ENDELEA KUPOKEA ADVENTIST WORLD KISWAHILI

Tunawathamini na kuwatambua wote waliojisajili na tuna taarifa mpya na za kusisimua kuhusu jinsi mnaweza kuendelea kusoma na kupata Adventist World.

KULIPATA KWENYE WHATSAPP

Kwa sababu ya umaarufu wa kulipata jarida hilo kwenye WhatsApp, tunahamia kwenye mfumo mpya wa kutangaza ambao utatuwezesha kuwasiliana nanyi mara kwa mara. Bonyeza kiungo kilicho hapo chini kujiunga na chaneli ya WhatsApp Broadcast ambapo tutakujulisha toleo jipya linapokuwepo.

KULIPATA KWENYE TOVUTI

Lipate jarida hilo kwenye tovuti yetu, kwa kukibonyeza kiungo kilicho hapo chini:

Tovuti hiyo vilevile inabeba Adventist World kwa lugha anuwai.

KULIPATA KWENYE FACEBOOK

Kiungo cha toleo la hivi karibuni la Adventist World huwekwa kwenye Ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi. Kwa “Liking” ukurasa huu utapokea taarifa zetu mpya na kuweza kututumia jumbe ukiwa na majibu yoyote.

HIFADHI MAKTABA YA JARIDA LA KISWAHILI KWENYE SIMU YAKO AU KOMPYUTA

Tumetengeneza maktaba ya kidijitali ya majarida yote ya Adventist World. Ili kulipata kusanyo hili kwa urahisi kwenye simu yako, fuata hatua zilizo hapo chini:

 

Bonyeza kiungo kilicho hapo chini ili kuipata maktaba.

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 

AU

Fuata maagizo hayo kuiweka maktaba hiyo kwenye simu yako au kompyuta.

 


Kwa maoni yoyote au majibu, tafadhali jiskie huru kututumia barua pepe kwenye kwambokaj@ecd.adventist.org. Tunapenda kusikia kutoka kwako na tunatazamia uhusiano mzuri na wasomaji wetu wa Adventist World-Kiswahili.

Asante sana na Mungu awabariki,
Timu ya Adventist World-Kiswahili

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa kwambokaj@ecd.adventist.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

Picha ya jalada: Kevin Carden / Lightstock

Barua ya Hesabu

Na Justin Kim

Hatuna uhakika sana hadi pale takwimu rasmi za makanisa yetu zitakapotoka mwaka huu, lakini wengine wanakadiria kwamba tunaweza kuwa na idadi ya Waadventista milioni 24 ulimwenguni kote katika mwaka wa 2025. Kwa harakati iliyoanzishwa mwaka 1844 na shirika lililoundwa mwaka 1863, idadi hiyo si mbaya.

 

Watu milioni ishirini na nne ni safari ndefu kutoka kwa waumini wachache wa wana marejeo zaidi ya miaka 160 iliyopita. Lakini kwa mwaka 2025 idadi hiyo bado ni ndogo zaidi ikilinganishwa na idadi ya watu wa kisiwa cha Taiwan na Sri Lanka.1 Au labda mji mmoja: Dhaka, Bangladesh.2 Japo tunaweza kuridhishwa na idadi ya watu milioni 24, ofisi inayohifadhi nyaraka, takwimu na tafiti, hivi karibuni imegundua kwamba tangu mwaka 1965 tumebatiza Waadventista milioni 45! Tangu hapo, watu milioni 19.3 kwa bahati mbaya walichagua kuliacha kanisa.3 Takwimu makini na kwa kweli ni fursa zilipotezwa!

 

Je, vipi kuhusu takwimu za Ukristo kwa ujumla? Ukristo, pamoja na madhehebu yake mengi, unadaiwa kuwa na watu bilioni 2.38.Kati ya watu bilioni 8.2 waliopo ulimwenguni, Wakristo wana asilimia kama 29 tu ulimwenguni, wakati Waadventista wakiwa na asilimia .29. Ongeza katika hesabu hii ukweli kwamba idadi ya watu ulimwenguni inaongezeka kwa idadi ya watu milioni 83 kila mwaka.5 Kwa makadirio haya, ni kwa namna gani Wakristo watazifikia roho bilioni 5.82 zilizosalia? Inawezekanaje kwa Waadventista kushiriki ujumbe wa marejeo kwa roho 8.176 bilioni zilizosalia?

 

Bila shaka, nguvu isiyo ya kiulimwengu, kuingilia kati kwa Roho Mtakatifu kutakamilisha kazi kwa kiwango kikubwa. Je, tukae tu pembeni bila kujihusisha tukitazama roho bilioni zikiangamia au tufanye kazi pamoja na Yule ambaye anaweza kuokoa roho trilioni?

 

Ellen White anaonya, “Kutokujali kwa kushangaza kuhusu wokovu wa roho kunaonekana kuwakamata wengi wanaodai kuwa Wakristo. Wadhambi wanaweza kuangamia wakiwa katikati yao na hawajihisi kuwa na mzigo wowote katika jambo hili. Je, Kristo atawaambia hawa wasiojali, ‘Vema mtumwa mwema na mwaminifu; ingia katika furaha ya Bwana wako?’ Furaha ya Kristo inathibitika katika kuziona roho zikiokolewa kupitia kafara aliyoifanya kwa ajili ya roho hizo.”6 

 

Na tuombe. Si kwa ajili ya watu bilioni 8, bilioni 19, 7,000, au watu 50 wanaobadilika. Hebu na tuombe kwa ajili ya uzoefu wetu kwa Yesu kwa kila mmoja, kisha kwa ajili ya mzigo huu mahsusi wa kuifikia roho moja kila saa.

1  Takwimu ya ulimwengu, “Nchi za ulimwengu mzima kwa idadi (2025),” https://www.worldometers.info/world-population/population-by-country/, ilisomwa Feb. 18, 2025.

 

2   Kumbukumbu za idadi ya watu ulimwenguni, “Idadi ya watu katika miji mikubwa 2024,” https://worldpopulationreview.com/cities, ilisomwa Feb. 18, 2025.

 

3    Tor Tjeransen, “Kanisa la Waadventista likiwakaribisha watu Millioni 1.4 Washiriki Wapya mwaka 2023,” Nov. 6, 2024, https://adventistreview.org/news/adventist-church-welcomes-1-4-million-new-members-in-2023/, ilisomwa Feb. 18, 2025.

 

4    Kumbukumbu za idadi ya watu ulimwenguni, “Katika nchi za Kikristo 2024,” https://worldpopulationreview.com/country-rankings/most-christian-countries, ilisomwa Feb. 18, 2025.

 

5  Baraza la Uchumi ulimwenguni, “kweli 11 kuhusu mabadiliko ya idadi ya watu ulimwenguni,” July 4, 2017, https://www.weforum.org/stories/2017/07/11-facts-about-world-population/, ilisomwa Feb. 18, 2025.

 

6  Ellen G. White, Fundamentals of Christian Education (Nashville:  Southern Pub. Assn., 1923), uk. 51.

Picha: Otieno Mkandawire

Jongimpi na Nomthandazo Papu, wakurugenzi wa huduma za familia wa Divisheni ya Kusini mwa Afrika – Bahari ya Hindi, wakizungumza wakati wa mkutano wa ndoa wa “Pamoja kwa Umilele” uliofanyika Durban, Afrika Kusini, kuanzia Desemba 4 hadi 7, 2024. Jumla ya wanandoa 520 walihudhuria tukio hilo la uzinduzi.

“Tunaweza kumtukuza Mungu kwa jinsi alivyofanya kazi pamoja nasi na kupitia kwetu. Tukio hili muhimu halihusiani tu na idadi. Linaonyesha maisha ya watu wengi yaliyoguswa, kuponywa, na kubadilishwa kupitia habari njema ya wokovu. Wateja wetu wa mtandaoni wanawakilisha watu ambao si tu watazamaji wa mambo ya kufurahisha, bali hutafuta muunganiko wa kina wa kiroho.” 

– Catherine Ontita, mkurugenzi wa Hope Channel Kenya, kuhusu ushindi wa wafuatiliaji 100,000 katika ukurasa wao wa YouTube. Ontita anayahusisha mafanikio hayo na utendaji wa Roho Mtakatifu na kujitoa kwa kikosi cha Uzalishaji.

Urafiki Nje ya Kanisa

Washiriki wa kanisa kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni walipiga kura zinazoonyesha ikiwa wanatumia muda wao kutengeneza urafiki na watu walio nje ya kanisa la Waadventista. 

Zaidi ya 100

Idadi ya wanafunzi wanaouza vitabu wanaoshiriki katika kugawa tumaini kupitia maandiko ya Kikristo katika miji mbali mbali katika mji mzima wa Uruguay. Kama matokeo ya moja kwa moja ya kazi yao, watu 97 tayari wameanza kujifunza Biblia. Uinjilisti wa vitabu kwa wanafunzi si tu fursa ya kukua kiroho na kukuza utume, bali pia unawasaidia kulipa ada zao wanaposhiriki ujumbe wa matumaini.

“Mwaka huu katika mkutano wa kila mwaka wa viongozi wetu, tuliamua kukutana Peru kujenga kanisa. Tulihitaji kuwaonyesha [viongozi wetu] hitaji hili, lakini pia tulihitaji kuwaonyesha visa vya mafanikio ya Union ya Kusini mwa Peru.” 

– Kenneth Denslow, mwenyekiti wa Lake Union Conference (LUC), kuhusu safari iliyojumuisha viongozi wa LUC. Wana kikosi walijiunga katika mpango wa kimataifa wa kujitolea wa Maranatha (Maranatha Volunteers Internationa project) kusini mwa Peru na kufanya kazi pamoja ili kujenga kanisa kwa ajili ya waumini wa Chillca. Mpango huu ulikuwa sehemu ya miisho ya umoja wa union ya Peru kusini, iliyoitwa Project Amigo.

“Tunaamini kuwa mradi huu utasaidia utafiti uliolenga kutatua matatizo mbali mbali ya kiafya katika jamii.”

—Ademola Tayo, mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Babcock, kuhusu sherehe kwa ajili ya Shule ya Famasia ya Dame Caroline Kessington Adebutu. Jengo jipya kwa ajili ya Shule ya Famasia linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu. Mradi wa ujenzi unaendana na wito wa shule wa kutoa elimu yenye ubora wa juu na mafunzo katika kutunza afya, hatimaye kusaidia maendeleo ya sekta ya afya nchini Nigeria.

 “Aina hii ya mafunzo ya ustawi wa jamii imekuja katika wakati mwafaka ambapo mashauri kuhusu afya ya akili yana umuhimu zaidi kuliko hapo awali. Kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Newbold, tunachukua hatua ya kufanya kazi ya kuandaa viongozi watakaowasilisha kwa usahihi mahitaji ya ustawi wa akili, wakionyesha tofauti dhahiri katika maisha ya vijana.” 

– Marcel Ghioalda, mkurugenzi wa vijana katika divisheni ya Ulaya, kuhusu tukio la mafunzo lililofanyika Newbold katika kitivo cha Elimu ya juu. Tukio hili liliongozwa na maprofesa mbali mbali kutoka katika Chuo Kikuu cha Loma Linda, lililoandaliwa ili kukuza ujuzi wa ufanisi wa ustawi na kuazimia kupunguza dalili za msongo wa muda mrefu, majeraha ya nafsi, na kupoteza.

Zaidi ya 100

Idadi ya wahasibu na wanateknolojia kutoka katika nchi zote za Divisheni ya Amerika-Kati, waliokutana kwa ajili ya Mkutano wa Kukuza Mipaka ya Teknolojia ambao ulilenga mkakati mpya wa kidijitali wa utume. Mkutano huu ulikusudia kuunganisha wahasibu wa union na wataalamu wa vifaa vya kielektroniki wa makanisa ulimwenguni kuanzisha na kuiweka teknolojia kama msaidizi mwenye nguvu katika kuendeleza utume wa kanisa. Tukio hili lilikamilishwa na wito wa kufanya kazi kwa bidii na kuanzisha mambo 

Mafunzo huunganisha maendeleo ya kiroho pamoja na mwelekeo mpana wa kiutamaduni.

Tracey Bridcutt, Adventist Record

Timu ya Catalyst kutoka Taasisi ya Divisheni ya Pasifiki Kusini (SPD) hivi karibuni iliendesha programu shadidi ya mafunzo katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha Fulton huko Fiji, ikiwaandaa vijana 55 kwa ajili ya mwaka wa huduma ya umishonari nchini Indonesia.

 

Wamishonari hawa vijana wanapojiandaa kuanza safari yao, programu hiyo ya mafunzo ya majuma mawili imeundwa ili kuwawekea msingi wa kiroho na kuwaandaa kimishonari kwa ajili ya mwaka wao wa mabadiliko wa huduma, waandaaji walisema.

Timu ya Catalyst, ikiongozwa na Gilbert Cangy, inaambatana na David na Carol Tasker; Mkurugenzi mwenza wa SPD wa huduma na mipango Nick Kross; Nicholas Kross; Eliki Kenivale; Carol Boehm msaidizi wa meneja na huduma za utume; na viongozi wa utume kutoka Indonesia.

 

“Wamishonari walio mafunzoni wanaongozwa katika ufahamu wa kina zaidi wa asili ya ufalme wa Mungu na uzoefu pamoja na Roho Mtakatifu wanapofundishwa kukuza tabia za kiroho zinazobadilisha maisha,” Cangy alisema.

 

Mafunzo hayo yanajumuisha maendeleo ya kiroho pamoja na mwelekeo mpana wa kiutamaduni kwa Indonesia, nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu. Wamishonari wanajifunza stadi zinazofaa kwa ajili ya utumishi wao, huku wakikazia sana njia za Kristo za huduma: kuchangamana na watu, kuonyesha huruma, kutimiza mahitaji yao, na kupata imani yao kabla ya kuwaalika wamfuate Yesu. Vipengele muhimu vya mafunzo ni pamoja na kushiriki shuhuda binafsi, kuendesha mafundisho ya Biblia, na kuongoza vikundi vidogo vya kimishonari.

 

Mwenyekiti wa Unioni Misheni ya Pasifiki (TPUM) Maveni Kaufononga, katibu wa wachungaji Linray Tutuo, pamoja na timu yao wako katika eneo la tukio ili kusimamia na kuihamasisha timu.

 

Kaufononga alionyesha heshima kubwa kwa wamishonari, akibainisha kwamba washiriki 50 wanatoka TPUM, na wengine watano kutoka Unioni Misheni ya Papua New Guinea.

 

“Tunaamini watakuwa tayari kwenda kabla ya mwisho wa mwezi huu [Februari],” Kaufononga alisema. “Viongozi kutoka Unioni Misheni ya Indonesia Magharibi wapo hapa, wakifanya kazi katika majukumu yao waliyopewa. Wengine watahudumu mashuleni, wengine katika makanisa mahalia, huduma za vyombo vya habari, na uanzishaji wa makanisa. Maelezo ya mwisho bado yanafanyiwa kazi.”

 

Mafunzo hayo yanapata maoni chanya kutoka kwa washiriki. “Ninapenda mbinu kamili za mafunzo ambazo zimejenga msingi wake katika kanuni za kibiblia,” mmoja wao alisema. “Sehemu bora zaidi kwangu ni furaha ya kuwa sehemu ya jamii inayohusika katika kujifunza Neno la Mungu pamoja,” mwingine aliongeza. “Kama mmishonari, sasa ninaelewa umuhimu wa kujua kuhusu mitazamo tofauti ya ulimwengu na marekebisho yanayohitajika tunapohamia katika mtazamo mpya,” wa tatu alieleza.

 

Mpango huu unafungamana na mkakati wa Kulenga Utume wa Konferensi Kuu, unaolenga kufufua dhamira ya Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa ufikiaji wa ulimwengu mzima na uinjilisti. SPD imeanzisha ushirikiano na Divisheni ya Kusini mwa Asia-Pasifiki (SSD) ili kusaidia na kuhimiza jitihada zao za utume. Indonesia ni mojawapo ya nchi 11 za SSD.

 

 

KUHUSU CATALYST 

Catalyst ni majuma 12 yaliyojikita kwenye stadi za uzoefu wa uanafunzi yanayoratibiwa mara kwa mara katika kampasi ya Chuo Kikuu cha Avondale nchini Australia na sasa katika vyuo vingine. Kwa mujibu wa waanzilishi wake, programu hiyo inaweza kuwaongoza vijana kufahamu binafsi uwepo wa Yesu unaobadilisha, kukua katika ujuzi wa Neno Lake na mapenzi yake kwa ajili ya maisha yako. Na kuwaandaa kwenda, katika jina Lake na katika nguvu za Roho Mtakatifu, kuwa wafanya-wanafunzi na kuleta mabadiliko katika jamii yao mahalia.

Tukio la Warsaw liliunganisha imani mbalimbali dhidi ya vurugu, ubaguzi, na kifo. 

Daniel Kluska, Unioni Konferensi ya Poland

Kama ilivyo kila mwaka mwezi Januari 27, siku ya ukombozi wa Auschwitz-Birkenau, kambi maarufu ya mateka wa vita na maangamizi ya Nazi (1940-1945), ukumbusho wa Siku ya Kumbukumbu ya Mauaji Makubwa ulifanyika huko Warsaw kwenye mnara wa Mashujaa wa Maeneo Yaliyotengwa ya Warsaw.

 

Wawakilishi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Poland, waliowakilishwa na mwenyekiti wa Unioni Konferensi ya Poland (PUC) Jarosław Dzięgielewski na mkurugenzi wa shughuli za umma na uhuru wa dini Andrzej Siciński, kwa mara nyingine walishiriki katika sherehe hiyo.

 

Hotuba za ukumbusho zilifuatiwa na maombi ya viongozi waalikwa wa mashirika mbalimbali ya kidini, likiwemo Kanisa la Waadventista.

 

Siciński aliomba:

Bwana Mungu,

“Usiue” yako rahisi ilikiukwa zaidi ya mara milioni moja huko Auschwitz-Birkenau. Mbele ya macho yetu, historia inaonekana kujirudia, ingawa bado haijawa katika namna ya kutisha.

 

Kwa hiyo, tunakuomba, Mungu, tuwe na ujasiri wa kusema HAPANA tunaposukumwa kuwatendea watu wengine kama watu duni. Kusema HAPANA tunapoambiwa vurugu ni jambo la lazima.

 

Mungu, tusamehe kwa uzembe wetu tulipopaswa kuitikia. Tunaomba radhi kwa kutosahau matukio hayo mabaya—kwamba tunakubali wenyewe kuharibiwa na kutosumbuliwa tena na maisha yetu mapya katika ulimwengu mpya; kwamba mara nyingi tunajali zaidi amani kuliko ukweli.

 

Asante, Mungu, kwa kuwa pamoja nasi, na, licha ya udhaifu wetu, bila kutuacha peke yetu. Pasipo Wewe na ufunuo Wako katika Neno Lako, huenda tungekuwa tayari tumezama katika chuki, sisi kwa sisi, na taifa dhidi ya taifa. Lakini Wewe ni upendo na rehema. Wewe ndiye amani yetu na tumaini la amani duniani.

 

Ndiyo maana tunakushukuru, Mungu, kwa amani ambayo imeanzishwa hivi karibuni huko Israeli baada ya miezi kadhaa ya mapigano.

 

Na ndiyo maana, Mungu, tunataka pia kukuomba ukomeshe migogoro mingine ya umwagaji damu haraka iwezekanavyo. Vuvia mioyo ya viongozi wa ulimwengu kuelekea jambo hili. Tunaamini katika nguvu Yako.

 

Tunataka kukuomba uwaweke karibu na moyo Wako wale wote waliodhurika katika migogoro hii—wote ambao wamepoteza wapendwa wao. Mawazo yetu hapa ni mahususi kwa ajili ya wazao wa wale walioangamia katika Mauaji hayo makubwa. Jeraha hili bado halijapona.

 

Na kwa wale, Bwana, waliopokonywa uhai kwa sababu tu walikuwa tofauti kwa namna fulani—katika macho ya watu wengine, dhaifu, wasiostahili kuishi—rejesha tena, Bwana, haki ya milele katika hukumu Yako ya mwisho hivi karibuni. Damu yao iliyomwagika inakulilia Wewe leo, Ee Mungu, kutoka katika dunia hii kwa ajili ya hukumu ya haki.

Sikia maombi yetu. Amina.

 

Baada ya maombi hayo wawakilishi wa ofisi, taasisi na mashirika mbalimbali waliweka mashada ya maua kwenye mnara huo.

 

“Ni ya kutisha kiasi gani kwamba katika mkesha wa kuadhimisha miaka themanini ya ukombozi wa kambi ya Auschwitz-Birkenau . . . mtu anasikia wito wa kuacha kuomba msamaha kwa makosa ya vizazi vilivyopita,” Siciński alisema. Ndiyo sababu tunataka kukumbuka matukio haya mabaya, [kwa sababu] kila mwanadamu, bila kujali jamii, rangi, au asili, anastahili kuheshimiwa kama mtoto wa Mungu.”

 

Kwa mujibu wa Siciński, njia bora ya kutoa heshima kwa kumbukumbu ya waathiriwa wa Mauaji Makubwa itakuwa kupinga kwa ujasiri itikadi yoyote inayohubiri unyanyasaji dhidi ya watu wengine. Wakati binadamu wanaposahau jambo hili, majanga mabaya hutokea, alisema.

Maonyesho yanajumuisha zaidi ya picha 100 kuhusu kazi ya shirika

Maonyesho yanajumuisha zaidi ya picha 100 kuhusu kazi ya shirika

Kwa takribani miaka 10 sasa, maelfu ya Wavenezuela wamevuka mpaka kwenda Brazili, wakikimbia ukosefu wa ajira na kusababisha mgogoro wa elimu, uhaba wa chakula, na ukosefu wa utulivu wa kisiasa. Kulingana na habari rasmi, ni Colombia na Peru pekee ambazo zimepokea watu wengi wa Venezuela kuliko Brazili.

 

Tangu mwaka 2018, Shirika la Maendeleo na Msaada la Waadventista (The Adventist Development and Relief Agency, ADRA) Brazili limetekeleza miradi saba inayolenga kuwahudumia wahamiaji. Mipango hiyo inalenga kuimarisha usalama wa chakula, udhibiti wa afya, na usafi, pamoja na msaada wa makazi na uhamishaji.

Kwa lengo la kuwa thabiti, kuzoea wakati huo huo mahitaji yanayobadilika ya wageni, usimamizi ni muhimu, anasema Telma McGeogh, meneja wa ADRA Brazili wa masuala ya uhamiaji. “Kazi yetu ya kwanza kwa kawaida ni kwenda kwenye eneo, kuangalia, na kutathmini mahitaji yaliyopo na kisha kuleta jibu linaloendana na hitaji hilo,” McGeogh alisema. “Tangu mwaka 2018 tumehudumia zaidi ya watu 270,000, kwa uwekezaji wa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 30.”

 

Ili kufahamisha umma na kukuza mipango ya ADRA Brazili, shirika hivi karibuni lilipanga maonyesho ya picha katika jiji la kusini la Porto Alegre. Picha hizo zinasimulia kisa cha baadhi ya mipango iliyotekelezwa kusaidia wakimbizi wa Venezuela nchini Brazili.

 

Jorge Wiebusch, mkurugenzi wa ADRA Brazili katika ukanda wa Rio Grande do Sul, aliangazia umuhimu wa tukio hilo. “Maonyesho haya yanasaidia watu kufahamu upana na ufikiaji wa kazi ya ADRA Brazili pande zote nchini mwetu,” Wiebusch alisema. “Nina shauku kuu sana na mradi huu.”

 

Picha zilisimulia visa vya baadhi ya wakimbizi, kama vile uzoefu wa Pedro Rafael Salazar, mzaliwa wa jimbo la Anzoátegui. “Yalikuwa maisha yenye changamoto nchini Venezuela,” Salazar alikiri. “Sikuwa na kazi nzuri ya heshima au chakula cha kutosha, na familia yangu ilikuwa ikiteseka. Hilo ndilo lililotusukuma kuhamia Boa Vista, ambako tulianza upya tena. Ilikuwa ngumu sana mwanzoni, kwani tuliishi mitaani na kulala kwenye kituo cha mabasi, katika vipande vya kadibodi,” alisimulia.

Kupitia kazi ya ADRA Brazili, Salazar aliona fursa ya kuanza upya. Moja ya miradi ya ADRA huko Boa Vista ilitoa takriban milo 2,000 kwa siku kwa wakimbizi wa Venezuela. Hatimaye Salazar aliweza kuchukua madarasa ya upishi, shukrani tena kwa msaada wa ADRA Brazili.

 

Mbali na kutoa milo na hati za malipo za kununua vifaa muhimu, ADRA Brazili pia hutoa mradi wa kuhamisha watu katika makazi mapya (SWAN), ambao huwasaidia Wavenezuela kupata kazi na kulipia gharama zao za kupanga kwa miezi kadhaa. “Shukrani kwa SWAN, familia ina kazi isiyotetereka,” alielezea mratibu wa mradi Verona Moura. “Tuliwaunga mkono katika mchakato mzima.”

 

Kama sehemu ya mpango wa SWAN, baadhi ya familia za wakimbizi zilihamishwa kwenda Rio Grande do Sul. Hii ilijumuisha familia ya Salazar, ambaye alipanda ndege ya Jeshi la Wanaanga la Brazili na hatimaye kutua katika jimbo la kusini.

 

“ADRA inaunga mkono mipango hii yote kwa sababu shirika hilo liliundwa na Kanisa la Waadventista ili kutimiza madhumuni yake ya kuwahudumia wanadamu ili kila mtu aishi jinsi Mungu alivyokusudia,” André Alencar, mratibu wa miradi ya kijamii wa ADRA Brazili alisema. “Na tunatimiza hili kwani tunasukumwa na haki, huruma, na upendo.”

Jinsi ujumbe wa Waadventista ulivyofikia mojawapo ya makabila kongwe zaidi nchini Nepal. 

Umesh Pokharel, kwa Adventist World

Rai ni moja ya makabila kongwe nchini Nepal, ikijumuisha mkusanyiko wa vikundi. Kihistoria, waliishi katika eneo kati ya mito ya Dudh Koshi na Tamur. Kwa kawaida Rai walijishughulisha na ufugaji wa wanyama na shughuli za kilimo.

 

Wanajulikana kwa heshima yao juu ya asili na roho za mababu. Rai wamekuwa wakifuata dini ya Kirat tangu nyakati za mababu. Dini ya Kirat imejikita kwenye imani ya viumbe vyote kuwa na roho na ibada kwa mababu. Hawa wa Rai hawaamini mbingu wala jehanamu. Hakuna uongozi wa kidini, lakini mashaman huongoza ibada zao za kidini.

 

 

JINSI UJUMBE WA WAADVENTISTA ULIVYOLIFIKIA KABILA LA RAI

Yam Bahadur Rai alizaliwa katika familia maskini ya wakulima katika kijiji cha mbali cha milimani mashariki mwa Nepal. Kijiji hicho hakikuwa na miundombinu ya kisasa, na jamii ilikuwa imejikita katika ushirikina na kuwategemea sana mashaman na waganga wa kienyeji katika masuala ya afya na ya kiroho.

 

Maisha ya awali ya Yam yalikuwa magumu. Tangu kuzaliwa kwake mara nyingi alikuwa mgonjwa. Kwa kutokuwa na elimu rasmi na huduma zisizotosheleza za afya, wazazi wake waliwageukia mashaman wakati afya yake ilidhoofika. Katika umri wa miaka 8 Yam alipata madoa kwenye mwili wake. Hapo awali akipuuzwa kama mtoto, hali ilizidi kuwa mbaya. Licha ya kafara za kuku na mbuzi, hali yake haikuimarika.

 

 

HATUA YA MABADILIKO

Mwishowe wazazi wa Yam walimpeleka kwa daktari, ambaye alimgundua kuwa na ukoma. Ugonjwa huo ulionekana kama laana au adhabu kwa makosa. Daktari, hata hivyo, alipendekeza kwamba Yam atafute matibabu katika Hospitali ya Ukoma ya Misheni huko Lalitpur, Nepal.

 

Hospitalini Yam alianza kupata matibabu ya bure. Wakati wa kukaa kwake kwa miaka miwili alikutana na James Nakarmi, msimamizi katika hospitali hiyo, na mke wake, Nirmala, muuguzi. Wote wawili walikuwa Waadventista wa Sabato waliojitoa. Wema wao, huruma, na utayari wa kuwaombea na kuwashauri wagonjwa vilimgusa sana Yam.

 

Alipokuwa akipatiwa matibabu, Yam alianza kujifunza jinsi ya kusoma na kuandika. Nakarmi alimpa Biblia na kumuingiza katika maombi. Baada ya muda, Yam alipata faraja na matumaini katika mafundisho ya Biblia. Baada ya mwaka wa kusoma na kuchunguza kwa makini imani ya Waadventista, Yam aliipokea imani na kubatizwa huko Kathmandu.

 

 

INJILI YALIFIKIA KABILA LA RAI

Yam aliporudi kijijini kwake, hakubeba mwili wake uliokuwa umeponywa pekee bali pia roho iliyofanywa upya na shauku ya kushiriki imani yake. Alimwalika Deep Bahadur Thapa, mchungaji na mkurugenzi wa zamani wa Ukanda wa Himalaya wa Kanisa la Waadventista, kijijini kwake. Kwa pamoja walitumia juma zima wakifundisha na kushiriki injili.

 

Juhudi zao zilizaa matunda. Watu sita wa kabila la Rai waliipokea imani ya Waadventista, na hivyo kuashiria mwanzo wa Kanisa la Waadventista miongoni mwa watu wa kabila la Rai. Ilikuwa ni hatua ya mabadiliko kwa jamii, kuwaleta katika njia mpya ya maisha iliyojengwa katika imani, elimu, na huduma za afya.

 

 

KUPANUKA TARATIBU

Ujumbe wa Waadventista ulifikia kabila la Rai mwezi Desemba 1992, na tangu wakati huo, umeenea taratibu. Katika muongo uliofuata, ujumbe wa Waadventista ulienea kwa haraka kupitia uhusiano wa familia na urafiki.

 

Kwa sasa kuna watu 16 wa kujitolea wa Global Outreach (GO) kutoka kabila la Rai, pamoja na wachungaji wawili waliowekewa mikono na wachungaji wawili wenye Shahada ya Teolojia kutoka chuo kikuu cha Waadventista. Kabila la Rai sasa lina zaidi ya waumini 4,000 Waadventista ambao wanatunza makanisa 19 ya Waadventista kote Nepal.

Wokovu kwa imani kupitia kwa neema 

NA DARIUS JANKIEWICZ

Mara tu baada ya kukutana na mke wangu mtarajiwa, alinielezea kuhusu tukio la kujaribu kushiriki imani yake. Baada ya kulelewa katika mazingira ya Kiadventista, amekuwa akifundishwa kuwa “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet. 3:15). Hivyo alipokuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu kisicho cha kidini huko Australia, alimshirikisha mwanafunzi mwenzake imani yake katika wokovu kupitia kwa Yesu. Kijana huyo aliyepatwa na mshangao alijibu, “Kuokolewa? Kuokolewa kutoka kwenye nini?” Kwa miaka mingi tangu wakati ule, mara kwa mara nimekuwa nikilitafakari swali hili. Kwa wengi wetu hasa katika ulimwengu wa Magharibi, wangeweza kujibu kuwa hakuna cha kuokolewa kutoka kwacho.

 

Kwa watu wasiokuwa na uhusiano wa kidini wanaoishi wakati wa sasa, wanaojifanya kukumbatia uelewa wa kibinadamu kuwa ni mzuri kwa asili, dhana ya “dhambi” au “kuwa na dhambi” ni dhana ya kisasili kilichopitwa na wakati ambacho kila mara kinawachukiza. Hata hivyo matukio ya ulimwengu wa sasa wakati mwingine huwasababisha hata wale walio na mtazamo wa ulimwengu wa watu wasio na dini kujihoji kuhusu wema wa asili ya binadamu. Kwa mfano, katika chapisho la hivi karibuni la mtandaoni lenye kichwa kisemacho “Machafuko kila mahali . . . Ni nini tatizo la Wanadamu?” mtoa maoni mmoja alilalamika, “Kwa kweli ninakatishwa tamaa na jamii ya wanadamu na shauku yake kubwa isiyo na maana inayoharibu aina zetu katika uso wa sayari dunia”Pale mwanadamu asiye na dini anapoweza kuchukulia masimulizi ya Biblia kama yasiyoaminika, Wakristo wanaamini kwamba maelezo pekee yenye maana kuhusu maisha ya mwanadamu yanapatikana katika Biblia, ambayo inaelezea tatizo la uovu, pamoja na ufumbuzi wake, ninaoamini kuwa ni mada tano zinazoungana.

 

 

UFUNUO WA TABIA YA MUNGU

Mada ya kwanza na ya muhimu zaidi katika Biblia ni ufunuo wa tabia ya Mungu ya upendo (1 Yn. 4:8), yaani, Mungu ni Muumbaji mwema na mwenye upendo aliyefanya kila kitu kwa nguvu Zake ili kutatua tatizo la uovu (Yer. 31:3; Zab. 86:15; 103:11). Mafundisho mengine yote ya Biblia yamejengwa katika msingi wa wazo hili. Kuanzia kitabu cha Mwanzo, tunamuona Mungu akimfukuza Adamu na Hawa, waliofanya dhambi na kuwapendekezea suluhisho. Mpango huu uliowekwa “tangu kuwekwa misingi ya dunia,” ulihusisha Mungu kufanyika mwanadamu na kutoa maisha Yake kwa ajili ya mwanadamu (Ufu. 13:8).

 

Kama ambavyo mama Ellen White alivyoandika: “Katika ukombozi Mungu alifunua upendo Wake kwa kafara, kafara kubwa mno, ya kina na kuu mno ambayo haipimiki.”Kupitia kwa kafara Yake ya upendo, Mungu hatimaye atakomesha tatizo la uovu, ataponya asili ya mwanadamu mdhambi na kufuta machozi yao yote (Ufu. 21:4). Wazo hili la upendo wa Mungu ni la kwanza na la mwisho katika mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu.

 

 

ASILI YA DHAMBI YA MWANADAMU

Kwa namna nyingine wazo hili la tabia ya Mungu ya upendo ni wazo la pili la kibiblia kwa mwanadamu mwenye dhambi. Wakristo wengi wanaamini kuwa anguko la wanadamu wa kwanza, linaloelezwa katika Mwanzo 3, liliathiri wanadamu wote. Hata hivyo, kiwango cha dhambi ya mwanadamu kimekuwa kikijadiliwa katika historia yote ya mwanadamu. Mdahalo huu unaendelezwa na maswali kama vile “Je, tumezaliwa tukiwa na asili ya dhambi?” au “Je, mwanadamu anafundishwa kuwa mdhambi?” yanazidi kuzua ubishi. Lakini Biblia inafundisha kwa uwazi kwamba Anguko lilisababisha matokeo ya kifo cha kimwili na cha kiroho cha mwanadamu na kuvunja ushirika wa mwanadamu na Mungu, likisababisha mwanadamu na vizazi vyake vyote vinavyofuata kuzaliwa katika uelekeo wa dhambi na kifo. Mtunga zaburi anaelezea hali ya mwanadamu kwa namna hii: “Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo” (Zab. 58:3; tazama pia Zab. 51:5; Yer. 17:9; Efe. 2:3). Vile vile, Ellen White anaelezea asili ya mwanadamu kwa namna hii: “[Sethi] alikuwa ni mwana wa Adamu kama alivyokuwa Kaini mdhambi, na hakurithi kutoka kwa Adamu asili njema zaidi ya Kaini. Alizaliwa katika dhambi.”

 

Wazo la pili la kibiblia la hali ya dhambi ya mwanadamu linaonekana kuungwa mkono na sayansi jamii ya sasa. Watafiti kutoka “Baby Lab” ya Chuo Kikuu cha Yale waligundua kuwa watoto hawazaliwi na maadili ya asili. Majaribio ya kisayansi yaliyofanywa kwa umakini yalidokeza kuwa mtoto mchanga mwenye umri wa miezi miwili anaweza kuonyesha maadili yenye mwelekeo wa uovu. Akitoa muhtasari wa ugunduzi uliofanywa na Baby Lab, kiongozi wa utafiti Paul Bloom alihitimisha kuwa, pamoja na kiwango cha wema, pia tunamiliki “silica za ubaya” ambazo zinaweza “kusambaa na kuwa uovu” kwa urahisi. Vivyo hivyo, Bloom, mtaalamu wa mageuzi, alipendekeza kwamba, “Mchungaji Thomas Martin katika karne ya kumi na tisa, hakukosea kabisa kuandika kuhusu ‘ukosefu wa maadili wa asili’ kwa watoto na kusema [kuwa] ‘tunakuja duniani tukiwa na asili iliyojaa hulka ya uovu.’ ”4

 

Kwa hivyo, Biblia, maandiko ya Ellen White, na, cha kushangaza, hata utafiti wa kisasa unathibitisha kwamba tunaingia duniani tukiwa tumezongwa na dhambi. Hili linaelezea kwa nini matendo yetu yote na misukumo yetu, licha ya kuonekana kuwa ya haki, ni “kama nguo iliyotiwa unajisi” kwa Mungu (Isa. 64:6) na kwa nini hakuna mtu anayeweza kudai kuwa na aina yoyote ya haki ya asili au iliyopatikana (Zab. 14:3; Rum. 3:10). Hivyo, swali lililoulizwa na rafiki ya mke wangu, “Kuokolewa? Kuokolewa kutoka kwenye nini? linaweza kujibiwa kuwa tunahitaji kuokolewa kutoka kwa nafsi zetu wenyewe. Isipokuwa tumeelewa wazo hili la pili la kibiblia la mwanadamu kuwa na asili ya dhambi, hatuwezi kuthamini kwa kweli kafara ya Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Kama ambavyo Ellen White alivyoelezea vizuri: “Hakuna upendo wa kina kwa Yesu utakaokaa katika moyo ambao haujatambua dhambi zake binafsi.”

 

 

MWOKOZI ATOSHAYE 

Mada ya tatu ya kibiblia, kuwa Mungu pekee ndiye Mwokozi wa mwanadamu, inadhihirika kama kamba  ya dhahabu katika Biblia yote. Katika Agano la Kale, kinyume cha mataifa ya waabudu miungu yaliyokuwa yakiwazunguka, watu wa Israeli walikumbushwa mara kwa mara kuwa Bwana, Mungu wao, ni mmoja (tazama, kwa mfano, Kumb. 6:4), na kwamba zaidi ya Mungu, hakuna “Mwokozi” (Isa. 43:11; Hos. 13:4). Mada ya nafasi ya pekee ya Mungu katika Agano la Kale kama Mungu wa kweli na Mwokozi pekee wa watu Wake inajirudia katika Agano Jipya.

 

Ni katika Agano Jipya tunapokutana na Yesu Kristo, ambaye anaelezewa kama Mungu mwenyewe na wakala pekee wa wokovu wa mwanadamu. “Kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu” mtume Petro kwa ujasiri alitangaza kwa viongozi wa Kiyahudi “litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Mdo. 4:12). Vivyo hivyo, mtume Paulo alisema “Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu” (1 Tim. 2:5-6). Kupitia maandiko yake, Ellen White pia anarudia wazo hili la kina la kibiblia. Aliandika kuwa, Yesu, ni “Mwokozi atoshaye . . . tumaini pekee la wokovu wetu.”Katika ulimwengu ambao vitu vingi vinadai kuwa kama “mwokozi” wetu, Maandiko yanatuelekeza kwa Mungu mmoja wa kweli, anayetoa tumaini kwa wanadamu. Hakuna kitu hata kimoja, hata utii wetu, kinachoweza kuchangia kwa kile ambacho Kristo, Mwokozi pekee wa mwanadamu, alikitimiza kwa ajili yetu pale msalabani.

WOKOVU KWA NEEMA KUPITIA KWA IMANI

Hili linatupeleka katika mada ya nne ya kibiblia ya wokovu kwa neema kupitia kwa imani. Ingawa mada hii ilipokelewa kikamilifu na waandishi wa Agano Jipyailizidi kuleta mabishano baada ya vifo vya mitume. Wakiathiriwa na falsafa ya Kigiriki, iliyothibitisha asili njema ya wanadamu, wanafikira wengi walioibuka baada ya mitume walianza kuhoji asili ya dhambi ya mwanadamu. Hili lilipelekea kanisa la baada ya mitume kuliasili wazo kwamba wanadamu wanaweza kuchangia katika mchakato wa wokovu, kwamba utii wao, pamoja na neema ya Mungu, ndio msingi wa wokovu. Uelewa huu wa wokovu wa mwanadamu ulidhihirika wazi zaidi kwenye “Agizo juu ya kuhesabiwa haki” katika Baraza la Trent ambalo lilikuwa ni jibu la Kanisa Katoliki ya Kirumi kwa mageuzi ya karne ya 16.

 

Hata hivyo, jambo hili haliendani na kile kinachoelezwa katika Biblia. Baada tu ya dhambi kuingia ulimwenguni, tunaona Mungu akimtafuta mwanadamu na si vinginevyo. Yehova Elohim ndiye anayetamka unabii wa kwanza wa Masihi ajaye, ambaye siku moja ataiangamiza dhambi iliyoingia ulimwenguni (Mwa. 3:15). Vivyo hivyo, katika kisa cha Ibrahimu na Isaka, ambapo Isaka anafungwa na kuwekwa madhabahuni (Mwa. 22:1-19), Mungu anajifunua kama Yehova Yire, Mungu mpaji pekee (fungu 14). Ibrahimu na Isaka hawakuokolewa kwa sababu ya utii wao mkamilifu. Bali, Mungu pekee ndiye aliyetenda kwa niaba yao kwa kuwapa kondoo wa kafara. Mada hii ya wokovu kwa njia ya neema inajirudia katika Agano la Kale lote na kuelezewa katika kisa kama kile cha mtoto mchanga aliyetelekezwa katika Ezekieli 16 na katika kisa cha Hosea na Gomeri.

 

Mada hii ya nne ya wokovu wa mwanadamu kwa neema kupitia kwa imani limedhihirishwa katika Agano Jipya lote, fungu la kipekee likiwa Waefeso 2:8-9: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Ellen White ameuelezea hivi ukweli huu wa kibiblia: “Ikiwa mtakusanya vitu vyote ambavyo ni vizuri na vitakatifu na vinavyopendeza kwa mwanadamu na kuviwasilisha mbele ya malaika wa Mungu kama vinavyochangia katika wokovu wa roho ya mwanadamu au katika kustahili kwake, jambo hili litakataliwa kama kosa la uhaini.”Isipokuwa pale tutakapopokea kwa mioyo yetu yote ukweli kuhusu wokovu kwa neema, kwa njia ya imani, daima tutatafuta kuifanya asili yetu kuwa njema na “uadilifu” wetu kuchangia katika wokovu wetu. Jambo hili kamwe halitaleta furaha itokayo katika ahadi ya hakikisho la wokovu.

 

 

UTII NA UTAKATIFU: TUNDA LA IMANI

Hii inatufikisha katika mada ya tano ya kibiblia, ambayo inashughulikia utii wa mwanadamu. Agano la Kale na Jipya humfunua Mungu kama anayetaka utii kwa wafuasi Wake. Wito wa Mungu katika Walawi 19:2, “Mtakuwa watakatifu kwa kuwa Mimi ni mtakatifu,” umerudiwa pia katika Agano Jipya lote (tazama kwa mfano, Mt. 5:48; Luka 6:36 na 1 Pet. 1:16). Hata hivyo, katika Agano la Kale na Jipya, Mungu ndiye wakala wa utakatifu wa watu Wake. Mungu ndiye aletaye utakatifu na utii kwa watu Wake: “Kwa kuwa Mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu” (Law. 21:8). Lakini ikiwa utii wa mwanadamu ni kazi ya Mungu katika maisha ya wafuasi Wake, je, ni wajibu gani tunaufanya sisi? Yesu anatoa jibu sahihi: “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu” (Yn. 15:4). Tunapokaa ndani ya Kristo, analeta utii ndani yetu, si ili tuokolewe bali kwa sababu tumeshaokolewa. Hivyo, utii ni matokeo ya wokovu, siyo msingi wa wokovu (Efe. 2:8-10). Au kama Ellen White alivyoandika, “Hatupati wokovu kupitia kwa utii wetu; maana wokovu ni zawadi ya bure ya Mungu, inayopokelewa kwa imani. Lakini utii ni tunda la imani.”

 

Utii kama tunda la imani unatukumbusha kuwa Mungu hajatuokoa kutoka kwetu sisi wenyewe, kama ilivyoelezwa hapo juu, bali pia ametukomboa kwa ajili ya utume maalumu, yaani, kuakisi upendo Wake kwa ulimwengu unaoangamia (Mt. 5:16; Efe. 2:10).

 

 

HITIMISHO

Biblia inasema “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn. 3:16). Ukweli huu mkuu umefunga pamoja mada tano za kibiblia zilizoelezewa hapo juu, ambazo ni kiini cha mafundisho yote ya Biblia. Hivyo, kama wafuasi wa Yesu, tunao uchaguzi: kutazama wema wetu, hivyo tusiwe na uhakika daima wa thamani yetu na tusipate kamwe uzoefu wa furaha ya kweli ya wokovu; au “tukimtazamia Yesu, mwenye kuanzisha na kutimiza imani yetu” (Ebr. 12:2), na kukaa ndani Yake kwa utulivu na furaha hata pale atakapokuja kutuchukua nyumbani.

1https://www.smh.com.au/national/nsw/conflict-everywhere-what-is-wrong-with-humans-20231010-p5eb1l.html (ilisomwa Januari 22, 2025).

 

2 Ellen G. White, Sons and Daughters of God (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1955), uk. 11.

 

3 Ellen G. White, The Spirit of Prophecy, vol. 1 (Battle Creek, MI: Seventh-day Adventist Pub. Assn., 1870), gombo la 1, uk. 60.

 

4 https://behavioralscientist.org/babies-and-the-science-of-morality/, ilisomwa Des. 21, 2024.

 

5 Ellen G. White, Steps to Christ (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1956), uk. 65. 

 

6 Ellen G. White, From Eternity Past (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1983), uk. 303. (Msisitizo umeongezwa.)

 

7 Ellen G. White, Faith and Works (Nashville: Southern Pub. Assn., 1979), uk. 24.

 

8 E. G. White, Steps to Christ, uk. 61. (Msisitizo umeongezwa.)

Darius Jankiewicz anahudumu katika Divisheni ya Pasifiki Kusini kama Katibu wa Fildi/Huduma ya Uchungaji na mratibu wa Roho ya Unabii. 

NA EDYTA JANKIEWICZ

Kukua katika nyumba ya Kiadventista, shuleni na kanisani, sikumbuki kama kuna wakati ambapo sikufahamu kuhusu kisa cha Yesu. Hata hivyo kwa namna fulani nilitekwa na dhana kwamba “kuamini” na “kufanya” mambo mema vilikuwa kiini cha kuokolewa. Jambo hili lilikuwa na maana kwa akili yangu changa, kwa kuwa katika ulimwengu ulionizunguka, hakukuwa na kitu cha bure. Lakini wakati fulani katika ujana wangu nilianza kusikia kwamba wokovu ulikuwa unapatikana kwa neema, kwa njia ya imani. Ilikuwa ni vigumu kwangu kuunganisha mambo haya na uelewa wangu wa kwanza.

 

Ikiwa wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu, “kuamini” na “kutenda” kwangu kuna nafasi gani? Ikiwa niliokolewa kwa neema, kwa nini matendo yangu yana umuhimu? Mgogoro huu baina ya neema na matendo unadhihirika katika Agano la Kale na Agano Jipya na vinaweza kueleweka kama kiini cha wazo kuu la ukombozi katika Maandiko.

 

 

MPANGO WA ASILI WA MUNGU KUHARIBIWA

Wakati Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano Wake, dhamira Yake ilikuwa tuwe watakatifu, kama Yeye alivyo mtakatifu (Mwa. 1:27; Ufu. 20:26). Cha kusikitisha, dhambi na kifo vilipoingia ulimwenguni, wanadamu wasingeweza kupendeza tena katika mfano wa Mungu (Mwa. 3; Rum. 5:12). Kama Ellen White anavyosema, mfano wa Mungu ndani ya mwanadamu “uliharibiwa na karibu uondolewe kabisa” na dhambi.1

 

Kwa neema Yake, mfano wa Mungu kwa mwanadamu haukupotea kabisa. Ukweli huu unafafanuliwa vizuri katika maelezo ya Yeremia kuhusu mfinyanzi na udongo: “Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi na tazama alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya (Yer. 18:3-4).2  

 

Dhambi ilipoingia ulimwenguni, mpango wa asili wa Mungu kwa mwanadamu uliharibiwa lakini si kabisa; hivyo, Mungu, mfinyanzi, hakukitupa chombo cha udongo kilichoharibika. Badala yake, kusudi la kwanza la Mungu kwa mwanadamu, kwamba tuwe watakatifu, kama Yeye alivyo mtakatifu, halikubadilika; kwa hiyo, kuumba upya mfano wa Muumba wetu ndani ya mwanadamu ikawa sehemu ya “kazi kuu ya ukombozi”

 

 

KAZI YA MUNGU YA KUMREJESHA MWANADAMU

Agano Jipya na la Kale yanaielezea kazi hii ya kumrejesha mwanadamu katika sura Yake kama kazi ya Mungu. Kwa mfano, katika Walawi 20:26 Mungu anasema, “Nanyi mtakuwa watakatifu… ili kwamba mwe Wangu.” Na katika Walawi 21:8 Mungu anasema, “Mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu.” Vivyo hivyo, wazo hili linarudiwa katika Agano Jipya. Kwa mfano, “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana Wake” (Rum. 8:29); na “sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho. (2 Kor. 3:18).

 

Mafungu haya yanaweka wazi kwamba Mungu ndiye wakala wa kumrejesha mwanadamu katika sura Yake. Kazi hii ya Mungu, ambayo wakati mwingine inarejelewa kama neema ya Mungu itakasayo, ni uhalisia uliopo na unaoendelea; japo Maandiko pia yanatuambia kuwa hitimisho la kurejeshwa katika mfano wa Mungu kwa mwanadamu litafanyika katika wakati ujao: “Sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1 Yn. 3:2).

 

Maandiko yako wazi kuwa tunaokolewa kwa neema ya Mungu inayotuhesabia haki, ambayo ni zawadi Yake kwa wanadamu (tazama Efe. 2:8-9; Tit. 3:5; Rum. 3:24). Tunapoelewa kwamba kweli hatuwezi kufanya lolote kujiokoa wenyewe, na tunapozama katika upendo ambao ulimshawishi Kristo kutuokoa, tunafungua mioyo yetu kwa Roho Wake na Mungu anaanza kazi Yake ya kufanya neema katika maisha yetu, polepole akibadilisha utu wetu wa kale na kutufanya zaidi kuwa kama Yeye (Efe. 4:22-24; Gal. 2:20-21; 2 Kor. 5:17; Flp. 1:6). 

 

 

HITAJI LA KUSHIRIKIANA NA MWANADAMU

Ingawa mchakato huu wa kurejeshwa na kuhuishwa ambao pia hujulikana kama kutakasa, ni kazi ya neema ya Mungu itakasayo, haimaanishi kuwa ushirikiano na mwanadamu hauhitajiki. Badala yake, bidii katika nidhamu ni sehemu ya maisha ya Mkristo. Kama Ellen White alivyoandika: “Neema Yake [itakasayo] inatolewa ili ifanye kazi ndani yetu katika kutaka na kutenda, lakini si kama mbadala wa juhudi zetu. Roho zetu zinapaswa kuinuliwa katika ushirikiano.”4 Kwa hiyo, juhudi zetu au ushirikiano wetu na neema ya Mungu itakasayo vinahitaji nini?

 

Wakristo wengi wanaamini kwamba juhudi zao zinahitaji kujaribu kuwa kama Kristo zaidi, hivyo wanajitahidi kujaribu kuwa na upendo zaidi, wema, wasio na ubinafsi n.k. Lakini majaribio haya yanalenga katika mitazamo na matendo yetu binafsi, mara nyingi yakileta kushindwa na kuwa na hatia. Maandiko yanatuhimiza kujifunza ucha Mungu (1 Tim. 4:7).Tunawezaje kufanya hivyo? Kama ambavyo Yesu alivyo kiini cha kuhesabiwa haki, ni Yesu huyo huyo pia, si matendo na mitazamo yetu, aliye kiini cha utakaso. Hivyo, ushirikiano au juhudi zetu si kujaribu kuwa kama Kristo, bali ni mchakato wa kuifundisha mioyo na mawazo yetu kukaa ndani ya Yesu (Yn. 15), yaani, kuwa na mahusiano ya kina na Yeye.

 

Lakini tunalifanyaje jambo hili? Katika muda wote wa maisha yangu, nimeelewa kwamba, kama ambavyo mahusiano yangu ya kibinadamu yalivyo, ikiwa nitatamani kuwa na mahusiano na Mungu, ninapaswa kupanga maisha yangu kwa namna ambayo itaweka muda wa kuwa pamoja na Yeye kuwa kipaumbele; na kufanya hivi kunanihitaji niwe na juhudi zisizokoma na nidhamu.

 

Ingawa kuna usambamba kati ya mahusiano ya kibinadamu na uhusiano na Mungu, hata hivyo, ukweli ni kuwa anguko letu lilitutenganisha kutoka kwa uhusiano wa ana kwa ana na Mungu. Kwa hiyo, tamaa yetu kwa ajili ya mahusiano ya kibinadamu huzidi tamaa yetu kwa ajili ya uhusiano na Mungu ambaye hatuwezi kumwona. Habari njema ni kwamba uhalisia wetu si mwisho wa mambo. Kama ilivyokuwa bustanini, Mungu ndiye alitafuta kurejesha uhusiano, akiita “uko wapi?” kwa mwanamume na mwanamke waliokuwa wamejificha kutoka Kwake. Mungu anaendelea kuanzisha kurejeshwa kwa uhusiano wetu na Yeye, kwa sababu shauku Yake katika suala hili ni kubwa kuliko shauku yetu. Mtume Paulo anaiweka hivi, “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Flp. 2:13).

KUKUA ILI KUWA ZAIDI KAMA YESU

Kwa neema Yake, ni Mungu anaanzisha ndani ya mioyo yetu shauku juu Yake; na Mungu ndiye anayetuwezesha kuitikia shauku hii kwa kuupa kipaumbele muda wa kuwa pamoja naye. “Lakini,” unaweza kuuliza, “Je, hatujaokolewa kwa neema? Juhudi zetu hazimaanishi kuwa tunatengeneza kipimo kipya cha wokovu, tukibadilisha juhudi kama vile kujitahidi kushika amri, kwa juhudi za kuwa pamoja na Mungu?” Juhudi zetu tunazozifanya kwa kudhamiria si kwa kusudi la kupata fadhila za Mungu. Wala juhudi zetu si kwa kusudi la kupata kibali katika familia. Kupitia neema Yake, tumekwishakuwa watoto Wake wapendwa. Badala yake juhudi zetu zinapaswa kuwa kwa ajili ya kutufanya tuweze kuwa na Mungu na kumfurahia. Na, kila mara, tunapojifunza kuufurahia uwepo wa Mungu, nidhamu yetu na juhudi zetu endelevu zinakuwa tabia zinazoongezeka zaidi na zaidi, kiasi kwamba muda pamoja na Mungu ni jambo ambalo hatuwezi kufikiria maisha yetu yatakosa. 

 

Hivyo kuwa na muda pamoja na Mungu kunatusaidiaje kurejesha mfano wa Mungu ndani yetu? Kadiri tutakavyomuweka Yesu katika maisha yetu na kuakisi maisha Yake kila siku, kama alivyoishi katika ulimwengu huu na kuhusiana na watu, tunazidi kuuona uzuri na ukamilifu Wake. Kadiri tunavyozidi “kuutazama uzuri wa Bwana” (Zab. 27:4), ndipo tunapogundua mahali ambapo hatujawa sawa na Yeye.Hii, basi, inatusaidia kukua katika shauku ya kuwa kama Yeye zaidi; kuakisi tunda la Roho lililodhihirishwa katika maisha Yake (Yn. 12:32; Gal. 5:22-23). Kila mara, kupitia neema ya Mungu inayotakasa, maneno na matendo hayo katika maisha yetu ambayo hayana upatanifu na njia za Mungu yanaendelea kubadilishwa, ili kwamba tuzidi kuakisi mfano Wake (1 Tim. 4:7). Kazi hii ya kubadilishwa kiroho ni msingi wa kazi ya Roho Mtakatifu na wajibu wetu wa msingi ni kumtegemea Mungu kabisa katika hatua hii; hata hivyo, tunawajibika pia kufanyia kazi wito wa Maandiko wa kushikilia maisha ya ucha Mungu.

 

Katika maisha yangu, nimetambua kuwa, ninapokutana na changamoto, niweke tegemeo langu kwa Mungu kwa kujikumbusha kuwa Yeye yupo pamoja nami, kwamba ametangulia mbele yangu na pia Yupo pamoja na mtu au hali iliyoniletea changamoto. Na ninawajibika kwa kufanya uamuzi wa makusudi unaoniongoza kutoka dhambini. Mchakato huu wa kurejeshwa (ambao Ellen White anauita “tunda la imani,”)“hauwezi kukamilika katika maisha haya ya sasa.”8 Kwa sababu ya dhambi, kamwe hakutakuwa na muda ambao hatutahitaji neema ya Mungu inayotuhesabia haki katika maisha haya. Kama ambavyo Ellen White anasema, “kila mara tutapaswa kupiga magoti na kulia miguuni pa Yesu kwa sababu ya mapungufu na makosa yetu; lakini hatupaswi kukata tamaa.”9 Badala yake, tukumbuke mpango wa mwisho wa Mungu kuwa, siku moja, “Kufumba na kufumbua . . . tutabadilika” (1 Kor. 15:52), Sura ya Mungu ndani yetu itarejeshwa kikamilifu, na “tutafanana Naye” (1 Yn. 3:2).

 

 

UKWELI MKUU

Jambo hili linaacha swali moja la mwisho: ikiwa kutakaswa kwetu si kwa makusudi ya kupata wokovu, je kuna kusudi gani? Kwa ajili ya jambo moja, ninaamini kwamba kwa sababu dhambi zetu zinatudhuru sisi na wengine, sababu moja inayomfanya Mungu kutamani tukue katika mfano Wake ni kwa sababu ya namna nyingi ambazo inamnufaisha kila moja. Mfano, ikiwa ninaenenda katika tabia ya kutofanya dhambi kutokana na hasira yangu (Efe. 4:26), wapo wengi watakaonufaika. Kwanza, mimi mwenyewe nafaidika kwa sababu nitaishi bila kuwa na aibu ya kushindwa kudhibiti hasira yangu. Pili, familia yangu na jamii nzima itanufaika pale ambapo hawataathiriwa na hasira yangu mbaya. Tatu, Mungu ananufaika pale ambapo watu wengine wataona kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yangu na kumtukuza Mungu (Mt. 5:16).

 

Mpango wa kwanza wa Mungu kwa ajili ya mwanadamu ulikuwa ni tuwe watakatifu, kama Yeye alivyo mtakatifu. Ingawa dhambi iliharibu mpango wa kwanza wa Mungu, shauku Yake kwa mwanadamu ilibaki kuwa ile ile. Hivyo, neema ya Mungu itakasayo ikageuka kuwa sehemu ya mpango wa wokovu. Hata hivyo, sote tunajua kuwa hata katika nyakati zetu za utakatifu zaidi tunapungua katika kiwango cha utukufu wa Mungu. Lakini kwa sababu “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee,” ili kupitia neema Yake itakasayo, “kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16). Huu ndio “ukweli mkuu” wa imani yetu, unaoturuhusu kupumzika kwa furaha katika aliyoyatimiza Yesu na kukaa katika upendo na neema Yake.10

1 Ellen G. White, Education (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1903), uk. 15.

 

2 Isipokuwa kama itaelezewa vinginevyo, nukuu zote za Biblia zimetolewa katika Swahili Union Version.

 

3 E. G. White, Education, uk. 15.

 

4 Ellen G. White, God’s Amazing Grace (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1973), uk. 111.

 

5 Nilikutana kwa mara ya kwanza na dhana ya kujaribu dhidi ya kufunzwa katika Bill Hull, The Complete Book of Discipleship: On Being and Making Followers of Christ (Colorado Springs, Colo: NavPress, 2006).

 

6 Ellen G. White, Steps to Christ (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn. 1892), uk. 64.

7 Ibid., uk. 61.

 

8 E. G. White, Education, uk. 13.

 

9 E. G. White, Steps to Christ, uk. 64.

 

10 Ellen G. White, The Faith I Live By (Washington, D.C.: Review and Herald Pub. Assn., 1958), uk. 50.

Edyta Jankiewicz anahudumu kama katibu wa huduma za uchungaji katika Divisheni ya Pasifiki Kusini.

Kuitikia wito 

NA TED N. C WILSON

Neno “njoo” huenda ni moja ya miito mizuri sana katika Maandiko. Katika Agano la Kale, tunamsikia Mungu akitusihi, “Haya, njoni, tusemezane . . . Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isa. 1:18).

 

Na katika Agano Jipya imeandikwa miito mingi ya Yesu inayofahamika vizuri:

 

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mt. 11:28).

 

“Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao” (Mat. 19:14).

 

“Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe” (Yn. 6:37).

 

Hata alipokaribia mwisho wa maisha Yake, Yesu “akasimama akapaza sauti yake akisema, ‘Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” (Yn. 7:37, 38). 

 

Mungu wetu ni Mungu wa wito–hatulazimishi au kututaka kwa nguvu, lakini kwa upendo na bidii, anatuita.

 

 

WITO MKUU

Labda moja kati ya wito mkuu katika Maandiko ni ule unaopatikana katika kitabu cha Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na ayatwae maji ya uzima bure.”

 

Tambua kwamba, hii ni mialiko miwili: Kwanza, Mungu anamuita kila mmoja anayetaka kuja na “ayatwae maji ya uzima bure.” Sehemu ya pili ya mwaliko umeelekezwa kwa wale wanaosikia na kusikiliza wito wa Mungu, ukiwatia moyo kuwaalika wengine kuja kwa Kristo.

 

Katika Biblia, tunaona mifano mingi ambayo Mungu anafanya kazi kupitia watu ili kuwaita wengine waje Kwake. Katika Agano la Kale, mtunga zaburi anasema, “Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba, kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho Yake, na kondoo za mkono Wake” (Zab. 95:6, 7).

 

Katika Agano Jipya, wakati Yesu alimualika Filipo kumfuata, Filipo aliitikia wito wake na mara moja alimualika rafiki yake Nathanaeli kukutana na Mwokozi. Wakati Nathanaeli alitambua kuwa Yesu alitokea Nazareti, alishangaa, “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” Badala ya kubishana, Filipo alitoa tu mwaliko, “Njoo uone” (Yn. 1:45, 46).

 

Mungu ameweka baraka nyingi kwa ajili ya wale wanaoalika wenzao kujifunza Kwake. Katika kumsihi muumini kuweza kujihusisha katika kuvuta roho za watu, Ellen White aliandika, “Mnayo heshima ya kushuhudia kwa ajili ya Yesu na kuitetea kweli Yake mahali po pote mtakapokuwa . . . Malaika wanatamani kufanya kazi hii na wataifanya kupitia mawakala wa kibinadamu waliojitoa kwa Kristo. Maisha yako yanaweza kuwa fursa kubwa kwa malaika watakatifu kufanya kazi kwa ajili ya kuwaokoa waliopotea.”1

 

Makumi kati ya maelfu ya Waadventista wa Sabato ulimwenguni kote wanaitikia wito wa kuwa sehemu ya Kila Mshiriki Kujihusisha Kikamilifu Ulimwenguni (Global Total Member Involvement). Mungu anataka kumfikia kila mtu kwa ujumbe wake wa ajabu wa wokovu na ukweli, wakati akitamani kuwapa upendeleo huu watu Wake, wakati mwingine hutumia njia ya kawaida sana kukamilisha kusudi Lake.

KWENDA KATIKA SAFARI YA MUNGU 

Katika mkutano mmoja wa kiinjilisti uliofanyika Papua New Guinea katika nyakati za majira ya kuchipua mwaka 2024, muinjilisti mmoja alisihi, akiwaalika wale waliotamani kubatizwa kusogea mbele. Mara ya kwanza, hakuna aliyetembea. Mara ya pili, mambo yalianza kubadilika. Ghafla, mbwa alitokea kutoka mahali pasipojulikana, alielekea mbele, akaketi chini na kuwaangalia watu. Punde kundi kubwa lilielekea mbele wakiitikia wito ule. Mungu alimtumia mbwa kuwaonyesha njia!

 

Miezi michache baadaye, katika mji wa San Francisco, California, mbwa mwingine alitumwa katika safari ya Mungu. Wamishonari kutoka katika kikundi kinachoitwa Streams of Light Ministry walipita mlango kwa mlango, wakiwakabidhi kifurushi kilichokuwa na kitabu cha Pambano Kuu, pamoja na kijitabu kidogo kinachohusu afya ya akili na kuwaalika katika mikutano ya injili. Katika mji mmoja, wanandoa walifungua mlango na mmishonari alianza kuelezea kile kilichokuwa ndani ya kifurushi cha zawadi. Wakisema hawakuvutiwa, mwanamume alianza kufunga mlango wakati mbwa wao aliruka kupitia nafasi iliyokuwa wazi, akavuta ile zawadi iliyokuwa mkononi mwa mmishonari na kukimbia nayo ndani kwa haraka!

 

“Vema!” yule mtu alicheka. “Nadhani tutaichukua zawadi hii!”

 

Sasa ni wakati wa kuanza kuwa sehemu ya mpango wa kiulimwengu wa Kila Mshiriki Kujihusisha Kikamilifu! Pale utakapokuwa m-bia na Mungu, hauwezi kutambua kile ambacho atakifanya ili kukusaidia kuwafikia wengine kwa ajili Yake!

 

Tunasoma katika kitabu cha The Acts of the Apostles, “Utume wa Injili ni kitambulisho kikuu cha umishonari cha ufalme wa Kristo. Iliwapasa wanafunzi wa Kristo kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya roho za watu, wakiwapatia wote mwaliko wa rehema. Haikuwapasa kusubiri watu wajilete kwao, walitakiwa kuwafuata watu wakiwa na ujumbe wao.” Mwandishi aliyevuviwa anaendelea kusema “Iliwapasa wanafunzi kuendelea mbele na kazi yao kwa jina la Yesu. Kila neno na tendo lao lilitakiwa kuwavuta watu kwenda kwa Kristo, kama jina lenye nguvu za kuweza kumwokoa mwenye dhambi. Imani yao ilitakiwa kujikita Kwake aliye chimbuko la rehema na uwezo.”2

 

Tutakapojitoa kwa mioyo yetu yote kuwa sehemu ya utume wa Mungu, tunaweza kudai, pamoja na Mtume Paulo, ahadi yenye nguvu inayopatikana katika Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu.”

 

Yesu anakuja haraka! Kuwa sehemu ya mpango wa kiulimwengu wa Kila Mshiriki Kujihusisha Kikamilifu leo!

1 Ellen G. White, barua ya 95, 1895, katika Letters and Manuscripts, vol. 10, uk. 122.

 

2 Ellen G. White, The Acts of the Apostles, (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1911), uk. 28.

Ted N.C. Wilson ni Mwenyekiti wa Konferensi Kuu ya Waadventista wa Sabato. Makala nyingine na vitabu vya maelezo zaidi vinapatikana katika X (awali Twitter):@pastortedwilson na kwenye Facebook: @Pastor Ted Wilson.

Kazi ya uvumilivu ya kukidhi mahitaji na kujenga mahusiano 

NA SANDRA DOMBROWSKI

Siku nyingi za juma kabla au baada ya kazi, Patrick Phipps huenda katika Global Impact Life Enrichment Services (GILES), kituo cha ushawishi kinachohudumia jamii ya Asia Kusini katika Queens Village, New York City. Ungemuona Patrick, fundi wa umeme kutoka Jamaica, huenda usingetambua kuwa yeye ndiye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa kituo hiki. Unaweza kumkuta akifagia sakafu au akikarabati mojawapo ya vyumba.

 

Michelle Babb, mtaalamu wa upimaji damu anayejitolea kama meneja wa biashara wa kituo hicho, pia huja baada ya kazi kukutana na watu na kuhakikisha kuwa kituo kinaendelea kufanya kazi kwa ufanisi.

 

Kwa nini fundi wa umeme na mtaalamu wa upimaji damu, ambao wote wana kazi za kudumu, waendeshe kituo cha kuboresha maisha kwa jamii yenye imani tofauti kabisa na yao?

 

Hata washiriki wa kanisa la Waadventista wa Sabato la Patrick wanamuuliza kwa nini hahudumii jamii yake mwenyewe badala yake. Hata hivyo, kuna jamii kubwa ya Wajamaika umbali wa bloku chache tu kutoka hapo.

 

Wateja wa kituo hicho cha jamii nao wanashangaa pia. "Wanauliza, 'Kwa nini mnataka kutusaidia? Kwa nini hamwasaidii watu wenu wenyewe?' " anasimulia Michelle.

 

"Tuko hapa kwa sababu kuna hitaji," Patrick anajibu kwa utulivu.

 

Hii ni jamii ambayo haijafikiwa, ikiwa na makundi ya watu ambao bado hawajakutana na upendo wa Yesu. Pia ni jamii yenye mshikamano mkubwa ambapo watu wana uaminifu wa dhati kwa imani za familia na mababu zao.

 

 

KUJENGA DARAJA

Patrick alishirikiana na kanisa lake la Waadventista wa Sabato ili kujaribu kuhudumia jamii hii, lakini hakuna mwanajamii aliyehudhuria kanisani kwao kwa ajili ya programu. Akitafuta suluhisho, Patrick akaamua kuandaa maonyesho ya afya kwenye bustani ya mtaa. Ikiwa jamii isingekuja kanisani, labda ingekuja bustanini. Na alikuwa sahihi. Jamii ilijitokeza kwa wingi, ikifurahia huduma za uchunguzi wa afya na taarifa za bure. Ilifanikiwa, lakini nini kilifuata? Tukio la mara moja halikutosha kujiunganisha na jamii na kukidhi mahitaji yao.

 

Patrick, Michelle, na wengine wachache walitambua kuwa walihitaji mahali pa kati ambapo jamii ingeweza kufika mara kwa mara. Mnamo Novemba 2018, waliweka pamoja fedha zao, wakakodi jengo dogo katika kitongoji cha makazi, na wakaanza kutoa masomo ya baada ya shule na malezi ya watoto, madarasa ya lugha ya Kiingereza, na maandalizi kwa mitihani ya leseni ya udereva, diploma ya shule ya sekondari, uraia, na zaidi.

 

Kwa jamii inayojumuisha hasa wahamiaji wapya, GILES ndicho kile wanachohitaji. Wanakuja kwa mara ya kwanza kwa sababu kituo hiki kinatimiza mahitaji yao, lakini wanarudi tena kwa sababu wanaheshimiwa na kuthaminiwa.

 

GILES hufunguliwa siku ya Sabato na wanafanya mijadala inayokusudia kuchochea majadiliano juu ya mada za kiroho. Wanaleta wazungumzaji wanaoshiriki mada za afya zinazotambulisha kanuni za Ufalme wa Mungu. Daktari wa tiba asilia anayewasilisha hotuba mara moja kwa mwezi anasisitiza kanuni za kiroho ndani ya sheria za afya. Mwanasaikolojia pia huja mara kwa mara kutoa hotuba kuhusu afya ya akili.

 

GILES pia huandaa kambi ya majira ya kiangazi ya mwezi mzima kusaidia watoto kujiandaa kwa mwaka mpya wa masomo na kuwapa burudani, mahali salama pa kucheza wakati wazazi wao wanapokuwa kazini. Watoto 70 hadi 80 wa shule za msingi huhudhuria tukio hili kila mwaka. Siku huanza kwa ibada, ambazo zina mafundisho ya maadili pekee—wazazi kutoka dini tofauti huhudhuria siku chache za kwanza kuhakikisha kuwa ni mafundisho ya maadili pekee —kisha siku hujawa na mafunzo ya kuwaandaa watoto na daraja la shule linalofuata, kazi za mikono na michezo, ziara kutoka idara ya zimamoto ya eneo hilo, na safari ya kwenda kwenye hifadhi  na maji. Mwaka mmoja, waliunganisha kambi la kiangazi na safari ya hifadhi ya maji. Na siku zote huwa kuna mahafali, ambapo maafisa wa jamii hualikwa.

 

Hii yote hufanyika bila msaada wowote wa kifedha kutoka nje. Miaka miwili iliyopita, walianza kutoza ada kidogo kwa wiki kwa ajili ya kambi la kiangazi na programu ya baada ya shule, ambayo hutumiwa kuwalipa posho wanajamii wanaojitolea. Lakini ili kulipia kodi ya jengo na gharama nyinginezo, Patrick na Michelle hutumia fedha zao wenyewe kimya kimya na kwa kujitoa. Nini kinawahamasisha? Patrick anasema tena, "Kuna uhitaji."

MATOKEO YANAYOPIMIKA

Nini matokeo ya kazi hii ngumu na nyeti? Kwa neno moja: mahusiano. Na mahusiano ndiyo moyo wa ukuaji katika Ufalme wa Mungu.

 

GILES ilianza kama kituo cha elimu na msaada chenye utume, na imekua hadi kuwa kitovu cha jamii. Vikundi vya ndani, kama vile kundi la wanawake wa Kipakistani wanaopinga ukatili, hutumia kituo hicho kwa mikutano yao. Walimu wa shule za Waadventista wa Sabato walio kwenye  likizo ya kiangazi na vijana wanaotafuta shughuli, hujitolea kwenye kambi la kiangazi. Wanasiasa wa eneo hilo pia huhudhuria mahafali ya kambi la kiangazi na matukio mengine, wakitumia fursa hiyo kujichanganya na raia wao. Misikiti ya eneo hilo huwatuma wanajamii wao kwenye kituo hicho, wakijua watapata msaada na suluhisho huku utamaduni wao na imani zao za kidini zikiheshimiwa.

 

Kwa sababu ya imani iliyojengeka kati ya timu ya GILES na jamii, wanachama wa timu wanakaribishwa kutembelea familia majumbani mwao na kusali pamoja nao. Mungu anajibu maombi yao kwa njia za ajabu.

 

"Baada ya kuwaombea," Michelle anasema, “huwa wanarudi na ushuhuda wa maombi yao yaliyojibiwa.”

 

Siku moja jirani aliyekuwa akiishi mkabala na kituo alikuja. "Nimepewa agizo la kufukuzwa nchini," alisema, akionekana wazi kuwa na wasiwasi mkubwa namna alivyoelezea suala lake la uhamiaji. “Je, kuna chochote mnachoweza kufanya kunisaidia?”

 

Patrick na wengine wanaojitolea waliomba pamoja naye. "Hatufahamu nini kilitokea," Patrick anasema, "lakini muda mfupi baadaye alipata kadi yake ya kijani kupitia barua," jambo ambalo bila shaka lilimaliza mtanziko wote.

 

Katika hali ya kusikitisha, mama mmoja alizuiliwa Kanada kwa sababu ya matatizo ya uhamiaji, akitenganishwa na binti yake mdogo huko New York. Mwanafamilia mmoja alikuja kituoni kuomba msaada kwa niaba yake. Patrick na wengine wanaojitolea waliiombea familia hiyo, na kimiujiza, siku mbili baadaye, mama huyo aliwasili New York.

“Lakini muujiza mkubwa zaidi ni namna ambavyo Mungu amekuwa akitutumia sisi kuwa kama nuru katika jamii,” alisema Patrick. “Hatuwezi kuwasimulia visa vyote kwa sababu ya asili ya tamaduni tunazozihudumia, Lakini Mungu anabadilisha maisha ya watu kwa sababu ya mahusiano ya upendo na kujali tuliyoyajenga kwa familia na watu binafsi.”

 

Patrick na Michelle wangependa kupanua huduma zao, hasa kwa sababu hivi karibuni wahamiaji wameingia kwa wingi sana ndani ya mji wa New York na kutafuta muda zaidi wa kutembela na kuombea familia majumbani kwao. Lakini kwa sasa, wanaridhika kutoa kile wanachoweza, kukidhi mahitaji yanayowezekana, kuendelea kushiriki nuru, na kumtegemea Mungu kukimu mengineyo.

 

Kujifunza zaidi kuhusu Global Impact Life Enrichment Services (GILES), tembelea www.gloimpact.org.

Sandra Dombrowski ni mwandishi huru kutoka Connecticut ambaye hufurahia kujifunza kuhusu vituo vyenye ushawishi.

Safari ya imani na urithi 

NA MICHAEL SOKUPA

Jiji la Kimberley, mji wa kihistoria wa uchimbaji madini nchini Afrika Kusini, lina nafasi maalumu  katika historia ya Kanisa la Waadventista wa Sabato. Ni hapa ambapo Uadventista uliota mizizi kwa mara ya kwanza barani Afrika. Kimberley ni nyumbani kwa maeneo kadhaa ya waanzilishi waliosahaulika kwa muda mrefu, ambayo ni muhimu katika kusimulia hadithi ya uongozi wa Mungu katika siku za mwanzo za kazi ya kimishonari ya Waadventista nchini Afrika Kusini.

 

Safari ya hivi karibuni ya utafiti huko Kimberley, iliyoongozwa na Merlin Burt, mkurugenzi wa White Estate; Markus Kutschbach, mkurugenzi wa Adventist Heritage Ministries; na Michael Sokupa, mkurugenzi mwenza wa White Estate, imefichua maeneo haya muhimu ya kihistoria. Ugunduzi wao unatoa mwanga mpya juu ya juhudi za awali za kimishonari za Waadventista barani Afrika.

 

 

MBINU ZA ZAMANI ZA UTUME NCHINI AFRIKA KUSINI

Zamani kazi ya utume ya Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Afrika Kusini ilitiwa nguvu na kuimarishwa sana kwa kuanzishwa kwa taasisi mbalimbali. Huko Kimberley, ukuaji wa kanisa ulikuwa wa polepole mwanzoni. Hata hivyo, uanzishwaji na ukuaji wa taasisi mbalimbali za Waadventista vilichangia sana kushinda ubaguzi wenye mizizi mirefu na kuendeleza utume miongoni mwa kabila mbalimbali za mji huo. Kupitia juhudi hizi, kanisa liliweza kuweka msingi imara kwa kazi yake. Hebu tuangalie kwa karibu zaidi baadhi ya matokeo muhimu ya kipindi hiki, tukiangazia taasisi zilizofanya kazi ya msingi katika kutengeneza utume wa zamani wa Waadventista huko Kimberley na kwingineko.

MAENEO YA URITHI YALIYOGUNDULIWA HIVI KARIBUNI

Shule, huko Kimberley

Kuna ushahidi mkubwa unaoonyesha kuwa shule ilianzishwa huko Kimberley katika miaka ya mwanzoni ya kuanzishwa kwa kanisa. Ishara ya kwanza ya hitaji la shule kama hiyo, inatoka katika Ripoti ya A.T. Robinson ya mnamo 1892, ambaye alieleza umuhimu wa kuwapa watoto wa Waadventista elimu katika eneo. Robinson aliandika:

 

"Kuna maswali mengi muhimu yanayohitaji kujadiliwa na bodi, na tunaomba kwa bidii kwamba Bwana atatoa hekima, ili kila hatua itakayochukuliwa iwe ni mapenzi ya Roho Wake. Swali la shule ni suala kubwa miongoni mwa ndugu zetu hapa, na linahitaji kupewa kipaumbele, kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watoto wa Waadventista wanaohitaji elimu."1

 

Ingawa eneo halisi la shule hiyo linabaki kutojulikana, mabaki yaliyopatikana katika Kanisa la Beaconsfield—Kama vile madawati na fremu zake—vinaashiria kuwa shule kweli iliwahi kuwepo. Sarah Peck, mmoja wa makatibu wa Ellen White, alihusika sana katika ukuaji wa mwanzo wa shule hiyo. Alifika Cape Town mnamo 1892 na baadaye akahamia Kimberley mwaka uliofuata kuanzisha shule hiyo.2

 

Mabafu ya Kimberley

Kanisa la Kimberley pia lilianzisha huduma ya afya kwa kutumia tiba ya maji kulingana na ushauri wa Ellen White. Mabafu ya Kimberley yalivutia watu wa matabaka yote, wengi wakitafuta nafuu ya  matatizo mbalimbali ya kiafya. Katika safari yetu ya utafiti, tuligundua anwani ya jengo la mabafu ya Kimberley katika orodha za mwaka 1901/1902, Na rekodi za umiliki wa ardhi zilithibitisha kuwa jengo hilo liliwahi kumilikiwa na Kanisa la Waadventista wa Sabato.3 Ugunduzi huu ni kiungo dhahiri kwa huduma za afya za zamani za kanisa barani Afrika, ukifichua sura ya kihistoria iliyokuwa haijasimuliwa.

 

Nyumba ya Hisani

Wakati wa Vita vya Afrika Kusini (1899-1902), Nyumba ya Hisani iliyoanzishwa huko Kimberley kwa ajili ya kusaidia maskini na wasio na ajira, ilikuwa msaada mkubwa kwa watu wengi. Ilikuwa karibu na mabafu ya Kimberley, na ilitoa malazi, chakula, na mboga mbichi kwa wakazi wakati wa kuzingirwa kwa Kimberley. Nyumba hii ya Hisani iliyotajwa kwenye kumbukumbu mwanzoni mwa mwaka 1900, ni ushuhuda wa kujitolea kwa kanisa katika kutoa msaada wa kijamii wakati wa changamoto.

 

Nyumba ya George van Druten

Nyumba ya George van Druten, mmoja wa Waadventista wa kwanza na mwanzilishi, pia iligunduliwa wakati wa safari hii ya utafiti. Shukrani kwa familia ya van Druten na msaada wa kiongozi wa eneo hilo na mchungaji Xhanti Mabenge, tuliweza kupata eneo hilo kwenye shamba la ndani. Ingawa mmiliki wa shamba hakuwa mahali hapo, wafanyakazi wake walituongoza kwenda kwenye eneo hilo. Huko, tulikuta magofu ya nyumba ya van Druten pamoja na kaburi lake na la mkewe.

 

George van Druten aliyejulikana kwa imani yake thabiti, alikuwa na duka huko Kimberley. Eneo la duka lake halijulikani bado. Wongofu wake, ushahidi mwaminifu, uhusiano wake na William Hunt, mmishenari wa mwanzo katika eneo hilo, na miaka ya mwisho ya maisha yake huko Kimberley, mahali ambapo alifariki huko, vimetengeneza sehemu muhimu ya urithi wa Waadventista huko.

 

Kaburi la William Hunt

Ugunduzi mwingine muhimu ulikuwa wa kaburi la William Hunt, mmishonari na Mwadventista wa mwanzo. Baada ya utafiti wa kina wa Markus, eneo halisi la kaburi la Hunt lilibainiwa ndani ya eneo salama la mgodi. Kampuni ya madini imekubali kuruhusu Kanisa la Waadventista wa Sabato kujenga mnara wa kumbukumbu katika kaburi hili, ambalo halikuwa limewekwa alama hapo awali. Hili litakuwa tukio la kudumu la kuonyesha kukumbuka huduma ya Hunt, ambaye kazi yake ya kimishonari iliweka msingi kwa wengi kubadili dini kwenda kwenye imani ya Kiadventista huko Afrika Kusini.

MATARAJIO

Tunapotafakari maeneo haya yaliyogunduliwa, tunakumbushwa umuhimu wa kuangalia nyuma na kuona jinsi Mungu alivyotuongoza katika historia yetu. Kama Ellen White alivyowahi kusema:

"Hatuna chochote cha kuogopa kuhusu siku zijazo, isipokuwa tukisahau jinsi ambavyo Bwana ametuongoza, na mafundisho Yake katika historia yetu ya zamani."5

 

Taasisi zilizoanzishwa na Kanisa la Waadventista wa Sabato huko Kimberley—shule, huduma za afya, na huduma za hisani—zote zilikuwa vyombo vya utume, vilivyosukumwa na muongozo wa Roho na kuhamasishwa na ushauri wa kiunabii wa Ellen White. Leo, tunapotembelea maeneo haya, tunaona urithi wenye nguvu wa imani, elimu, na huduma ambao unaendelea kulisukuma mbele Kanisa la Waadventista wa Sabato huko Afrika Kusini na kwingineko.

1 A.T. Robinson, “South Africa,” Review and Herald, gombo la 69, Na 8, Feb. 23, 1892, kur. 122,123.

 

2 Willeta Raley Bolinger, “Denomination’s First Woman Missionary Reaches 100” Review and Herald, Apr. 25, 1968, uk. 15.

 

3 Mark Henderson, The Kimberley Yearbook and Directory for 1902 (Kimberley, South Africa: Diamond Market Printing Works, 1902), uk. 436. 

 

4 General Conference Bulletin, Apr. 1, 1900, uk. 143.

 

5 Ellen G. White, Life Sketches of Ellen G. White (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1915), uk. 196.

Michael Sokupa ni mkurugenzi mwenza wa machapisho ya Ellen G. White huko Silver Spring, Maryland, Marekani.

Mwongozo wa kuanza haraka 

NA JANET PAGE

Je, ushawahi kusikia kuhusu jinsi maombi yanaweza kuibadilisha jamii yako? Ushawahi kusikia kuhusu kutembea kwa maombi? Kutembea kwa maombi ni huduma rahisi lakini yenye nguvu, iliyo mwafaka kwa watu wa umri wote, ambayo inaunganisha kutembea na kuomba, kukifunika kitongoji kilicholengwa au hata jiji na neema ya Mungu. Hivi hapa vidokezo vichache vya kukusaidia kupanga tukio la kutembea kwa maombi.

 

 

JIUNGE NA WAUMINI WENGINE

Unganisha imani yako na ya wengine ili kusaidia mtiririko wa maombi kwa mtindo wa mazungumzo ya kuvutia. Makundi makubwa wakati mwingine hushindwa kumpa kila mtu nafasi ya kushiriki. Kikundi cha watu wawili au watatu hufanya kazi vizuri zaidi. (Kwa mfano, kundi la watu nane kwa kawaida linaweza kugawanyika kuwa kwenye makundi ya watu wawili wawili wanapotembea, lakini wabaki wakionana au warudi kukutania mahali fulani.)

 

 

TENGA MUDA

Kutoa saa moja au mbili kamili kunawapa waombaji nafasi nzuri ya kushughulikia maandalizi na mijadala ya ufuatiliaji, ingawa mengi yanaweza kufanyika kwa muda mfupi.

 

 

CHAGUA ENEO

Muombe Mungu akuongoze. Ni bora zaidi kujifunza furaha ya kutembea kwa maombi katika maeneo ya ugenini; utarudi haraka kwenye eneo lako ukiwa na ndoto mpya. Vituo vya biashara na dini vinavutia sana, lakini hakuna kitu kinachofanana na kugusa familia, shule, na makanisa katika maeneo ya makazi. Tumia sehemu zilizoinuka za ardhi kuombea kitongoji kizima. Kaa muda mrefu katika maeneo maalum yanayoonekana kuwa ya muhimu. Unapoamua mahali pa kwenda katika jamii mpya, unaweza kuchagua kuungana na Mkristo anayehudumu katika eneo hilo ili maombi yako yaweze kuhusiana moja kwa moja na mipango ya huduma inayotekelezwa.

 

 

OMBA KWA UTAMBUZI

Ombea watu unaowaona. Unapofanya hivyo, utaona roho wa Mungu akiurekebisha upya moyo wako kwa usikivu wake mwenyewe. Ongeza majibu haya ya utambuzi kwa utafiti uliofanywa kabla. Tumia maarifa ya matukio ya zamani na mitindo ya sasa ili kusitawisha maombi. Juu ya yote, omba kwa Maandiko. Ikiwa huna kifungu maalum cha kuanzia, chagua mojawapo ya maombi ya kibiblia, na utagundua kwamba karibu yanaomba yenyewe.

 

 

MZINGATIE MUNGU

Fanya ahadi za Mungu badala ya  hila za Shetani kuwa msingi wa maombi yako. Utambuzi wako wa nguvu za giza wakati mwingine unaweza kuonekana kuwa unazidi mwongozo maalum wa Mungu kwa hali fulani. Fikiria urahisi wa kuanza kwa kutoa ombi la moja kwa moja mbele ya kiti cha enzi cha Mungu kabla ya kuanza mapambano ya moja kwa moja na nguvu za giza barabarani. Tafuta amri kutoka mbinguni ya kuzuia uovu ili watu wenye nguvu za Mungu waweze kuleta baraka za Mungu alizokusudia kwa ajili ya mji.

 

 

KUKUSANYIKA NA KUTOA TAARIFA

Shiriki kile ulichopitia na kuomba. Kusema baadhi ya ufahamu wako na imani yako kutawatia moyo wengine, pamoja na wewe mwenyewe. Panga mipango ya kutembea kwa maombi zaidi.

 

 

KURATIBU JUHUDI

Washirikishe watu wengine wanaosali ili kujiunga na marafiki waombee maeneo maalum. Kama kiongozi, unaweza kutaka kusaidia kuunda na kuchanganya vikundi vya maombi. Waombe waombaji wanaotembea kuandika kumbukumbu za maandishi zinazoonyesha ni maeneo gani yamefunikwa na aina gani ya maombi yameombwa. Changanya maarifa yenu ili kubaini ikiwa Mungu anakumbusha kulenga tena maeneo fulani. Hatimaye, lenga kufunika mji wako mzima, isipokuwa Mungu aelekeze vinginevyo.

Janet Page alihudumu kama katibu mwenza wa huduma ya wake wa wachungaji na familia zao, pamoja na huduma za maombi katika Konferensi Kuu kwa miaka kumi na miwili mpaka alipostaafu mnamo mwaka 2022. Yeye na mumewe Jerry kwa sasa wanaishi California, Marekani.

Katika jitihada za kushiriki nawe baadhi ya vipengele muhimu vya jibu kwa swali lako, nitatumia Mathayo 6:19-21 na muktadha wake. Nitafafanua neno “hazina” kama utajiri au vitu ambavyo ni vya thamani kwetu na tunavyomiliki kama rasilimali, pesa, vitega uchumi, n.k.

 

 

UTAJIRI NI MZURI

Yesu anawaona wanadamu kama viumbe ambao, kama chungu (Mithali 6:6-8),  hutafuta, hukusanya, na kuhifadhi kwa usalama. Anaonekana kupendekeza kwamba tunakusanya mali kwa sababu mambo yasiyotarajiwa yanaweza kutokea wakati wowote na tunataka kuyakabili kwa njia ya uwajibikaji na ijengayo. Tunatafuta na kukusanya, lakini tunahitaji mahali salama pa kuhifadhi hazina. Kwa Yesu, hazina ni nzuri, lakini lililo muhimu zaidi ni mahali tunapoiweka. Kama mahali sahihi pamepatikana, hivyo tungepata pumziko. Mahali tunapochagua pataathiri maisha yetu, kwa maana pataonyesha thamani yetu ya kweli: “Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mt. 6:21).

 

  

CHAGUZI MBILI

Kwa mujibu wa Yesu, tuna chaguzi mbili tu: mbingu au dunia. Katika mahubiri Yake, Yesu tayari ameonyesha kuwa duniani jina la Mungu halitukuzwi (Mt. 6:9) na mapenzi Yake hayatimizwi (Mt. 6:10). Utajiri wetu hauko salama duniani kwa sababu unatishiwa na nguvu za uharibifu za asili na ubinafsi wa mwanadamu. Kuhifadhi hazina zetu duniani kwa ajili ya usalama kunamaanisha kuwa mwishowe tutabaki mikono mitupu. Yesu anatuahidi mbingu, ufalme wa mbinguni, kama mahali bora zaidi, kwa kuwa umejaa amani, na wale wanaoweka hazina zao huko watapata amani. Mbinguni hakuna uovu katika asili wala katika moyo wa mwanadamu.

 

 

SARAFU YA MBINGUNI

Hatuwezi kuweka kwenye hifadhi ya mbinguni dhahabu, fedha, dola, au mali isiyohamishika, n.k. Ili utajiri uweze kuhifadhiwa mbinguni, unapaswa kubadilishwa kuwa sarafu ya mbinguni. Kimsingi, mtaji wetu ni maisha yetu na hazina ni matokeo ya jinsi tunavyoyatumia.

 

Kwa hivyo, kuweka hazina mbinguni kunahusiana zaidi na jinsi tunavyotumia na kusimamia utajiri wetu wa kidunia, na kwa nia na desturi zetu, kuliko kwa mali yenyewe. Hii inamaanisha kwamba, kwanza, utajiri unatakiwa kutumika kulingana na kanuni kuu: “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii” (Mt. 7:12). Rasilimali zetu zinapaswa kutumika kuwabariki wengine.

 

Pili, hazina yetu inapaswa kuwekwa kwa ajili ya kumtumikia Bwana pekee. “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. . . . Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” (Mt. 6:24).

 

Tatu, Kukusanya hazina mbinguni kunamaanisha kupanga upya vipaumbele vyetu: “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” (Mt. 6:33). Yesu anasisitiza kuwa wanadamu ni watafutaji kwa asili, lakini katika utafutaji wao wanapaswa kuupa kipaumbele ufalme wa Mungu. Maisha yetu na kila tunachomiliki vinapaswa kuwekezwa katika ukuaji wa ufalme wa Mungu. Kwa hivyo, tunatoa fungu la kumi na sadaka kubwa kwa ajili ya kujenga ufalme wa Mungu duniani. Ikiwa hazina inawekwa mbinguni kupitia jinsi tunavyotumia mali yetu duniani na kwa kuwa na msukumo sahihi, basi hazina yetu ya juu zaidi itakuwa ni tabia inayofanana na ya Yesu ambayo itahifadhiwa milele.

Angel Manuel Rodríguez, Th.D., amestaafu baada ya kutumika kama mchungaji, profesa, na mwanateolojia.

Kuzuia kusinyaa kwa tishu ya mifupa kabla hakujaanza 

Mama yangu ana kusinyaa kwa tishu ya mifupa na hivi karibuni alivunjika mkono baada ya kujikwaa. Ninaweza kufanya nini ili kuzuia kusinyaa kwa tishu ya mifupa ninapozeeka?

Kusinyaa kwa tishu ya mifupa ni hali inayosababisha mifupa kuwa dhaifu na rahisi kuvunjika. Huathiri zaidi wanawake waliokoma hedhi. Hii ina uhusiano na kupungua kwa homoni ya estrojeni, ambayo inahitajika ili kudumisha uzito na uimara wa mifupa. Mkakati wa kuzuia  kusinyaa kwa tishu ya mifupa ni kuzingatia marekebisho ya mtindo wa maisha, uboreshaji wa lishe, mazoezi ya mara kwa mara, na matibabu ya kitabibu ili kulinda afya ya mifupa.

 

Lishe inafanya kazi makini sana katika kujenga na kudumisha mifupa imara. Ulaji wa kutosha wa kalsiamu na vitamini D ni muhimu. Kalsiamu ni madini ya msingi kwenye mifupa, na vitamini D husaidia mwili kufyonza madini hayo kwa ufanisi. Wanawake wanapaswa kulenga ulaji wa kalsiamu wa miligramu 1,000 (mg) kwa siku kabla ya kufikisha miaka 50, na miligramu 1,200 (mg) baada ya miaka 50. Vyakula vyenye kalsiamu kwa wingi ni pamoja na bidhaa za maziwa, mboga za majani, mlozi, na nafaka zilizoongezewa virutubisho.

 

Vitamini D, inayojulikana kama "vitamini ya jua," inaweza kuzalishwa kwenye ngozi kupitia mwanga wa jua. Hata hivyo, vyanzo vya chakula kama viini vya mayai, vyakula vilivyoongezewa, virutubisho, au hata samaki wenye mafuta (kama salmoni na makrill) vinaweza kuwa muhimu, hasa katika maeneo yenye mwanga mdogo wa jua. Kiwango kinachopendekezwa cha vitamini D kwa siku ni 600–800 vipimo vya kimataifa (IU), kutegemea na umri na hali ya afya.

 

Shughuli za mwili ni muhimu katika kujikinga na kusinyaa kwa tishu ya mifupa. Mazoezi ya kubeba uzito na yale ya kustahimili yanafaa zaidi. Shughuli kama kutembea, kukimbia, mazoezi ya viungo vinavyoongeza hewa, na tenisi husaidia kuimarisha mifupa na misuli, kuboresha uwiano wa mwili, na kupunguza hatari ya kuanguka. Mazoezi ya kustahimili, kama kunyanyua uzito au kutumia bendi za mazoezi, husaidia kuongeza zaidi uzito wa mifupa.

 

Ratiba thabiti ya mazoezi ya mara kwa mara ni muhimu kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 na 30 wakati uzito wa mifupa unafikia kilele chake. Shughuli za kila siku za wanawake wazee hupunguza kasi ya upotevu wa mifupa na kuboresha afya kwa ujumla. Kudumisha uzito mzuri wa mwili ni muhimu. Kuwa na uzito mdogo kupita kiasi kunaweza kusababisha kupungua kwa uzito wa mifupa, wakati uzito kupita kiasi unaweza kuongeza hatari ya kuvunjika kwa mifupa ya nyonga na mgongo wa chini.

 

Uvutaji wa sigara ni sababu kuu ya hatari ya kusinyaa kwa tishu ya mifupa; hupunguza kiwango cha estrojeni na huathiri ufyonzaji wa kalsiamu. Wavutaji wanapaswa kutafuta msaada wa kuacha kuvuta ili kulinda mifupa yao na afya kwa ujumla. Matumizi ya pombe pia yanaweza kuongeza hatari ya kusinyaa kwa tishu ya mifupa.

 

Wanawake waliokoma hedhi walio katika hatari kubwa ya kusinyaa kwa tishu ya mifupa wanaweza kunufaika na tiba ya kubadilisha homoni (HRT). Hata hivyo, HRT si chaguo linalofaa kwa kila mtu; hatari na faida zake zinapaswa kujadiliwa na daktari wako.

 

Dawa kama bisphosphonates hupunguza upotevu wa mifupa. Modulatori za vipokezi vya estrojeni (SERMs) zinaweza kuwa na matokeo ya kulinda mifupa. Uchunguzi wa uzito wa mifupa wa mara kwa mara, hasa kwa wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 65 au wale walio na vihatarishi, inaweza kusaidia kutambua mapema upotevu wa mifupa na kuelekezwa matibabu.

 

Kuongeza uelewa kuhusu osteoporosis ni muhimu kwa ajili ya kuizuia. Wanawake wanapaswa kuelimishwa kuhusu vihatarishi, umuhimu wa matibabu ya mapema, na jinsi uchaguzi wa mtindo wa maisha unavyoathiri afya ya mifupa. Majadiliano ya kutia moyo na watoa huduma za afya kuhusu afya ya mifupa na uchunguzi vinaweza kusaidia kugundua mapema na kupata matokeo bora.

 

Kuzuia kusinyaa kwa tishu ya mifupa kwa wanawake kunahitaji mbinu nyingi zinazoambatana na lishe sahihi, mazoezi ya mara kwa mara, mtindo wa maisha wenye afya, na, ikilazimu, matibabu ya kitabibu. Kwa kuipa kipaumbele afya ya mifupa mapema na kwa uthabiti, wanawake wanaweza kupunguza hatari ya kusinyaa kwa tishu ya mifupa na kufurahia shughuli na maisha yenye afya mpaka mwisho! (Angalia Mithali 3:5-8).

Zeno L. Charles-Marcel, daktari wa magonjwa ya ndani aliyeidhinishwa na bodi, ni mkurugenzi wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu.

 

Peter N. Landless, daktari wa magonjwa ya moyo aliyeidhinishwa na bodi na mkurugenzi mstaafu wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu, pia ni daktari wa magonjwa ya ndani aliyeidhinishwa na bodi.

“Haya, jaribu saladi ya dandelion!”

 

José aliishi katika jamii ndogo ya milimani kaskazini mwa San Francisco, California. Familia yake ya Kimeksiko ilikuwa maskini, na chakula chao kilikuwa rahisi, mara chache kilijumuisha saladi za kifahari. Kisha José alipata kitabu cha Catherine Gearing, kitabu kilichoahidi maisha bora. Kichwa chake kilisomeka A Field Guide to Wilderness Living, na jalada lake lilionyesha mlima mzuri, ziwa, moto wa kambi, na hata mbwa kipenzi.

 

José alisoma kila neno, akapigia mstari mapishi yake aliyopenda, kisha akaelekea msituni karibu na nyumbani kwake, akiwa na hamu ya kupata vyakula vitamu vilivyoahidiwa, akijifunza kuhisi uwepo wa Mungu karibu naye, akifurahi kujua kuwa Mungu aliumba yote haya kwa ajili yake!

 

Mpaka Catherine Gearing alipompa mwongozo, José hakujua ni wapi angepata mnanaa au kwamba dandelion zilikuwa chakula. Alihifadhi maelekezo yake akilini na kujaribu ladha za mimea hiyo ya njano na kijani iliyoenea karibu na nyumba yake ya mlimani. Punde familia yake ikaanza kufurahia saladi tamu za dandelion!

 

Kwa bahati mbaya, kitabu hicho kilikuwa cha jalada laini na kilianza kuchakaa kadri alivyokisoma, kikiwa kimepigiwa mstari, na kukunjwa pembe za kurasa muhimu zaidi. Kaka yake José alimpa suluhisho.

 

"Vipi kama nitakuwekea jalada gumu kwenye kitabu chako cha dandelion?" Alifanya kazi katika karakana ya kujalidi vitabu huku akisoma huko Montemorelos, Mexico.

 

Kitabu kipya kilichofunikwa kwa jalada gumu kilikuwa kizito zaidi, lakini José alikibeba kila mahali, akijaribu suluhisho la porini la Catherine kwa kila tatizo alilokumbana nalo.

 

"Kitabu hiki kimebadilisha maisha yangu," José alimwaambia kila mtu aliyekuwa tayari kumsikiliza, na hata wale waliocheka saladi zake za dandelion na kugeuza pua zao mbali na mnanaa wake safi.

 

 

WITO WA HUDUMA

Majira ya joto alifikisha miaka 16, rafiki yake mchungaji alimshawishi José kujiunga na kikundi kilichoitwa Community Crusade Against Drugs na kuuza vitabu mlango kwa mlango huko San Francisco. "Ilikuwa njia pekee niliyoweza kupata pesa za kutosha kujilipia ada yangu ya shule," José anakumbuka. “Tulikuwa vijana kadhaa tukifanya kazi pamoja. Nilijiachia masharubu ili nionekane mkubwa kidogo, na mchungaji wa kanisa dogo la Kihispania alituruhusu mimi na Javier kulala katika vyumba vya Shule ya Sabato. Tulihitajika kusafisha kila kitu kila Ijumaa, lakini ilifanikiwa. Tulikuwa hata na bafu!”

 

Saa za kazi zilikuwa ndefu, lakini majira yote ya joto walitembelea maelfu ya nyumba huko San Francisco Kusini. Kila jioni, baada ya kumpeleka mmoja wa wenzao nyumbani kwake kwenye Treasure Island, José na Javier walirudi kwenye magodoro yao ya kulalia ndani ya vyumba vya Shule ya Sabato. Njiani, walipitia mkahawani kwa ajili ya chipsi na sharubati ya maziwa.

 

"Chipsi zilikuwa chakula chetu,” José anacheka, “na sharubati ya maziwa ilikuwa kitindamlo chetu," 

Asubuhi moja walipokuwa wakijiandaa kuondoka kwenye hoteli yao ya Shule ya Sabato, simu ya kanisa iliita. José alijibu.

 

"Halo. Hili ni Kanisa la Waadventista wa Sabato?"

"Ndio."

 

“Jina langu ni Nancy, na mimi ni muuguzi katika Kituo cha Matibabu cha Chuo Kikuu cha California. Tuna mgonjwa hapa anayetarajiwa kufanyiwa upasuaji nyeti sana, na angependa mchungaji kutoka kanisani kwake aje kuomba naye. Mnaweza kufanya hivyo tafadhali?”

 

“Samahani mama, lakini hili ni kanisa la Kihispania, na mchungaji wetu hajui hata neno la Kiingereza, hivyo hawezi kusaidia. Subiri kidogo, labda naweza kupata namba ya kanisa la Kiingereza . . .”

 

Alitafuta namba katika saraka ya kanisa na kumpatia muuguzi.

 

“Hakufurahia kupiga simu nyingine. Lakini hata hivyo nilimpatia namba hiyo na kisha nikaharakisha kuendelea na kazi.”

 

Usiku huo, karibu saa tano usiku, José na Javier walipoagiza chipsi na malti zao, José ghafla alikumbuka ile simu.

 

José alishika bega la Javier. “Hakuna mtu aliyekwenda kumuona yule mwanamke. Tunapaswa kwenda kumuona. Sidhani kama yule muuguzi alipiga simu kwa kanisa lingine, na sidhani kama mchungaji alikwenda kuomba pamoja naye anaenda kufanyiwa upasuaji nyeti sana kesho, tunapaswa kwenda huko.”

 

“Hapana. Muda wa kutembelea umepita sana,” Javier hakukubaliana. “Tumechelewa sana kwenda kwa sasa. Hata hivyo hawawezi kuturuhusu. Tuangalie. Sisi ni watoto wenye nywele ndefu, malapa, na suruali za mlegezo chini. Tunaonekana kama mahipi wa Kimeksiko.”

 

“Lakini yule mwanamke alitaka mchungaji Msabato kuomba pamoja naye. Tunatakiwa kwenda kumuona,” José alisema. “Twende!”

 

 

KUSHINDA VIZUIZI 

Wawili hao walitoka kwenye mkahawa na kukimbia juu ya mtaa wa sokoni juu ya vilima

kadhaa vya mteremko mkali vya San Francisco kuelekea hospitalini. Nafasi pekee ya maegesho

waliyoipata ilikuwa ng’ambo ya barabara kutoka kwenye mlango wa nyuma wa hospitali.

 

“Kila kitu kimefungwa,” Javier alisema. “Tutafikaje ndani?”

 

“Kweli, hawawezi kuturuhusu kuingia kwa mlango wa mbele,” José alisema. “Tujaribu huu.”

 

Wavulana walikimbia kuvuka barabara kwenye vivuli kando ya mlango na kujaribu kufungua. Haukuwa umefungwa! Kwa muda mfupi walikuwa ndani ya hospitali, bila wazo la jinsi ya kufika kwa mwanamke ambaye alikuwa anafanyiwa upasuaji kesho yake asubuhi.

 

“Harakisha” alisema José akimvuta Javier kupita ukumbi kuelekea kwenye lifti. “Mungu atatusaidia!”

 

José alibonyeza kitufe cha ghorofa ya 9. “Tujaribu hii.”

 

“Mlango utakapofunguka, tutatoa vichwa vyetu nje na kisha tutachukua hatua.”

 

Vijana hawa walitoka kwenye lifti na kuingia kwenye korido ya giza ambayo ilionekana kuwa ndefu sana.

 

Mbali kidogo, kivuli cha muuguzi kilionekana kwenye mwanga wa mbali.

 

Walitembea polepole, kandambili zao zikiigonga sakafu, na walifika kwa muuguzi ambaye bila shaka

alikuwa na hofu na wahipi hawa wawili wa Kimeksiko.

 

“Samahani kwa kuchelewa “José alianza, “lakini asubuhi ya leo muuguzi alipiga simu kusema kwamba kuna mwanamke atafanyiwa upasuaji wa saratani kesho, na alitaka mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato aje kumuombea. Sisi si wachungaji, lakini tunaweza kuomba. Utatupeleka kwake tafadhali?”

 

 Muuguzi aliwatazama wawili hao na akaenda kuchukua simu ili kuita walinzi.

 

“Saa za kutembelea zimekwisha saa nne zilizopita,” alisema, akiwa anainua simu.

 

“Najua,” José alionyesha tabasamu lake zuri. “Lakini saa za kutembelea hazitumiki kwa wahudumu wa dini, sivyo?”

 

Alisimama mbele yao, kama ukuta usiohamishika. Kisha akasema, “Sipendi hivi, lakini nifuateni. Ninamjua mwanamke anayetaka maombi.”

 

Aliwaongoza chini kwenye korido nyingine ndefu na kugonga taratibu mlango uliofungwa.

 

“Mchungaji yuko hapa,” alisema akiwaongoza José na Javier ndani ya chumba.

 

Taa ya usiku ilikuwa inawaka na mwanamke kwenye kitanda alikuwa akilia.

 

“Usiniambie kwamba ninyi ni Waadventista,” alishangaa. “Hamuonekani kama wachungaji. Mnaonekana kama wahipi wa Kimeksiko! Mnafanya nini hapa?”

 

“Tunatoka katika kanisa la Waadventista wa Sabato,” alisema José, akitumaini kumaliza hili haraka iwezekanavyo. “Tuko hapa kuomba pamoja na wewe.”

 

“Nakufa kwa saratani, na sasa, saa sita usiku, wahipi wawili wa Kimeksiko Waadventista wanatembea kutoka mitaa ya San Francisco kuja kuomba pamoja na mimi. Sitasahau hili!”

 

José alisogea karibu na kitanda. “Jina lako nani bibie?”

 

“Mimi ni Catherine Gearing,” alisema mwanamke huyo. “Labda umesoma kitabu changu, The Field Guide to Wilderness Living?”

 

José alishika mikono yake yote miwili. “Wewe ni Catherine Gearing! Nimekariri kila ukurasa wa kitabu chako. Umenifunza kuhisi uwepo wa Mungu karibu nami. Ulibadilisha maisha yangu!”

 

 Uwepo wa Mungu ulijaza chumba, na saa iliyofuata ilijaa hadithi za furaha, vicheko vya sauti, maombi mengi, na matumaini.

Dick Duerksen, mchungaji na msimuliaji wa hadithi, anaishi Portland, Oregon, Marekani.

Reba
Maombi na wema barabarani 

Na Cathlynn Doré Law

Kila asubuhi, Bibi huvaa kitambaa chake timtim cha joto cha kichwa, viatu vyake vya kutembelea, hubeba mkoba wake mgongoni, na kuchukua fimbo yake ya kutembelea mlangoni ili kuanza safari ndefu ya kwenda kuchukua barua zake. Alipenda kuandika barua na kupokea barua! Kila siku, alikuta bili, majarida, na wakati mwingine barua kwenye kisanduku chake cha barua. Aliziweka kwenye mkoba wake wa mgongoni kwa ajili ya safari ndefu ya kurudi nyumbani.

 

Siku moja, Bibi alipokuwa akipita kwenye uwanja wa jirani yake, alisikia mbwa akibweka kwa sauti kubwa. Macho yake yakatafuta uwanjani. Hakika, mbwa wa manjano alikuwa akikimbia moja kwa moja kuelekea kwake.

 

“Nitampuuza,” aliamua, bila hata kumwangalia mbwa aliyekuwa akibweka.

 

Lakini badala ya kumpuuza Bibi, mbwa alijipenyeza chini ya uzio uliowatenganisha na akaanza kumfuata. Mbweko wake ulionekana kuwa wa kutisha zaidi alivyokaribia.

 

Bibi aligeuka na kusema kwa sauti ya kuamuru, “Rudi nyumbani!”

 

Mbwa mkubwa alisimama na kujirudisha chini ya uzio.

 

“Ah-h-h-h,” Bibi akatikisa kichwa, “Kwa hiyo mbweko wako ni mbaya zaidi kuliko kung’ata kwako! Hebu tuwe marafiki,” alimuita huku mbwa mkubwa akimtazama kutoka upande wa pili wa uzio. Mbwa alimtazama na akarudi nyumbani -mwake.

 

Asubuhi iliyofuata, Bibi alisikia mbweko uleule wa kawaida. Safari hii, mbwa mkubwa alikuwa akikimbia nyuma ya trekta iliyokuwa ikitembea polepole.

 

Trekta iliposimama karibu naye, Bibi akapunga mkono, “Habari jirani!” Kulikuwa na mzigo mkubwa wa nyasi kwenye ndoo ya trekta.

 

Baada ya mazungumzo kidogo kuhusu hali ya hewa, Bibi akasema, “Kwa hiyo huyu lazima awe mbwa wako. Ana sauti kubwa sana!” alicheka.

 

“Oh, hatakuumiza,” jirani alitabasamu. “Jina lake ni Reba.” Baada ya mazungumzo kidogo, alienda na mzigo wake wa nyasi kwenda kulisha ng’ombe kwenye uwanja.

 

Kuanzia hapo, kila Reba alipokimbia uwanjani na kubweka karibu na uzio, Bibi alimsalimia.

 

“Habari, Reba, sasa sisi ni marafiki kwa kuwa najua jina lako.” Reba angepepesa macho na kugeuza kichwa, akimtazama Bibi kwa jicho moja. Bado hakuwa akimwamini.

 

Siku moja ya baridi kali, badala ya kumwona Reba akikimbia uwanjani kama kawaida, kulikuwa na kitu tofauti. Bibi alisimama na kuchungulia kuona kilikuwa ni nini. 

 

Reba alipokaribia, Bibi alitweta.

 

“Unatembea kwa kuchechemea! Nini kilichotokea?” Bibi aliuliza. Lakini bila shaka, Reba hakuweza kujibu, aliendelea tu kubweka na kumtazama Bibi kwa wasiwasi.

 

Moyo wa Bibi ulijawa na huruma alipoona mguu wa Reba uliovimba. Ulikuwa umeongezeka mara mbili kwa ukubwa wa kawaida na ulikuwa mwekundu. Bibi alitikisa kichwa chake taratibu, akipiga kidoko.

 

“Pole sana, msichana,” Bibi alinong’ona. “Naweza kufanya nini?” Bibi aliwaza kwa sauti.

 

Aliporudi nyumbani, alimwambia Babu kuhusu mguu wa Reba uliovimba.

 

“Huenda alinaswa kwenye mtego,” Babu alisema. “Asipopata viua-sumu kadhaa, maambukizi yanaweza kuendelea na anaweza kufa.”

 

“Ulipokuwa na maambukizi mguuni, tungeuosha kwa maji moto halafu ya baridi ili kuongeza chembe nyeupe za damu kwa ajili ya uponyaji. Tunaweza kufanya hivyo?” Bibi aliuliza kwa macho yaliyosihi.

 

Babu alitikisa kichwa chake taratibu. “Sijui.”

 

“Lakini utajaribu pamoja na mimi, sivyo?” Bibi alimsihi.

 

“Sawa, kama unataka,” Babu alikubali. “Wewe weka vitu pamoja, na nitakupeleka kwa majirani.”

 

Uso wa Bibi uliojikunja kwa wasiwasi ulibadilika haraka kuwa tabasamu pana.

 

Alienda bafuni na kukusanya vitu ambavyo vingesaidia kutibu mguu wa Reba. Alichungulia kwenye kabati. “Bendeji, kamba ya kufungia, dawa ya kuchua, mkaa . . .” Bibi alirudia mwenyewe kwa upole.

 

Alipokuwa na kila kitu kwenye ndoo mbili, Babu alingurumisha gari lenye magurudumu manne. 

Ilichukua dakika chache tu kufika kwenye njia ya changarawe kuelekea kwenye nyumba ya jirani yao. Walipogeuka kwenye njia ya kuelekea kwenye nyumba, Mibweko ya Reba ilianza. Akiizima injini, Bibi alimuona.

 

“Njoo hapa, msichana,” alinyoosha mkono wake. Lakini Reba alirudi nyuma kwa haraka na akaendelea kubweka kwa sauti. Babu alienda kwenye nyumba na kubisha hodi. Hakukuwa na jibu. Baada ya kubisha kwa mara ya pili kwa sauti kubwa, bado hapakuwa na jibu.

 

“Haya,” Bibi alishusha pumzi, “Hatuwezi kumtibu bila ruhusa.

 

Na hataniruhusu nimsogelee—sembuse kumgusa,” Bibi alikiri. Hakukuwa na la kufanya zaidi ya kupanda kwenye gari lao la miguu minne na kurudi nyumbani. Bibi kwa huzuni aliweka vitu.

 

Siku iliyofuata, Reba alijipenyeza chini ya uzio na kumfuata Bibi akibweka mpaka Bibi aliposhindwa kuvumilia tena.

 

Bibi akasimama, akageuka kumuelekea Reba, akafumba macho, na kuomba, “Ee Mungu Muumba, Unaweza kuona Reba na mguu wake uliojeruhiwa. Ulimuumba na Unampenda. Tumejaribu kumsaidia, lakini hakuna tunachoweza kufanya. Unaweza kumponya tafadhali? Kwa jina la Yesu, Amina.”

 

Majira ya baridi kali, Bibi alikanyaga theluji katika matembezi yake kuelekea kwenye sanduku la barua. Alisikiliza na kumtafuta Reba, lakini hakusikia mbweko. Hakuna umbo la miguu mitatu lilionekana likichechemea kwenye nyasi. Bibi alianza kukubali mabaya zaidi. Reba huenda alipoteza pambano lake dhidi ya maambukizi kwenye mguu wake na akafa.

 

Kisha, asubuhi moja ya masika, wakati Bibi alikua akiepuka madimbwi ya matope yaliyoyeyuka kutoka kwenye theluji, alisikia mbweko. Alitazama kwa mshangao kuelekea barabara ya vijijini.

 

“Re–ba?” alisema taratibu.

 

Reba alipokaribia, Bibi aliona mguu wake ukigusa barabara polepole.

 

“Reba! Ni wewe!” Bibi alishangaa. Reba alisimama karibu zaidi kuliko wakati wowote ule. Bibi aliutazama mguu wake uliokuwa umejeruhiwa. “Haujavimba,” aliona.  “Na unaubebesha uzito kidogo,” machozi yalitoka kwenye macho ya Bibi. “Mungu amekuponya,” alinong’ona. Akisimama hapo hapo barabarani, alizungumza na Mungu.

 

“Umefanya, Mungu Baba,” Bibi alisema huku machozi yakidondoka mashavuni mwake. “Umemponya Reba wakati sikuwa na msaada wa kufanya chochote kumsaidia. Ahsante kwa kuwa mwaminifu sana.”

 

Wakati Bibi anafungua macho yake, Reba alikuwa amesimama kimya mbele ya Bibi. Taratibu sana Reba alisogea kuelekea kwa Bibi. Akipepesa macho yake makubwa, alinusanusa mkono wa Bibi aliokuwa ameunyoosha. Taratibu, Bibi alilainisha nywele za Reba za kwenye paji la uso.

 

Reba alizidi kupona, na muda si mrefu, alikuwa akikimbia kawaida kwenye uwanja, akibweka kwa nguvu. Bibi alitabasamu peke yake.

 

“Umefanya, Mungu Baba,” alijirudia mwenyewe.

Cathlynn Doré Law ni mwandishi na mwalimu mstaafu anayependa kusafiri na familia yake.

Mchapishaji
Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review
Justin Kim

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa
Hong, Myung Kwan

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World 
Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun, Dong Jin Lyu

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review
Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani
Enno Müller, Beth Thomas, Jonathan Walter 



Wahariri waliopo Seoul Korea


Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali
Gabriel Begle

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi
Daniel Bruneau

Meneja wa Shughuli
Merle Poirier

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri
Marvene Thorpe-Baptiste

Wahariri/Washauri wengine
E. Edward Zinke

Meneja wa Fedha
Kimberly Brown

Mratibu wa Usambazaji
Sharon Tennyson

Bodi ya Utawala
Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong, Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Tae Seung Kim; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

Maelekezo ya Usanifu na Muundo
Types & Symbols

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:
Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

Tafsiri
Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

Msomaji wa prufu
Lilian Mweresa

Usanifu wa toleo la Kiswahili
Daniella Ingram, Ashleigh Morton, Teya Esterhuizen, Digital Publications

Uchapishaji wa Kidijitali
Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu
Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott
/Types & Symbols

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org Tovuti: www.adventistworld.org

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

Vol. 21, No. 4

swipe down
powered by
SEND-IT.ME

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Please wait ...