

Kuanzia Agosti 2025, “Adventist World” itaunganishwa na jarida la Adventist Review. Kwa nembo mpya, muundo mpya, na mtazamo mpya, tutaendelea kukuhudumia kwa maudhui ya kibiblia, yenye kusisimua, na yanayofaa kwa Waadventista wa Sabato.
Unaweza kuendelea kusoma jarida lililounganishwa la Adventist Review kwa Kiswahili kupitia majukwaa yafuatayo: WhatsApp, Facebook, na maktaba yetu ya kidijitali. Kila mwezi, kiungo cha toleo jipya kitawekwa kwenye majukwaa haya. Kama ilivyo kawaida, tutakujulisha mara toleo jipya litakapotolewa.
Hivi ndivyo unavyoweza kufikia majukwaa hayo:
Upatikanaji wa WhatsApp
Bofya kiungo au skani Msimbo wa QR ili kufungua chaneli ya Matangazo ya WhatsApp (WhatsApp Broadcast) ya Adventist Review Swahili:


Usisahau kubonyeza kitufe cha ‘FOLLOW’ kilicho juu upande wa kulia wa skrini ya WhatsApp, na pia washa arifa (unmute notifications) kwa kubonyeza ikoni ya ‘BELL’ (juu kulia), ili usikose toleo lolote jipya kutoka kwetu.

Upatikanaji wa Facebook
Bofya kiungo hapa chini au skani Msimbo wa QR ili kufungua ukurasa wa Facebook wa Adventist Review Swahili:


Kwa kubonyeza "Like" kwenye ukurasa huu, utapata habari zetu za hivi punde na utaweza kututumia ujumbe kwa maoni yoyote unayotaka kushiriki.

Upatikanaji wa Maktaba ya Kidijitali
Maktaba yetu ya kidijitali ina mkusanyiko wa majarida yote ya Adventist Review Swahili. Unaweza kuhifadhi mkusanyiko huu kwenye simu yako au kompyuta kwa ufikiaji rahisi na wa haraka. Bofya kiungo hapa chini au skani Msimbo wa QR ili kufungua:


Fuata maelekezo ya kufunga maktaba hii kwenye kifaa chako (simu au kompyuta). Usisahau kusajili (subscribe), ili tuweze kukutaarifu kila toleo jipya linapotolewa.
Kwa maoni au mrejesho wowote, tafadhali jisikie huru kututumia barua pepe kupitia anwani kwambokaj@ecd.adventist.org. Tunathamini sana mawasiliano kutoka kwako, na tunajivunia kuwa na uhusiano mzuri na wasomaji wetu wa Adventist Review Swahili.
Asante sana kwa ushirikiano wako, na Mungu akubariki sana.
Timu ya Adventist Review Swahili
















Mchoro wa Kifuniko na Dennis Wardzala




Katika baadhi ya maeneo ya Kanisa letu zuri la Waadventista wa Sabato duniani kote, desturi isiyo na hatia ya kumpa mchungaji mmoja kanisa moja imeanza kuota mizizi. Ingawa zipo sababu mbalimbali zilizochangia kupokelewa kwa mfumo huu, nyingi zikiwa na nia njema ya kuimarisha uongozi na huduma ya kichungaji, bado mfumo huu unawakilisha wazo hatari linalozuia ukuaji wa kiroho na kuathiri maendeleo ya kazi ya utume. Mfumo huu huwafanya waumini kumtegemea mno mchungaji, badala ya kushiriki kikamilifu katika huduma za kanisa mahalia. Kwa kufanya hivyo, unadhoofisha fundisho la kibiblia linalofundisha kuwa waumini wote wameitwa kuhudumu kama makuhani wa Bwana.
Kwa asili yake, mfumo wa kumpa mchungaji mmoja jukumu la kuongoza kanisa moja huzalisha aina ya Ukristo unaojikita katika mahitaji binafsi na utegemezi. Kwa kuwa mchungaji ndiye anayehubiri kila Sabato, kutembelea wagonjwa, kuendesha uinjilisti na kusimamia shughuli zote za huduma, washiriki wa kanisa hujiona kama watazamaji badala ya washiriki hai wa kazi ya Kristo. Wanaanza kuona kanisa kama mahali pa kupokea huduma tu kama wanunuzi wa ibada badala ya kuwa wanafunzi wanaoshiriki kikamilifu. Matokeo yake, mzigo wa huduma unamlemea mchungaji peke yake, hali inayodhoofisha maisha ya kiroho ya kanisa. Inazima ubunifu, uongozi, na ushiriki wa waumini. Badala ya kushiriki baraka, waumini wanajifunza tu kuzipokea. Mchungaji anageuka kuwa mtendaji wa pekee, huku kanisa likibaki kama watazamaji. Mwishowe, kusanyiko linakosa uhai na nguvu ya kiroho, na hubadilika kuwa kundi lisilokuwa na mvuto wala ushawishi katika jamii.
Washiriki humtegemea mchungaji kwa kila hitaji la kiroho, na mara nyingi hupuuzia wajibu wao wa kuhudumu, kufundisha na kuongoza. Baadhi huwafanya wachungaji kuwa wasafishaji wa kanisa, madereva wa magari ya kanisa, na hata walezi wa vijana hadi jioni. Mchungaji anapokuwa likizo, shughuli za kanisa hupungua au kusimama kabisa. Na mchungaji akihamishwa, hamasa hupungua, msukumo hupotea, na lawama hurushwa kwa konferensi ya kanisa mahalia. Je, ni maandiko gani ya Biblia yanayounga mkono maisha ya kanisa ya aina hii?

Kanisa la Agano Jipya lilistawi chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu na waumini waliowezeshwa kuhudumu. Paulo aliunda timu za wazee na kuwafundisha waumini kushiriki kueneza Injili. Kristo Mwenyewe aliwafundisha wanafunzi wake kumi na wawili si kwa ajili ya kumtegemea kimwili kila wakati, bali ili waweze kubeba ujumbe Wake hata baada ya Yeye kuondoka. Hata hivyo, katika maeneo mengi ya Kanisa la Waadventista duniani, shughuli zote za kiroho zimekwenda mikononi mwa mtu mmoja tu, mchungaji.
Mbaya zaidi, mfumo huu huzuia kuanzishwa kwa makanisa mapya. Uinjilisti wa kuifikia jamii, mabadiliko ya kijamii, na ufundishaji wa Neno la Mungu hupooza kwa sababu hautegemei ushiriki hai wa washiriki. Baadhi ya makanisa yametambua ukosefu wa ukuaji, lakini badala ya kuwahamasisha washiriki kushiriki zaidi, wameongeza idadi ya wachungaji.
Zipo njia bora zaidi. Wachungaji wanapaswa kusaidia waumini kushiriki katika uinjilisti, si kufanya kila kitu wao wenyewe mbele ya kanisa. Wakati wachungaji wanaposaidia makanisa madogo au kuanzisha makanisa mapya, washiriki wanapaswa kuinuka, kuhudumu, na kumiliki utume wa malaika watatu. Huu ni mtindo wa maeneo ambayo kihistoria washiriki walishirikiana na wachungaji katika mtaa, hadi wakaweza “kukua” na kuingia katika mfumo wa mchungaji mmoja kwa kanisa moja. Hata hivyo, ukuaji wa kanisa haupaswi kutumika kama sababu ya kubaki katika mfumo usiofaa. Kanisa halipaswi kusubiri mtu mmoja afanye kile ambacho Mungu aliwaita kufanya kwa pamoja kama mwili mmoja.
Baadhi ya mawazo hatari hutokana na uhuru wa kiteolojia, sheria za kidini au uzoefu wa maisha ya kila siku. Lakini wazo hili hatari limetokana na nia isiyo na hatia, kutaka mchungaji mmoja aweze kufanya kila jambo. Ni wakati wa kukataa mifumo inayolidhoofisha kanisa na kuchochea ukuaji wake kupitia ushirikiano wa kweli. Hebu tufanye kazi hii kwa pamoja.

Justin Kim, Mhariri wa Adventist Review





Idadi ya watu waliobatizwa katika juhudi za pamoja za uinjilisti zilizoendeshwa na makanisa ya Waadventista wa Sabato wa Phu Nhuan na Ho Chi Minh International. Mfululizo huu wa siku mbili, uliofanyika Juni 6–7, ulikuwa sehemu ya mpango wa Harvest (Mavuno) 2025 wa Divisheni ya Asia-Pasifiki Kusini, kampeni ya mwaka mzima inayohamasisha makanisa ya eneo hilo kushiriki kikamilifu katika uinjilisti na huduma za kijamii. Vietnam, ambayo ipo ndani ya dirisha la 10/40 — eneo ambalo bado lina upatikanaji mdogo wa injili kwa watu wengi — inaendelea kutoa fursa muhimu za ukuaji wa kiroho na kazi ya kimisionari, kama ilivyodokezwa na viongozi wa kanisa wa eneo hilo.

“Ujumuishaji wa kweli hujenga mazingira ambayo kila mtu ana sauti, nafasi, na thamani. Dhamira hii inaakisi upendo wa Mungu, ambao unatamani kuwaokoa wote bila ubaguzi.”
– Rainer Wanitscheck, Mkurugenzi wa Huduma za Watu wenye Mahitaji Maalum wa Waadventista. (Adventist Possibility Ministries – APM) katika Divisheni ya Inter-Ulaya, akielezea mkutano wa kwanza wa APM uliofanyika Costa de Lavos, Ureno, tarehe 6–8 Juni. Tukio hilo liliwakutanisha watu wenye ulemavu, walezi wao, viongozi wa maeneo, wachungaji, na familia kwa kipindi cha mafunzo, mapokezi yenye joto la upendo, na uchambuzi wa Neno la Mungu. Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu lilikuwa kuhimiza ujumuishaji na kuthamini mchango wa watu wenye ulemavu ndani ya Kanisa la Waadventista wa Sabato.


“Jengo hili ni zaidi ya muunganiko wa matofali na chokaa. Linaakisi imani yetu kwa Yesu kama Mganga Mkuu na wajibu wetu wa kuendeleza huduma Yake ya uponyaji kwa njia za vitendo na zinazoonekana.”
– Ma Rizaline Alfanoso, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya katika Divisheni ya Asia-Pasifiki Kusini, akizungumzia hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa jengo jipya la huduma ya hemodialysis katika Chuo cha Mountain View, mji wa Valencia, Bukidnon, Ufilipino. Tukio hilo liliashiria hatua muhimu katika juhudi za chuo hicho kuhudumia jamii kwa huduma bora za afya zilizojaa huruma yenye msingi wa Kristo. Jengo hili linatarajiwa kutoa huduma ya dialysis inayofikika kwa urahisi, hasa kwa wagonjwa wanaoishi katika maeneo ya mbali ya Bukidnon na mikoa jirani, ambako huduma kama hizi bado ni adimu.




Idadi ya familia huko Amaluza, Ecuador, ambazo zimeonyesha nia ya kupokea masomo ya Biblia majumbani mwao. Jamii hii, iliyoko katika jimbo la Loja kusini mwa Ecuador, imejikita sana katika mila za kidini na ni vigumu kufikiwa. Hata hivyo, kitabu cha utume cha mwaka huu kimeleta mabadiliko makubwa. Kitabu cha The Key to Change (Ufunguo wa Mabadiliko) kimewawezesha washiriki wanajitolea kufikisha ujumbe wa tumaini, mabadiliko, na imani kwa familia nyingi majumbani mwao.

“Akina mama ndio kiini. Imani yao huweka mwelekeo nyumbani, na ushawishi wao huunda afya ya kiroho ya kanisa.”
– Oyuntuya Batsukh, Mkurugenzi wa Huduma za Wanawake na Familia wa Misheni ya Mongolia, akizungumzia tukio lililowakutanisha wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa uongozi wa kiroho nyumbani na kanisani. Tukio hilo lilisisitiza nafasi ya msingi ya kina mama katika kurithisha imani kwa kizazi kijacho. Jumla ya wanawake 101 walihudhuria ana kwa ana, huku zaidi ya watu 70 wakishiriki kwa njia ya mtandaoni. Tukio hilo la siku kadhaa lilijumuisha ujumbe wa kutia moyo kutoka kwa viongozi wa misheni, warsha za vitendo kuhusu malezi na kuwasaidia watoto waliopotoka, vipindi vya maombi, pamoja na ushirika wa kiroho wenye kuleta maana ya kina.

ZAIDI YA 7,000
Idadi ya washiriki waliohudhuria Kongamano la Wanaume Waadventista la 2025 lililoandaliwa na Konferensi ya Umoja wa Magharibi mwa Kenya. Kwa kaulimbiu “Kubadilishwa kwa Neema,” tukio hilo lilitumika kama mwito wa upya wa kiroho, uongozi wa kiungu, na mabadiliko katika jamii, kwa mujibu wa waandaaji. Moja ya mambo muhimu katika siku hiyo ilikuwa ni mahafali ya washiriki 1,270 waumini wa kawaida waliomaliza kozi ya uanafunzi wa Kikristo. Waandaaji walisisitiza kwamba tukio hilo halikuwa la mkusanyiko wa kawaida, bali lilikuwa “wakati wa mwelekeo mpya na kujitoa upya.” Lilichochea tena dhamira ya kiroho kwa maelfu ya wanaume kote katika eneo hilo na kuwaagiza waishi kwa unyenyekevu, nguvu, na imani isiyotetereka.






Erton Köhler amechaguliwa kuwa rais wa ishirini na mmoja wa Mkutano Mkuu (General Conference - GC) wa Kanisa la Seventh-day Adventist. Kamati ya Uteuzi ya Mkutano Mkuu wa 62, uliofanyika St. Louis, Missouri, Marekani, ilipendekeza jina lake, na wajumbe walipitisha kwa kura 1,721 dhidi ya 188 tarehe 4 Julai wakati wa kikao cha mchana.
Köhler ni rais wa kwanza kutoka Amerika Kusini, na pia rais wa pili kuzaliwa katika Nusu ya Dunia Kusini. Anachukua nafasi ya Ted N. C. Wilson, ambaye amekuwa rais wa GC tangu kuchaguliwa katika Mkutano Mkuu uliofanyika Atlanta, Georgia, mwaka 2010. Wilson amejielekeza sana katika huduma zinazolenga kumgusa mtu binafsi pamoja na jamii kwa ujumla, ikiwemo mipango kama Global Total Member Involvement, Revival and Reformation, I Will Go, Mission to the Cities, na uinjilisti unaojumuisha huduma za afya.
Köhler alitoa hotuba fupi alipokubali uteuzi huo. “Unaweza kufikiria jinsi wakati huu ulivyo mgumu. Hakuna anayekuwa tayari kwa jambo kama hili. Sina maneno ya kusema sasa. Lakini kabla ya jambo lolote lingine, ningependa kuwaambia kwamba nitasonga mbele kwa kuhuisha imani yangu kwa Bwana na kwa kanisa Lake.”
Alisisitiza mstari wa Biblia ambao familia yake hutumia mara kwa mara katika ibada ya jioni ya Ijumaa: Isaya 41:10 — “Usiogope, kwa maana Mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana Mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia; nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Köhler alitumia hotuba yake ya kukubali uteuzi kueleza shukrani zake kwa kanisa, wakiwemo wale “wenye maoni tofauti.”
“Ninyi ni sehemu ya familia, na tunawathamini pia,” alisema.
Köhler alimshukuru Wilson kwa uongozi wake. “Shukrani za dhati kwa Mchungaji Ted na Nancy Wilson, ambao kwa pamoja wameliongoza kanisa hili kwa miaka 15 iliyopita. Ameonyesha mfano wa kiongozi mwenye uadilifu—mtu ambaye nimejifunza kumthamini na kutambua uongozi wake wa kujitoa kwa ajili ya kanisa. Asante sana kwa uongozi wako, na Mungu akuongoze katika hatua zako zinazofuata.”
Köhler amekuwa Katibu wa Mkutano Mkuu (GC) tangu mwaka 2021, baada ya mtangulizi wake, G. T. Ng, kustaafu. Alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi hiyo, aliahidi kuwa mtu wa kupatikana na kuhudumu kwa moyo “uliolenga kikamilifu katika kutimiza misheni ya kanisa.” “Nitakuwa tayari kusikiliza na kujifunza,” alisema. “Kazi yangu ni kujenga madaraja, siyo kuta.”
Wakati wa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Mkutano Mkuu (GC), Köhler alikuwa akihudumu kama Rais wa Divisheni ya Amerika Kusini (South American Division – SAD), nafasi aliyokuwa nayo tangu mwaka 2007. Katika kipindi chake SAD, Köhler alikuwa nguvu ya msingi nyuma ya ukuaji mkubwa wa vyombo vya habari, pamoja na mafanikio ya Novo Tempo — matangazo ya saa 24 kupitia setilaiti na mitandao ya televisheni ya kulipia barani Amerika Kusini. Alikuwa rais mwenye umri mdogo zaidi kuongoza divisheni hiyo akiwa na miaka 38 tu.
“Sisi ni kanisa la ulimwengu lenye utume wa ulimwengu mzima,” alisema Katibu wa GC, Köhler, wakati wa Ripoti ya Katibu Mkuu katika Baraza la Mwaka la 2022. “Hatuwezi kuangazia tu mahitaji yetu ya ndani; tunahitaji kutazama changamoto za dunia nzima ili hatimaye kuihubiri injili ya ufalme kwa ulimwengu wote.” Na akaongeza, “Katika Idara ya Ukatibu tunafanya kazi tukiwa na mtazamo thabiti juu ya jukumu hilo.”
Köhler aliongoza mpango wa "Mission Refocus" (Mwelekeo Mpya wa Utume), ambao ni mkakati wa Idara ya Ukatibu ya Mkutano Mkuu kwa kipindi cha 2022 hadi 2025. Mpango huu ulijumuisha mkazo katika kuwarudisha washiriki waliopotea, kutengeneza wanafunzi wa Kristo (disciple-making), na kurahisisha mchakato wa wito wa kimataifa kwa watumishi wa kanisa.
Köhler alizaliwa kusini mwa Brazil na alikua akiwa na shauku ya kufuata nyayo za baba yake, ambaye alikuwa mchungaji wa Waadventista. Alikamilisha shahada ya kwanza ya teolojia katika Chuo cha Mafunzo ya Waadventista (ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Waadventista cha Brazil) mwaka 1989, na alihitimu tena kutoka chuo hicho hicho mwaka 2008 akiwa na shahada ya uzamili katika teolojia ya uchungaji. Kwa sasa, anaendelea na masomo ya Shahada ya Udaktari wa Huduma (Doctor of Ministry) katika Chuo Kikuu cha Andrews.
Kuanzia mwaka 1990 hadi 1994, Köhler alihudumu kama mchungaji wa kanisa mahalia katika jiji la São Paulo. Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana wa Konferensi ya Rio Grande do Sul, na mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana wa Muungano wa Kaskazini Mashariki mwa Brazil. Mwezi Julai 2002, Köhler alirejea katika Konferensi ya Rio Grande do Sul kuhudumu kama Katibu. Mwaka uliofuata, alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana kwa nchi nane zinazounda Divisheni ya Amerika Kusini. Baada ya kuhudumu kwa miaka minne katika nafasi hiyo ya uongozi wa vijana, mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Rais wa Divisheni ya Amerika Kusini.
Köhler amefunga ndoa na Adriene Marques, ambaye ni muuguzi, na wamebarikiwa kuwa na watoto wawili.




Kongamano la Nne la Kimataifa la Chaplensia la Waadventista lilifunguliwa rasmi siku ya Jumatatu, Juni 30, chini ya kaulimbiu: “Mwitikio wa Mchapleni katika Dunia Yenye Dhiki”. Tukio hili lililofanyika St. Louis, Missouri, liliwakutanisha machapleni 482 wa Kanisa la Waadventista wa Sabato waliokuwa wamesajiliwa pamoja na wake au waume 125, kwa ajili ya kutafakari juu ya miaka arobaini ya huduma ya chaplensia na kujadili mahitaji ya kiroho ya dharura katika dunia yenye misukosuko.

Msukumo Kutoka katika Maono ya Dhati
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Ivan Omaña—Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Chaplensia za Kanisa la Waadventista wa Sabato (ACM) katika Mkutano Mkuu (GC)—aliweka msingi wa kiroho wa tukio hilo kwa kuwatia moyo washiriki juu ya ukuaji na uthabiti wa huduma ya chaplensia. “Uongozi wenu, kujitolea kwenu, bidii yenu isiyoyumba, na uwakili wenu kama wachungaji na walezi wa kiroho ndivyo vilivyofanikisha mkusanyiko huu wa kimataifa. Ukuaji wa huduma hii katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita ni ushahidi wa uaminifu wenu na imani yenu kwa huduma ya chaplensia,” alisema Omaña.
Baadaye, alielekeza macho ya washiriki kwenye changamoto kubwa zinazokumba dunia kwa sasa. “Tunakutana katika kipindi cha kihistoria ambapo vita vinaendelea, migawanyiko ya kisiasa inazidi kuwa mikali, hali ya kiuchumi haieleweki, na mateso ya mtu mmoja mmoja yanaongezeka—kuanzia kwenye kambi za wakimbizi hadi vyumba vya dharura vilivyojaa, kutoka magerezani hadi vyuo vikuu. Migogoro si tena tukio la nadra; sasa imekuwa hali ya kawaida. Na katika dhoruba hii, wachapleni wapendwa, Mungu ametuita sisi kuwa uwepo wake hai hapa duniani,” alisisitiza.
Aliwatia moyo wachapleni kuhudumu kwa weledi, moyo wa kujitoa, na huruma, wakiiga mfano wa Maandiko na moyo wa kujitolea wa waanzilishi wa mapema wa Kanisa la Waadventista.

Hakuna Kitu Kinachoweza Kunitikisa
Ibada ya jioni iliongozwa na Chaplain Andrew Harewood, ambaye alihubiri ujumbe wenye mvuto uliotokana na Matendo ya Mitume sura ya 20. Katika hotuba yake, Harewood alisisitiza umuhimu wa imani, uvumilivu, na uongozi wa kiroho, akiwahimiza washiriki kuukataa uzembe wa kiroho na kuukumbatia ujasiri unaotokana na imani. “Uongozi ni kuwa kabla ya kufanya,” alisema. “Usipoteze muda kupambana na kunguru—endelea kuruka juu.”
Harewood alihitimisha kwa wito uliogusa mioyo ya wengi: “Lazima tupone sisi kwanza kabla ya kuponya wengine.”
Wake wa Wachapleni Washiriki kwa Mara ya Kwanza
Kwa mara ya kwanza, wake wa wachapleni walishiriki katika Kongamano la Kimataifa la Chaplensia. Mpango maalum uliandaliwa ili kutambua mchango wao katika kusaidia huduma ya wachapleni. Miongoni mwa shughuli zao, walitekeleza mradi wa kutoa msaada kwa jamii mnamo Julai 1, katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Agape, ambako waligawa misaada ya vifaa muhimu kwa wakazi waliokumbwa na kimbunga.
“Tulivaa mashati yetu ya buluu na viatu vya kutembea kwa urahisi, tukajinyoosha kazini, na kuwa mikono ya Yesu,” alisema Debra Anderson, mke wa Paul Anderson, mchungaji mstaafu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Joyce Johnson, mke wa Washington Johnson—Mkurugenzi wa Huduma za Chaplensia katika Divisheni ya Amerika Kaskazini—aliendesha semina maalum ya kuwasaidia wake wa wachapleni kihisia na kiroho.
Kongamano Lajumuisha Vikao Mbalimbali vya Kitaalamu
Kongamano la Kimataifa la Chaplensia liliambatana pia na ibada za kuabudu pamoja na vikao vya maendeleo ya kitaaluma. Vikao hivi vililenga mada mbalimbali ikiwemo Elimu ya Kipastorali ya Kliniki (Clinical Pastoral Education – CPE), huduma kwa waathirika wa mshtuko wa kiakili, maadili ya kijeshi, na mwitikio wa dharura katika nyakati za misukosuko. Vikao hivyo vilijumuisha pia mipango mipya ya CPE katika maeneo yanayozungumza Kifaransa na Kireno, pamoja na matukio ya kushiriki ushuhuda na kubadilishana uzoefu, yaliyodhihirisha upanuzi unaoendelea wa huduma ya chaplensia ya Waadventista, kwa mujibu wa waandaaji wa kongamano hilo.




Sehemu kubwa ya watu duniani hawatapata uzoefu huu kamwe, Lakini kuna kiwango fulani cha chini cha joto ambapo theluji huanza kutoa mlio wa kipekee inapokanyagwa na viatu au inapoguswa na matairi ya gari. Hewa huwa kali na yenye ukali wa baridi, na mara nyingi Vipande vidogo vya barafu vinavyong’aa angani. Ni ulimwengu wa kimya—labda kwa sababu nyuzi joto -40°C/F huwafanya watu wabaki ndani ya nyumba, au labda ni kwa sababu maeneo yenye halijoto ya aina hii huwa na idadi ndogo ya watu tangu mwanzo. Theluji ina uwezo wa kufyonza sauti, na hivyo kuwaletea watu wasio na mapenzi na kelele mazingira bora kabisa.
Kuendesha gari katika mazingira haya ni rahisi na la kufurahisha zaidi kuliko unavyoweza kudhani. Theluji hujaa kwenye mashimo ya barabara, ikiyajaza na kufanya uso wa barabara kuwa laini na kupitika kwa urahisi. Mito huwa njia fupi za kufikia mahali kwa haraka kwa sababu huganda kiasi cha kuruhusu magari kupita juu yake. Na tena, kwa kuwa hakuna watu wengi, unaweza kusafiri umbali mrefu bila kukutana na mtu yeyote.
Hata hivyo, kuendesha kwa umbali mrefu kama huo kunaweza kuchosha. Wakati mwingine nilifikiria kuwa ningeweza hata kusoma kitabu nikiwa ninaendesha. Mawazo yangu ilikuwa hivi: kwa kuwa mara kwa mara lazima niangalie geji za gari, kwa nini basi nisiangalie pia kwenye kitabu na kusoma mstari mmoja au miwili? Unachohitaji kufanya ni kuweka kitabu juu kabisa ya usukani na kuhakikisha pembe zake mbili za juu zinabaki kati ya mistari ya barabara. (Usijaribu kufanya hivi nyumbani; njia hii haifanyi kazi kabisa endapo kutatokea kongoni dume barabarani. Siku moja, gari langu liliteleza na boneti ikaingia chini ya tumbo la kongoni dume mkubwa sana. Nilisimamisha gari karibu kabisa naye—sentimita chache tu kabla ya kumgonga. Alinitazama kwa hasira, akakanyaga juu ya gari langu, kisha akatoweka msituni.)

Kupitisha Wakati
Usiku, haikuwezekana tena kusoma. Mara nyingi, taa za kaskazini (aurora borealis) zingeonekana angani, na pazia lake la kijani lililokuwa liking’aa karibu na juu ya kioo cha mbele cha gari langu—likiwa karibu kiasi kwamba ungeweza kudhani unaweza kuligusa—lilinichochea sana kufikiri na kuwaza mambo ya ajabu. Ili kufanya usiku usiwe wa kuchosha, wakati mwingine (ikiwa mwezi ulikuwa mpevu) ningezima taa za gari na kuendesha gizani: ule mstari wa giza uliokuwa kati ya mashamba meupe ya theluji ndiyo uliokuwa barabara. (Narudia tena, usijaribu kufanya hivi nyumbani; Nilikuwa kijana na mpumbavu, na hili ni jambo hatari kupindukia—ikiwa si kwa sababu nyingine, basi kwa sababu unazihitaji taa za gari ili kuona macho ya paa walioko msituni wakisubiri kuruka barabarani muda wowote.) Iwapo kila njia nyingine ingeshindikana, ningesikiliza redio ili kupitisha muda. Kaskazini hakukuwa na vituo vingi vya redio—ungeweza kunasa vichache tu. Hata hivyo, kwa sababu fulani, ningeweza kunasa vituo zaidi wakati wa usiku wa baridi na anga lililo wazi. Usiku mmoja, muda mfupi baada ya saa sita, nikiwa safarini peke yangu kwenye barabara ndefu na tulivu, ghafla nikakumbana na kipindi cha Art Bell. Niliamini kwa shida kile nilichokuwa nikikisikia: watu walikuwa wakipiga simu kuingia hewani wakisimulia matukio ya ajabu—baadhi walidai kuwa wamewaona Sasquatch (viumbe wa ajabu), wengine wakasema wametekwa na viumbe wa angani, huku wengine wakieleza kuhusu majaribio ya kisaikolojia ya serikali na nadharia mbalimbali za njama. Bwana Bell alichukulia kila simu kwa uzito mkubwa.
“Kweli? Niambie zaidi.”
Ilikuwa kama ajali ya gari hewani—singeweza kujizuia kusikiliza. Katika kipindi cha wiki chache zilizofuata, nilijikuta nikipata “elimu ya juu” kuhusu nadharia za njama. Hata hivyo, mara kwa mara ilinibidi kuzima redio, kwa sababu baadhi ya mada zilikuwa zinaelekea maeneo ambayo Mkristo Mwaminifu wa Adventista hastahili kufikia kamwe. Iwapo mgeni wake alikuwa ni mshirikina anayezungumza na wafu, hapo nilikata kabisa. Maelekezo yetu kuhusu mambo kama hayo yako wazi kama kioo.
Kwa namna fulani, taarifa hizo zilinisaidia. Kwenye mikutano mikubwa ya injili, mara kwa mara kulikuwa na mtu mmoja au wawili waliovutiwa na masuala kama hayo, na walifurahi kushangaa kwamba nilielewa kile walichokuwa wakizungumzia—na walishangaa hata zaidi kuona kwamba bado niliwatendea kwa heshima. Hilo lilikuwa sehemu ya mafanikio ya Art Bell, baada ya yote. Wakati mwingine, dunia huwahudumia watu vizuri zaidi kuliko sisi.
Karibu kila mara nilijua pa kuanzia katika Biblia ninapozungumza na watu waliokwisha zama kwenye mambo hayo.

Si Kama Ilivyozoeleka
Kwa kweli, sikuwa nasikiliza mara kwa mara—ilikuwa tu wakati wa zile safari ndefu za usiku wa manane nilipokuwa nikivuka maeneo ya kaskazini yaliyoganda kwa baridi. Lakini mwishoni mwa miaka ya 1990, nilimsikia Art Bell akizungumza kuhusu jambo aliloliita Kasi ya Majira—neno alilobuni ili kuelezea hali ya wasiwasi iliyokuwa ikiwakumba watu wengi kutokana na mwendo wa kasi wa mabadiliko duniani. Iwapo jamii ilihisi kana kwamba inasambaratika, na wewe binafsi hukuelewa kabisa mwelekeo wa siku zijazo, basi ulikuwa unapitia kile alichokiita “Kasi ya Majira.”
Ilikuwa ni mtazamo wa kipekee wa zama mpya wa kuelezea jambo la kweli kabisa. Watu wengi wanatambua kwamba maisha hapa duniani hayako tena kama kawaida. Ulimwengu tuliouzaliwa umebadilika, na kila siku inazidi kuwa vigumu kuelewa dunia tuliyoingia sasa. Kwa mtazamo wa Art Bell, hiyo ilikuwa ni nguvu ya ajabu iliyokuwa ikikukumbusha kwamba dunia iko karibu kubadilika kutoka hali moja ya maisha kwenda nyingine. Kwangu mimi? Ni ukumbusho kwamba Yesu alikuwa sahihi kabisa alipowapa wanafunzi wake dalili za kuangalia: njaa, tauni, matetemeko ya ardhi, na vita.
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi Wake, “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” (Luka 21:28).1 Rafiki zangu wa zamani wameniuliza kwa nini niko mtulivu wakati dunia inaonekana kama inaharibika kila mahali. “Ni kwa sababu mambo haya yote yanaenda sawa kabisa na vile nilivyotarajia,” huwaambia. “Na tayari nimeuona mwisho wa mchezo mzima. Mwisho wake ni mzuri kuliko mnavyoweza kufikiri.”
Wakati Art Bell alianza kuzungumzia nadharia yake ya “Kasi ya Majira,” alitaja mlipuko wa Jengo la Biashara Duniani—ambalo wengi wetu tumesahau jaribio la kwanza la mwaka 1993—kama dalili kwamba dunia yetu ilikuwa inasambaratika. Hakuwa na wazo la jinsi tukio hilo lingekuwa dogo baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 (9/11). Alitaja pia mmomonyoko wa kijamii, maendeleo ya teknolojia kwa kasi, tauni—kwa kweli, karibu kila jambo ambalo Yesu alilitaja. Alitambua dalili hizo bila kuzielewa kikamilifu.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa wengi wa majirani zako sasa hivi. Wanaweza wasikuambie waziwazi, lakini wengi wao wanafuatilia kwa makini. Ahadi za dunia ya kisasa zilivunjika katika karne ya ishirini tulipogundua kwamba hakuna maendeleo ya kiteknolojia yanayoweza kutatua matatizo ya moyo wa mwanadamu. Mwisho wa karne ya kumi na tisa ulikuwa wakati wa shauku na hamasa kubwa kwa watu wengi. Lakini matumizi ya mashine katika vita na uharibifu mkubwa wa karne ya ishirini vilizuia hamasa hiyo kuendelea. Falsafa ya baada ya zama za kisasa imepunguza uwezo wa watu wa kuamini ukweli wa kweli. Hata hivyo—labda kwa sababu Mungu ameweka umilele moyoni mwa mwanadamu (Mhubiri 3:11)—bado tunaonekana kuwa tunaweza kutambua kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa kabisa ndani yetu.
Fursa ya Kushuhudia
Nimewahi kushuhudia mara nyingi utambuzi huo ukifanyika. Katika mikutano ya huduma za injili, mara nyingi huanza na tukio la 9/11 na kuonyesha vifuniko vya jarida la Time tangu wakati huo hadi sasa—nikivionyesha haraka kwenye skrini. Uso wa hadhira hauoneshi hofu; bali ni faraja—faraja kwamba kuna Mtu anayeonekana kuelewa kinachoendelea hapa duniani, na Ana mpango wa kutatua matatizo hayo. Labda ndiyo maana Yesu alijumuisha mawazo haya katika orodha ya dalili za kufuatilia: “Hii itakuwa fursa yako ya kushuhudia” (Luka 21:13). Awali alisema haya katika muktadha wa mateso—utaweza kushuhudia kwa watesaji wako—lakini mimi nimeyakubali kama ahadi ya kuwafikia wengine.
Baadhi ya watu huona kuanguka kwa mifumo ya kidunia kama ishara kwamba Yesu anakaribia kuja, na hawakosei. Lakini kama hilo ndilo pekee unalolizingatia, ni rahisi kupata hofu. Unapofikia hapo, unakuwa unajishughulisha sana na nafsi yako, ukijiuliza: “Nitawezaje kustahimili?” Hii ni njia isiyo sawa na isiyofaa ya kujibu unabii, na ni tofauti na maelekezo ya Yesu ya mara kwa mara ya kusema, “Usiogope.” Wakati huo huo, tumeambiwa kuwa hatukuzi imani yetu kwa kuchora michoro ya unabii au kujaribu kugundua maelezo ya Mungu kuhusu maisha ya baadaye. Sio kwamba unabii hauna umuhimu; kwa kweli, ni muhimu sana — ndiyo sababu mimi ni muumini leo. Lakini basi, tunawezaje kukua?
“Njia pekee ya kukuza neema,” tumeambiwa, “ni kufanya kazi ambayo Kristo ametuhimiza kuifanya bila kujali maslahi yetu binafsi—yaani, kushiriki kadiri ya uwezo wetu katika kusaidia na kubariki wale wanaohitaji msaada tunaoweza kuwapa.” 2
Hii si mojawapo ya njia; ni njia pekee.

Yesu Anakuja Hivi Karibuni
Na ni katika hatua hii ndipo ninaona ushahidi wa wazi kwamba kweli Yesu anakuja hivi karibuni. Ninashuhudia unyofu wa ujumbe wetu ambao haukuwepo miongo kadhaa iliyopita. Ni kweli, ulimwengu unasambaratika, lakini wakati huo huo, Roho wa Mungu anafungua milango kwa njia ambayo haijawahi kutokea hapo awali.
Rafiki zangu walikuwa wapole sana waliposikia nitakuwa Mkristo (na mhubiri!). Lakini hivi karibuni, wananijia kwa wingi. “Ni toleo gani la Biblia ninapaswa kuisoma?” “Je, Biblia inasema nini kuhusu kukatishwa tamaa?” Na, baada ya janga lililoenea duniani kote, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na shambulio la ghafla la Hamas tarehe 7 Oktoba, “je, Biblia inasema kitu chochote kuhusu kinachoendelea duniani?”
Kwa sasa ninatoa mafundisho mengi ya Biblia kwa kiwango ambacho sikuwahi kufikiri kutoa miaka michache tu iliyopita. Mwitikio ninaoupata ni mkubwa! Nina amani ya moyo kwa mara ya kwanza maishani mwangu! Ni kana kwamba mlango mkubwa wa fursa umefunguka ghafla—na si mimi tu niliyeyaona haya. Sina mawazo ya kufikirika kwamba hali hii itadumu milele, kwa sababu unabii unaonyesha haitakuwa hivyo. Lakini ikiwa ipo fursa hiyo, basi ni lazima itumike. Hii ni ishara zaidi kwamba Mungu anajiandaa kuingilia historia ya mwanadamu milele.
Miaka kadhaa iliyopita, nilijikuta nimekwama katika kijiji kidogo huko Aktiki kutokana na dhoruba kali. Nilikuwa na maboksi ya Biblia kwa lugha ya Inuktitut ambazo nilikuwa nimezinunua kwa ajili ya kugawa. Asubuhi moja ya Jumapili, niliona watu wakiingia katika kanisa dogo, nami nikaamua kuungana nao. Mwanamke mmoja mwema wa Kinuït alijitolea kunitafsiria kile kilichokuwa kinaendelea. Mchungaji mlei alisimama na nakala pekee ya Biblia iliyokuwapo katika kijiji kile, na akaanza kusoma kutoka Mathayo sura ya 24. Alimalizia kwa maneno haya: “Tena hii Habari Njema ya Ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14).
Akaacha kusoma na kuangalia timu ya watu niliokuwa nao, waliokuwa wamevalia makoti mekundu na wamekaa kwenye safu ya mwisho ya kanisa. “Na kwa nini mko hapa?” aliuliza. Haikuwa kawaida kwao kupokea wageni katika maeneo yale.
“Nafurahi kwamba umeuliza hilo,” nikamjibu. “Tuko hapa kuwagawia Biblia ili kwamba ule mwisho uje.” Huo ulikuwa mwanzo wa kazi ya ajabu miongoni mwa mojawapo ya makundi ya watu ambao hawajawahi kufikiwa kabisa duniani.
Kuna “kasi ya majira” kweli. Ingawa haitokei kwa namna ambayo watangazaji wa redio wa Kizazi Kipya wanavyodhani. Kuna jambo linaendelea—hakika kuna msukumo mkubwa: siwezi hata kuhimili wimbi la ghafla la maombi ya watu wanaotaka kusali au kujifunza Biblia. Inaonekana kweli kwamba Yesu yuko karibu kurejea.
Usipuuzie kinachoendelea. Tafadhali, usipuuzie.

1 Nukuu zote za Biblia zinatolewa kutoka tafsiri ya SUV (Swahili Union Version).
2 Ellen G. White, Njia Salama (Mountain View, CA: Pacific Press Publishing Association, 1982), uk. 80.

Shawn Boonstra ni mhariri mwenza wa Adventist Review.




Kama ilivyodhihirishwa katika mifano na kutabiriwa katika Maandiko, Kristo, kwa wakati uliowekwa, aliingia katika Patakatifu pa Patakatifu pa hekalu la Mungu mbinguni. Nabii Danieli anamwonyesha akija katika kipindi hiki kwa Mzee wa Siku: “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliyefanana na mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbinguni, akamkaribia”—si duniani, bali—“yule Mzee wa Siku, wakamleta karibu naye.”
Ujio huu umetabiriwa pia na nabii Malaki: “Naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafla…” Ujio wa Bwana katika hekalu Lake ulikuwa wa ghafla, na usiotarajiwa kwa watu Wake. Hawakuwa wakimsubiri mahali pale. Walimtarajia aje duniani, “katika mwali wa moto, huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wale wasioitii injili ya Bwana wetu Yesu Kristo.”
Ishara Zilizotabiriwa
Mara tu baada ya kutimia kwa baadhi ya ishara alizozitabiri Mwokozi kuhusu ujio Wake wa pili, kulitokea mwamko mkubwa wa kidini katika ulimwengu wa Kikristo. Watafiti wa unabii walihitimisha kuwa wakati wa mwisho ulikuwa umekaribia. Walinukuu maandiko kutoka kitabu cha Danieli: “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” Wakiwa na dhana kwamba dunia ndiyo ilikuwa patakatifu, walielewa kuwa utakasaji uliotajwa katika Danieli 8:14 ulikuwa ukimaanisha usafishaji wa dunia kwa moto wakati wa kuja kwa Kristo mara ya pili. Walipoendelea kuchunguza Maandiko kwa bidii wakitafuta mwanga zaidi, na walipolinganisha kipindi hiki cha kinabii na kumbukumbu za kihistoria, waligundua kwamba siku elfu mbili na mia tatu zilifikia mwaka 1844....
Lakini watu bado hawakuwa tayari kukutana na Bwana wao. Kulikuwa na kazi ya maandalizi waliyoitwa kuikamilisha. Nuru ilifunuliwa kwao, ikielekeza mawazo yao kwenye Patakatifu pa Mungu mbinguni. Kwa kumfuata kwa imani Kuhani wao Mkuu katika huduma Yake ya mbinguni, majukumu mapya yangewekwa wazi. Ujumbe mwingine wa onyo na mwongozo ulipaswa kufikishwa kwa kanisa…
Wale watakaokuwa hai duniani wakati huduma ya maombezi ya Kristo itakapofikia kikomo katika Patakatifu pa mbinguni, itawapasa kusimama mbele za Mungu Mtakatifu pasipo Mwombezi. Mavazi yao yanapaswa kuwa safi yasiyo na mawaa, na tabia zao lazima zitakaswe kwa damu ya kunyunyizwa. Kwa neema ya Mungu na kwa jitihada zisizolegea, wanapaswa kushinda katika mapambano dhidi ya uovu. Wakati ambapo hukumu ya upelelezi inaendelea mbinguni, wakati dhambi za waumini waliotubu zinaondolewa kutoka Patakatifu, kunapaswa kuwepo kazi ya pekee ya utakaso miongoni mwa watu wa Mungu duniani: kazi ya kuondoa dhambi na kutakasa tabia. Kazi hii imeelezwa kwa uwazi zaidi katika ujumbe wa Ufunuo 14.
Kazi hii itakapokamilika, wafuasi wa Kristo watakuwa tayari kwa kuonekana Kwake. “Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale na kama katika miaka ya zamani.” Kanisa ambalo Bwana atalipokea wakati wa kuja Kwake litakuwa “kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi, wala lolote kama hayo”; “zuri kama mwezi, safi kama jua, wa kutisha kama wenye bendera.”

Waadventista wa Sabato wanaamini kuwa Ellen G. White (1827–1915) alipokea karama ya unabii ya Kibiblia, ambayo aliitumia katika huduma ya umma kwa zaidi ya miaka sabini. Dondoo hili limetolewa kutoka Southern Watchman, Januari 24, 1905.




"Usilie mbwa mwitu!" Huenda ulisikia msemo huu kutoka kwa wazazi wako ulipokuwa ukikua, au pengine nawe umewahi kuwaonya watoto wako kwa maneno hayo. Kwa wale wasiofahamu methali hii, maana yake ni: "Usiite msaada kama hakuna dharura; la sivyo watu hawata kuamini utakapokuwa kwenye hatari ya kweli." Wazo kwamba watu wanaweza kupuuza kilio halisi kwa sababu ya uongo wa awali ni la kutisha.
Ingawa sidhani kama nilikuwa na tabia hiyo, nakumbuka tukio moja ambapo, baada ya kurukaruka na kubingirika juu ya kitanda cha wazazi wangu bila ruhusa, nilianguka na kugonga kwa nguvu sehemu ya nyuma ya kichwa changu kwenye ukingo wa chuma wa rejeta ya zamani. Nikiwa nimelala chini kwa mshtuko, nilipogundua kuwa damu ilikuwa ikitiririka kutoka kichwani na nikaanza kuwaza mabaya zaidi, nililia kwa sauti nikiomba msaada. Hakuna aliyeitika. Hali hiyo iliendelea kwa muda mfupi hadi nilipoweza kujinyanyua na kujikokota kupitia korido kuelekea kwa mama yangu, ambaye hakuwa amesikia kilio changu kwa sababu alikuwa akiwasindikiza wageni waliokuwa wakiaga. Nikiwa na damu mikononi, nilimnong’oneza kwa sauti dhaifu, “Nahitaji kwenda hospitalini,” na papo hapo tukaelekea huko.
Cha kushukuru, nilihitaji kushonwa tu. Ingawa kilio cha msaada kilikuwa halisi, uzoefu wa kupaza sauti ya kuashiria hatari bila kusikika ulikuwa wa kutisha. Tukio hilo lilinifundisha jambo la kina zaidi: kwamba tukipiga kelele mara kwa mara, au bila kueleweka vizuri, iwe ni kweli au la, tunahatarisha kutoaminiwa wakati ambapo tunahitaji kusikilizwa zaidi.
Sehemu ya kuwa Mwadventista ni pamoja na kupiga mbiu ya onyo kuhusu nyakati za mwisho na utimilifu wa unabii, na kwa hakika, hilo ni jambo la haki. Tunaishi katika siku za mwisho; Yesu anakuja hivi karibuni, labda hata katika kizazi chetu, jambo ambalo tunalitumainia sana, na muda uliobaki ni mfupi sana. Kila ninapohubiri katika mikutano ya injili, huwasilisha ishara za nyakati pamoja na maelezo ya kibiblia kuhusu hali ya kisiasa na kidini inayoendelea duniani. Wakati huo, hutambua tena kwa kina jinsi hali tuliyo nayo ni ya dharura na inahitaji mwitikio wa haraka. Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa kwa watu wa Mungu: kupata usawa wa mkazo unaofaa, kupiga mbiu ya onyo kwa njia inayofaa, na kuhakikisha kwamba hatupotezi lengo kuu la unabii.
Kelele zenye Mashaka
Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya watu hupaza sauti ambazo ningezifananisha na kelele zenye mashaka, mbiu za onyo zisizo na uthibitisho, ambazo huweza kudhoofisha uaminifu wetu kwa urahisi. Hebu nitoe mfano: Nilipokuwa kijana, mhubiri maarufu alitembelea shule yetu na kutangaza kwamba Yesu anaweza kurudi baada ya takriban miaka miwili. Alitoa hoja hiyo kwa misingi ya kuwa hangeweza kuhuisha baadhi ya mikataba ya huduma yake ya kiinjili baada ya kipindi hicho, hivyo akahitimisha kuwa mwisho ulikuwa umekaribia.
Aidha, alizungumza kuhusu magereza ya siri yaliyojengwa katika vyumba vya chini vya makanisa ya Kikatoliki, yaliyodaiwa kuandaliwa kwa ajili ya waaminifu wanaoshika Sabato wakati wa dhiki ya mwisho, pamoja na mada zingine kama hizo.
Miaka ishirini imepita tangu hotuba hiyo itolewe. Ingawa ilinipa hofu kidogo, kwa kuwa moyo wangu haukuwa umebadilika kikamilifu, na ilinifanya kufikiri kwa muda, haikusaidia kuimarisha imani yangu, wala haikunisukuma kumkabidhi Mungu maisha yangu kwa upendo. Ilipofika miaka miwili iliyokuwa imetajwa, na hakuna kilichotokea, nilielewa kwamba nilikuwa nimeshawishika na hofu badala ya ukweli.
Mfano mwingine: Kila mara papa anapofariki dunia, husikika tena wazo kwamba papa aliyekufa au anayefuata ndiye atakayekuwa wa mwisho. Watu huleta "ushahidi" wa kubahatisha ili kuunga mkono madai hayo.
Ni kweli kwamba siku moja kutakuwa na papa wa mwisho — kama ambavyo kutakuwa na mchungaji wa mwisho katika kanisa langu, au rais wa mwisho katika nchi yangu. Lakini kubashiri juu ya jambo hilo hakutawasaidia vijana wabaki kanisani, wala hakutawavutia wale wanaotafuta kumjua Kristo kwa upendo wa kweli.
Naweza pia kutaja wahubiri wanaojitangaza kwenye YouTube ambao, kana kwamba wana karama ya kipekee, hutoa maudhui yasiyokwisha yanayovutia vichwa vya habari—wakidai kufichua “ajenda za siri” kuhusu wanasiasa, viongozi wa dini, waigizaji, na hata viongozi wa kanisa letu wenyewe.
Lakini je, tabia hii ya kuchochea hofu kweli inamsaidia mtu yeyote? Je, si kwamba kwa kiasi kikubwa inaharibu aina ya ujumbe wa matumaini ambao tumeitwa kuutangaza?
Je, watu watataka kutusikiliza—achilia mbali kutuamini—wakati mengi ya wanayosikia yakitolewa kwa jina letu ni madai ya kubahatisha, yanayochochewa na hofu, na ambayo hatimaye huonekana kuwa ya uongo? Najiuliza.
Basi, je, kuna “ajenda ya siri”? Mpango mkubwa unaomhusu kila mwanadamu duniani? Ndiyo, bila shaka upo. Shetani ana njama ya dhahiri ya kumpinga Mungu na kuwaangamiza watu Wake. Hii si hadithi ya kubuni—ndicho kiini cha pambano kuu linalozungumzwa katika Biblia.
Kwa kweli, Shetani anatumia watu, mashirika, na matukio mbalimbali ili kuendeleza ajenda hiyo (ambayo, kwa mwanafunzi wa Biblia, haijafichwa sana).
Je, watu wanapaswa kufahamu kuhusu jambo hili? Bila shaka. Lakini, kushikilia kwa nguvu sana na kuvumbua taarifa zisizo na uhakika kuhusu mambo ya giza siyo sehemu ya injili. La hasha—si hivyo kabisa.

Msisimko wa Kelele
Kama mchungaji, nimekuwa nikilishuhudia jambo hili mara kwa mara: washiriki wa kanisa na watu wanaotafuta kweli, hujenga uzoefu wao wa kiroho na uaminifu wao kwa kanisa kwa msingi wa habari za hivi punde zenye kusisimua au madai yanayooana na masimulizi wanayopendelea.
Hisia ya msisimko — ya “kufahamu” kilicho kweli kinachoendelea — mara nyingi huchukuliwa kimakosa kuwa ni uamsho wa kiroho au uaminifu wa imani. Msisimko huu wa kelele unaweza kwa urahisi kuchukua nafasi ya furaha ya wokovu na maisha yanayomtegemea Kristo kikamilifu.
Cha kusikitisha, mwelekeo huu wa kuangazia sana mambo ya kusisimua mara nyingi huambatana na mitazamo ya kuhukumu, tabia za sheria kali, na moyo usiotaka kurekebishwa.
Ni kweli kwamba lazima tuwe waangalifu (Mathayo 24:42), lakini tuhakikishe kuwa uangalizi wetu umejengwa juu ya imani katika Yesu — si katika vyanzo vya mashaka. Tukifanya hivyo, tutageuza uharaka unaochochewa na hofu kuwa uelewa wenye tafakari uliojaa tumaini.
“Kwa maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” (2 Timotheo 1:7).
Kuridhika Kupita Kiasi katika Nyakati za Mwisho
Kwa upande mwingine wa sarafu, wapo wale ambao, kwa sababu mbalimbali, hawatarajii, wala hawatamani kuona nyakati za mwisho zikitimia katika maisha yao, au angalau si kwa mtazamo wa kitamaduni wa Waadventista.
Miaka michache iliyopita, nilimsikia mzungumzaji mmoja akihubiri kwenye mimbari akieleza jinsi alivyofahamu kile kinachotabiriwa katika Ufunuo 13, ikiwa ni pamoja na mateso yajayo. Lakini akahitimisha kwa kusema, “Natumai sitakuwa miongoni mwa walio hai wakati huo.”
Wengine hujikita katika tafsiri tata za maandiko ili kupinga ufahamu ulioimarika kuhusu unabii wa nyakati za mwisho, na hata kupuuza umuhimu wa maandiko ya Ellen White kwa kanisa la sasa. Bidii ya kushiriki katika mahubiri ya kitamaduni ya injili, na kuweka mkazo kwenye ujumbe wa nyakati za mwisho, sasa huonekana kuwa ni ukali wa kidini, ushupavu wa kisheria, au jambo la kizamani lisilofaa kwa kanisa la karne ya ishirini na moja.
Watu wengine huonekana kujivuna kwa akili zao, labda kwa sababu wanaogopa kubadilika, na kwa sababu hiyo, hukataa kufikiria kwamba tunaishi katika nyakati za hatari. Wanafikiri kila kitu kinaendelea kawaida, na hakuna cha kutia wasiwasi. Mtazamo huu unafanana na wa wale waliowahi kudhihaki ujumbe wa kurudi kwa Yesu kwa kusema: “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake?” (2 Petro 3:4). Hali hii pia ni kama upofu wa kiroho wa kanisa la Laodikia (tazama Ufunuo 3:14–22).

Je, Waadventista Wanapaswa Kuwa Wapiga Kelele?
Kuna wakati ambapo, katika mahubiri yetu, ni muhimu kuonyesha wazi maovu yanayotendeka na kufichua uongo unaoenea katika dunia hii. Maandiko yanasema, “Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee” (Waefeso 5:11). Hata hivyo, jambo hili halipaswi kamwe kuchukua nafasi ya ujumbe mkuu wa unabii wote — kumtangaza Yesu Kristo.
Bila shaka, kuna haja ya kuwaambia watu kuhusu ishara za kurudi kwa Yesu, lakini mara nyingi tunaonekana kuwa na hamasa zaidi kuhusu ishara zenyewe kuliko kuhusu Yeye anayekuja — na kwa nini kurudi Kwake ni habari njema! Ufunuo 14:6 haiiti ujumbe huu “Injili ya milele” bila sababu. Kurudi kwa Yesu ni habari njema! Kwa nini? Si kwa sababu inamaanisha kutakuwa na vita zaidi, vurugu zaidi, njama za kishetani, viongozi wa kisiasa na wa kidini wa kutia shaka, au miungano ya ajabu tunayopenda kuchambua kupita kiasi. La hasha! Ni habari njema kwa sababu Yeye, Tumaini la vizazi vyote; Yeye, Mkombozi wa mioyo yetu yenye dhambi; Yeye, Anayependa nafsi zetu na Mponyaji wa majeraha ya wanadamu — yuko karibu kuja kwa utukufu mkuu!
Anarudi, si tu kuwaokoa wale wanaomwamini kutoka kwa wanyama wa Ufunuo 13 au maafa yaliyoelezwa katika Mathayo 24. Anarudi kumchukua bibi arusi Wake — marafiki Wake waliokombolewa, wa thamani ya milele — na kuwarejesha nyumbani Kwake mbinguni, kwa ushirika usiokoma, furaha ya milele, na upendo mkamilifu katika utakatifu na utukufu.
Sauti ya Hakika
Ikiwa hatufanyi hivyo, tutakuwa tukikanusha jina letu na agizo la kinabii la Ujumbe wa Malaika Watatu. Lakini tunapaswa kupiga tarumbeta yenye sauti ya hakika — yenye tumaini na utayari, si hofu na msisimko. Sauti inayochochea imani kwa Yesu na Neno Lake lote, badala ya wasiwasi juu ya ulimwengu unaoporomoka na usioweza kutoa suluhisho lolote kwa moyo usiotulia. Imba wimbo mzuri na wenye nguvu wa Kristo — uimbe kwa uwazi na uimbe vizuri!
Hatari ya kweli inayohitaji kelele ya kweli na yenye sauti kubwa kupigwa ulimwenguni kote si sana kwamba Yesu anakuja hivi karibuni, bali ukosefu wa ufahamu kwamba Yeye tayari anagonga kwenye milango ya mioyo yetu, akisubiri kuruhusiwa kuingia.

Jonathan Walter ni mhariri msaidizi wa Adventist Review.




Swali: Nimesikia kuwa matumizi ya kupita kiasi ya vifaa vya kidijitali yanaweza kusababisha matatizo ya kiakili. Je, makundi yote ya umri yako hatarini?
Jibu: Wazimu wa kidijitali na upweke wa kidijitali ni changamoto mbili zinazozidi kuenea, zikiwa na uhusiano wa karibu na matumizi ya kupita kiasi au mabaya ya teknolojia za kisasa kama vile simu za mkononi, vishikwambi na kompyuta. Hali hizi zimeanza kujitokeza katika makundi yote ya umri na kusababisha wasiwasi kuhusu afya ya akili, elimu, na mahusiano ya kifamilia duniani kote.
Neno “wazimu wa kidijitali” linamaanisha upungufu wa kiakili unaofanana na dalili za wazimu za awali, inasababishwa na matumizi ya muda mrefu ya kupita kiasi ya vifaa vya kidijitali. Hali hii ilielezewa kwa mara ya kwanza na Dkt. Manfred Spitzer, mtaalamu wa neva kutoka Ujerumani, akibainisha jinsi utegemezi mkubwa wa teknolojia unavyoweza kusababisha matatizo ya kumbukumbu, ukosefu wa umakini, na kushuka kwa uwezo wa kutatua matatizo. Hili linaathiri zaidi vijana wadogo, ambao ubongo wao bado uko katika hatua za ukuaji. Hata hivyo, watu wazima na wazee pia hawako salama, hasa wale wanaoishi maisha ya kukaa muda mrefu bila shughuli za kiakili kama kusoma au kushiriki mawasiliano ya kijamii, na badala yake kutumia muda mwingi mbele ya skrini.
Dalili za kawaida za wazimu wa kidijitali ni pamoja na usahaulifu, kushindwa kuwa makini, uwezo mdogo wa kuzingatia kwa muda mrefu, na mkao mbaya unaotokana na matumizi ya kupita kiasi ya vifaa vya kidijitali. Mtu pia huweza kuonyesha mabadiliko ya hisia na ukosefu wa utulivu wa kihisia. Kadri muda unavyosonga, matumizi haya huathiri sehemu ya mbele ya ubongo inayohusika na fikra za juu, jambo linaloweza kusababisha kushuka kwa uwezo wa kiakili kwa njia ya kudumu.
Kwa upande mwingine, upweke wa kidijitali ni hali ya upweke au kujitenga kijamii inayotokana na tabia fulani za matumizi ya teknolojia. Ingawa vifaa vya kidijitali hurahisisha mawasiliano, mara nyingi husababisha kupungua kwa mawasiliano ya ana kwa ana na ukosefu wa uhusiano wa dhati. Hali hii huathiri watu wa makundi mbalimbali, wakiwemo watoto wanaozama kwenye michezo ya video; vijana wanaotumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii; na wazee wanaotegemea mawasiliano ya kidijitali lakini wakikosa ushirikiano wa ana kwa ana na jamii.

Ili kuepuka wazimu na upweke wa kidijitali, mtu anahitaji kufanya mabadiliko katika tabia na kupata msaada wa kijamii. Elimu ya umma kupitia kampeni za kuelimisha kuhusu matumizi salama ya teknolojia ni muhimu sana, hasa ili kuongeza uelewa juu ya hatari za matumizi ya kupita kiasi. Kwa watoto na vijana, ni muhimu kuweka mipaka ya muda wa kutumia skrini, kushiriki mara kwa mara katika shughuli za nje, na kufanya kazi za ubunifu au kijamii. Vilevile, shule zinaweza kuanzisha vipindi maalum vya “bila teknolojia” ili kusaidia kukuza maendeleo ya kiakili na kijamii.
Kila mtu anashauriwa kujifunza na kufanyia kazi mazoezi ya usafi wa kidijitali, kama vile kutenga muda maalum wa kutokuwa kwenye vifaa vya kidijitali, kutumia programu za kudhibiti muda, na kutoa kipaumbele kwa mawasiliano ya ana kwa ana. Tafakari juu ya Neno la Mungu, njia Zake, na matendo Yake, pamoja na kushiriki katika shughuli za kuimarisha uwezo wa ubongo, kama vile michezo ya kumbukumbu, kusoma, au kujifunza ujuzi mpya—vinaweza kusaidia kupunguza athari za wazimu wa kidijitali.
Kwa wazee, msaada wa kijamii, mafunzo ya kidijitali, na fursa za mawasiliano ya ana kwa ana vina umuhimu mkubwa katika kuzuia upweke wa kidijitali. Matumizi ya teknolojia kwa kiasi yanaweza kuwa na manufaa, yakiwemo kuboresha uwezo wa kiakili na kupunguza athari za uzee kupitia kanuni inayojulikana kama “3 Cs”: changamoto (complexity), uhusiano (connection), na fidia (compensation).
Matumizi yasiyodhibitiwa ya vifaa vya kidijitali yanaendelea kuwa tishio kwa afya ya kiakili, kihisia, na kijamii. Kuchukua hatua mapema katika makundi yote ya umri kunaweza kusaidia kukuza tabia bora za matumizi ya kidijitali na kulinda ustawi wa akili katika enzi hii ya kiteknolojia. (Soma Wafilipi 4:8–9).

Zeno L. Charles-Marcel, daktari aliyeidhinishwa na bodi, ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu. Peter N. Landless, mtaalamu wa moyo aliyeidhinishwa na bodi na Mkurugenzi Mstaafu wa Huduma za Afya za Waadventista katika Konferensi Kuu, pia ni daktari wa mfumo wa mwili aliyeidhinishwa na bodi.




Tuko wapi katika mpangilio huu wa matukio ya wakati wa mwisho? Kielelezo hiki cha unabii wa wakati wa mwisho kinatokana na Danieli, Ufunuo, na aya zingine muhimu kuangazia matukio ya mwisho ya Pambano Kuu – na tumaini linalofuata mara tu baada ya zahama hii.





Mara nyingi tumekuwa na sababu mbalimbali za kutowaalika watu nyumbani kwetu. Siongelei hapa kuhusu kila mtu ninaposema “sisi.” Hapana, huu ni ushuhuda wa wazi wa hali yangu binafsi. Ikiwa nyumba yetu siyo ndogo, basi haina viti vya kutosha. Kuna vurugu nyingi; sina chakula kizuri cha kuwahudumia; au napenda utulivu na sipendelei kuwa na watu mara kwa mara (kukosa maisha ya kijumuiya). Kisha linakuja suala kuhusu wageni wetu maalum. Siwajui — vipi ikiwa hawatapatana na watoto wangu? Vipi kama watawafundisha wanangu tabia zisizofaa? Vipi kama hawatakuwa watu wa kuvutia? Au hata zaidi, siwajui, na kwa sababu yoyote ile, siwapendi.
Waebrania 13:2 inasema wazi: “Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.” Matoleo mengine ya Biblia, kama New American Standard Bible na English Standard Version, hutafsiri neno “Msisahau” (epilanthanomai) kama “msipuuze.” Waebrania 13:2 inatufundisha kuwa hatupaswi kuwa watu wasiojali na wasiosikiliza, kwa sababu hilo linaweza kutufanya tupuuze mambo muhimu.
Zaidi ya hayo, ukarimu siyo jambo la kuvutia kwa macho tu, bali ni ishara halisi ya moyo wa kumsaidia mtu mwingine. Hebu tuchunguze mfano wa Ibrahimu katika kitabu cha Waebrania ili kuelewa vizuri zaidi maana na umuhimu wa ukarimu.
Ukarimu wa Ibrahimu
Ilikuwa ni wakati wa jua kali la mchana alipomwona wageni wamesimama karibu, naye akakimbia kuwakaribisha waingie nyumbani kwake wapate chakula na kupumzika. Usumbufu na gharama binafsi ya kuwakaribisha wageni hawa, kama inavyoelezwa katika Mwanzo 18, ni dhahiri na haiwezi kupuuzwa. Gharama hiyo ilikuwa ya kimwili (kwa kuwa Ibrahimu anakimbia na kuharakisha huku na kule – aya ya 2, 6, 7), ya mali (anapotayarisha chakula na huduma nyingine – aya ya 6–8), na ya kijamii (anapowaomba wengine wamsaidie kutimiza jukumu hilo – aya ya 6, 7). Katika yote hayo, ni Ibrahimu anayewaomba kwa unyenyekevu wageni hao wamruhusu awatendee kwa wema (aya ya 3–5).
Ibrahimu hakuwafahamu watu hao walikuwa kina nani. Ukarimu wake haukusababishwa na matarajio ya kuwahudumia malaika, bali ulitoka katika tabia yake ya ndani. Je, hili halikukumbushi maneno ya Yesu katika Mathayo 25? “Ndipo wenye haki watamjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Ni lini tulikuona u mgeni tukakukaribisha, au u uchi tukakuvika? Ni lini tena tulikuona mgonjwa au kifungoni, tukakujia?’ Naye Mfalme atajibu, akiwaambia, ‘Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi’” (aya ya 37–40). Wale watakaourithi uzima wa milele hawafanyi matendo ya ukarimu ili kujipatia malipo au sifa mbele za Mungu. Matendo yao hutiririka kwa kawaida kama matokeo ya haki waliyopewa kwa neema ya Mungu.
Tazama tena orodha ya matendo yaliyotajwa na Yesu — unaona nini? Je, huoni ukarimu ukijitokeza wazi? Ukarimu unaonekana wazi hasa katika kishazi “kumkaribisha mgeni”, hasa tukiliangalia katika muktadha wa kisa cha Ibrahimu. Na vipi kuhusu kuwalisha wenye njaa au kuwapa maji wenye kiu — je, hayo si matendo ya ukarimu? Kuwavika walio uchi, kuwajalia wagonjwa na kuwajulia hali walio kifungoni — si yote haya yanahitaji kujitoa binafsi kwa ajili ya kuwahudumia wengine?
Hakika, kila tendo linalotajwa na Yesu linahusisha gharama ya muda, mali, au hisia — yote yakielekeza kwenye moyo wa ukarimu wa kweli. Zingatia pia kwamba wema alioutoa Ibrahimu haukuombwa na wale waliounufaika. Wageni hawakumsihi awaoshee miguu wala kuwapa chakula. Ibrahimu mwenyewe ndiye aliyegundua fursa ya kutoa huduma, naye akaitikia kwa haraka. Kondoo katika Mathayo 25 huona mahitaji na hujitokeza kuyakidhi bila kutarajia malipo. Ukarimu ni huduma ya kujitolea kwa ajili ya wengine, hata kama inahitaji mtu kubeba gharama binafsi.
Kwa hakika, ni kiburi cha kujifikiria ambacho hutuzuia kuishi maisha ya ukarimu — iwe kinatokana na maslahi binafsi au ukosefu wa imani. Maslahi binafsi, au kujipenda kupita kiasi, hutuzuia kutoa upendo wa kujitoa kwa wengine. Tutawasaidia wengine mradi tu haitusumbui. Lakini mara tu msaada huo unapotugharimu au kutugusa binafsi, tunapuuza wajibu wetu. Hii inaonyesha kwamba hatujabadilishwa na upendo wa kujitoa kafara wa Kristo. Mioyo yetu hufungwa tunapokutana na mahitaji ya wengine yanayopingana na maslahi yetu binafsi. Hata hivyo, Yesu hakuzuia chochote kwa ajili ya kuziokoa roho zetu zisizo na msaada. Kama angekuwa anawaza kuhusu manufaa yake mwenyewe, tusingekuwa na tumaini.

Ukarimu wa Mjane
Wakati mwingine tunakumbwa na hofu halisi, zisizoelezeka kwa urahisi. Tunaamini kwamba tukiwasaidia wengine, bila shaka tutajikuta bila mahitaji yetu ya msingi. Jibu la Maandiko ni mfano wa mjane wa Sarepta. Alikuwa akijiandaa kwa mlo wake wa mwisho wakati Mungu alimpatia fursa ya kuonyesha ukarimu (1 Wafalme 17:8–16). Ilimgharimu juhudi za kimwili kumchotea Eliya maji na kuoka mkate, rasilimali za kiuchumi kutoa chakula chake cha mwisho, na hata mtaji wa uhusiano pale alipomnyima mwanawe chakula hicho kabla ya kifo kinachosababishwa na njaa. Kwa kuzingatia hali yake, ombi la Mungu kupitia kwa Eliya linaweza kuonekana kuwa la kudhulumu, lisilo la haki, na lisilo na huruma. Hata hivyo, Mungu alimwambia: “Usiogope” (aya ya 13).
Katika kukabiliana na hofu halisi zinazozunguka maisha ya ukarimu, Mungu anatuambia: “Usiogope.” Vipi ikiwa nitamsaidia mtu asiye mwema, halafu atumie kile alichopata kwa njia ya uovu? Usiogope. Vipi ikiwa nitamkaribisha mtu asiye na shukrani nyumbani kwangu? Usiogope. Vipi ikiwa nitashiriki upendo wa Yesu, lakini akakataa kumkubali Kristo? Usiogope. Vipi ikiwa nitatoa nilichonacho, kisha nibaki bila kitu? Usiogope!
“Eliya akamwambia, “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, ‘Lile pipa la unga halitapungua, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi’” (aya za 13–14). Mungu anamwalika mjane wa Sarepta kumhudumia mtumishi Wake kwanza na kumwamini kwamba atashughulikia mahitaji yake baadaye. Anamwalika kuishi mafundisho ya Mathayo 6:33, yanayojikita katika aya ya 25–32: Kujua kwamba Mungu anaweza kukupatia mahitaji yako, sasa amini kwamba atafanya hivyo, na uishi maisha ya imani hiyo.
Katika kukabiliana na hofu zetu, za kweli na zisizofikirika, Mungu anatualika kumwamini Yeye — kuamini utoaji Wake na ulinzi Wake. Mkristo hawezi kupuuza udhuru wa msingi wa kushindwa kuwahudumia walio wanyonge (na daima kuna mtu aliyemnyonge zaidi yako!). Kwa hiyo, Petro anatuhimiza: “Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung’unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu” (1 Petro 4:9–10). Maagizo haya hayaji peke yake; muktadha wake, katika aya ya 7, unasema: “Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia.” Je, sisi ambao tunajitambulisha kama wale wanaotarajia ujio wa pili wa Kristo, hatupaswi kuliweka moyoni agizo hili?

Ukarimu wa Waadventista
Wazo la ukarimu limejikita ndani ya mojawapo ya maandiko ya msingi yanayounda utambulisho wetu wa kidini kama Waadventista. Sura ya Isaya 58, ambayo inahitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa Sabato na ahadi zinazotolewa kwa kuitunza, inaelezea maisha ya mtu anayeshika Sabato kwa kweli. Ni sura inayowahutubia wale “wanaofurahia kumkaribia Mungu” (aya ya 2) — yaani, waumini wa kanisa.
Baada ya Mungu kuwakemea watu Wake kwa udini wa juujuu na usio na maana, hawaachi bila kuwaelekeza kile anachokitaka kutoka kwao. Kwanza kabisa, dini ya kweli ni “kufungua vifungo vya uovu, kulegeza mizigo mizito, kuwaacha huru waliodhulumiwa, na kuvunja kila nira”; “kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako; na umwonapo mtu aliye uchi, umvike; wala usijifiche na mtu wa damu moja nawe” (aya ya 6–7).
Watu wanaoshika Sabato kwa uaminifu mara nyingi hunukuu Isaya 58:13 kama mwongozo wetu wa jinsi ya kuitunza Sabato. Sabato, ikiwa ni siku ya pumziko, haipaswi kutumiwa kwa kujifurahisha kwa mambo ya binafsi. Lakini onyo la kuacha “kufanya mambo upendayo siku ya Sabato yangu takatifu,” linapowekwa katika muktadha wa sura nzima, halihusiani na starehe au sherehe za kawaida. Furaha ya watu wa Mungu, kama inavyoonekana mwanzoni mwa sura hii, ilikuwa katika kusoma Maandiko (“hufurahia kujua njia zangu”) na ibada (“hufurahia kumkaribia Mungu”). Hata hivyo, licha ya maarifa yao na namna zao za kidini, mioyo yao haikubadilishwa; hivyo, walishindwa kuwajali wale walio katika uhitaji.
Yakobo anahitimisha kwa kusema: “Dini iliyo safi na isiyo na mawaa mbele za Mungu Baba ni hii: kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda nafsi yako usichafuliwe na dunia” (Yakobo 1:27). Kwa njia nyingine, kama bado haijabainika wazi kupitia aya zilizotangulia: ingawa tunapaswa kuwa wema kwa watu wote walioko karibu nasi, Wakristo wameitwa kuwaonyesha wema wa pekee wale walio na uhitaji zaidi. “Waisraeli, katika sikukuu zao zote, waliwahusisha maskini, wageni, na Walawi—ambao walikuwa wasaidizi wa makuhani hekaluni, walimu wa dini, na wamisionari. Watu hawa walizingatiwa kama wageni wa heshima wa jamii, waliopaswa kushiriki ukarimu wa watu katika kila sherehe ya kijamii na ya kidini, na kutunzwa kwa huruma walipokuwa wagonjwa au wenye mahitaji. Hao ndio wale tunaopaswa kuwapokea kwa ukarimu katika nyumba zetu.”*
Tukikumbuka kwa makini yale ambayo Kristo ametutendea, tunawezaje kutojali mahitaji ya wale walio karibu nasi? Tunapotoa kutoka katika rasilimali zetu binafsi kuwasaidia wenye uhitaji, tunajifunza kumtumaini Mungu zaidi, tunakuwa wasio na ubinafsi, na kufanana zaidi na Yesu. Kutenda wema kama Wakristo ni njia ya kubadilishwa mioyo, lakini mara nyingi tunapuuza nafasi hiyo.
Kwa kuwa ujio wa Kristo umekaribia sana, mtu anayeshika Sabato hawezi kumudu kupuuza nafasi yoyote ya kuonyesha wema. Mungu amejibu kila pingamizi, na ameahidi baraka kwa wale wanaotii. Kwa hiyo, wakati upendo wa wengi unazidi kupoa kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu, na tuendelee kupenda kama Kristo alivyotupenda—tukiwapenda si wale tu wanaopendeka, bali hasa wale wanaohitaji sana wema wetu.


* Ellen G. White, The Ministry of Healing (Mountain View, Calif.: Pacific Press Pub. Assn., 1905), uk. 352.

Sikhululekile Daco ni mmoja wa wahariri wenza wa jarida la Adventist Review.




Mtu mmoja ambaye nilimuheshimu sana, mfanyabiashara tajiri, alikuwa amejiingiza katika siasa kwa sababu alitaka kuleta kanuni za Kikristo katika uwanja wa umma.
“Ndugu, jihadhari,” nilimwambia, “utalazimika kupuuza kanuni hizo. Nina hakika hilo.”
Kwangu, hili halikuhitaji kufikiri sana. Kuanzia mwaka 1984 hadi 1999, nilihusika na kazi ya uhuru wa kidini, ikiwa ni pamoja na miaka takribani saba kama mhariri wa Liberty. Huu ulikuwa wakati wa ustawi wa Mrengo wa Kulia wa Kidini (Religious Right) Marekani, wakati mamilioni ya Wakristo, wakihamasishwa na aliyekuwa rais Ronald Reagan, waliamua kuwa Wakristo wanapaswa kurejesha maadili ya kiungu nchini Marekani. Hata hivyo, jambo hili liliwafanya wote kujichafua — na haijalishi nia yao ilikuwa njema kiasi gani — Wakristo hawa walifanya mbinu mbaya na chafu kwa wapinzani wao wa kisiasa, na walifanya hivyo kwa jina la “Yesu.” Ingawa hawakufanikisha kwa ukamilifu, Mrengo wa Kulia wa Kidini uliweka msingi wa kile kinachoendelea sasa Marekani.
Kinachoendelea sasa, kupitia Utaifa wa Kikristo (Christian nationalism), ni Mrengo wa Kulia wa Kidini uliowezeshwa kwa kiwango kikubwa mno. Wanaume waliovaa mavazi ya wanawake wakisoma hadithi kwa watoto wa chekechea; wanaume waliobadili jinsia wakiharibu michezo ya wanawake; majimbo yanayoruhusu watoto kubadilisha jinsia zao... Haya yote hayakuwa yanayoweza kufikiriwa wakati huo. Marekani imepoteza mwelekeo kabisa katika maeneo mengi—hivyo haishangazi kwamba mamilioni ya Wakristo wanaamini kuwa ni lazima kuchukuliwa hatua, na je, kuna njia bora zaidi kuliko kutwaa mfumo wa kisiasa?

Lakini haijawahi kufanikiwa. Katika kitabu Pambano Kuu, Ellen White aliandika jinsi kanisa la awali “lilipoteza Roho na nguvu za Mungu,” lilipotegemea nguvu za serikali kutekeleza mafundisho yake, na matokeo yake kuwa upapa — mnyama wa Ufunuo 13 na 14. Katika siku za mwisho, kanisa lisilo na nguvu za kiroho na lililopotoka Marekani litaufanya sanamu ya mnyama; yaani, litatumia mamlaka ya serikali kutekeleza mafundisho yake, kama alivyofanya mnyama wa kwanza. Kama hili si utaifa wa Kikristo, basi basi ni nini? Bila shaka, kila baada ya miaka michache, blogu za Waadventista wa mrengo wa kushoto huchapisha makala za kejeli zikidai kwamba mafundisho yetu ya unabii yamepitwa na wakati; kwamba Ellen White aliandika kwa ajili ya wakati wake tu, si wetu; kwamba tunahitaji kufikiria upya kuhusu matukio ya mwisho; au kwamba Roma imebadilika… maneno yasiyokuwa na maana. Hali hii inaonesha ukosefu wa ufahamu kuhusu jinsi ujumbe wetu wa unabii unavyotegemea maandiko matakatifu.
Kwa upande mwingine, Waadventista wengi wanaohofia mmomonyoko wa maadili katika nchi na serikali zao, wanapaswa kuwa waangalifu wasijikute wameshikilia mtazamo wa utaifa wa Kikristo. Hata hivyo, wasiwasi wao ni halali. Sisi ni Waadventista wa Sabato, tunatangaza ujumbe wa malaika watatu, ambao kiini chake ni nafasi ya Marekani katika kutekeleza chapa ya mnyama — si tu Marekani, bali dunia yote: “akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama” (Ufunuo 13:14). Ingawa hatujui ni lini haya yote yatatukia, kwa sasa ni nani zaidi ya wafuasi wa utaifa wa Kikristo wanaoweza kulitekeleza hilo?
Tafadhali, fikiria upande mmoja wa vita vya kitamaduni nchini Amerika ukiwa na bunduki milioni 35 (wanaojiunga na itikadi za mrengo wa kulia; wenye umoja na waliojitayarisha), wakati upande mwingine haujui hata choo gani cha kutumia (wanaojiunga na itikadi huru; wasio na umoja) — hatuhitaji hata nabii kujua nani atashinda.
Nilipomuuliza rafiki yangu, aliyeingia siasa, baada ya mwaka mmoja au miwili kama alilazimika kukiuka maadili ya Kikristo aliyotarajia kuyaleta kwenye uwanja wa umma, alijibu: “Kuanzia siku ya kwanza kabisa.”
Haswa.

* Ellen G. White, Pambano Kuu (Ufunuo Publishing House., 2023), uk. 367.

Clifford Goldstein ni mhariri wa Adult Bible Study Guide. Kitabu chake kipya ni An Adventist Journey, kilichochapishwa na Inter-American Division Publishing Association (IADPA).




Sabato si siku ya kawaida tu; ni mwaliko kutoka kwa Mungu tusimamishe shughuli zetu na tumkaribie tena Muumba wetu. Baada ya siku sita za kuumba mbingu, dunia, na kila kiumbe hai, Mungu alipumzika siku ya saba. Aliibariki siku hiyo na akaifanya kuwa takatifu (Mwanzo 2:2, 3). Mungu hakupumzika kwa sababu alichoka, bali alituwekea mfano—kumbukumbu ya kila wiki kuwa tunapata pumziko Kwake na tunaamini kazi Yake inayotufanyia mema.
Katika Kutoka 20:8–11, Mungu aliwaagiza watu Wake “ikumbuke siku ya Sabato” kwa kuifanya takatifu. Sabato ilikuwa nafasi ya kuacha shughuli za kila siku, kufurahia uwepo wa Mungu, na kumwamini Yeye kama chanzo cha kila kitu tunachohitaji. Kwa kupumzika, watu wa Mungu walionyesha kwamba maisha yao na mafanikio yao ya kiroho hayakutegemea juhudi zao binafsi, bali uaminifu wa Mungu.
Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu aliinua thamani ya Sabato. Watawala wa kidini walikuwa wameifanya Sabato kuwa siku ya sheria ngumu na kanuni tele. Katika Marko 2:27, Yesu aliwakumbusha Mafarisayo, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.” Tamko hili lilisisitiza kwamba Sabato ni baraka iliyokusudiwa kurejesha na kuleta upatanisho na Mungu—sio kitu cha kusumbua au kuumiza.
Sabato inahusu imani pia. Kwa kuacha kazi zetu na kutoa muda wetu kwa Mungu, tunakubali kuwa Yeye ndiye Mwenyezi Mungu na Msimamizi wa maisha yetu. Kama ilivyoelezwa katika Isaya 58:13-14, kuitunza Sabato huleta furaha na baraka tunapomwabudu Mungu na kufuata mpango Wake.

Sabato katika Siku za Mwisho na kwa Milele
Zaidi ya kuwa kumbukumbu ya kila juma ya nguvu za uumbaji wa Mungu na hitaji letu la kupumzika, Sabato pia ina nafasi muhimu katika unabii wa siku za mwisho. Kabla ya Yesu kurudi, Sabato itakuwa ishara ya watu wa Mungu na uaminifu wao Kwake. Ezekieli 20:20 inasema, “Zitakaseni Sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu”. Huku dunia ikikumbwa na shinikizo la kuharibu ukweli wa Biblia, Sabato inasimama kama alama ya uaminifu wa kweli kwa Muumba wetu.
Kitabu cha Ufunuo kinaelekeza kwa kundi la waumini waaminifu ambao “wanazishika amri za Mungu, na imani ya Yesu” (Ufunuo 14:12). Miongoni mwa amri hizo ni amri ya nne: kuikumbuka siku ya Sabato na kuitakasa. Kuiheshimu Sabato ya Mungu, hasa wakati ambapo wengi wanaikataa, ni alama ya kujitolea kwa Kristo na Neno Lake. Inadhihirisha kuwa tunaamini mamlaka Yake badala ya mila na desturi zilizotengenezwa na watu.
Pamoja na hayo, Sabato si tu baraka ya leo—ni zawadi ambayo tutaendelea kuisherehekea hata milele. Biblia inatuambia hili katika Isaya 66:22–23, ambapo inasema kwamba katika mbingu mpya na nchi mpya, “Sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele Zangu.” Katika makao yetu mapya, Sabato bado itakuwa wakati wa ibada na ushirika pamoja na Muumbaji wetu na watu wengine.
Kwa kuitunza Sabato leo, hatushiki tu amri za Mungu, bali pia tunatazama mbele kwa imani maisha yasiyo na dhambi, mateso, na utengano. Sabato ni mwonjo wa kila juma la mbinguni—siku inayotuelekeza kwenye pumziko la milele linalopatikana katika Kristo na urejeshwaji wa kila kitu.

Uboreshaji wa Sabato
Katika Israeli ya kale, Sabato iliwaleta pamoja familia na jamii katika ibada na ushirika. Leo hii, bado Sabato inatumika kama wakati wa kuimarisha uhusiano — na Mungu, familia, na wengine. Ni nafasi takatifu ya kutafakari juu ya wema Wake, kushiriki upendo Wake, na kujenga uhusiano wa karibu zaidi ndani ya familia zetu na jamii za imani.
Ingawa njia za kuitunza Sabato zinaweza kutofautiana, shughuli za ubunifu zinazotupeleka karibu na Mungu, familia, na wengine zinaweza kufanya siku hii kuwa na maana zaidi. Hapa kuna baadhi ya mawazo ya kusaidia kuitunza Sabato kwa njia yenye maana:
Shughuli za Pamoja za Familia
MATEMBEZI KATIKA MAZINGIRA ASILIA
Fanya matembezi katika maeneo ya asili na furahia uumbaji wa Mungu. Unapotembea, fikiria mistari kama Zaburi 19:1: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” Himiza kila mwanafamilia kutafuta kitu cha kuvutia na kukihusisha na somo kuhusu uweza au upendo wa Mungu.
MAIGIZO MAFUPI YA BIBLIA
Badilisha visa maarufu vya Biblia kuwa maigizo mafupi. Watoto wanaweza kuigiza hadithi kama ile ya Daudi na Goliathi (1 Samweli 17), Esta, au Yona (Yona 1–4). Hii huwasaidia kuelewa na kuingiza kweli za Biblia kwa njia ya kufurahisha na yenye kuvutia.
CHUPA YA SHUKRANI
Pamba chupa kubwa kwa njia nzuri. Weka vipande vya karatasi na kalamu karibu na chupa, kisha waalike wanafamilia kuandika mambo wanayoshukuru kwa juma zima na kuyaweka ndani ya chupa. Ijumaa usiku au Sabato alasiri, soma karatasi hizo pamoja kama familia. Familia yetu inafurahia desturi hii, kwani inatukumbusha jinsi Mungu anavyotutunza na jinsi maombi yetu yanavyopokelewa.
Jihusishe na Huduma ya Jamii
KUTOA VIFURUSHI VYA HUDUMA KWA MAJIRANI
Kumhudumia mwingine ni njia bora ya kumheshimu Mungu siku ya Sabato. Kama familia au kikundi, tengenezeni vifurushi vya huduma kwa majirani, wazee, au wale wanaohitaji. Weka pia barua za mikono zenye ahadi za Biblia zinazotia moyo na matumaini.
KUANDAA CHAKULA CHA PAMOJA
Fungua nyumba yako au tumia ukumbi wa kanisa kwa ajili ya chakula rahisi cha kushirikiana na marafiki, majirani, au watu wa jamii ambao wanaweza kuwa peke yao. Waebrania 13:2 inatukumbusha “msisahau kuwaonyesha ukarimu wageni” (NIV).
USAFI NA MATEMBELEZI YA MAOMBI
Changanya utunzaji wa mazingira na maombi kwa kujitolea kusafisha bustani au mtaa wa jirani. Wakati unaposafisha eneo hilo, ombea watu wanaoishi karibu.
Kuimarisha Ibada
KUANDIKA YALIYOTUKIA KUWA USHUHUDA WA UAMINIFU WA MUNGU
Fikiria wema wa Mungu katika maisha yako wiki nzima kwa kuandika baraka au maombi yaliyojibiwa. Tumia mistari kama vile Mezuri 3:22-23 kukukumbusha upendo Wake.
MUZIKI NA SIFA
Kusanyika na familia au marafiki kwa ajili ya kuimba nyimbo za ibada au sifa. Pia, mnaweza kujadili maana ya maneno ya nyimbo zenu mnapozipenda zaidi.
SANAA YA MISTARI YA BIBLIA
Tengeneza sanaa inayotokana na mistari ya Biblia. Hii inaweza kuwa kuchora picha au kutengeneza mabango yanayoangazia ahadi za Biblia kama ile ya Yeremia 29:11.
Hitimisho
Sabato ni siku maalum ya kutafakari wema wa Mungu na kufurahia baraka Zake pamoja na familia na marafiki. Shughuli yoyote utakayoichagua, ziwe za kukufanya uwe karibu zaidi na Mungu na watu wengine, na kufanya Sabato iwe siku ya furaha. Kwa kuiheshimu Sabato leo, tunajiandaa kwa moyo kwa ajili ya pumziko la milele na ibada katika uzima wa milele.

Beth Thomas ni mhariri msaidizi wa Adventist Review.




Lugha ya kitabu cha Mambo ya Walawi mara nyingi ni ngumu kueleweka na kutafsiriwa, na kirai unachokitaja ni ushahidi wa changamoto hiyo. Kinachochanganya zaidi ni kwamba Mungu anaelezewa kuwa anavutiwa na harufu ya dhabihu—jambo ambalo kwa mtazamo wa sasa linaweza kuonekana kuwa gumu kueleweka. Je, kuchoma mnyama kunaweza kutoa harufu ya kupendeza kweli? Hapa kuna tafsiri inayowezekana.
Tatizo la Tafsiri
Kirai cha Kiebrania reakh nikhoakh kinaundwa na nomino mbili: reakh maana yake “harufu” au “manukato” na nikhoakh “ya kupendeza,” “ya kustarehesha,” au “ya kuridhisha”. Kinapotumiwa pamoja, kirai hiki kinaweza kufasiriwa kwa njia mbili kuu: “Harufu ya kupendeza”, maana yake inaweza kuwa kwamba dhabihu hiyo inampendeza Mungu. Na “Harufu ya kutuliza” au “ya kuridhisha”, ikionyesha kuwa madhumuni ya dhabihu ni kumtuliza Mungu au kupatanisha hasira Yake.
Baadhi ya wachambuzi wamedokeza kuwa kitenzi ndicho kinachohusishwa na ghadhabu ya Mungu (kwa mfano, Ezekieli 5:13), lakini si nomino nikhoakh yenyewe. Hii inamaanisha kuwa tafsiri yoyote ile, iwe inasisitiza kupendeza au kutuliza, lazima iungwe mkono na muktadha wa kifungu husika.
Maana ya Kitamathali
Taswira ya Mungu akinusa harufu ya dhabihu ni ya kushangaza, na mara nyingi huchukuliwa kama lugha ya kisitiari yaani, matumizi ya lugha ya kibinadamu kumwelezea Mungu (kwa kuwa sisi hunusa vitu). maneno haya yanapotumiwa kumhusu Mungu, lugha hii hueleweka kuwa ya kishairi au kifananisho, si halisi; haipaswi kufasiriwa kwa maana ya moja kwa moja. Jambo hili linaonekana wazi katika kitabu cha Ezekieli, ambapo Bwana, akitangaza kurudi kwa watu kutoka uhamishoni, anasema: “Nitawatakabali [ratsah, ‘kuwa na upendeleo kwao’] kama harufu ya kupendeza” (Ezekieli 20:41). Lugha ya mfumo wa dhabihu inatumiwa kuonyesha ukubalifu wa Mungu kwa watu wake. Kuunganishwa kwa kitenzi “kutakabali” na kirai “harufu ya kupendeza” kunaonesha kuwa kilichokusudiwa ni dhabihu inayokubalika. Hivyo basi, watu wanaelezewa kama dhabihu ya kupendeza, inayokubalika kwa Mungu.
Maana ya Kitamathali katika Dhabihu
Maana ya kitamathali pia inapatikana katika Mambo ya Walawi 26:31, na inaonekana kuelezea maana ya “harufu ipendezayo” katika muktadha wa patakatifu. Muktadha huu ni mjadala kuhusu adhabu ya Mungu kwa wale waliokiuka agano: “Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitaisikia harufu [riakh] ya manukato yenu yapendezayo [reakh nikhoakh, ‘manukato ipendezayo’].” Katika muktadha huu, Mungu anakataa kunusa “harufu ya kupendeza.” Wataalamu wengi hufasiri hili kuwa Mungu anakataa dhabihu. Maana yake ni kwamba, wakati Mungu anapotajwa ‘kutinusa’ dhabihu, maana yake ni kwamba anakubali dhabihu hiyo. Kwa hivyo, lugha hii hutumika kwa maana ya kitamathali, si kwa maana halisi ya uwezo wa Mungu wa kunusa. Ni muhimu kuelewa kuwa Mungu hakatai dhabihu kwa sababu aliiwahi kunusa na ikanuka vibaya, wala haikubali dhabihu kwa sababu alinusa harufu nzuri. Ni wazi kuwa kitenzi “kunusa” kinatumika kwa maana ya kukubali dhabihu, si kwa maana halisi ya hisia ya harufu. Mfano mwingine wa matumizi haya ya kitamathali unapatikana katika Amosi 5:21–22: “Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa [riakh, ‘kunusa; kukubali’] na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona.” Taswira hizi zimekusanywa moja baada ya nyingine ili kuonyesha jinsi Mungu anavyokataa ibada ya Waisraeli. Kwa hiyo, wakati maandiko yanapotaja kwamba Mungu “alinusa harufu ya kupendeza,” maana yake ni kwamba alikubali dhabihu hiyo—si kwamba alipata harufu nzuri kwa maana ya kawaida. Huenda mtu akaona kirai hiki kama nahau, kinachobeba maana ya kukubali au kupendezwa.

Ángel Manuel Rodríguez, Th.D., ni mstaafu aliyehudumu kama mchungaji, profesa, na mwanateolojia.




Mnamo mwaka 2016, Kanisa la Waadventista huko Papua New Guinea (PNG) liliwahamasisha washiriki kuanzisha vikundi vya maombi kama sehemu ya mpango ulioitwa PNG kwa Kristo. Washiriki walipenda wazo hilo, na makanisa mengi yalianza kuwa na mikutano ya maombi kila Jumanne na Jumatano saa 11:00 jioni. Kama sehemu kuu ya kila ombi, vikundi hivyo vilimwomba Mungu awamimie Roho Mtakatifu, kama ilivyoahidiwa katika Matendo ya Mitume 1:8.
Ilipofika mwaka 2018, watu wengi walihisi kuwa Mungu alikuwa akiwaalika katika kipindi cha mavuno. Kanisa lilianza kupanga kampeni mbalimbali za uinjilisti katika zaidi ya maeneo 2,000 nchini kote. Wazungumzaji wa kimataifa walialikwa kwa sababu ilifahamika kuwa uwepo wao ungeongeza mvuto na kuwahamasisha maelfu kuhudhuria mikutano hiyo.
“Nilialikwa kuwa miongoni mwa wazungumzaji wa mikutano ya PNG kwa Kristo ya mwaka 2020, na nilihuzunika sana nilipoarifiwa kwamba kila kitu kimesitishwa kutokana na UVIKO-19,” anakumbuka Mchungaji Terry Johnson, rais wa Union ya Australia. “Kwa hakika, kampeni ya mavuno iliahirishwa hadi mwaka 2024, jambo lililotoa muda wa ziada kwa ajili ya maombi na maandalizi.”
Kwa namna nyingi, kuahirishwa kwa kampeni hiyo huenda kulikuwa jambo bora zaidi lililotokea kwa kampeni ya mwaka 2024, kwa kuwa kuliendeleza hali na mtindo tofauti wa kanisa.
Makundi Madogo, Mavuno Makubwa
Wakati wa janga la UVIKO-19, serikali ya Papua New Guinea (PNG) iliruhusu makanisa kukutana katika makundi ya watu wasiozidi 150. Hivyo, Kanisa la Waadventista wa Sabato liliwahimiza washiriki kuwaalika watu katika makundi madogo nyumbani kwao au makanisani kwa ajili ya masomo ya Biblia na ibada.
Kufikia mwezi wa Nne mwaka 2024, takriban vikundi vidogo 10,000 vilikuwa vikiendelea kukutana katika nyumba za washiriki wa PNG. Vikundi hivi vilikuwa msingi mkubwa uliosaidia kufanikisha ubatizo wa watu zaidi ya 220,000 katika Jimbo la Misheni la Papua New Guinea, wakati wa kampeni ya mavuno ya mwaka huo.
Mhandisi mmoja alitumia sehemu ya nyuma ya nyumba yake kuanzisha mahali pa kusoma Maandiko. Alijenga kibanda kidogo kwa kutumia turubai, na kila Sabato, pamoja na mara moja au mbili katika wiki, aliwahamasisha majirani kuungana na familia yake kwa ajili ya kusoma Maandiko na kuabudu pamoja. Majirani wake kumi walibatizwa kutokana na mwaliko huo wa kipekee.
Hadithi hii ilienea nchi nzima.
Fikiria vikundi zaidi ya 9,000 vya kusoma Biblia na kuabudu vikikutana mara mbili au tatu kwa wiki kwa angalau miaka miwili! Watu waligundua kuwa unapokuwa wazi kwa nguvu ya Neno la Mungu, Mungu hufanya mambo makubwa maishani mwako. Kanisa lilibatiza zaidi ya watu 40,000 mwaka 2022 na tena mwaka 2023.
Mwito wa Mungu wa kuvuna ulianza kuwa na sauti kubwa zaidi!
Kampeni ya Papua New Guinea kwa Kristo ilipangwa kuanza rasmi mwezi nne 2024.

Tegemea Mambo Yasiyotarajiwa
“Sikuwa najua nitakuwa wapi nikihubiri hadi wiki nne kabla ya tarehe ya kufika,” anasema Mchungaji Johnson. “Nilijua labda ningekuwa katika mji wa Lae, kwa sababu hapo ndipo ofisi ya mkutano wa umoja (union conference) iko, na nilihitaji upatikanaji wa mtandao ili niendelee na majukumu yangu kama rais wa muktano wa umoja wa Australia.”
Siku kuu ya kusafiri ilikuwa tarehe 24 Aprili! Wazungumzaji wengi wageni waliruka hadi Port Moresby, wakiwa tayari kukumbatia kauli mbiu ya nchi hiyo: “Tegemea Mambo Yasiyotarajiwa.”
“Nilisafiri kwenda Lae pamoja na wasemaji wengine saba,” anasema Mchungaji Johnson. “Huko Lae tuligundua kuwa timu yetu ilibeba jukumu la kusaidia kuendesha programu za uinjilisti katika maeneo tisa tofauti. Mimi niliteuliwa kufanya kazi katika Uwanja wa Michezo wa Omili Oval, ulio upande wa kaskazini mwa mji.”
Mchungaji Johnson aliambiwa kutarajia watu takriban 2,000 katika kila mkutano wa jioni. Lakini usiku wa kwanza walikuwepo zaidi ya watu 7,800! Na usiku wa mwisho kulihudhuriwa na watu 13,900!
Zaidi ya watu 75,000 walihudhuria kila usiku katika maeneo tisa tofauti mjini Lae. Wakati wa mikutano hiyo, Mchungaji Johnson alikaribisha watu 540 waliokuwa wametaka kubatizwa. Kumbuka, mikutano hii ilikuwa ya mavuno. Wengi wa watu hawa walikuwa tayari wakijiandaa kwa kusoma Biblia na kuhudhuria kanisa. Mikutano hii ilizaa matunda mazuri kutokana na kazi ngumu ya washiriki pamoja na maombi yao mengi.
“Tafadhali fahamu,” Mchungaji Johnson aliwaambia wachungaji waliokuwa wakimsaidia, “Sijahubiri mfululizo wa masomo ya uinjilisti kwa muda mrefu kwa sababu nimekuwa nikifanya kazi za utawala. Kwa hiyo, msiwe na matarajio makubwa sana.”
Viongozi walicheka, na mmoja wao akamgusa Mchungaji Johnson begani na kusema, “Usijali. Hili halikuhusu wewe; linamhusu Mungu na Neno lake. Mungu ndiye aliyekuchagua uwe hapa. Hatukujua ni nani angekuja, lakini tunafurahi sana kwamba ni wewe uliyefika.”
Ratiba ya kila jioni ilikuwa na kipindi cha dakika 90 cha mafundisho ya afya na muziki kutoka kwa vikundi vya nyimbo na waimbaji kutoka makanisa ya PNG. Baada ya hapo, kulikuwa na saa moja ya mahubiri. Usiku wa kwanza, Mchungaji Johnson alisikiliza sehemu kubwa ya muziki, kisha akauliza ni nani ambaye angetafsiri mahubiri yake kwa watu.
“Hakuna, Mchungaji,” akajibu mzee mmoja wa kanisa la huko. “Kama tutatafsiri, mahubiri yatachukua muda mrefu sana, karibu masaa mawili. Tunaamini Mungu atakutafsiria mwenyewe.”
“Nadhani waliniona nikiwa nimeshtuka,” anakumbuka Mchungaji Johnson, “kwa sababu siongei hata neno moja la New Guinea Pidgin, ambayo ndiyo lugha ya kawaida nchini humo.”
“Mchungaji,” mmoja wa wazee alizungumza haraka, “kama huamini, unahitaji imani. Tafadhali piga magoti, na tutakuombea tena.” Mchungaji Johnson alipiga magoti. Wazee nao walipiga magoti, wakaweka mikono yao juu yake, na wakaomba.
“Bwana, kuwa pamoja na Mchungaji Johnson. Tunajua hajaizoea hali ya ‘kutegemea yasiyotarajiwa’ kama ilivyo hapa kwetu, lakini tunakuamini na tunaamini kuwa Wewe utasababisha miujiza na kusogeza milima. Bariki maneno yatakayotoka kinywani mwake, kwa kuwa hayatakuwa maneno yake, bali yako.”
Na huo ulikuwa mwisho wa sala. Baada ya maombi, Mchungaji Johnson alisimama na kupanda jukwaani, akiwa na shauku ya kufanya kile alichoweza kwa bidii—huku Mungu akitafsiri!

Upepo Mkali Wenye Nguvu
Mchungaji Johnson alipomaliza kuhubiri, alirudi nyuma ya jukwaa na kuketi akiwa amechoka sana, akihitaji muda wa utulivu. Lakini wachungaji na wazee walimpeleka haraka nje, ambako kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wakipaza sauti kwa shangwe na kumtukuza Mungu... kwa lugha ya New Guinea Pidgin.
“Sikuweza kuelewa hata neno moja wanalosema,” anasema Mchungaji Johnson. “Hivyo mmoja wa wachungaji alinitafsiria.”
“Mchungaji,” watu walisema, “tulidhani unaweza kuzungumza lugha yetu, kwa sababu ulipokuwa unahubiri, tulihisi upepo ukivuma masikioni mwetu, na upepo huo ulipopita, tuliweza kukuelewa. Ulikuwa ukizungumza Pidgin fasaha kabisa!”
“Lo! Tukio hilo linanigusa sana kila ninapolikumbuka,” anasema Mchungaji Johnson. “Kila mara ninapofikiri kuhusu kilichotokea, nakumbuka watu wakieleza jinsi upepo ulivyovuma masikioni mwao, kisha namkumbuka mchungaji aliyeniambia, ‘Hili halikuhusu wewe, bali lilihusu Neno la Mungu.’”
Katika kipindi chote cha kampeni, Mchungaji Johnson alihubiri jumla ya mahubiri 18 yaliyokuwa na “upepo wa ajabu.” Na si kwenye eneo lake pekee—watu katika maeneo mengine pia walipata tukio kama hilo la Pentekoste. Walisema walihisi upepo ukivuma masikioni mwao wakati mhubiri alipokuwa anahubiri.
“Matendo 1:8 sasa yana maana mpya na ya kina zaidi kwangu,” anasema tena Mchungaji Johnson. “Sidhani kama nitaweza kuhubiri kama zamani. Sasa ninaelewa kwa macho yangu mwenyewe jinsi Roho Mtakatifu anavyomiminwa katika maisha yetu.”

Dick Duerksen ni mchungaji na msimuliaji wa hadithi anayeishi mjini Portland, Oregon, Marekani.




Katika dunia yenye mfululizo wa matukio ya haraka yanayobadilisha maisha, hebu tuitazame ahadi ya ajabu zaidi—tukio litakalobadilisha maisha kwa kiwango cha juu kabisa: ujio wa pili wa Yesu Kristo!
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “....Maana naenda kuwaandalia mahali. Na ikiwa nikienda kuwaandalia mahali, nitarudi tena na kuwapokea kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo” (Yohana 14:2–3, SUV). Ahadi hii ya kurudi Yesu anairudia mara tatu katika Ufunuo 22: “Tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki” (mst. 7); “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo” (mst. 12); na tena “Naam, naja upesi” (mst. 20).
Lakini, “haraka” ina maana gani hasa? Kwa mtazamo wa kibinadamu—hasa katika dunia ya sasa ya mitandao ya kijamii kama Instagram—chochote kinachochelewa kidogo tu huonekana kama kimechelewa sana.
Waadventista wa Sabato wamekuwa wakihubiri kuhusu ujio wa pili wa Kristo kwa zaidi ya miaka 180. Hata hivyo, baadhi yao, kutokana na kuvunjika moyo, wameanza kupoteza hisia ya umuhimu na uharaka wa tukio hili—hisia ambayo inapaswa kuathiri na kuongoza kila nyanja ya maisha ya Mwadventista.
Hata hivyo, kitabu cha Waebrania kinatuhimiza: “Basi msitupilie mbali ujasiri wenu; maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyatenda mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki ataishi kwa imani; naye akirudi nyuma, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi si wale wa kurudi nyuma, hata kupotea; bali ni wale wa kuamini, hata kuokolewa roho.” (Waebrania 10:35–39, SUV).
Imekuwa heshima ya kipekee kwa Nancy na mimi kuhudumia kazi ya kanisa duniani kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita, nikiwa katika nafasi ya rais wa Mkutano Mkuu. Tunapokamilisha kipindi chetu cha utumishi, tunawahimiza washiriki wa kanisa kote ulimwenguni kushiriki kikamilifu katika kumtukuza Kristo, Neno Lake, haki Yake, huduma ya patakatifu, uwezo Wake wa kuokoa katika pambano kuu, ujumbe wa malaika watatu, ujumbe wa afya, na agizo lake la mwisho kwa dunia—kueneza habari njema ya wokovu. Hili linajumuisha pia hitaji la kumwomba Mungu atupe mvua ya masika ya Roho Mtakatifu, tukitazamia kwa shauku ujio wa pili wa Kristo unaokaribia. Maranatha!




Adventist Review ilianzishwa mwaka 1849, inachapishwa na Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato, kupitia Divisheni ya Kaskazini mwa Asia-Pasifiki.
BODI YA UCHAPISHAJI
Ted N. C. Wilson, Mwenyekiti; Guillermo Biaggi, Makamu mwenyekiti; Justin Kim, Katibu; Audrey Andersson, G. Alexander Bryant, Zeno Charles-Marcel, Williams Costa, Paul H. Douglas, Mark A. Finley, James Howard, Erton Köhler, Geoffrey Mbwana, Magdiel Perez Schultz, Artur Stele, Ray Wahlen, Karnik Doukmetzian, Mshauri wa Kisheria
BODI YA USIMAMIZI – SEOUL, KOREA
Yo Han Kim, Mwenyekiti; Justin Kim, Katibu; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Tae Seung Kim; Ray Wahlen; Wajumbe wa kudumu: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson
MHARIRI MKUU
Justin Kim
WAHARIRI WENZA
Sikhululekile Daco, John Peckham, Shawn Boonstra
MKURUGENZI MWENZA
Greg Scott
MKURUGENZI WA MAWASILIANO/MHARIRI WA HABARI
Enno Müller
WAHARIRI WASAIDIZI
Beth Thomas, Jonathan Walter
WAHARIRI WALIO SEOUL, KOREA
Jae Man Park, Hyo-Jun Kim, SeongJun Byun
MENEJA WA FEDHA
Kimberly Brown
MKURUGENZI WA MIFUMO NA UBUNIFU
Daniel Bruneau
MIONGOZO YA USANIFU NA MUUNDO
Types & Symbols
KAMATI YA ADVENTIST REVIEW – DIVISHENI YA AFRIKA MASHARIKI NA KATI
Blasious Ruguri, Moses Ndimukika Maka, Tom Ogal, Emanuel Pelote, Yohannes Olana
TAFSIRI
Ufunuo Publishing House, Union Misheni ya Kusini mwa Tanzania
MSOMA PRUFU
Joyner Buhatwa
USANIFU WA TOLEO LA KISWAHILI
Daniella Ingram, Ashleigh Morton, Digital Publications
UCHAPISHAJI WA KIDIJITALI
Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)
USANIFU WA SANAA NA UBUNIFU
Brett Meliti, Ellen Musselman/Types & Symbols
TEKNOLOJIA YA MPANGILIO
Fred Wuerstlin
MHARIRI WA NAKALA
James Cavil
MENEJA WA UENDESHAJI
Merle Poirier
MRATIBU WA TATHMINI YA UHARIRI
Marvene Thorpe-Baptiste
MSHAURI MWANDAMIZI
E. Edward Zinke
MATANGAZO YA BIASHARA
Glen Gohlke
USAMBAZAJI
Sharon Tennyson
TOVUTI
KWA WAANDISHI
Miongozo kwa waandishi inapatikana katika tovuti yetu www.adventistreview.org chini ya ukurasa. Kwa mawasiliano zaidi, tuma barua pepe kwa manuscripts@adventistreview.org
Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka Biblia ya Kiswahili Union Version, 1952, iliyochapishwa na Bible Society.
The Adventist Review (ISSN 0161-1119) ni jarida kuu la Kanisa la Waadventista wa Sabato®. Linachapishwa kwa wakati mmoja ulimwenguni kote katika nchi za Argentina, Australia, Austria, Brazil, Ujerumani, Indonesia, Korea, Afrika Kusini, na Marekani. Linachapishwa kila mwezi na Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato®, 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904, Marekani. Ofisi za uhariri na fedha za Korea ziko katika Divisheni ya Kaskazini mwa Asia-Pasifiki, 67-20 Beonttwigi-gil, Paju-si, Gyeonggi-do 10909, Jamhuri ya Korea.
Hatimiliki © 2025, Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato®.
Gombo la 202, Na. 16




