huku milima ikiwa mbali. Zaidi ya yote, anataka kwa shauku kutazama uso wa Mwokozi wake mpendwa, ambaye amekuwa rafiki yake mwaminifu kwa miaka yote hii.

 

“Baada ya hapo nataka kumwona mke wangu mpendwa, Sumathi,” alisema kwa sauti iliyojawa na hisia kali. “Tulikuwa tumeoana kwa miaka 29 (alifariki mwaka 2020 kutokana na kupasuka kwa mshipa wa damu katika ubongo), lakini sikuwahi kuona uso wake. Alijitoa kwa ajili yangu, akawa mikono yangu na miguu yangu—na hasa macho yangu—katika ulimwengu ambao ni giza na katili. Nina deni la kila kitu kwake.” Anatamani pia kumwona binti yake mpendwa, Seleina. “Nimekuwa nikijiuliza mara nyingi jinsi anavyoonekana. Yeye pia amejitoa sana kwa ajili yangu; na anaendelea kunitunza kwa upendo usioisha, uvumilivu na uaminifu wa hali ya juu.”

 

“Kama siyo upofu wangu,” Sharath Babu anatafakari, “huenda ningevutwa, kama wengi wengine, kuweka maslahi binafsi (nguvu, cheo, hadhi) mbele ya ufalme wa Mungu. Lakini sina ajenda yoyote kama hiyo. Shughuli Yake tu ndiyo ya kwangu.”

 

Baba yake Sharath Babu aliishi hadi umri wa miaka 80, na akashuhudia furaha ya mwanawe kuoa na kuwa baba, kuwekewa mikono katika huduma ya injili mnamo mwaka 2000, kutunukiwa shahada ya udaktari (D.Min.) kutoka katika Chuo Kikuu cha Andrews mwaka 2001, kupanda ngazi za taaluma hadi kufikia cheo cha profesa wa chuo na seminari, na hatimaye kuteuliwa kuwa profesa mshiriki, wa dini katika Chuo Kikuu cha Andrews, Michigan, Marekani. Ibilisi ni mwongo.

 

Huenda unapitia kipindi cha giza—talaka, ugonjwa hatari, changamoto za kifedha, kuvunjika moyo katika taaluma, au hata upofu wa kimwili. Labda umejikuta ukikabiliana na usiku unaoonekana kutoisha? Usikate tamaa. Mungu ambaye hafanya kazi wakati wa giza, Mungu ambaye hasinzii wala halali (Zab. 121:3, 4) yuko upande wako. Mungu yule yule anayeongoza mwezi katika mbingu—hata katika usiku wa giza—ameahidi kukuongoza kupita katika usiku wa giza lako.

 

Kisa cha Sharath Babu ni ushahidi chanya kwamba giza haliwezi kushinda wakati Mungu yuko upande wako.

Pratap Rao ni mweledi mstaafu wa maabara ya tiba, anayeishi Laurel, Maryland, Marekani.

Fundisho la patakatifu linaunganisha ujumbe wa Mungu wa nyakati za mwisho katika simulizi la ulimwengu mzima, linalounganisha mafundisho ya Mungu, uumbaji, chanzo cha dhambi, wokovu, kanisa na mambo ya mwisho, kwa lengo la kufichua, kupitia Kristo, upendo wa Mungu.

 

 

UKARIBU WA MUNGU 

Katika umilele, Mungu alifanya uamuzi wa kiwango kikubwa, kuishi ndani ya wakati na anga Aliyoumba kwa ajili ya viumbe Wake (linganisha Zab. 93:1-2, 5; Yer. 17:12). Anaishi ndani ya uumbaji usioweza kumdhibiti (1 Fal. 8:27; Yn. 1:1-3). Kujishusha kwa Mungu? Ndiyo. Kafara. Upendo wa Mungu wa kujitoa Mwenyewe ulimfanya kushuka na kuwa karibu na viumbe Wake. Viumbe wenye akili watafurahia ushirika na urafiki pamoja Naye, na kuwepo Kwake kulikobainishwa kutatoa mshikamano kwa historia ya ulimwengu.

 

 

UASI, AHADI NA HEKALU 

Matukio mawili yaliharibu uumbaji. Kwanza, kerubi alitamani kuwa kama Mungu katika makao ya mbinguni (Isa. 14:13-14), akianzisha mgogoro uliomfanya yeye na wafuasi wake kufukuzwa kutoka katika makao ya Mungu (linganisha Ufu. 12:7-8). Pili, wanadamu walijiunga na kerubi aliyeanguka (Mwa. 3:1-7), wakavunja uhusiano na Mungu. Lakini, ili kurejesha uhusiano huu, Mwana wa Mungu alichagua kushuka katika dunia yenye viumbe wenye dhambi (Yn. 1:14).

 

Kwanza, Mwokozi aliahidiwa kwa wanadamu (Mwa. 3:15, 21), ambaye kupitia Kwake wanaweza kufikia hekalu la mbinguni (linganisha Rum. 3:21-26; Ebr. 10:19-20). Pili, Mungu aliandamana na wanadamu kama msafiri mwenzao katika dunia yenye dhambi na mauti, akiendeleza matumaini kupitia sadaka ya kuteketezwa (Mwa. 8:20; 22:9-14). Tatu, Mungu aliunda taifa, Israeli, akalikabidhi ahadi ya Mwokozi (Mwa. 12:1-3), na akachagua kuishi katika maskani ya duniani iliyokuwa mfano wa hekalu la mbinguni (Kut. 25:8-9; 1 Fal. 8:29-30). Nne, hema takatifu lilikuwa mfano wa hekalu la mbinguni (Ebr. 8:5) na huduma ya ukuhani ilitangulia huduma ya Kristo (Ebr. 8:1-2). Mwaka uligawanywa katika huduma mbili—huduma ya kila siku ya upatanisho (Law. 17:11; Hes. 28:3-4) na huduma ya kila mwaka ya hukumu (Law. 16)—zikifanyika katika sehemu takatifu na takatifu zaidi za patakatifu kwa mtiririko huo, zikionyesha maendeleo katika mchakato wa upatanisho.

 

 

MASIHI NA HEKALU

 Kisha Mwokozi alishuka, Imanueli (Gal. 4:4; Mt. 1:23). Baada ya kupaa Kwake, historia ya ulimwengu iligawanyika katika vipindi viwili, kulingana na huduma ya ukuhani wa duniani. Danieli anaonyesha huduma ya Masihi katika hekalu la mbinguni ndani ya kipindi cha unabii cha siku 2,300. Sehemu ya kwanza ya unabii (majuma 70; Dan. 9:24-26) inatuelekeza kwenye ujio wa Masihi na kuanza kwa huduma Yake ya ukuhani (huduma ya kila siku) katika sehemu takatifu mnamo mwaka 31 B.K., ikihusisha matumizi ya faida za kafara Yake kwa waumini.

 

Sehemu ya pili inatambua mwaka 1844 (Dan. 8:14; linganisha na Ebr. 9:23) kama wakati ambapo Kristo anaanza siku ya upatanisho katika sehemu takatifu zaidi (linganisha Ufu. 11:10; 14:6-12). Huduma Yake kama Mhukumu inamaliza mgogoro wa ulimwengu (Dan. 7:9-10, 13-14, 21-22, 26; 12:1). Hukumu inatatua, kwanza, tatizo la dhambi duniani kupitia hukumu ya kabla ya ujio wa Kristo inayowathibitisha watu wa Mungu na kuhuisha kikamilifu kwao njia ya kufikia makao ya Mungu (Yohana 14:1-3). Pili, hukumu ya waovu inatatua tatizo la ulimwengu wenye dhambi. Wakiwa mbele ya Mwana-Kondoo, wataona dhabihu ya Kristo msalabani (Ufu. 14:10; 20:11-15) na watatambua kuwa, kama wenye dhambi wasiotubu, wanastahili kifo (linganisha Ufu. 6:15-17). Hukumu inahitimishwa na kutambuliwa kwa tabia ya upendo na haki ya Mungu (Fil. 2:9-11; Ufu. 5:11-13). Hatimaye, tutakuwa na njia ya kufikia kwa Mungu katika hekalu Lake la mbinguni, sasa lililoko kwenye sayari ya dunia (Ufu. 21:2-4).

Ángel Manuel Rodríguez, Th.D., ni mstaafu baada ya kuhudumu kama mchungaji, profesa, na mwanateolojia.

Njia inayoelekeza kwa afya bora 

Je, ni hatua gani za kuvunja tabia mbaya za kiafya na kuanzisha tabia njema?

Kuvunja tabia za zamani na kujenga mwenendo mpya wa kiafya kunahitaji mpango wa kimfumo na wa maombi. Hii inajumuisha kutambua hitaji la mabadiliko, kupanga kwa makini na kuwa na uthabiti wa makusudi. Zingatia hatua hizi ili kusaidia katika mabadiliko kutoka kwenye mifumo ya zamani hadi tabia bora za kiafya:

Tambua tabia na vichocheo vyake

 

Tambua tabia unayotaka kuacha. Fahamu namna inavyoathiri afya yako na kwa nini ni muhimu kuibadilisha.

 

Fahamu vichocheo visababishi, kama vile muda maalum, hisia, au mazingira. Kwa mfano, kula kupita kiasi kunaweza kusababishwa na msongo wa mawazo au kuchoka.

Weka malengo yaliyo wazi na yanayoweza kufikiwa

 

Weka malengo maalum, yanayoweza kupimika, yanayoweza kufikiwa, yanayohusiana na maisha yako, na yenye muda maalum (Set specific, measurable, achievable, relevant, and time-bound [SMART]).  Mfano: kuongeza mazoezi au kupunguza uzito.

 

Jikite katika tabia moja au mbili kwa wakati mmoja ili kuepuka kulemewa.

 

Badala ya kusema, “Nataka kula chakula chenye afya,” sema, “Nitakula aina tatu za mboga kila siku kwa mwezi ujao.”

Fahamu sababu yako 

 

Fikiria juu ya sababu za kina za mabadiliko. Kuunganisha malengo yako na maadili binafsi, kama vile kumheshimu Mungu Mwumbaji, kuwa na nguvu zaidi na kumtumikia Yeye, familia na wengine, kunaimarisha motisha.

Badilisha, usiondoe tu

 

Badala ya kuacha tabia mbaya bila mbadala, jenga tabia njema. Kwa mfano, badala ya vinywaji vyenye sukari, kunywa maji safi; ongeza kwa utaratibu matunda mabichi kwenye mlo wako.

Tengeneza mpango wa hatua kwa hatua

 

Gawanya mchakato katika hatua ndogo zinazoweza kudhibitiwa. Kwa mfano, ikiwa lengo lako ni kufanya mazoezi mara kwa mara, anza na matembezi ya dakika 10, kisha polepole ongeza muda na kiwango cha mazoezi. Andaa mavazi ya mazoezi mapema ili kupunguza visingizio.

Tumia vidokezo vya mazingira

 

Badilisha mazingira yako ili yaweze kusaidia tabia mpya. Ondoa vyakula visivyo vyenye afya nyumbani na weka vitafunwa vyenye lishe bora.

 

Tumia vidokezo vya kuona au vya sauti ili kukumbusha, kama vile kuweka viatu vya mazoezi ya kukimbia karibu na mlango au kuweka kengele ya simu.

Jenga uwajibikaji

 

Shiriki malengo yako na rafiki, mwanafamilia, au kikundi cha msaada. Hii huongeza motisha.

 

Fuatilia maendeleo yako kwenye daftari au programu maalum; sherehekea hatua ndogo za mafanikio.

Fanya kwa uthabiti

 

Kurudia tabia mpya kwa muda huimarisha mwelekeo mpya na kudhoofisha wa zamani. Watafiti wanapendekeza kuwa inachukua wastani wa siku 66 kuunda tabia mpya.

Kuwa na subira

 

Tegemea changamoto; zichukulie kama fursa za kujifunza. Tafakari na rejesha mikakati yako inapohitajika.

 

Lenga maendeleo badala ya ukamilifu.

Tuza mafanikio

 

Thibitisha tabia mpya kwa zawadi zisizo za chakula unapofanikisha hatua fulani, kama vile, kuhudhuria tamasha au kununua kitabu kipya.

Tafakari na urekebishe

 

Pitia maendeleo yako mara kwa mara na urekebishe malengo yako inavyohitajika.

 

Huenda ukahisi maamuzi yako ni dhaifu kama kamba za mchanga. Kuwa jasiri: “Kwa kutumia vizuri uwezo wa hiari, mabadiliko makubwa yanaweza kufanyika katika maisha yako. Kwa kukabidhi ridhaa yako kwa Kristo... utapata nguvu kutoka juu ya kukuweka imara.”¹

 

Kwa neema ya Mungu, unaweza kupiga hatua ya makusudi na kujenga mtindo wa maisha wenye afya na mabadiliko ya kudumu. Maranatha.²

1 Ellen G. White, Steps to Christ (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1892), uk. 48.
 

2 Huduma za Afya za Waadventista hutoa zana kwa wataalamu wa afya, wachungaji na wadau wa afya ili kusaidia mchakato wa mabadiliko ya tabia kwa wale wanaowahudumia kutumia mtazamo wa ushauri wa mtindo wa maisha. https://www.healthministries.com/lifestylecoaching/

Zeno L. Charles-Marcel, daktari bingwa aliyeidhinishwa na bodi, ni mkurugenzi wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu. Peter N. Landless, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa nyuklia na moyo kwa kutumia mbinu na dawa za nyuklia na mkurugenzi mstaafu wa Huduma za Afya za Waadventista wa Konferensi Kuu, pia ni daktari bingwa aliyeidhinishwa na bodi.

Zipo nyakati ambazo uvumba wa mbinguni hujaza moyo wako.

 

Yesu alipiga simu shuleni siku ya Alhamisi mchana. “Habari” alisema. “Mimi ni Yesu na nitakuja kanisani Sabato hii ili kushiriki ujumbe na kanisa”

 

Mwandishi mwendesha ofisi wa shule alipata hofu na akampigia simu mzee wa zamu. Mchungaji aliondoka kwa sababu ya mwisho wa juma. Mzee wa kanisa alimpigia Mchungaji, akamwambia kuhusu simu hiyo na akamuuliza nini cha kufanya.

 

“Uwe mkarimu Kwake,” alijibu Mchungaji Dale

 

Badala yake, walipata hofu, wakapiga simu katika ofisi ya konferensi na kisha kwa polisi wa eneo hilo. Siku ya Sabato asubuhi walikuwa tayari, wenye shauku ya Yesu kuja.

 

 

KUMPOKEA YESU

Yesu, akiwa amepooza baadhi ya sehemu na akitegemea magongo ya kutembelea ya aluminiamu, alifika ndani ya teksi na kuelekea milango ya mbele ya kanisa.

 

“Ndiyo, Mimi ni Yesu,” alitangaza. “Na ninao ujumbe”.

 

Kanisa walimfukuza.

 

Walimwambia Mchungaji Dale kilichotokea. “Ninafikiri ilikuwa ni kama vile kufukuzwa Nazareti,” Mchungaji Dale alinywea.

 

Jumanne, aliporudi nyumbani, Mchungaji Dale aligundua mahali Yesu alipokuwa akiishi, alimwomba Mzee wa kanisa ajiunge pamoja naye na kuenda kumtembelea.

 

Yesu alikuwa kijana mdogo, akiishi kwenye nyumba ndogo, moyo wake umejawa ukarimu na tumaini.

 

“Nilitaka kuliambia kanisa kwamba Mungu anawataka wajali watu wenye kuumia na wenye njaa,” Yesu alisema.

 

“Ni hayo tu.”

 

“Vipi kuhusu kwenda kanisani pamoja nami Sabato hii?” Mchungaji Dale alimwalika.” Utakuwa mgeni wangu.”

 

“Lo!” Yesu alijibu. “Ni miaka 40 sasa tangu nibatizwe pale, miaka 30 tangu mara ya mwisho kuwa ndani ya malango. Nitapenda kwenda pamoja nawe.”

 

Kwa hiyo ilipangwa, na Mchungaji Dale alianza kuandaa Sabato. “Mungu ameniambia kwamba mahubiri yatakuwa yanahusu Bartimayo kipofu aliyempazia Yesu sauti kando ya njia ya Yeriko, hususani ile sehemu ambayo Petro alimwambia ombaomba kipofu mwenye makelele kuwa “Nyamaza!” Mungu pia ameniambia kutakuwa na kupakwa mafuta wakati wa huduma.” 

 

Kupakwa mafuta kwa Angela. Yeye na Mume wake Gil ni wazawa wa Navajo kwa asilimia 100.

 

Angela alikuwa amempokea Yesu hivi karibuni, lakini alikuwa anapitia changamoto ya kutisha ya kiafya. “kwa hivyo nilimwomba Jeff, mmoja wa viongozi wa kanisani kwetu, kumpaka mafuta,” anaeleza Mchungaji Dale. “Ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya kitu chochote kama kile, Lakini alikubali, na nikaleta mafuta yangu maalum ya ubani.”

 

Mchungaji Dale alisimulia kisa cha Bartimayo kipofu akiwa na mgeni wake maalum, Yesu, alikaa kiti cha pembeni, gongo lake likimsubiria koridoni. Wakati Mchungaji Dale alipomwomba Yesu aungane na Angela na Jeff kwenda mbele pamoja naye, Yesu alisukuma gongo lake mbele, akiomba kimyakimya wakati wa kupakwa mafuta kwa Angela.

 

“Kuna kupaka mafuta kwingine ambako pia tunahitajika kufanya siku ya leo,” Mchungaji Dale aliongea na mkutano mzima. “Huyu mtu hapa ni rafiki yangu mpya. Jina lake ni Dennis, japo baadhi yenu mnaweza kumfahamu kwa jina la Yesu. Angela, utakuwa radhi kumpaka mafuta Dennis na kumwombea siku ya leo?” Angela alichukua mafuta na kudondosha, matone kadhaa juu ya Dennis.

 

“Lo! inanukia vizuri kuliko mafuta yangu ninayopaka baada ya kunyoa!” Dennis alisema kwa sauti. “Je, naweza kupata zaidi?”

 

“Mpatie yote anayotaka,” Mchungaji Dale alimwambia Angela. Angela Alimwagia nusu ya chupa kwenye mikono ya Dennis na Dennis kwa haraka alijipaka katika uso wake wote na alifikicha kwenye nywele zake. 

 

Dennis, sauti yake ikiwa imejaa machozi, alipiga kelele. “Lo! Hii ni nzuri sana!” Na mkutano ulijiunga na sherehe.

 

 

MAANDIKO KUWA HALISI

Baada ya mlo wa kushiriki chakula kilicholetwa na washiriki, Dennis alimwambia Mchungaji Dale na Angela kuhusu kuja kanisani Sabato iliyopita.

 

“Wakati najiandaa kuondoka nyumbani, Mungu aliniambia niweke fedha zangu zote kwenye pochi yangu. Sikufahamu ni kwa nini mpaka nilipokuwa ndani ya teksi na dereva alipoanza kuniambia kuhusu majaribu anayopitia. Familia yake ipo kwenye changamoto ya kifedha na watoto wake wanapata shida kukabiliana na hali hiyo. Maisha yake kwa kweli ni magumu!”

 

Dennis aliguswa sana na kisa cha dereva teksi hivyo alifungua pochi yake na akampatia dereva fedha zote ambazo Mungu alimwambia kubeba. “Kwa ajili yako,” alisema. “Kutoka kwa Yesu”

 

Dennis alipokuwa akisimulia kisa cha fedha, kumbukumbu za Mchungaji Dale zilikwenda kwenye siku Yesu alipomwona mwanamke mjane akitoa sarafu zake mbili za mwisho kwenye hazina ya hekalu. “Ilikuwa ni kama maandiko yanatimia hapa kwenye mji wetu mdogo!”

 

Usiku wa Sabato Angela alimleta Mume wake Gil, kwenye “Underground Oasis,”  mkutano wa jioni ambao Mchungaji Dale aliongoza, ndani ya ghala la zamani mjini. Gil hakuwa amempokea Yesu na alikuwa anapambana na pepo waliokuwa wanafanya maisha yake yawe mabaya duniani. Pepo walishambulia katikati ya mkutano, na Mke wa Mchungaji Dale, Simona alitembea kuelekea kwa Gil na akawaamuru pepo “kumtoka sasa hivi!” 

 

Pepo walitii.

 

Gil, akiwa mtupu na mwenye shauku ya kujazwa, alimwomba Yesu kuingia maishani mwake na aliomba kubatizwa! Kila mmoja alishangilia. “Ilikuwa ni kama vile pepo walivyotolewa kwa Mgerasi mtu wa mwituni” 

 

Baada ya sherehe kutulia kidogo, Lakini wakati mkutano ulikuwa bado unaendelea, mmoja wa wageni, mtu mkubwa sana, alimuuliza Mchungaji Dale kama wanaweza kuzungumza. Wawili hao walisogea upande wa chumbani.

 

“Jina langu ni Eric,” alisema mtu huyo. “Mimi ni mzaliwa wa Eskimo kwa asilimia 100 kutoka Alasaka lakini sasa hivi mimi ninaendesha teksi hapa mjini. Ninapata ahueni kutoka kwenye mambo mengi na maisha yamekuwa magumu kweli. Baadhi ya watu hawana raha na Mwalaska mnene kama mimi. Halafu majuma kadhaa yaliyopita, mtu anayeitwa Dennis alinikodisha nimpeleke kwenye kanisa la Waadventista wa Sabato Jumamosi asubuhi. Alikuwa ni mzee mwema sana ambaye alihitaji moja ya magongo ya chuma yaliyojikunja kwa ajili ya kuegemea. Ni mtu mkarimu sana. Ndani ya teksi aliuliza kuhusu familia yangu, na ijapokuwa kwa kawaida huwa simwambii yeyote kuhusu familia yangu, kitu fulani kilinifanya nimwambie Dennis kila kitu. Nilimwambia kuhusu watoto wangu, matatizo yetu ya kifedha na ugonjwa wa mke wangu, na vile tulikuwa tukiishi kwa shida.”

 

Mchungaji Dale alisikiliza kwa kuduwaa. kwa namna ya kushangaza Mungu alivyokuwa akiunganisha visa vingi kwa pamoja.

 

“Wakati tupo kwenye teksi,” Eric aliendelea. “Dennis alitoa pochi yake na kunipatia bunda kubwa la noti za fedha. Akasema ni kwa ajili yangu, kutoka kwa Yesu. Niliipokea, Lakini nilikosa raha kwa kweli. Ilikuwa ni fedha nyingi. Dola 1700 kamili! Kiuhalisia, sikuwa huru sana kwamba sijawahi kutumia fedha kama hiyo kwa ajili yangu au familia yangu. Dennis ameshanipigia mara nyingi na kuniuliza kama niko radhi kwenda sokoni na kununua baadhi ya vyakula, na kwenye duka la vifaa vya ujenzi na kununua baadhi ya vitu alivyokuwa anahitaji. Siku zote alikuwa akinipatia fedha zaidi, lakini nilikataa, na badala yake nilitumia zile fedha alizonipatia. Nimetumia mamia kadhaa ya dola ya zawadi za fedha zake kumnunulia vitu Dennis.”

 

Mchungaji Dale alianza kuuliza swali, lakini aliacha wakati Eric alisukuma mfuko mdogo  kwenda kwake.

 

“Mchungaji, hii ni fedha ambayo Dennis alinipatia. Nimetumia mamia ya dola zake, lakini dola 1700 zote bado zipo humu kwenye mfuko! Hii inawezekanaje? Nimeamua kuwa hii ni fedha ya Mungu na kwamba ninahitaji kumrudishia Dennis. Unafikiri hiyo itakuwa sawa?”

 

Mchungaji Dale alitabasamu, akimtafakari mwanamke mjane na mwanawe katika mji mdogo wa Sarepta.

Dick Duerksen, Mchungaji na msimuliaji, anaishi Portland, Oregon, Marekani.

Sauti ya muziki wa baragumu ulioimbwa katika lugha ya kigeni ilinivutia kama ambavyo hali ya hewa ya joto ya kitropiki ilivyonivutia nilipokuwa nikiondoka uwanja wa ndege. Jipu (aina ya gari) kubwa lililong’aa lenye michoro ya michubuko ndani na nje kandokando ya gari aina ya Mercedes na BMW wakati tukielekea katika jiji la Manila nchini Ufilipino. Baiskeli iliyofungwa mapipa saba yenye ujazo wa galoni 45 yaliyokuwa tupu iliserereka katika barabara iliyopo upande wa pili kwenye mtaa uliokuwa na watu wengi. Katika kituo cha kwanza, tulisikia harufu ya nguruwe kabla hata hatujawaona. Lori lenye sehemu tatu za juu lililojazwa nguruwe waliokuwa wakilia kwa sauti lilitoka katika kituo cha gesi. Nyuma ya lori hilo, kulikuwa na bango lililoandikwa “Mungu Utubariki.” 

 

Baadaye, kikundi chetu cha utume kilisubiri feri kwa muda mrefu kidogo tukiwa tumeketi kwenye madawati. Giza lilipokaribia kuingia, hatimaye tulipanda mashua, licha ya maji kuwa na mawimbi makali. Papo hapo nililala usingizi. Baada ya kusafiri kwa mashua, tulikuwa bado na safari ya gari mwendo wa saa mbili. Mwisho, baada ya saa 36 za safari, tulifika “Glair Inland Resort,” makazi yetu kwa majuma mawili yaliyofuata. Jina hili lilitukaribisha vyema, na kwa hakika nilijiandaa kuburudika katika mahali pa matembezi. Lakini uhalisia ulikuwa tofauti. Mimi na mume wangu tulipangwa kwenye chumba kidogo kilichokuwa na meza ndogo na kitanda chenye shuka moja nyembamba na blanketi. Asubuhi, tuliamshwa na msururu wa mchwa wengi waliokuwa wakitembea ndani ya chumba kile. Tulitumia bafu moja na watu wengine watano. Bomba la maji lilikuwa ama likifungwa au kufunguliwa. Lilipofunguliwa, matone yalitoka kwa nguvu na ungeweza kuhisi kwamba yangeondoa ngozi yako! Maji yalikuwa ni ya baridi kila wakati, na mahali hapo hawakuweka taulo.

 

Nilipotoka nje, hata hivyo, wakati jua kali la kitropiki liliangazia miti ya nazi na kumetameta juu ya uso wa mabwawa yaliyozungukwa na maua mazuri, ulimwengu ulianza kuvutia. Na tulipopata kifungua kinywa cha maembe, nanasi na vyakula vingine vya kitropiki, niliamua kuwa ningeweza kutumika!

 

Nilikuwa sehemu ya kikundi cha wainjilisti kilichotengeneza vituo 22 vya injili kwa wakati mmoja katika vijiji tofauti tofauti. Wote tuliishi pamoja katika kituo kikuu. Kila mchana, gari kubwa lililochorwa kwa rangi nzuri lilitusafirisha na kutupeleka katika vijiji mbalimbali, mahali ambapo tulifanya mikutano ya injili tukisaidiana na waumini wa kanisa mahalia. Kwa haraka nilivutiwa na watu wenye furaha na utamaduni rahisi. Jambo la kusisimua zaidi ilikuwa ni fursa ya kutoa mafunzo ya afya na kushiriki uinjilisti katika kijiji jirani. 

 

Jioni moja, chura alirukaruka akipita dawati nilipokuwa nimeketi, na siku nyingine mbwa alijiunga nasi kanisani. Wadudu walijaa kuzizunguka taa na kufunika maonyesho ya kompyuta. Mara nyingi, tuliwafagia mbele ya kitambaa cha maonyesho. Mara mbili, mfumo wa vipaza sauti uliacha kufanya kazi, na mara nyingi hakukuwa na umeme, hivyo tulitumia jenereta. Chumba cha jenereta kilikuwa katika banda la nje, jenereta lilifanya chumba hicho kuwa na kelele.

 

Kikundi cha wasichana wachache walipenda kunifuata kila nilipokwenda, wakichungulia kupitia nyufa zilizokuwa katika kuta za jengo huku wakichekacheka. Kuendesha pikipiki gizani bila kuwa na taa za mbele iliongeza ujasiri!

 

Katika Sabato yetu ya mwisho pale kijijini, nilikutana na Alrene. Kwa aibu, aliniambia, “majuma machache yaliyopita, nilikuwa nimelala katika chumba changu bwenini nilipokuona wewe na mume wako katika njozi.” Wakati huo huo, rafiki yake alimpigia simu na kumwamsha. Rafiki yake alimpigia simu ili kumwalika katika mikutano yetu. Alipohudhuria, alitukumbuka katika ndoto yake.

 

Mtu mwingine aliota kwamba amemwona Yesu. Siku iliyofuata, alipita katika kanisa ambalo mikutano yetu ingefanyika na kuona bango lenye picha ya Yesu lililokuwa likitangaza mikutano yetu. “Ilikuwa ni picha ile ile niliyoiona kwenye ndoto yangu!” alisema. Akaanza mafundisho ya Biblia, na pale tu mikutano yetu ilipoanza, alihudhuria. Ni jambo la kustaajabisha kuona kwamba Mungu bado anatuma ujumbe kwa watu!

 

Tulisafiri kwenda baharini katika juma la mwisho kwa ajili ya ubatizo. Tulijiunga na msafara mrefu wa magari, baiskeli zenye magurudumu matatu, magari makubwa, na pikipiki nyingi. Maelfu ya watu kutoka katika vituo vyote 22 vya mikutano walijumuika nasi na watu 1,176 walibatizwa ndani ya dakika 45 tu.

 

Nimeona kwa mara ya kwanza namna Mungu anavyoweza kutumia ndoto kumwongoza mtu kuja Kwake. Lakini ninafurahi sana kwani Mungu hutoa nafasi katika taharuki. Nimepata shangwe kuu kuwepo mahali ambapo Roho wa Mungu hufanya kazi. Ukipata nafasi yoyote kwenda katika safari ya utume, usikatae! Nenda! Kama huwezi kusafiri umbali mrefu, nakualika kushiriki imani yako kwa jamii yako!  Jihusishe katika mpango wa kuwafikia wengine kanisani kwako, mweleze mtu mmoja habari za Yesu, au mwalike rafiki kanisani. Kuwa sehemu ya ujasiri huu. Daima utapata thawabu.

* Nukuu za Maandiko zilizoashiriwa kama SUVB ni kutoka kwa Swahili Union Version Bible. Haki zote zimehifadhiwa.

Janice Schmidt ni mke wa mchungaji, anayewafundisha watoto wake wanne nyumbani na kufanya kazi kama mhakiki katika jimbo la Indiana, Marekani.

Mchapishaji
Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review
Justin Kim

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa
Hong, Myung Kwan

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World 
Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun, Dong Jin Lyu

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review
Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani
Enno Müller, Beth Thomas, Jonathan Walter 



Wahariri waliopo Seoul Korea


Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali
Gabriel Begle

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi
Daniel Bruneau

Meneja wa Shughuli
Merle Poirier

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri
Marvene Thorpe-Baptiste

Wahariri/Washauri wengine
E. Edward Zinke

Meneja wa Fedha
Kimberly Brown

Mratibu wa Usambazaji
Sharon Tennyson

Bodi ya Utawala
Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong, Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Joel Tompkins; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

Maelekezo ya Usanifu na Muundo
Types & Symbols

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:
Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

Tafsiri
Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

Msomaji wa prufu
Lilian Mweresa

Usanifu wa toleo la Kiswahili
Daniella Ingram, Ashleigh Morton, Teya Esterhuizen, Digital Publications

Uchapishaji wa Kidijitali
Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu
Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott
/Types & Symbols

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org Tovuti: www.adventistworld.org

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

Vol. 21, Na. 2

swipe down
powered by
SEND-IT.ME

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Please wait ...