powered by
send-it.me

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa prayer@adventistworld.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

 

Picha ya jalada: Ivan Ruiz-Knott, Types & Symbols

Bado ninaweza kuiskia sauti ya bibi yangu wa kumzaa mama. Mama wa imani, aliyeamka saa zisizowiana na kuomba kwa muda uliopitiliza. Hakuwahi kukosa mkutano wa maombi, sala za jioni, mafundisho ya Biblia, shule ya Sabato, au ibada. Hakuhudhuria tu mikutano ya kanisa, bali pia alishiriki katika ushuhudiaji na uinjilisti pia. Alifundisha Biblia, akajitolea kufadhili miradi ya utume, na akamwambia kila mtu aliyekuwa tayari kusikiliza kuhusu Yesu na kurudi Kwake.

 

Bado ninaweza kumsikia akizungumza kuhusu Mungu. Alionekana mwenye ari alipowazungumzia wajukuu wake. Angetoa michoro yake ya uinjilisti iliyojalidiwa na kuonyesha sanamu ya Danieli 2, wanyama wanne wa Danieli 7, chati ya unabii wa siku 2300, na mwana-kondoo aliyekuwa akitolewa kafara kwenye madhabahu ya shaba (ukiwemo mchoro wa patakatifu) ambaye alimwashiria Yesu! Kusema kweli, nilidhani angetekwa na maono ya kunyakuliwa kwa sababu ya bidii aliyoidhihirisha.

Wakati mmoja, alipokasirishwa na dereva wa gari la kanisa (ambaye kila wakati alichelewa kuja kumpeleka ibadani) aliamua kusomea jaribio la udereva.  Mamlaka ya Usalama wa Usafiri wa Korea ilivutiwa sana kwamba mzee alipita jaribio hilo mpaka wakampongeza hadharani kwa kufanikiwa kwake—aliaibika. Baada ya tukio hilo, mjomba wangu alimnunulia motokaa ya manjano angavu, kwanza kwa sababu alimwonea fahari, lakini pia kwa sababu alitaka kuhakikisha kuwa kila mtu angemwona barabarani.

 

Bado ninaweza kuisikia sauti yake leo hii. Ingawa alifariki takribani miaka mitano iliyopita, wengi bado wanakumbuka sauti na mvuto wake. Biblia iko wazi kwamba haangalii kutoka mbinguni, wala roho yake haiishi nyumbani kwake. Badala yake, amelala bila fahamu katika kaburi lililoko Pocheon, Korea Kusini.

 

Lakini bado bibi yangu anaishi. Si kwa mwili, wala mawazo, bali maombi yake bado yanaishi. Si kwa sababu bado yuko hai, bali kwa sababu Mungu aliyasikia na bado anayatambua maombi haya; matokeo ya maombi haya ni zaidi ya muda wake wa kuishi. Ku-omba kunaweza kupita, lakini maombi hayapiti masikio ya Bwana wetu.

Ukweli wake bado unaishi. Mafundisho ya Biblia aliyoyatoa, saa alizozitumia kusoma Maandiko na utafiti bado unaendelea katika akili za wale walioisikia sauti yake. Ukweli uliokuwa kwenye ushauri wake, mienendo yake ya kiroho, maagizo yake, utambulisho wake, na malezi yake bado unaendelea kwenye maisha ya watoto na wajukuu wake, wa kiroho na wa ukoo wake.

 

Tumaini lake la ufufuo bado linaishi kwa wengine. Ingawa moyo wake umekoma kudunda sasa hivi, kuna mioyo mingi leo hii inayodunda kwa tumaini lilo hilo, ikitamani sana kumwona akiwa amefufuliwa wakati Bwana Yesu atarudi, ikitamani kuona maombi yake yakijibiwa na Roho Mtakatifu, na ikitamani kuisikia sauti yake tena baada ya sauti ya Baba yetu kumwamsha katika utukufu wa milele.

Carlos Tenold (kushoto), meneja wa Programu ya Maandiko ya Wanafunzi ya Nyumba ya Uchapishaji ya Norway, akimshukuru Gideon Machogu, kutoka Kenya, kwa kazi yake. Machogu alikuwa mmoja wa wanafunzi 32 waliosajiliwa 2023. Programu hiyo, iliyozinduliwa 1965, haitatolewa tena baada ya 2023.

"Taasisi ya Kimataifa ya Masomo ya Juu ya Waadventista—Adventist International Institute of Advanced Studies (AIIAS) imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa programu hii ya masomo mchanganyiko kwa wanafunzi waliohitimu chuo ambao hapo awali hawakupata fursa ya kujihusisha na kukutana kwa sayansi na imani katika mtazamo ambao ni halisi kitaaluma na wenye msimamo wa imani. Tunaamini kuwa mpango huu utaziimarisha taasisi za elimu na makanisa katika eneo letu."

—Ginger Ketting-Weller, mwenyekiti wa AIIAS, kuhusu programu iliyoongezwa hivi karibuni ya cheti kwa waliohitimu chuo juu ya imani na sayansi. Programu hii imekusudiwa mahsusi kwa ajili ya waelimishaji na wachungaji katika Divisheni ya Kusini mwa Asia na Pasifiki nayo inakubaliana na imani ya Waadventista wa Sabato kuhusu uelewa wa Neno la Mungu na uchunguzi wa ulimwengu wa asili kupitia lenzi ya sayansi.

ZAIDI YA 150

Idadi ya wajumbe waliohudhuria Semina ya Mafunzo ya Maendeleo ya Uongozi ya Unioni Tatu za Ufilipino kwa ajili ya huduma za watoto ambayo ilifanyika katika Jiji la Cebu, Ufilipino. Tukio hili lililochukua siku tatu, lenye mada, "Kuziba Pengo: Kila M.T.O.T.O. ni wa maana sana," lililenga kukuza mazingira ya kulea na kuwawezesha viongozi kuhakikisha mustakabali mzuri zaidi kwa watoto kupitia katika utunzaji, uponyaji, kutia moyo, upendo, na nidhamu. Semina hiyo ilileta pamoja jumuiya ya watu wenye nia moja waliohamasishwa na shauku ya pamoja ya kuanzisha mazingira ya kuwatunza watoto, bila kujali usuli wao au asili yao.

Utambulisho Wangu katika Kristo

Washiriki wa kanisa waliulizwa ni gani kati ya kauli hizi inayoelezea kujitolea kwao kwa Yesu Kristo.

8,000

Idadi ya nakala za Biblia maalum ya Abide ambayo imezinduliwa na Elimu ya Waadventista katika Divisheni ya Pasifiki Kusini (SPD) ambayo imekusudiwa kwa wafanyakazi wote waliopo katika shule za Waadventista wa Sabato. Biblia ya Abide ina rasilimali za ziada ambazo zilikusudiwa kuwa msaada katika kipindi cha muda binafsi pamoja na Mungu na ukuaji katika uhusiano wa binafsi pamoja na Yesu, ambao kisha hufanya kazi kama mwongozo wa kushiriki upendo wa Yesu na wengine kwa ujasiri.

"Aina hii ya mradi huhamasisha na kwa kiasi fulani huijaza nguvu mpya hamu ile ya kuhudumu, huku ukifuata nyayo za Yesu. Ni upendo unaosonga mbele. Tunatumaini kwamba maeneo mengine ya kanisa hivi karibuni yatafuata na kujiunga na wawakilishi wao wa ADRA wa eneo mahalia kufanya kazi kwa ushirikiano."

– Luís Mário Pinto, makamu wa mwenyekiti kule Divisheni ya Amerika Kusini (SAD), kuhusu mradi wa pamoja kati ya Shirika la Maendeleo na Misaada la Waadventista (ADRA) nchini Brazili. Mnamo Septemba 17 wafanyakazi wanaohudumu katika makao makuu ya SAD walishiriki katika mradi wa Upendo Unaosonga Mbele.

"Lengo la juhudi hii lilikuwa ni kuimarisha uhusiano wa vijana na kupendezewa kwao na Mungu kupitia katika kumtumikia Yeye, kutumikiana kila mmoja na mwenzake, na kuitumikia jamii. . . . Tulitaka kushiriki katika kusisitiza tena njozi na msimamo wa Kanisa la Waadventista na uwakili wao katika utunzaji na upendo kwa mazingira huko Saint Lucia.”

– Richard Randolph, mkurugenzi wa huduma za vijana wa Misheni ya Saint Lucia ndiye pia mratibu mkuu wa tukio hilo, kuhusu mradi wa huduma ya jamii uliofanyika katika Misheni ya Saint Lucia. Zaidi ya vijana 100 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 walisafisha, wakachimba, na kupanda dazeni kadhaa ya mitende na mimea yenye kuchanua maua kama sehemu ya mkutano wa kila mwaka wa vijana uliofanyika katika kisiwa hicho.

ZAIDI YA 4,000

Idadi ya katoni za maziwa ambazo zilikusanywa na wanafunzi katika Shule ya Waadventista ya Porto Alegre nchini Brazili. Shule hii ilishirikiana na shirika lisilo la faida la Brasil Sem Frestas ("Brazili bila Mapengo") ili kuzisaidia familia zilizo katika mazingira magumu, hasa wakati wa mvua kubwa na hali ya hewa ya baridi, kwa kufunika nyumba zao za mbao kwa katoni za maziwa zilizokatwa ili kujazia mapengo. Chini ya uongozi wa mwalimu wa shule ya msingi Jozy Araújo, wanafunzi wa darasa la tatu na la nne walianza kukusanya katoni za maziwa kutoka kwa familia zao na marafiki. Mradi uliendelea kwa miezi miwili. Ulizinduliwa kwa programu maalum ambapo wanafunzi walijifunza kuhusu mchakato wa kufunika kwa kutumia katoni ya maziwa, waliona picha za matokeo ya mwisho, na kutazama video zilizoonyesha hisia za watu ambao walikuwa wamefaidika na mpango huo.

"Katika karne hii ya 21, mbinu za uinjilisti wa mapokeo—uinjilisti wa nyumba kwa nyumba, makambi, mikutano ya uinjilisti—bado zina nguvu, lakini mtu ambaye huenda asifikiwe na mkutano wa injili anaweza kuhisi kuguswa na baadhi ya maonyesho yetu ya sauti na picha. Tumeitwa kuuambia ulimwengu kwamba Yesu anakuja hivi karibuni.”

—Abel Márquez, mkurugenzi mtendaji wa Hope Channel katika Divisheni ya Amerika ya Kati na mkurugenzi wa mawasiliano wa Divisheni ya Amerika ya Kati, kuhusu tamasha la pili la filamu lililofanywa na Unioni Misioni ya Venezuela Mashariki. Mkutano wa mwaka huu ulionyesha filamu fupi fupi zaidi ya dazeni katika Casa del Artista huko Caracas mnamo Agosti 26. Zaidi ya watu 400 walikusanyika kwa ajili ya kutazama filamu hizi, ambazo zilikuwa katika makundi/jamii za tamthilia, makala za video, na filamu ionyeshayo hali halisi.

"Tunapaswaje, katika shule za Waadventista wa Sabato, kujiandaa kwa ajili ya siku zijazo?" Jo-hee Park, mkuu wa Chuo Kikuu cha Sahmyook, aliuliza mwanzoni mwa hotuba yake katika mkutano wa Global Adventist Internet Network (GAiN) Asia katika Kisiwa cha Jeju, Korea, Septemba 15. "Ni kwa jinsi gani tunawafanya watu waje makanisani mwetu na katika shule zetu?"

 

Katika dakika chache zilizofuata, Park, mzee wa kanisa la Waadventista ambaye ana shahada ya udaktari katika uhandisi na amefundisha habari za matibabu kwa miaka 21, alimtambulisha Adamu, roboti ambayo inatumia akili za bandia (AI) kujibu maswali yako ya Biblia na kukufundisha imani na mafundisho ya Waadventista.

 

Park anasema aliipa roboti hii jina la Adamu kutokana na mkakati wa kidijitali wa Chuo Kikuu cha Sahmyook, ambao ameuita "Edeni ya Kidijitali." Alielezea kwamba ameijaribu roboti hii ya kizazi cha pili kwa muda mrefu sasa. "Niliifanya roboti hii kujifunza Biblia," alisema, "ikiwa ni pamoja na imani 28 za msingi za kanisa letu." Inaweza kuwasiliana kwa lugha kadhaa, Park alisema.

 

Pia alielezea kwamba Adamu anaweza kujifunza kila fundisho na imani, kwa sababu amepangwa kufanya hivyo. Ili kumjaribu, Park alimuuliza roboti ikiwa angeweza kushiriki aya moja ya Biblia wakilishi inayozungumza kuhusu upendo. Sekunde chache baadaye, Adamu alikariri Yohana 3:16—"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee." Kisha akaongeza, kwa kile ambacho washiriki walikichukulia kuwa "sauti halisi ya mwanadamu," "Aya hii inaangazia upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu."

 

"Ukimuuliza maswali zaidi, unaweza kuona ni kiwango gani AI imefikia," Park alisema.

 

Park alisisitiza kuwa kuna tahadhari muhimu. Kwa kutumia AI, "kuna uwezekano wa taarifa potofu," alisema, "kwa sababu roboti zitaamini kile ambacho AI inasema. Roboti za AI kama hii zitakapopatikana ulimwenguni kote, ni lazima tuhakikishe kwamba roboti hiyo inaweza kufundisha imani zetu za msingi na kuziwasilisha kwa njia sahihi. Ni dhamira ambayo tunayo kwa ajili ya siku zijazo, kujifunza jinsi ya kutumia na kuuliza roboti hiyo maswali sahihi."

 

Alielezea kuwa kwa sasa, mhadhara maarufu sana nchini Korea ni ule unaojaribu kuelezea jinsi ya kutengeneza rasilimali sahihi, hivyo inawezesha kuongeza matumizi ya roboti kama vile Adamu. Jinsi unavyouliza maswali huamua majibu unayoyapata, Park alisema. "Ni muhimu kupata mafunzo ili kujifunza jinsi ya kuuliza maswali hayo," alisisitiza.

 

Park alisema kwamba siku chache baada ya uwasilishaji wake, roboti hiyo ingepelekwa ofisini kwake katika Chuo Kikuu cha Sahmyook. "Nitatumia mwaka ujao kumfundisha," Park alisema. "Kwa hiyo, wanafunzi watakapomuuliza Adamu maswali, atajibu kulingana na mafunzo ambayo ninapanga kumpa."

 

Aliongeza, "Ukija katika chuo kikuu chetu baada ya mwaka mmoja, Adamu atakutembeza katika chuo chetu na kufanya kazi kama mlinzi wa chuo. Atapatikana kwa saa 24 kwa siku saba za juma na atakuwa mwema kila wakati.”

 

Park pia alitangaza kwamba wazo ni kwamba kila mwanafunzi apate roboti ndogo, ambayo inaweza kujibu maswali ambayo hatimaye wanaweza kuwa nayo. "Hivi sasa, Adamu hayuko tayari kabisa, na [kile ninachokisema] kinaweza kuonekana kama kitu ambacho kitatokea katika siku za baadaye sana, lakini hiki kitapatikana mapema kuliko mnavyofikiria," alisema.

 

"Ninajua kuwa ninyi nyote ni viongozi na wataalamu katika maeneo fulani," Park alisema. "Hebu na tufanye kazi pamoja na kuchunguza ni jinsi gani tunaweza kulifanikisha hili."

Viongozi, washiriki waungana kwa ajili ya kutetea kuwapo kwa mikusanyiko maridhawa ya waumini na jamii. (Leaders and members rally on behalf of healthy congregations and communities)

 

Maelfu ya Waadventista wa Sabato walitetea kutoka kwenye mimbari za kanisa, mitaa ya jiji, na jamii mbalimbali ukomeshaji wa vurugu wakati wa kampeni ya "enditnow" iliyofanyika Agosti 26 hadi 27 katika Divisheni ya Amerika ya Kati (IAD) ya Kanisa la Waadventista. Kampeni ya enditnow ni mpango wa kila mwaka wa kimataifa ambao unatafuta kuwahamasisha Waadventista wa Sabato na vikundi vingine vya jamii kutetea kutokuwapo na vurugu—matumizi ya nguvu ulimwenguni kote.

 

"Wakati mwingine tunadhani kwamba mnyanyasaji anaweza kuwa mgeni anayeruka kutoka dirishani au kumkaribia mtu kutoka kwenye kichochoro cha giza, lakini kwa kawaida si hivyo," Edith Ruiz, mkurugenzi wa huduma ya wanawake wa IAD, alisema. "Unyanyasaji hutokea wakati ule mtu anapotumia nguvu ya ushawishi wake kujinufaisha kutokana na mtu aliye katika mazingira magumu."

 

Wakati wa lengo la mwaka huu, viongozi wa huduma za wanawake walitoa mahubiri na kutumia rasilimali zilizozingatia mada, "Mbwa mwitu katika Mavazi ya Kondoo: Pale Wale Wanaodai Kuwa Wafuasi wa Yesu Wanapowadhuru Wengine."

 

Kwa kuwa unyanyasaji unafanyika nyumbani na kila mahali, ni muhimu kujua kwamba jinsi tunavyomfanyia mnyanyasaji tukiwa kama wanaonyanyaswa huleta tofauti kubwa katika kiwango cha uponyaji ambao kila mmoja anaweza kupitia, Ruiz alisema. "Lazima tusikilize kwa mioyo yetu na kuwa macho kwa ajili ya wale wanaoweza kuwa waathiriwa wa unyanyasaji. Yesu, mchungaji wetu mwema, anaweza kuponya mahitaji ya kimwili na ya kihisia, kutoa lishe ya kiroho, na kuleta amani, lakini ni lazima tufanye sehemu yetu makanisani na shuleni na kila mahali,” alisema.

 

Nchini Venezuela, washiriki wa kanisa waliingia mitaani kuwafanya watazamaji wapate kujua kwamba unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto ni lazima ukomeshwe. “Hapana kwa unyanyasaji. Hapana kwa unyanyasaji wa watoto. Hapana kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake. Ndiyo kwa Kristo. Ndio kwa maisha," ni baadhi ya kelele zilizosikika mitaani. Makanisa yalifungua milango yao kwa ajili ya jamii kupaza sauti zao kupinga vurugu katika namna yake yoyote na kuwatia moyo wasikilizaji kuwa na bidii katika kupinga vurugu katika kila pembe ya nchi hiyo.

 

Panama ilishuhudia mamia ya washiriki wa kanisa vijana na wazee wakiandamana wakiwa na mabango makubwa yaliyowahimiza watu kutokuruhusu vurugu imfikie mtu mwingine tena. Vijana waliandamana pamoja wakiwakilisha shule yao ya Waadventista ili kukuza utambuzi dhidi ya unyanyasaji katika shule, bustani, na vituo vya watoto.

 

"Ikomeshe" ilikuwa ndilo lengo makanisani katika eneo lote la Unioni ya Kusini Mashariki mwa Meksiko. "Makanisa yetu yalifanya semina, shuhuda, na mazungumzo juu ya jinsi ya kukabiliana na unyanyasaji na jinsi ya kuwa macho dhidi ya unyanyasaji na kuendelea kukuza utambuzi ili makanisa yetu yawe mahali salama kwa wote," Silvia Arjona, mkurugenzi wa huduma za wanawake wa Unioni ya Kusini Mashariki mwa Meksiko, alisema.

 

Kule Kolombia, mamia ya makanisa mahalia yalifanya programu za enditnow ili kuwakumbusha washiriki wa kanisa kuwa macho kwa tabia mahususi za watoto walioathiriwa na unyanyasaji, dalili ambazo wanawake wanaweza kuzionyesha, pamoja na familia na utambuzi wa unyanyasaji dhidi ya wazee. Kwa kuongezea, jamii kadhaa zilitembelewa ambapo watoto walipewa mazungumzo na shughuli za maingiliano ili kuwawezesha kutambua aina yoyote ya unyanyasaji na jinsi ya kusema kwa sauti zaidi juu yake.

 

Wakikabiliwa na vurugu zinazoendelea nchini Haiti, makanisa yalichukua msimamo dhidi ya vurugu wakati wa programu za asubuhi na mchana za Sabato.

 

Mwanasaikolojia Laurcelie Alcimé aliwahutubia washiriki wa kanisa katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha Haiti kilichoko Carrefour, Port-au-Prince. "Mara tu unapotambua aina yoyote ya vurugu, iwe ni ya kifedha, kingono au kisaikolojia, ujue kuwa uko mbele ya unyanyasaji, na ni lazima uchukue hatua, utafute msaada, na utegemee imani yako," alisema.

Shirika la Maendeleo na Misaada la Waadventista (ADRA) lilianza sherehe zake za maadhimisho ya miaka 40 barani Afrika kwa kupanda miti 40,000 ya matunda kote nchini Zimbabwe. Mpango huo, ulioanza mwezi Agosti, unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba. 

 

Mada ya mradi wa #pandamtiwamatunda ni "Ulinzi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi," ambayo inaangazia urithi wa ADRA wa kutekeleza juhudi za kivitendo za kupunguza matokeo ya mabadiliko ya tabianchi na kuboresha afya ya jamii.

 

"Matokeo hasi ya maangamizi ya hali ya hewa yanaonekana ulimwenguni kote," mwenyekiti wa Kimataifa wa ADRA Michael Kruger alisema. "Shirika letu la hisani ulimwenguni limeshuhudia moja kwa moja jinsi ambavyo hali mbaya ya hewa, ukataji miti, mioto ya mwituni, na maendeleo vimesababisha kutoweka kwa mabilioni ya miti.

 

"Tunapoadhimisha sikukuu hii ya ukumbusho wa miaka 40 ya ADRA ya kukabiliana na majanga, misaada ya kibinadamu, na msaada wa maendeleo," Kruger aliongeza, "tumejitoa kukuza mipango kama vile upandaji miti ambayo si tu kwamba inaweza kusaidia kuboresha ubora wa hewa asilia, kupunguza mmomonyoko, na kuondoa uchafuzi bali pia kuzalisha faida za ustawi kwa wakazi katika jamii zote."

 

ADRA ilizindua #plantafruittreeinitiative—mpangowapandamtiwamatunda mwezi Agosti, kwa msaada wa maafisa wa Tume ya Misitu ya Zimbabwe, kwa kudhamini onyesho la umma la upandaji miti kwenye maeneo ya kambi na kupanda miti 1,000 ya mwanzo katika shule za nchi hii, mashamba, makazi, na taasisi katika mikoa kumi.

 

Maadhimisho ya kuweka kivuli yanaendelea mwezi huu kwa upandaji wa miti 200 zaidi ya matunda mnamo Septemba 9 katika uwanja wa gofu wa Country Club Newlands Zimbabwe huko Harare. Mwenyekiti wa Kimataifa wa ADRA Michael Kruger, wawakilishi wa USAID mshirika wa ADRA, viongozi wa serikali, mabalozi kutoka katika ofisi mbalimbali za ubalozi, na zaidi ya watu 3,000 waliojitoa kutoka makanisani wanatarajiwa kushiriki katika sherehe ya upandaji miti.

 

"Tunatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi yana jamii pana ya matokeo na bila kuepukika yana athari kubwa katika hatua za uingiliaji kati kwa hisani na kwa ajili ya maendeleo," mkurugenzi wa ADRA Zimbabwe Judith Musvosvi alisema. "ADRA imejitolea kwa dhati kukuza uendelevu wa mazingira na kuongeza uelewa juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Miti ya matunda imechaguliwa mahsusi kwa jitihada hii kwa sababu ina uwezekano mdogo wa kukatwa katika siku zijazo. Tumegundua kuwa itakuwa vigumu kwa mtu yeyote kukata mti wa matunda, eti, kwa ajili ya kuni.”

 

ADRA inaalika jumuiya zote, shule, makanisa, na mashirika ya umma na ya binafsi ulimwenguni kote kujiunga na vuguvugu hii kwa kupanda miti katika vitongoji na kushiriki uzoefu wao mtandaoni kwa kutumia msemo #GoGreenWithADRA—KuwaKijaniPamojaNaADRA. Mwaka huu, kwa Siku ya Kitaifa ya Kuweka Kivuli, shirika hili la kimataifa lilizindua kampeni nchini Marekani mnamo Aprili 28 katika Chuo cha Waadventista cha Atholton huko Columbia, Maryland. Ili kuadhimisha sikukuu ya miaka 40 ya ADRA, wanafunzi walipanda miti 40 kwenye tukio hilo.

 

"ADRA ni mleta mabadiliko chanya," Miya Kim, mkuu wa Chuo cha Waadventista cha Atholton, alisema. "Tunajua ADRA haitoi tu msaada wa muda kwa watu walio katika shida lakini pia hukaa katika jumuiya na kushirikiana nao ili kujenga kwa ajili ya siku zijazo. Tunataka wanafunzi wetu wapate kuwa waleta mabadiliko chanya na pia kuona umuhimu wa kuwekeza ndani ya na kuitunza dunia yetu na watu wake. Tunataka wajue kuhusu matokeo dhahiri na yenye kubadilisha maisha ambayo hata kupanda mti mmoja tu kunaweza kuwa nayo kwa watu."

 

Shirika hili linamtia moyo kila mtu apate # KuwaKijaniPamojaNaADRA kwa kupanda miti miwili au zaidi katika ujirani wao ili kushiriki katika ufumbuzi wa asili ambao utasaidia kupunguza utoaji wa kaboni kwa miaka ijayo.

 

Shirika la Kimataifa ya ADRA inafanya kazi katika nchi zaidi ya 130. Kazi kuu ya shirika hili ni kuwasaidia watu wenye mahitaji na sehemu zilizo hatarini sana za watu, kuboresha maisha yao na kuwafanya wawe na bidii zaidi na wenye kufanikiwa kupita katika hali ngumu za maisha, ili waweze kuishi kama Mungu alivyokusudia.

Maelfu ya vijana Waadventista wa Sabato kutoka Adventist Review walikutana mnamo Agosti 30 hadi Septemba 3 kwa ajili ya Kambi la Vijana la "Beyond the Mountain" katika Hifadhi ya Kanda San Pedro de Ancón huko Lima, Peru. Tukio hilo liliandaliwa na Idara ya Huduma za Vijana ya Kanisa la Waadventista katika Unioni Misheni ya Kusini mwa Peru.

 

Tukio hili la mafunzo lilitaka kuwandaa maelfu ya vijana kuwa wamishonari popote Mungu anapowaita: katika mji wao, nchi yao, au nje ugenini. Zaidi ya vijana 10,000 wanaotoka pwani, milimani, na maeneo ya misitu ya kusini mwa Peru walihudhuria.

 

Washiriki walipokea mafunzo maalum kwa ajili ya utume wa uinjilisti kupitia semina, programu za kujitolea za Waadventista za kitaifa na za kimataifa, na uwasilishaji wa mwongozo wa kujifunza Biblia ya "Vito 28 vya Vijana Waadventista", waandaaji walisema. Wakati huo huo, vijana walifurahia burudani mbalimbali za kuchaguliwa katika ukumbi mkubwa unaojumuisha bwawa kubwa, maeneo ya kiikolojia, mikahawa, soko na huduma zingine zinazofanya maisha kuwa mazuri.

 

Siku za kambi pia zilionyesha matamasha ya moja kwa moja yaliyofanywa na vikundi kadhaa vya muziki, ikiwemo Zimrah (kutoka Ajentina), Dulce Alabanza (kutoka Kolombia), na waimbaji kadhaa wa Peru. Maonyesho ya tamthilia yalisisitiza na kushiriki ujumbe wa kibiblia.

 

Msemaji mkuu wa wazo la jioni alikuwa ni mwinjilisti wa Nuevo Tiempo Joel Flores. Mkurugenzi wa vijana wa Unioni Misioni ya Brazili Kaskazini Sósthenes Andrade na Eduardo Lucas, mchungaji ambaye ni mmishonari nchini India, waliongoza baadhi ya semina zilizotolewa.

 

 

SHEREHE ZENYE MAANA

Wakati wa kambi hiyo, viongozi wa kanisa wa kikanda walihudhuria uzinduzi wa mpango wa Utume wa Kalebu wa mwaka 2024. "Wakati wa sherehe ya uzinduzi, maelfu ya vijana walioko kusini mwa Peru walionyesha msisimko mkubwa juu ya matarajio," waandaaji walisema.

 

Wakati huo huo, wachungaji 190, wasimamizi wa kanisa, na vijana wakubwa waliwekwa kuwa viongozi wapya wa Vijana wa Kiadventista chini ya mada inayoongoza, "Wokovu na Huduma." Pia, vijana 176 walijiandikisha katika mpango wa Huduma ya Kujitolea ya Waadventista ya Divisheni ya Amerika Kusini, na wengine 192 walijiandikisha kwa ajili ya programu ya Mwaka Mmoja katika Utume, viongozi wa kanisa wa kikanda waliripoti. Mamia zaidi walijisajili kwa ajili ya mipango mingine kadhaa ya uinjilisti na utume nchini Peru na ng’ambo, viongozi walisema.

 

Siku ya mihemko ya juu ilikamilishwa na sherehe ya ubatizo, ambapo watu 304 waliamua kushuhudia hadharani imani yao. Washiriki hawa wapya walikaribishwa kwa furaha kubwa, viongozi kutoka Unioni Misheni ya Kusini mwa Peru waliripoti. "Tunataka kuendelea kuwaongoza maelfu ya vijana na pia washiriki watu wazima katika maombi na matendo ya umishonari," viongozi walisema. "Ni lengo letu kuendelea kushiriki injili, tukifanya kazi pamoja kila wakati na tukiwa tumeshikamana."

 

 

KUHUSU MRADI WA UTUME WA KALEBU

Mradi wa Utume wa Kalebu ni mpango wa uinjilisti wa Kanisa la Waadventista uliokuzwa katika Divisheni ya Amerika Kusini (SAD). Lengo lake ni kukuza ushiriki wa vijana Waadventista katika huduma ya hiari wakati wa likizo za shule kote katika nchi nane za Amerika Kusini ambazo zinaunda eneo hilo la kanisa. Mradi huu unahimiza mtu yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka kumi na sita kushiriki kikamilifu katika uinjilisti wa jamii na uinjilisti kupitia kutembelea nyumbani, masomo ya Biblia, na shughuli zingine. Wale wanaoshiriki katika Mradi wa Utume wa Kalebu kwa kawaida huitwa "Kalebu," na kwa kawaida huenda kwenye uwanja wa utume wakiwa wamevaa mashati na kubeba mabegi ya mgongoni, Biblia, na vifaa vingine vilivyopigwa muhuri wenye jina na nembo ya mradi.

 

Kulingana na viongozi wa kanisa, mafanikio makubwa kabisa ya Mradi wa Utume wa Kalebu yalikuwa ni kujihusisha vizuri kwa vijana moja kwa moja na kikamilifu katika utume wa Kanisa la Waadventista. "Mradi huu ulisaidia kusababisha utambuzi wa uinjilisti miongoni mwa vijana katika msingi wa ushirika wao wenyewe pamoja na Mungu, [na] uliamsha wito wa umishonari kwa maelfu," walisema.

“Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Yesu aliuliza. "Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii," wanafunzi wake walijibu.

 

"Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?" Yesu aliuliza (Mt. 16:13-15).

 

Juu ya swali hili la utambulisho wa Kristo, kila kitu kinategemea—ukiwemo utambulisho wangu, utambulisho wako, na utambulisho wa kila mtu mwingine.

 

"Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai," Petro alijibu kwa usahihi (Mathayo 16:16).

 

Yesu wa Nazareti aliingia ulimwenguni kama mwana wa mwanadamu, aliyezaliwa na mwanamke wa kawaida wa Galilaya. Ikiwa ungempita kwenye barabara ya vumbi, huenda usingemtambua. Yesu alionekana kama mtu wa kawaida, lakini alikuwa zaidi ya hivyo. Alikuwa Mwana mtakatifu wa Mungu—"Neno." "Alikuwa Mungu" na "Mwanzo alikuwako kwa Mungu" (Yohana 1:1-2).

 

Neno huyu huyu "Alifanyika mwili, akakaa kwetu" (Yohana 1:14). Kwa hivyo, aliitwa "Imanueli," jina ambalo linamaanisha "Mungu pamoja nasi" (Mathayo 1:23). Ni kwa kupitia Kwake tu—Mungu wa kweli na mwanadamu wa kweli—ndipo wanadamu wangeweza kupatanishwa na uungu ili wanadamu waweze kuishi na Mungu milele zote.1

 

Lakini bado hatujawa pamoja na Mungu kwa jinsi aliyokuwa amekusudia hapo mwanzoni— jinsi ile ambayo wanadamu wa kwanza waliishi pamoja na Mungu katika Edeni kabla ya dhambi, wakati ule Mungu “akitembea bustanini wakati wa jua kupunga" (Mwa. 3:8). Kuingia kwa dhambi kulivuruga sana ukamilifu wa uwepo wa Mungu pamoja nasi. Shetani akawa "mkuu wa ulimwengu huu" wa muda (Yohana 12:31; 14:30; 16:11) na uovu, mateso, na kifo vilikuwa ndio sehemu ya uzoefu wote wa mwanadamu.

 

Lakini Mungu aliitikia kwa neema ya kushangaza, akiahidi kwamba uzao wa Hawa utakuja na kukiponda kichwa cha nyoka (Mwa. 3:15)—ikitabiri kwamba Kristo angevumilia mateso ya mwisho ili apate kumshinda Shetani na hatimaye kuondoa uovu, ili Mungu apate kuwa nasi tena kwa ukamilifu, milele zote.

 

 

UWEPO WA MUNGU NI MUHIMU KWA IMANI YA WAADVENTISTA

Wengi hutambua uwepo wa Mungu kama mada kuu ya Maandiko.2 Kwa hiyo, uwepo wa Mungu ni muhimu kwa teolojia na utambulisho wa Waadventista, ukiwa ndani hasa ya jina letu - Waadventista wa Sabato. Sehemu ya "Waadventista" ya jina letu inatambulisha imani yetu juu ya Kuja kwa Kristo Mara ya Pili, ambapo baada ya hapo "tutakuwa pamoja na Bwana milele" (1 Thes. 4:17). Sehemu ya "Sabato - Siku ya Saba" inasisitiza Sabato, siku ya saba iliyotengwa kwa ajili ya ibada na ushirika wa kupumzika pamoja na Mungu kama ukumbusho wa kazi za Mungu za uumbaji (Kut. 20:11) na ukombozi (Kum. 5:15).

 

Kwa njia hizi na nyingine nyingi, imani ya Waadventista imeunganishwa na tumaini la ushirika usiovunjika pamoja na Mungu. Kwa ujumla, jina Waadventista wa Sabato linaangazia uwepo wa Mungu pamoja nasi katika "wakati" (zawadi ya Sabato) na urejesho wa mwisho wa uwepo binafsi wa Mungu pamoja nasi (Ujio wa Pili).

 

Kando ya hizi husimama mfumo wa patakatifu, ambao kupitia huo Mungu hufanya njia ya kuwa pamoja nasi licha ya vurugu iliyoletwa na dhambi. Kisa kizima cha ukombozi kinazunguka uwepo wa Mungu, huku kazi za Kristo za upatanisho zikileta utimilifu wa mwisho wa ahadi za Mungu za kuwa pamoja na watu wake.

 

Hebu tuangalie kwa karibu zaidi nguzo hizi tatu za imani na utambulisho wa Waadventista—Sabato, patakatifu, na Ujio wa Pili.

 

 

KARAMA YA SABATO

Wengine wanaiona Sabato kama mzigo, lakini ni kinyume chake—karama kuu ya neema! Sabato ni zawadi ya uwepo wa Mungu; siku ambayo tunaweza kupumzika katika kazi Zake kwa hiyo hatupaswi kufanya kazi (kinyume cha dini iliyojengwa katika kazi). Kama Jacques Doukhan anavyoelezea: "Kwa kuitii amri ya nne, muumini hatangui thamani ya neema" bali "kwa utii wa sheria ya Mungu, muumini anaonyesha imani juu ya neema ya Mungu."3

 

Sabato ni ishara kwamba Mungu anawaokoa watu Wake—Mungu anawatakasa (anawafanya kuwa watakatifu) watu wake kama kazi Yake ya neema, ambayo ndani yake waumini wanaweza kupumzika. Kama Mungu anavyotangaza katika Ezekieli 20:12, “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.”

 

Sabato kwa hiyo inasimama kama ishara ya utambulisho wa watu wa Mungu, wale ambao ni Wake na wameokolewa na Yeye. Wakati huo huo, Sabato inakataa majaribio yoyote ya kuweka thamani au utambulisho wetu juu ya tija au mafanikio yetu, tukiwaita watu kupumzika katika kile ambacho Mungu amekifanya na kile anachokifanya.

 

Sabato pia ni siku ya ukombozi, ikikumbusha jinsi Mungu alivyowaokoa Israeli kutoka utumwani Misri (angalia Kum. 5:15). Isaya 58 inazidi kuiweka Sabato katika muktadha wa jinsi Mungu anavyoshughulika kuhusu haki, akiwaita watu wa Mungu "Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira," kuwagawia "wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa" nyumbani kwetu, kuwavika walio uchi na kutojificha kwa ndugu na dada zetu na mahitaji yao (Isa 58:6-7)—aina ya mambo yale ambayo Yesu alishutumiwa kuyafanya katika siku ya Sabato (Mathayo 12; Yohana 5; linganisha. Luka 4:18-19). Hasa, katika sura ile inayohusu Sabato katika Tumaini la Vizazi Vyote, Ellen White aliandika: "Kila dini ya uongo inawafundisha wafuasi wake kutokujali mahitaji, mateso, na haki za wanadamu."4

 

Kwa njia hii na nyinginezo, Sabato inasimama kama ishara ya utii kwa Kristo na ufalme Wake wa upendo na haki visivyo na ubinafsi dhidi ya mamlaka za ulimwengu huu zinazomfuata joka, Shetani (angalia Ufu. 12-14). Sabato vile vile inasimama kama hekalu katika wakati; siku ambayo Mungu anaitenga kwa ajili ya pumziko na uhusiano, kufurahi katika upendo wa Muumbaji wetu na Mtegemezi.

 

Tofauti na ulimwengu wetu uliojawa na kutaka mafanikio, ambako hukuza wasiwasi na kuchoka sana, Sabato inatupa wakati wa kusherehekea kazi ya Mungu kwa ajili yetu badala ya kuzingatia kazi zetu—kuzungumza na Yeye, kufurahia kile ambacho amekifanya badala ya kufukuzia kile tunachoweza kujitahidi kufanya sisi wenyewe, kupumzika ndani Yake. Katika zama ambapo watu wanazidi kuwa wapweke, wenye shughuli nyingi, wenye wasiwasi, na wenye kuvurugwa mawazo, wakati kama huo mtakatifu unazidi kuwa muhimu.

       

Miongoni mwa mambo mengine, Sabato hutoa wakati mtakatifu kwa ajili ya uhusiano usioweza kuvurugwa pamoja na Mungu na watu wengine. Ni zawadi iliyoje! Kristo anawaalika: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mt. 11:28).

 

 

HABARI NJEMA YA PATAKATIFU

Kando ya Sabato—hekalu katika wakati—panasimama patakatifu. Maskani takatifu na mahekalu ya duniani yalikuwa ni mfano wa kupaonyesha kabla patakatifu pale pa mbinguni ambapo Kristo anatuombea kama kuhani wetu mkuu (Ebr. 8:1, 2; 9:11, 12), kutupatanisha na Mungu milele zote.

 

Hii ni habari njema mno! Hata hivyo, wengi hawaelewi jinsi habari hii ilivyo njema!

 

Wengi wanapofikiri juu ya patakatifu, wanafikiria hukumu—na wala si kwa namna iliyo chanya. Kwa juu juu, hili linaeleweka. Wengi wetu hatupendi kuhukumiwa. Lakini, kwa wale wanaohitaji ukombozi, hukumu ni nzuri sana kwa kweli—njia ya Mwana-Kondoo ya upendo usiokuwa na ubinafsi hushinda na kushika nafasi ya njia ya kikatili na ya uonevu ya Joka.

 

Hebu fikiria mtu fulani akiwa katika chumba cha mahakama, akisubiri hukumu. Kila kitu kinategemea hukumu hiyo. Je, hukumu itakuwa nzuri au mbaya? Hawezi kuelewa kwa hakika. Anasubiri kwa kile kinachoonekana kama umilele. Hatimaye, hukumu inatajwa. Ana hatia kwa mashtaka yote. Mhalifu anaamriwa kulipa fidia kamili.

 

Je, mtu huyu anafadhaika au anafurahi sana? Hiyo itategemea ikiwa mtu huyo ni mshitakiwa au ni mwathiriwa wa yule aliyepatikana na hatia, akitumainia sana ukombozi.

“Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Yesu aliuliza. "Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii," wanafunzi wake walijibu.

 

"Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?" Yesu aliuliza (Mt. 16:13-15).

 

Juu ya swali hili la utambulisho wa Kristo, kila kitu kinategemea—ukiwemo utambulisho wangu, utambulisho wako, na utambulisho wa kila mtu mwingine.

 

"Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai," Petro alijibu kwa usahihi (Mathayo 16:16).

 

Yesu wa Nazareti aliingia ulimwenguni kama mwana wa mwanadamu, aliyezaliwa na mwanamke wa kawaida wa Galilaya. Ikiwa ungempita kwenye barabara ya vumbi, huenda usingemtambua. Yesu alionekana kama mtu wa kawaida, lakini alikuwa zaidi ya hivyo. Alikuwa Mwana mtakatifu wa Mungu—"Neno." "Alikuwa Mungu" na "Mwanzo alikuwako kwa Mungu" (Yohana 1:1-2).

 

Neno huyu huyu "Alifanyika mwili, akakaa kwetu" (Yohana 1:14). Kwa hivyo, aliitwa "Imanueli," jina ambalo linamaanisha "Mungu pamoja nasi" (Mathayo 1:23). Ni kwa kupitia Kwake tu—Mungu wa kweli na mwanadamu wa kweli—ndipo wanadamu wangeweza kupatanishwa na uungu ili wanadamu waweze kuishi na Mungu milele zote.1

 

Lakini bado hatujawa pamoja na Mungu kwa jinsi aliyokuwa amekusudia hapo mwanzoni— jinsi ile ambayo wanadamu wa kwanza waliishi pamoja na Mungu katika Edeni kabla ya dhambi, wakati ule Mungu “akitembea bustanini wakati wa jua kupunga" (Mwa. 3:8). Kuingia kwa dhambi kulivuruga sana ukamilifu wa uwepo wa Mungu pamoja nasi. Shetani akawa "mkuu wa ulimwengu huu" wa muda (Yohana 12:31; 14:30; 16:11) na uovu, mateso, na kifo vilikuwa ndio sehemu ya uzoefu wote wa mwanadamu.

 

Lakini Mungu aliitikia kwa neema ya kushangaza, akiahidi kwamba uzao wa Hawa utakuja na kukiponda kichwa cha nyoka (Mwa. 3:15)—ikitabiri kwamba Kristo angevumilia mateso ya mwisho ili apate kumshinda Shetani na hatimaye kuondoa uovu, ili Mungu apate kuwa nasi tena kwa ukamilifu, milele zote.

 

 

UWEPO WA MUNGU NI MUHIMU KWA IMANI YA WAADVENTISTA

Wengi hutambua uwepo wa Mungu kama mada kuu ya Maandiko.2 Kwa hiyo, uwepo wa Mungu ni muhimu kwa teolojia na utambulisho wa Waadventista, ukiwa ndani hasa ya jina letu - Waadventista wa Sabato. Sehemu ya "Waadventista" ya jina letu inatambulisha imani yetu juu ya Kuja kwa Kristo Mara ya Pili, ambapo baada ya hapo "tutakuwa pamoja na Bwana milele" (1 Thes. 4:17). Sehemu ya "Sabato - Siku ya Saba" inasisitiza Sabato, siku ya saba iliyotengwa kwa ajili ya ibada na ushirika wa kupumzika pamoja na Mungu kama ukumbusho wa kazi za Mungu za uumbaji (Kut. 20:11) na ukombozi (Kum. 5:15).

 

Kwa njia hizi na nyingine nyingi, imani ya Waadventista imeunganishwa na tumaini la ushirika usiovunjika pamoja na Mungu. Kwa ujumla, jina Waadventista wa Sabato linaangazia uwepo wa Mungu pamoja nasi katika "wakati" (zawadi ya Sabato) na urejesho wa mwisho wa uwepo binafsi wa Mungu pamoja nasi (Ujio wa Pili).

 

Kando ya hizi husimama mfumo wa patakatifu, ambao kupitia huo Mungu hufanya njia ya kuwa pamoja nasi licha ya vurugu iliyoletwa na dhambi. Kisa kizima cha ukombozi kinazunguka uwepo wa Mungu, huku kazi za Kristo za upatanisho zikileta utimilifu wa mwisho wa ahadi za Mungu za kuwa pamoja na watu wake.

 

Hebu tuangalie kwa karibu zaidi nguzo hizi tatu za imani na utambulisho wa Waadventista—Sabato, patakatifu, na Ujio wa Pili.

 

 

KARAMA YA SABATO

Wengine wanaiona Sabato kama mzigo, lakini ni kinyume chake—karama kuu ya neema! Sabato ni zawadi ya uwepo wa Mungu; siku ambayo tunaweza kupumzika katika kazi Zake kwa hiyo hatupaswi kufanya kazi (kinyume cha dini iliyojengwa katika kazi). Kama Jacques Doukhan anavyoelezea: "Kwa kuitii amri ya nne, muumini hatangui thamani ya neema" bali "kwa utii wa sheria ya Mungu, muumini anaonyesha imani juu ya neema ya Mungu."3

 

Sabato ni ishara kwamba Mungu anawaokoa watu Wake—Mungu anawatakasa (anawafanya kuwa watakatifu) watu wake kama kazi Yake ya neema, ambayo ndani yake waumini wanaweza kupumzika. Kama Mungu anavyotangaza katika Ezekieli 20:12, “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.”

 

Sabato kwa hiyo inasimama kama ishara ya utambulisho wa watu wa Mungu, wale ambao ni Wake na wameokolewa na Yeye. Wakati huo huo, Sabato inakataa majaribio yoyote ya kuweka thamani au utambulisho wetu juu ya tija au mafanikio yetu, tukiwaita watu kupumzika katika kile ambacho Mungu amekifanya na kile anachokifanya.

 

Sabato pia ni siku ya ukombozi, ikikumbusha jinsi Mungu alivyowaokoa Israeli kutoka utumwani Misri (angalia Kum. 5:15). Isaya 58 inazidi kuiweka Sabato katika muktadha wa jinsi Mungu anavyoshughulika kuhusu haki, akiwaita watu wa Mungu "Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira," kuwagawia "wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa" nyumbani kwetu, kuwavika walio uchi na kutojificha kwa ndugu na dada zetu na mahitaji yao (Isa 58:6-7)—aina ya mambo yale ambayo Yesu alishutumiwa kuyafanya katika siku ya Sabato (Mathayo 12; Yohana 5; linganisha. Luka 4:18-19). Hasa, katika sura ile inayohusu Sabato katika Tumaini la Vizazi Vyote, Ellen White aliandika: "Kila dini ya uongo inawafundisha wafuasi wake kutokujali mahitaji, mateso, na haki za wanadamu."4

 

Kwa njia hii na nyinginezo, Sabato inasimama kama ishara ya utii kwa Kristo na ufalme Wake wa upendo na haki visivyo na ubinafsi dhidi ya mamlaka za ulimwengu huu zinazomfuata joka, Shetani (angalia Ufu. 12-14). Sabato vile vile inasimama kama hekalu katika wakati; siku ambayo Mungu anaitenga kwa ajili ya pumziko na uhusiano, kufurahi katika upendo wa Muumbaji wetu na Mtegemezi.

 

Tofauti na ulimwengu wetu uliojawa na kutaka mafanikio, ambako hukuza wasiwasi na kuchoka sana, Sabato inatupa wakati wa kusherehekea kazi ya Mungu kwa ajili yetu badala ya kuzingatia kazi zetu—kuzungumza na Yeye, kufurahia kile ambacho amekifanya badala ya kufukuzia kile tunachoweza kujitahidi kufanya sisi wenyewe, kupumzika ndani Yake. Katika zama ambapo watu wanazidi kuwa wapweke, wenye shughuli nyingi, wenye wasiwasi, na wenye kuvurugwa mawazo, wakati kama huo mtakatifu unazidi kuwa muhimu.

       

Miongoni mwa mambo mengine, Sabato hutoa wakati mtakatifu kwa ajili ya uhusiano usioweza kuvurugwa pamoja na Mungu na watu wengine. Ni zawadi iliyoje! Kristo anawaalika: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mt. 11:28).

 

 

HABARI NJEMA YA PATAKATIFU

Kando ya Sabato—hekalu katika wakati—panasimama patakatifu. Maskani takatifu na mahekalu ya duniani yalikuwa ni mfano wa kupaonyesha kabla patakatifu pale pa mbinguni ambapo Kristo anatuombea kama kuhani wetu mkuu (Ebr. 8:1, 2; 9:11, 12), kutupatanisha na Mungu milele zote.

 

Hii ni habari njema mno! Hata hivyo, wengi hawaelewi jinsi habari hii ilivyo njema!

 

Wengi wanapofikiri juu ya patakatifu, wanafikiria hukumu—na wala si kwa namna iliyo chanya. Kwa juu juu, hili linaeleweka. Wengi wetu hatupendi kuhukumiwa. Lakini, kwa wale wanaohitaji ukombozi, hukumu ni nzuri sana kwa kweli—njia ya Mwana-Kondoo ya upendo usiokuwa na ubinafsi hushinda na kushika nafasi ya njia ya kikatili na ya uonevu ya Joka.

 

Hebu fikiria mtu fulani akiwa katika chumba cha mahakama, akisubiri hukumu. Kila kitu kinategemea hukumu hiyo. Je, hukumu itakuwa nzuri au mbaya? Hawezi kuelewa kwa hakika. Anasubiri kwa kile kinachoonekana kama umilele. Hatimaye, hukumu inatajwa. Ana hatia kwa mashtaka yote. Mhalifu anaamriwa kulipa fidia kamili.

 

Je, mtu huyu anafadhaika au anafurahi sana? Hiyo itategemea ikiwa mtu huyo ni mshitakiwa au ni mwathiriwa wa yule aliyepatikana na hatia, akitumainia sana ukombozi.

Joka na wafuasi wake hatimaye watahukumiwa, lakini wote wanaotubu uovu na kuupokea kwa moyo upendo wa Mungu usio na ubinafsi watasamehewa na kutakaswa (linganisha 1 Yohana 1:9). Na, kilio kitakwenda kwa Mungu: "Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa." Na: "matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa" (Ufu. 15:3-4).

 

Kwa njia ambazo hata siwezi kuanza kuelezea hapa, mfumo wa patakatifu unaonyesha upendo mzuri na kazi ya Kristo kwetu na ndani yetu—kutukomboa na kutubadilisha ili tuweze kuwa pamoja na Yeye milele.

 

 

TUMAINI KUU LA UJIO WA PILI

Hili linaturudisha kwenye tumaini kuu la Ujio wa Pili. Kama ilivyoonyeshwa hapo awali, jina "Waadventista" linatutambulisha kama watu wanaosubiri kwa hamu na kujiandaa kwa ajili ya ujio wa pili wa Kristo.

 

Baada ya kurudi kwa Kristo, Mungu ataweka "maskani" Yake tena pamoja na sisi (Ufu. 21:3). “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita (Ufu. 21:4).

 

Kwa sasa, Waadventista wamepewa jukumu la kutangaza ujumbe wa malaika watatu (Ufu. 14:6-12) upate kusaidia kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya kurudi kwa Kristo hivi karibuni—kujiandaa kuwa pamoja na Mungu tena kwa ukamilifu. Miongoni mwa mambo mengine, Ujumbe wa Malaika Watatu unaangazia jinsi njia ya joka, ambaye kwa ubinafsi anajaribu kubadili sheria ya Mungu, kulazimisha ibada, na kuutawala ulimwengu, ilivyo kinyume kabisa na njia ya Mwanakondoo—njia ya upendo usio na ubinafsi.

 

Katika Ujio wa Pili, uwepo binafsi wa Mungu pamoja nasi hatimaye utarejeshwa kikamilifu. Kisa cha Maandiko ni kisa cha jitihada ya Mungu ya kutafuta kurejesha ukamilifu wa uwepo wa Mungu pamoja nasi kama alivyokuwa amekusudia hapo awali. Mungu anataka sana kuwa pamoja nasi kiasi kwamba Kristo alifanyika kuwa mwanadamu—"Mungu pamoja nasi" katika mwili na akafa kwa ajili yetu.

 

Mwishoni, itakuwa hatimaye kwamba "maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao," na hakutakuwa na uovu tena, wala mateso, wala kifo–milele zote (Ufu. 21:3-4; 1 Kor. 2:9).

 

Ujumbe wa Waadventista ni teolojia ya ajabu ya uwepo wa Mungu—iliyoingiliana sana na kisa cha ukombozi kama kisa cha Mungu pamoja nasi. Huu ni ujumbe wa furaha kubwa na tumaini na upendo—Mungu pamoja nasi tena milele! Hatupaswi tu kuwasilisha imani yetu na kuifundisha kama habari nzuri sana, bali pia kuiishi na kuipenda ipasavyo.

 

 

UTAMBULISHO ULIOSIMAMA IMARA KATIKA KRISTO

Tunaposubiri na kujiandaa kwa ajili ya kurudi kwa Kristo, kila mmoja wetu ni lazima alijibu swali la Kristo kwetu wenyewe, "Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?" (Mt. 16:15).

 

Unasema kwamba Yeye ni nani? Jinsi unavyolijibu swali hili haihusu tu utambulisho Wake, bali pia utambulisho wako. Kwamba unalitambua hili au la, Yeye ndiye Muumbaji wako, Yeye ndiye Bwana wa wote na jina pekee ambalo kwalo tunaweza kuokolewa (Mdo. 4:12).

 

Kama kiumbe wa Mungu, aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu, tayari wewe ni wa thamani isiyopimika na Mungu anakualika katika uhusiano wa kina zaidi pamoja na Yeye. Ikiwa unamwamini Kristo, basi uko ndani ya Kristo kwa imani—mtoto aliyeasilishwa (aliyefanywa kuwa mwana) na Mungu, na kuwa na haki zote za urithi zinazohusika (angalia Rum. 8:15-17). Huo ndio utambulisho wako wa mwisho.

 

Kama Waadventista, imani yetu ina kiini chake katika uwepo wa Mungu—utambulisho wetu umefungamanishwa pamoja na kungojea na kujiandaa kwa ajili ya kurudi kwa Kristo, tukijiona kuwa tumekufa kwa ajili ya dhambi, lakini tukiwa hai katika Kristo (Rum. 6:11). Hatimaye, basi, utambulisho wetu umesimama imara katika Kristo—ambaye alikuwapo na aliyeko na atakayekuja, ambaye kupitia Kwake kila kitu kiliumbwa, ambaye alitoa maisha Yake kwa ajili yetu, alifufuka kutoka kwa wafu, hata sasa anatuhudumia kama kuhani wetu mkuu katika patakatifu pa mbinguni, na hivi karibuni atarudi kuwachukua kwenda nyumbani pamoja naye wale wote wanaolitumaini jina Lake–wapate kuwa pamoja na Mungu milele. Huo ndio utambulisho wetu—watoto wa Mungu, waliosimama imara katika Kristo, kwa tumaini. Hebu tukumbuke kila wakati sisi ni nani na tuishi kulingana na imani yetu ya Waadventista ipasavyo.

Je, mimi ni nani? Pengine hili ni mojawapo ya maswali magumu mno tunayoweza kujiuliza. Jibu linazingatia mambo mengi.

 

Mtu anaweza kusema, "Mimi ni msichana wa Kiarabu," au "mchezaji wa Ujerumani," au "afisa wa polisi wa Yankee." Msichana wa Kiarabu ni maelezo ya jumla mno na hutoa taarifa chache kuhusu muktadha wa mtu huyo. Angeweza kuwa Mwislamu binti wa mfalme huko Dubai, Mmisri Mkristo, au msichana mkimbizi wa Syria.  Mchezaji huyo wa Kijerumani angeweza kuwa Mnijeria wa kabila la Yoruba ambaye wazazi wake walitoka Togo. Anaweza kuwa mchezaji wa soka raia wa kuandikishwa wa Ujerumani mwenye uraia wa nchi mbili kwa sasa. Afisa wa polisi wa Yankee angeweza kujitambulisha zaidi kama mkana Mungu anayefanya kazi huko New York, ambaye hivi karibuni tu amefanya kipimo cha DNA na kugundua kuwa ana urithi wa Kiholanzi, Mmarekani kwa kuzaliwa, Mwafrika mweusi, Irelandi, na Mongolia.

 

Kama tunavyoweza kuona, utambulisho wetu unaweza kuelezewa kwa vipengele vingi tofauti: uraia, biolojia, jiografia, dini, utamaduni, na taaluma, kwa kutaja vichache.

 

 

VIPENGELE VYA UTAMBULISHO

Njia ambazo kwazo tunatambuliwa na serikali na jamii, mara nyingi ziko nje ya uchaguzi wetu. Utambulisho wetu unaathiriwa na kuundwa kabla hata hatujazaliwa, kwa kuzingatia sifa bainishi za kibaolojia na miundo ya kijamii. Tunapokua na kuwa wakubwa zaidi, fursa za kuimarisha utambulisho wetu zinaongezeka. Elimu na mivuto ya kijamii huchukua jukumu kubwa katika kile tunachochagua kuingiza katika utambulisho wetu.

 

Kulingana na mahali tunapoishi na kiasi cha uhuru tulionao, tunaweza kupinga mawazo fulani na kufanya uchaguzi mgumu ambao unaweza kubadilisha utambulisho wetu. Hizi zinaweza kujumuisha kubadili dini yetu, ushirika wa kisiasa, na hata utaifa. Baadhi ya uchaguzi huu unaweza kuwa matokeo ya hali ngumu. Kwa mfano, mkimbizi wa kidini aliyeteswa anaweza kuamua kubadilisha utambulisho wake wa kitaifa kwa sababu ya kutendewa kikatili katika nchi yake.

 

Baadhi ya vipengele vya utambulisho wetu wa kijamii na kitamaduni hueleweka vizuri zaidi pale tunaporudi nyuma na kufanya ulinganisho na tamaduni zingine. Nilizaliwa nchini Brazili lakini nilifahamu tu baadhi ya vipengele vya kina vya urithi wangu wa kitamaduni wa Brazili nilipoondoka nchini mwangu na kuweza kuona utambulisho wangu kwa mtazamo tofauti. Kuingiliana na Wajerumani na Walatino (wenye asili ya Kireno na Kihispania) nje ya Brazili kuliniruhusu kuelewa sifa zangu bainifu za tabia za kitamaduni za Kijerumani na Kilatini kwa uwazi zaidi.

 

Baada ya kuishi nje ya nchi zetu za asili kwa muda mrefu tunaweza kupata uzoefu wa mgogoro wa utambulisho. Mgogoro huu unajitokeza pale tunapovikubali baadhi ya vipengele vya utamaduni mpya zaidi ya utamaduni wetu wenyewe. Wakati mwingine, kunaweza kuwa na mgongano wa maadili. Mengi ya maadili haya hayahusu mema na mabaya, bali ni njia tofauti tu za kufanya mambo. Kwa mfano, mtu kutoka katika utamaduni ambao una mtindo wa mawasiliano uliofanywa kuwa tofauti kidogo anaweza kufikiri kuwa watu kutoka kwa utamaduni wenye mwelekeo wa moja kwa moja kuwa ni jeuri pale wanapozungumza moja kwa moja. Pale maadili yetu yanapopewa changamoto, ndivyo pia inavyokuwa kwa utambulisho wetu.

 

 

IMESIMAMA IMARA KATIKA UUMBAJI

Wale wanaoamini kuwa Biblia ni ufunuo wa mpango wa Mungu wa wokovu kwa sayari hii na kwao kama watu binafsi, wanaona utambulisho wao kimsingi kama watoto wa Mungu (angalia Mwa. 1:26, 27; Rum. 8:16). Maandiko yanafundisha kwamba waliumbwa na Mungu ili wakue katika maarifa na furaha. Tunapoukubali ukweli huu wa kibiblia, unabadilisha uelewa wa utambulisho wetu wenyewe. Tunatambua kwamba wakati sisi ni raia wa mahali fulani au ni wahusika wa kikundi fulani cha watu, utambulisho wetu wa msingi umesimama imara katika kisa kikuu cha kibiblia cha historia ya mwanadamu na kile ambacho Mungu amekifanya na atakifanya ili kurejesha kila kitu kwenye ukamilifu. Tunaelewa kuwa kuna kanuni ya maadili mema na mawazo bora ya jinsi tunavyopaswa kuishi na kutendeana kila mtu na mwenzake.

 

Kisa kikuu cha Biblia kinajumuisha dhana ya ufalme mpya ambao Yesu alikuja kuuanzisha, uliojengwa katika msingi wa upendo, haki, heshima, na uhuru. Hata linapokuja katika suala la uhuru wetu, tunaelewa kwamba katika uchaguzi mbalimbali tunaofanya maadili mema ya Mungu na sheria Yake, kama ilivyodhihirishwa katika Biblia, huweka kiwango cha mwenendo wa jinsi tunavyopaswa kuishi. Tunachagua kiwango cha Mungu kwa sababu Yeye anajua kile kinachofaa kwetu hata pale kinapopingana na mapendeleo na mielekeo yetu wenyewe. Tunaiamini ahadi kwamba Mungu anatupa kipimo kipya cha utambulisho, kupitia kwa Yesu, ambacho kinapita na kuongoza ufahamu mwingine wote wa utambulisho wetu wenyewe. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” (Ezek. 36:26).

 

 

JINSI MAMBO YANAVYOWEZA KUVURUGIKA

Uelewa sahihi wa utambulisho unapaswa kuwaongoza watu kuwapenda na kuwaheshimu wengine. Kwa bahati mbaya, mambo mabaya mno hutokea wakati watu wanapofanya mambo kwa namna ile ile tena na tena na kubagua katika msingi wa tofauti za utambulisho. Hii hutendeka kuzingatia jamii, rangi ya ngozi, uhusiano wa kidini, na wa kisiasa. Inaonekana kwamba mwanadamu daima atapata sababu ya kubagua. Hiyo ni kwa sababu ubaguzi umejengwa juu ya msingi wa asili ovu ya wanadamu wote. Watu wa usuli wote wa kitamaduni wamefanya mambo mabaya ajabu dhidi ya majirani zao na wageni.

 

Nilipokuwa ninakua na kujifunza kuhusu vipengele fulani vya utambulisho wa watu, kwanza niliufahamu ubaguzi wa rangi kama aina ya ubaguzi kati ya watu wa rangi tofauti za ngozi. Niliushuhudia katika nchi yangu ya nyumbani. Wakati, nikiwa na umri wa miaka ishirini na moja, nilikwenda Afrika kama mtu wa kujitolea, niligundua angalau ubaguzi kama huo, kama si zaidi, kati ya makabila fulani kama ulivyo ubaguzi kati ya wale wenye rangi za ngozi tofauti katika nchi yangu mwenyewe. Nilishtuka. Inawezaje kuwa hivyo?

 

Baadaye, kwa kuogofya, ulimwengu ulikabiliwa na ukweli wa kusikitisha wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Katika mojawapo ya nchi zilizo ndogo zaidi ulimwenguni, takribani maili 100 kwa urefu, makabila mawili makuu yaligongana. Matokeo yake ni kwamba zaidi ya watu 800,000 waliuawa.1 Wakati huo idadi ya watu wa nchi ilikuwa karibu milioni 7.2 Hiyo ingemaanisha angalau 11% ya idadi ya watu waliuawa. Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Yale unakadiria kuwa hadi asilimia 14 ya watu walikufa wakati wa mauaji hayo ya kimbari.3

 

Kwa kuhusianisha hili, kwa kutumia makadirio ya asilimia ya Yale kwa idadi ya watu wa Marekani, tungekuwa na idadi ya kushangaza ya watu milioni 46 waliouawa katika muda chini ya mwaka mmoja. Nchini Afrika Kusini leo, hiyo ingekuwa watu milioni 8.4 na nchini Korea Kusini ingekuwa zaidi ya watu milioni (7) saba. Watu wanaweza kufanya mambo mabaya ya kutisha kwa kila mmoja pale wanapoyakubali maoni yaliyopotoshwa ukweli ya utambulisho wa mwanadamu. Kama nilivyosema hii imekwisha kutokea na inaendelea kutokea kila mahali.

 

 

KUSIMAMA IMARA KATIKA KRISTO

Jiunge na Yesu. Alivunja vizuizi vyote kwa kupenda na kuchangamana na watu wote. Katika wakati alipokuwapo duniani Wayahudi waliwabagua majirani zao Wasamaria kiasi kwamba Myahudi hangezungumza na Msamaria. Kwa kemeo la moja kwa moja, Yesu alionyesha kwa mfano jirani wa kweli kwa kusimulia kisa cha Msamaria mwema katika Luka 10:25-37. Alimwonyesha Msamaria aliyebaguliwa kama mfano wa wema/huruma na upendo wakati ambapo hata viongozi wa kidini walishindwa katika wajibu wao.

Katika kitabu cha Tumaini la Vizazi Vyote (The Desire of Ages), Ellen White anaelezea vizuri jinsi Yesu alivyowatendea Wasamaria: "Yesu alikuwa ameanza kubomoa ukuta wa mgawanyiko kati ya Myahudi na Mmataifa, na kuhubiri wokovu kwa ulimwengu. Ingawa alikuwa ni Myahudi, alichangamana kwa uhuru na Wasamaria, akikataa desturi za Mafarisayo za taifa Lake. Mbele ya chuki zao aliukubali ukarimu wa watu hawa waliodharauliwa. Alilala chini ya paa zao, akala pamoja nao mezani pao, akishiriki chakula kile kilichoandaliwa na kuhudumiwa na mikono yao—alifundisha mitaani mwao, na kuwatendea kwa wema na adabu kubwa.”4

 

Ni kawaida kabisa kuwa na utambulisho wa kitaifa au wa kijamii. Hatuishi katika hali ya kutengwa. Sisi ni sehemu ya vikundi ambavyo vinashikilia utambulisho wa kitamaduni na kijamii unaofanana. Tatizo ni pale tunapowatumia vibaya au kuwatendea vibaya wale ambao wanaweza kutofautiana nasi. Utambulisho wetu haupaswi kamwe kutuongoza katika kulegeza masharti ya maadili yetu ya Kikristo. Yesu kamwe hakuwahi kuvunja sheria. Kwa kweli, aliinua kiwango akionyesha kwamba unaweza kuvunja sheria moyoni mwako kwa kuwachukia wengine (Mt. 5:21, 22). 

 

Utambulisho wetu umetiwa doa na kupotoshwa kutoka katika mpango wa awali wa Mungu. Lakini tumaini lipo. Si katika kufuata kile tunachofikiri utambulisho wetu unapaswa kuwa, bali ni kwa kumwamini yule aliyetuumba.

 

Ili kuiweka mashine iendelee kufanya kazi vizuri tunahitaji kufuata kitabu cha mwongozo cha mtengenezaji wake kuhusu jinsi ya kuitumia kwa ubora zaidi. Tukisema, sasa ni yangu na niko huru kuirekebisha na kuitunza jinsi ninavyotaka, tunaweza kupata matatizo makubwa. Je, ungependa kusafiri kwa ndege ya shirika la ndege linalomilikiwa na mtu anayepuuza kitabu cha mwongozo na kutunza ndege kulingana na matakwa yake mwenyewe? Nadhani unaielewa hoja yangu. Kanuni ni ile ile. Muumbaji wetu anajua kile kilicho bora kwetu. Anajua pia kwamba adui ameharibu uumbaji wake wa awali. Kwa bahati nzuri tunaweza kuchagua kukarabatiwa. Anataka kuumba upya na kupiga chapa mpya ya utambulisho ndani yetu. Mioyo yenye chuki inakuwa mioyo yenye upendo. “Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu” (1 Yohana 4:7).

 

Sasa swali, "mimi ni nani?" si gumu tena ikiwa tunamsikiliza Muumbaji. "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu” (Yohana 1:12, 13).

 

Utambulisho mpya? Mimi ni mpya? Ndiyo! “ ‘Tazama, nayafanya yote kuwa mapya!’ Kisha akasema, ‘Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli’ ” (Ufu. 21:5).

Makala hii, ya mwisho katika mfululizo wenye sehemu mbili, inazingatia changamoto nane zaidi zinazolikabili Kanisa la Waadventista wa Sabato leo na majibu ya kibiblia yanayotolewa kupitia Neno la Mungu. Tunaamini na kusimama kwa ujasiri juu ya Biblia na mashauri ya Mungu kwetu kupitia kwa Roho ya Unabii kama inavyotolewa katika maandishi ya Ellen G. White. Kwa kujifunza zaidi, tembelea imani za msingi zilizotajwa kwa ajili ya kuunga mkono maandiko ya Biblia na zaidi.

Patakatifu pa Agano la Kale, kama ilivyodhihirishwa kwa Musa, ni mfano wa patakatifu pa mbinguni. Kila kipengele hufunua upendo mkuu wa Mungu kwa viumbe vyake na ukatikati wa kafara na neema ya Kristo katika mchakato wa wokovu. Kanisa linaamini na kutangaza kwamba kazi ya chumba cha kwanza cha patakatifu ilikamilishwa pale Kalvari wakati Kristo alipokufa kama Mwanakondoo. Maandiko yanaonyesha kwamba mwaka 1844 Kristo aliingia katika chumba cha pili cha patakatifu halisi pa mbinguni ili kuanza hukumu ya upelelezi, naye kwa sasa anatuombea kama kuhani wetu mkuu. Huduma ya patakatifu inadhihirisha huduma kamilifu ya Kristo, ikiinua haki yake ya kutuhesabia haki na kututakasa kama njia yetu pekee ya kuuendea uzima wa milele. Hivi karibuni Yesu ataondoka kutoka katika patakatifu pa patakatifu, naye atabadilisha mavazi yake ya kikuhani na kuvaa mavazi yake ya kifalme, na kutupeleka nyumbani ili tupate kuwa pamoja naye wakati wa ujio Wake wa pili hivi karibuni.

Kanisa la Waadventista wa Sabato linafundisha kwamba Mungu aliiumba dunia hii hivi karibuni katika siku sita halisi zenye saa 24. Ninaamini kabisa katika mpangilio mfupi na si wakati wa kina, nikikubali ishara za historia ya kibiblia na Roho ya Unabii kwamba dunia hii ina umri wa miaka kama 6,000 hivi. Mungu alipouumba dunia hii, alisema, nayo iliumbwa mara moja, si katika vipindi virefu vya muda. Sabato ya siku ya saba ni ukumbusho wa Uumbaji. Inaelekeza kwa Mungu kama Muumbaji na Mkombozi wetu na ni muhimu katika kukamilisha ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12.

Fundisho la uongo la hivi karibuni, "uhalisi wa upendo," limekuzwa katika baadhi ya taasisi za elimu ya juu za Waadventista. Inatokana na imani kuwa "ukiokolewa mara moja, unakuwa umeokolewa milele," ambayo katika hii tabia si muhimu, maadam "Mungu anakupenda na hajali juu ya kile unachokifanya ikiwa umekubaliwa katika upendo Wake." Hili ni fundisho la uongo la hatari sana na halipaswi kukubaliwa, kwani linaharibu uelewa wa haki na utakaso wa Kristo. Usijaribiwe na fundisho hili la uongo.

Umuhimu wa kuja kwa Kristo mara ya pili unapaswa kuenea katika kila kipengele cha maisha kwa Waadventista Wasabato, lakini wengine wanaonekana wamepoteza hisia hii ya uharaka. Hali zilizo ngumu kuelezeka na zinazozidi kuwa mbaya katika ulimwengu huu uliochoka inabidi zituamshe kuona uharaka wa kutangaza ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12 tunapokutazamia kurudi kwa Kristo. Yesu alionyesha mara tatu katika Ufunuo 22 kwamba anakuja haraka. Hebu tuishi na hisia ya uharaka ambayo itamruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi kupitia kila mmoja wetu, tukishiriki na wengine hitaji la kuanguka chini ya msalaba na kuwa tayari kwa ajili ya Ujio wa Pili kupitia katika neema ya Yesu Kristo.1

Washiriki wengine wanaonekana kama vile wameusahau utambulisho na sababu ya kuwepo kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato kama kanisa la Mungu la waliosalia. Mungu aliliita Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa maana maalum—kumwinua Kristo na haki Yake. Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12—kuwarejesha watu kwenye ibada ya kweli ya Mungu. Mungu ameliita Kanisa hili kama vuguvugu la pekee lenye ujumbe wa pekee kuhusu utume wa pekee, uliojikita katika Kristo na utume wake wa wokovu. Ujumbe mbalimbali katika Biblia na Roho ya Unabii hutusaidia kuona kwamba Waadventista wa Sabato wameitwa na Mungu kama watu wa pekee na waliotengwa.2

 

Tumeitwa na kuchaguliwa kwa ajili ya utume wa kuwaandaa watu kwa ajili ya kurudi kwa Bwana kuliko karibu. Jina letu ni hubiri, likituambia tumetoka wapi, ni nani tunamwabudu, na wapi tunakwenda. Furahia kuwa Mwadventista wa Sabato na ushiriki ujumbe wa Marejeo na kila mtu!3

Kanisa la Waadventista wa Sabato halihusiki katika kuridhia muungano wa madhehebu yote ya Kikristo pamoja na jamii au mashirika na mavuguvugu mengine ya kidini. Hakuna kinachoweza kuutia hatarini uelewa wetu wa kibiblia wa ukweli. Tunaamini katika kufanya urafiki na vikundi vingine vya kidini na vya umma ili kuwasaidia kuelewa sisi ni akina nani na jinsi tunavyochangia kwa namna chanya katika jamii kwa kufuata njia ya Kristo ya kuwasaidia watu kimwili, kiakili, kijamii, na kiroho. Ninapata fursa mara kwa mara ya kukutana na maafisa wa umma na kushiriki nao kuhusu Waadventista wa Sabato ni nani na kile tunachokiamini, na ninaishia kuwaombea viongozi hawa wa umma. 

 

Uwepo wa Waadventista wa Sabato katika vikundi mbalimbali vya maafisa wa umma au wa kanisa haimaanishi kwa namna yoyote kwamba Waadventista wa Sabato wamekuwa sehemu ya wanaoupenda muungano wa madhehebu yote ya Kikristo (ekumeni) na kwamba wameachana na imani yoyote ya msingi ya kibiblia au kwamba watakuja kuacha. Baadhi ya taswira za matukio ya mambo ya umma zimewasilishwa vibaya, zikijaribu kuonyesha kwamba kanisa linahusika na ekumeni. Hivi sivyo ilivyo. Jihadharini na shutuma za uongo kwamba Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa "Babeli" na kwamba limetia hatarini au limekubali kulegeza masharti ya ukweli wa kibiblia. Sisi ni kanisa la Mungu la waliosalia na tutaendelea kusimama imara juu ya Neno la Mungu. Tunajua kabisa kile tutakachokabiliana nacho katika siku zijazo, nasi tunaamini kwa moyo wote katika uelewa wa kinabii wa nafasi yetu katika matukio ya mwisho ya historia ya dunia kama ilivyoainishwa katika vitabu vya Danieli na Ufunuo na Pambano Kuu.

Kanisa la Waadventista wa Sabato linafahamu kwamba Roho Mtakatifu hufanya kazi kupitia mifumo yenye miundo ambayo imepangwa na mbingu yenyewe. Kanisa hili lilipangwa kwa namna ya pekee na mahususi kama vuguvugu la Mungu la siku za mwisho la Marejeo ili lipate kutangaza ujumbe wa malaika watatu na kilio kikuu cha mwisho kwa ulimwengu ambao unahitaji sana ujumbe wa haki, neema, na wokovu wa Kristo. 

 

Kanisa limejengwa juu ya mfumo wa kamati ambao unaruhusu uingiliaji wa moja kwa moja wa Roho Mtakatifu katika jinsi maamuzi yanavyofanywa anapowaongoza viongozi na washiriki katika kufanya maamuzi. Pale maamuzi ya kamati katika ngazi ya ulimwengu yanapofanywa katika msingi wa mafundisho ya kibiblia na Roho ya Unabii na kuongozwa na maombi ya unyenyekevu, mawazo ya binafsi na imani zinapaswa kuwekwa kando, na mamlaka ya kanisa la ulimwengu yanapaswa kuheshimiwa na kukubaliwa. Pale ambapo watu au mashirika hayafuati kanuni za kibiblia za mamlaka ya kanisa, kanisa haliwezi tu "kuwafukuza" watu au kuondokana na mashirika bila kutumia njia makini sana, ya kibiblia ya kujaribu kuwasaidia kutambua makosa yao.

 

Muundo wa kanisa si mpangilio wa kiutawala msonge; umejengwa juu ya imani za kawaida za kibiblia, makubaliano ya sera, na kujitoa kufanya kazi pamoja chini ya uwezo wa Roho Mtakatifu. Ingawa kuna hatua za kinidhamu ambazo zinaweza kutumika, kanisa linafanya kazi kwa uangalifu kuwarejesha watu kwenye umoja katika Kristo kupitia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Biblia na Roho ya Unabii zimejawa na ushauri unaotuongoza kukubali mamlaka ya kanisa la ulimwengu iliyokutana, ambapo tunafanya maamuzi juu ya imani za kibiblia, vipengele vya Mwongozo wa Kanisa, maamuzi ya utawala, na mada zingine maalum zilizoletwa kwa uwakilishi wa kanisa la ulimwengu.4  

 

Roho ya Unabii inaelekeza kwamba tunapaswa kufanya kazi kwa upatanifu kila mtu na mwenzake na pamoja na Mungu. Katika ngazi ya kanisa mahalia, konferensi/misheni, unioni, na divisheni, maamuzi yote yanapaswa kufanywa kwa mujibu na ushirikiano na maamuzi yaliyofanywa yanayohusu dunia yote. Mamlaka ya kanisa si mchakato fulani wa kiutawala msonge, bali ni mchakato wa uwakilishi duniani kote unaoongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa unyenyekevu kama wa Kristo tunapaswa kuyaheshimu mamlaka ya kanisa katika ngazi zote kadiri Mungu anavyowaongoza watu wake katika siku za mwisho za historia ya dunia. Tumeitwa "kusonga mbele kwa pamoja,"5 na kwa umoja katika Kristo (Yohana 17; Efe. 4), katika imani yetu, na utume kwa ulimwengu kadiri tunavyoukaribia ujio wa Kristo hivi karibuni.

Kuna mashambulizi ya kudumu juu ya kukubalika kwa Roho ya Unabii kama ilivyotolewa na Mungu kupitia maandiko ya Ellen G. White. Roho ya Unabii ilitolewa kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato (Ufu. 12:17; 19:10) kama karama ya thamani kubwa kutoka kwa Mungu na inafaa/inahusika leo kama ilivyokuwa wakati ule ilipoandikwa. Jumla kubwa ya maandishi ya Ellen White yalitolewa na Mungu kwa ajili ya kuliongoza kanisa Lake la waliosalia katika maeneo yote ya maisha, yakituelekeza kwa Kristo na Neno Lake Takatifu, Biblia. Vikiwa vimetolewa na Mungu, Biblia na Roho ya Unabii hutufundisha jinsi ya kuwasilisha kwa ulimwengu ujumbe wa mwisho wa onyo, kuwaita watu wapate kurejea katika ibada ya kweli ya Mungu (Ufu. 14:6-12). 

 

Kwa bahati mbaya, kuna wale wanaoikashifu, kuishushia hadhi, na kuikataa Roho ya Unabii. Tunapaswa kuwa na umoja katika kuthamini na kuheshimu mashauri ya moja kwa moja ya Mungu tuliyopewa kwa undani kuhusu ukuaji wa kibinafsi wa kiroho, maisha ya kanisa, na utume wetu wa ulimwengu kama ulivyotolewa katika Roho ya Unabii. Ninawasihi mpate kuwa na msimamo thabiti wa kusoma Neno la Mungu na Roho wa Unabii na kufuata maagizo ya Mungu kwa ajili ya watu wake waliosalia wa siku za mwisho, ambao wanautangaza kwa ulimwengu ujumbe wa Kristo wenye nguvu, wa kinabii, wa kuokoa. Yesu Anakuja hivi karibuni!

Katikati ya kampasi ya chuo kikuu ambapo ninasoma na kufanya kazi, kuna nguzo iliyo na bendera ya Ajentina. Kila siku, wanaipandisha alfajiri na kuishusha jioni. Siku ya Uhuru wa nchi nyingine inapoadhimishwa, hata hivyo, pia bendera ya nchi hiyo hupandishwa kwenye nguzo fupi. Daima ninavutiwa na picha ya mabadiliko ya mara kwa mara ya bendera kwenye nguzo ile fupi. Bendera pekee ambayo inadumu kuwapo kila siku ni bendera ya nchi yangu.

 

Ninapozungumza na marafiki na wanafunzi wangu, ninatambua jinsi mabadiliko katika jamii yanavyotuathiri. Kidogo kidogo, inaonekana, hata uelewa wetu sahihi wa ukweli wa Biblia uko katika tishio la mabadiliko. Nimestushwa mno na utambuzi wa jinsi ninavyoweza kuongozwa kwa urahisi katika kuchanganyikiwa ikiwa sitakuwa makini. Ninaona jinsi ninavyohitaji kuomba kwa bidii na kusoma Biblia ili nipate kuweka nanga mahali pake.

 

Nilipowatembelea dada yangu na shemeji yangu msimu uliopita wa joto, nilihudhuria kanisani pamoja nao katika sehemu ya kaskazini ya nchi yetu. Walikuwa katika "Siku Kumi za Maombi" katika kanisa dogo sana, lakini lililo na watu wenye shauku kubwa ambao tungeweza kushiriki pamoja nao ushuhuda na nyakati nzuri za ibada kila jioni. Kama ilivyo kawaida katika programu hiyo, nilipewa kadi ya kuandika majina ya watu ambao nilitaka kuwaombea kila siku. Ilikuwa ishara sahili, lakini iliwasha kwa mara nyingine shauku ya kuzingatia zaidi maombi na maombezi. Baadhi ya watu hawa hawajui kwamba ninawaombea, lakini nimekuwa nikijaribu kutafuta njia za kufanya mambo madogo madogo ili kuonyesha kuwa ninawajali.

 

Azimio lingine nililofanya linahusisha kusoma Biblia nzima pamoja na mfululizo wa Pambano la Vizazi Vyote kwa mara nyingine tena. Wakati huu niliamua kutafakari visa hivi nikiwa na watu kwenye orodha yangu ya maombi akilini. Imekuwa ni baraka iliyoje! "Siku hizo kumi" zimegeuka kuwa zaidi ya mia moja, nazo zimenikumbusha majibu ya Mungu—"ndiyo," "hapana," na "subiri"—pale ninapoomba juu ya mambo maalum.

 

Wakati Wamidiani walipowatawala, Israeli walikuwa wamepoteza uhusiano wao wa karibu na Mungu kwa muda mrefu. Wengi wa majirani zao walikuwa wamewatawala, na ilibidi waendelee kuwatawala. Mawazo mengi ya kidunia yalikuwa yamepumbaza akili zao. Mazao ya ardhi yao yalikuwa yakiibiwa na bendera nyingine ilikuwa ikipepea juu yao. Lakini malaika wa Bwana akamjia Gideoni na, kati ya mambo mengi, alimwambia: “Bwana yu pamoja nawe . . . Enenda . . . Si mimi ninayekutuma? . . . Hakika nitakuwa pamoja nawe . . . Nitangoja hata utakaporudi” (Waamuzi 6:12-18).

 

Ni vizuri kiasi gani kuona kwamba licha ya kuondoka kwetu, mashaka yetu, na ukosefu wetu wa imani, bado tunapewa fursa za kuamsha tena moto wa uhusiano wetu pamoja na Mungu. Bado kuna muda. Lakini muda ni wa thamani kubwa, haupaswi kuchukuliwa kuwa ni wa kawaida tu.

 

Katika nchi zetu, tunaweza kusherehekea Siku ya Uhuru mara moja kwa mwaka, lakini alama muhimu kabisa katika kisa cha maisha yetu inapaswa kuwa ile inayokubali masharti ya Azimio la Kumtegemea Mungu na Neno Lake Kila Siku. Hebu hiyo na iwe ndio bendera yetu ya kweli na ya pekee. Bado anatualika tupate kuwa karibu zaidi Naye kuliko tulivyowahi kuwa, na kufanya kazi pamoja Naye kuwasaidia wale ambao bado hawajajisalimisha Kwake.

Huenda ni wachache tu ambao wamewahi kusikia kuhusu John na Cheryl Kershner, daktari wa meno wa Kiadventista na mkewe kutoka Frederick, Maryland. Wanandoa hawa ni watu mashuhuri katika eneo lao mahalia na maarufu huko Zaoksky, iliyoko mwendo wa saa mbili kwa gari kusini mwa Moscow. Wamefanya takribani safari 60 kwenda Zaoksky katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, wakiwekeza kiasi kikubwa cha muda, nguvu, na rasilimali katika taasisi kuu ya elimu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato katika iliyokuwa Muungano wa Kisovieti.

 

John, ambaye alistaafu mnamo Juni 2023 katika siku yake ya kuzaliwa ya 80, alikuja Zaoksky kwa mara ya kwanza muda mfupi baadaye kabla ya kuanguka kwa Soviet mnamo 1991. Alianzisha kliniki ya muda ya meno, akileta vifaa vyake mwenyewe apate kutumia saa nyingi sana akirekebisha meno ya watoto, wanafunzi, wahadhiri, wafanyakazi, marafiki, na majirani wa chuo hicho kikuu.

 

Wagonjwa watarajiwa waliitazamia kwa hamu ziara yake iliyofuata. Orodha ya watu waliosubiri kuzibwa na kung’olewa meno mara nyingi ilijazwa wiki kadhaa kabla ya kuwasili kwake. Hakuwahi kumkwepa mtu yeyote. Hata akiwa amekawia kufika kwa sababu ya safari ndefu ya ndege ya saa 10 kutoka Marekani, John kwa jinsi ile ile alianza kazi mara tu alipofika chuoni pale. Mtu mmoja wakati fulani aliniambia, “Meno ya nusu ya wakazi wa Zaoksky yanang'aa kwa tabasamu murua, na nusu nyingine walisubiri kwa hamu John aje kurekebisha meno yao, pia.”

 

Kwa kawaida John alileta timu ndogo ya waganga wa meno ya Waadventista wengine, Wakristo, na hata wakana Mungu. Zaoksky ilitoa fursa hiyo kushuhudia kwa madaktari hao wa meno na madaktari wa usafi kuhusu upendo wa Mungu. Kila timu ilifanya kazi kwa bidii na haikuwahi kulalamika.

 

 

ZAWADI ADIMU

John ana karama adimu ya urafiki, akijua jinsi ya kuwakubali na kuwathamini wengine. Licha ya ujuzi mdogo wa lugha ya Kirusi, John alitembelea nyumba za familia za Kirusi na kufanya urafiki wa kudumu maisha yote na wanafunzi wa chuo kikuu na viongozi, wafanyakazi wa ujenzi, madereva, walimu, wachungaji, na wafanyakazi wa jikoni. Mahali pale ambapo John alikuwepo, sherehe na burudani zingefuatia hakika. Mazungumzo ya mezani na urafiki havikuwa vya kusahaulika.

 

"Tunafurahishwa sana kwa kuona kina cha upendo ambao Bwana ameweka moyoni mwa John," alisema Alexander Salnikov, fundi mwenye kipaji ambaye, pamoja na mkewe, Masha, wamemkaribisha John nyumbani kwao zaidi ya mara 50. "Anajua jinsi ya kupenda kwa dhati, kuwapenda wale wanaoteseka."

 

John alipata marafiki kila mahali: katika hospitali ya mtaa na kanisa la kijiji, miongoni mwa maafisa wa serikali za mitaa, na kwenye ndege. Wakati fulani, alipewa jina la utani la "Ivan Ivanovich," jina la kawaida mno nchini Urusi. Cha kupendeza, baada ya kupata marafiki nchini Urusi, John mara nyingi aliwaalika wapate kumtembelea kule Maryland. Baadhi ya watu ambao hakuweza kuwasaidia na vifaa vyake vichache vya meno huko Zaoksky waliishia kutibiwa katika kliniki ya John huko Frederick.

 

Ni watu wangapi waliopata msaada wa meno? Hakuna mtu anayejua kwa hakika na ikiwa John anajua, hasemi.

 

 

ZAIDI YA MENO

Msaada umeenda mbali zaidi ya meno. Yelena, binti wa Vasiliy Novosad, ambaye alisimamia ujenzi wa Zaoksky mnamo mwaka wa 1986, aligunduliwa kuwa na saratani akiwa ni msichana wa miaka 17 mwishoni mwa miaka ya 1990. Kwa kuona kwamba hakuwa na nafasi ya kupata matibabu madhubuti nchini Urusi, John alimpeleka kwenye Ubalozi wa Marekani huko Moscow kuomba viza ya Marekani. Kwa furaha yao, afisa wa ubalozi alikubali ombi hilo. Baadaye, John na Cheryl walimtunza Yelena kabla na baada ya operesheni iliyofanywa kwa mafanikio nchini Marekani. Pia walilipia ada ya masomo yake ili kuhudhuria chuo kikuu huko Marekani.

 

Wanafunzi wengi wamepokea elimu ya Waadventista kwa kupitia msaada wa John. Kwa kuwatambua vijana wenye vipaji ambao walikuwa wamejitoa kwa Yesu na wenye shauku ya kusomea tiba, John amesaidia kuwaweka wengi wao kupata masomo katika Chuo Kikuu cha Tiba cha AdventHealth University huko Florida, Chuo Kikuu cha Andrews huko Michigan, Chuo Kikuu cha Loma Linda huko Kalifornia, na Southern University–Chuo Kikuu kilichoko huko Tennessee. Mara nyingine, amelipia karo yeye mwenyewe, na mara nyingine amepata wafadhili.

 

Katika tukio moja la kukumbukwa, aliingilia kati kwa niaba ya mwanafunzi mmoja ambaye ilikuwa aanze masomo ya udaktari wa meno ambaye alikuwa na deni kubwa katika Chuo Kikuu cha Andrews. Yeye na mkewe walichangia ndege yao ya binafsi kwa programu ya vyombo vya anga ya chuo kikuu hicho kwa ajili ya kulifidia deni hilo. Katika kisa kingine, John alimtambua kijana mmoja wa kike ambaye hakuweza kulipa karo yake ya miaka miwili ya mwisho katika Kitivo cha Meno cha Chuo Kikuu cha Loma Linda. Alimpata mtu aliyelipia karo. Wanafunzi wameguswa mno na wema wa John na kuuona kama jibu la Mungu kwa maombi ya dhati ya machozi.

John na Cheryl walitokea kuupenda muziki wa Kirusi nao wamewafadhili kwa sehemu au kikamilifu wanafunzi zaidi ya 50 katika idara ya muziki ya Zaoksky kwa miaka mingi. Bila ya msaada wao wa ukarimu, idara hii huenda isingeweza kuendelea kuwapo kupitia miaka kadhaa iliyokuwa migumu. John alisaidia kununua vyombo vya muziki na kuchangia pesa ili kwaya ya Zaoksky iweze kusafiri na kufanya matamasha kote nchini Urusi na nje ya nchi. Mnamo 2009, John aliandaa na kuunga mkono kifedha safari ya kwaya ya Fletcher Academy kutoka Carolina ya Kaskazini kusafiri kwenda Zaoksky. Wanafunzi hao 45 walipokelewa vizuri walipokuwa wakiimba katika juma la mikutano ya maombi na katika matamasha kadhaa.

Mtu asiyejitanguliza, John anasema kidogo juu ya juhudi zake za utume kwa Zaoksky. Ufasaha wake ni kazi zake. Kiti cha magurudumu kilichonunuliwa kwa ajili ya msichana mlemavu. Pesa zilizotolewa kwa ajili ya kununua dawa. Nauli za ndege zilizolipwa kwa niaba ya wanafunzi wanaokabiliwa na matatizo ya kifedha. Chanjo. Mavazi. Chakula. Kompyuta kadhaa. Vitabu vya kufundishia. Tiketi za ndege kwa ajili ya mwanamuziki wa kufanya tamasha kwa ajili ya jamii ya Zaoksky. Tiketi zaidi za ndege kwa ajili ya mchungaji wa kuendesha juma la maombi huko Zaoksky. Orodha inaendelea bila kukoma. Ni mbingu peke yake inajua majina yote na hali zote ambazo familia ya Kershner waliingilia kati ili kuleta nafuu katika maisha ya mtu fulani.

 

Bila shaka, upendo wao kwa Zaoksky unaakisi upendo wao kwa Yesu. Cha kusikitisha, Cheryl aliaga dunia mwezi uliopita wa Machi. Urithi wao utakuwa ni wa kudumu nao utaendelezwa na watu wengine wenye mawazo ya utume watakaotiwa moyo na kujitoa kwao kwa Yesu kwa utulivu. Kama ishara ya shukrani za Zaoksky kwa ajili ya msaada wa John kwa wanafunzi, kituo cha wanafunzi cha chuo kikuu kimepewa jina lake kwa ajili ya heshima yake.

Mmoja wa wenzetu, Tim Lale, hivi karibuni alisimulia kisa cha wazazi wake wamishonari na mwisho wao wa tanzia walipokuwa wakihudumu nchini Zimbabwe. Tunashiriki toleo lililorekebishwa la simulizi lililochukuliwa kutoka katika Ensaiklopidia ya Waadventista wa Sabato.1 -Wahariri

 

Don Lale na mkewe Ann walikuwa ni walimu wa Kiadventista waliohudumu kama wamishonari nchini Zimbabwe wakati mnamo 1981 walipouawa kikatili na walioshukiwa kuwa waasi wa Msumbiji katika shambulio la alfajiri katika shule ambayo walikuwa wanafundisha. Waasi hawa walikuwa wakifanya ulipizaji kisasi dhidi ya shambulio la vikosi vya Afrika Kusini, na familia hii ya Lale walikuwa ni waathiriwa wasio na hatia wa hasira yao kali.

 

 

MAISHA YA AWALI NA ELIMU

Don Lale alizaliwa mwaka wa 1931 katika Kisiwa cha Wight, Uingereza. Alipokuwa kijana, alijiunga na Jeshi la Kifalme la Anga na, alipokuwa akifanya kazi nchini Mauritius, alianza kujifunza masomo ya Biblia kutoka kwa familia ya Kifaransa ambayo yalimpelekea kuwa Mwadventista. Aliporudi Uingereza, alibatizwa na kujiunga na Chuo cha Newbold. Kwa muda Lale alifanya kazi katika Stanborough Press katika Idara ya Photo-Litho.

 

Mnamo Machi 18, 1962, Lale alimwoa Ann E. Smith. Ann alikuwa amesoma katika Chuo cha Newbold ambapo alihitimu kama mwalimu wa Biblia. Ann alifanya kazi katika Sanitariamu ya Stanborough na kama mwalimu wa Biblia katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la New Gallery huko London. Wakati Stanborough Press ilipohamia Grantham mnamo 1966, familia hii ya Lale ilihama pamoja nayo. Lale aliendelea kufanya kazi katika vyombo vya habari hadi pale yeye na Ann walipojiandikisha kujiunga na kozi ya mafunzo ya ualimu ya miaka mitatu katika Chuo cha Elimu cha Stoke Rochford huko Grantham. Baada ya kuhitimu wote wawili walifanya kazi katika shule za Grantham.

 

 

KUHAMIA AFRIKA

Mnamo Januari 1975, Lales waliitwa kuhudumu katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu huko Gwelo (sasa Gweru) huko Rhodesia (sasa Zimbabwe). Nchi ilikuwa ikipitia kipindi cha kutokuwa na utulivu kufuatia vita vya ukombozi ambavyo viliwapambanisha majeshi ya wazalendo kupigana na utawala wa Waziri Mkuu Ian Smith. Katika barua iliyochapishwa katika British Advent Messenger mnamo 1975, familia ya Lale walikuwa wameyakubali na kujiandaa vyema kwa ajili ya maisha katika Afrika, wakitembelea na kufurahia vivutio ambavyo vilikuwamo Rhodesia. Waliandika, "Hali ya kisiasa inazidi kuwa isiyo na uhakika wakati wa mchana na vita vya kigaidi vimeongezeka, lakini tunaamini kwamba Bwana atakuwa kimbilio letu na nguvu yetu."2 Walihudumu huko Gweru kwa miaka miwili, na watoto wao wawili wa kiume walihudhuria shule mahalia. Timothy, mkubwa kati ya wawili hao, alienda katka shule ya bweni huku Andrew akisafiri kila siku kwenda shuleni.

 

Mnamo Agosti 1977 walihamia Shule ya Anderson, kilomita 17 (maili 10) mashariki mwa Gweru. Walihama kwa sababu ya hali ya hatari katika eneo la Gweru na kukaa Anderson kwa miaka mitatu. Mbali na mzigo wa kawaida wa kufundisha, Don alikuwa msimamizi wa bweni la wavulana. Mnamo Julai 1978 walirudi Uingereza kwa ajili ya likizo wakiwa na watoto wao Timothy na Andrew, baada ya hapo walirudi katika Shule ya Anderson. Mnamo Aprili 1980 Rhodesia ilikuwa taifa huru la Zimbabwe.

 

 

KIFO NA MATOKEO YAKE

Mnamo Desemba 1980, familia ya Lale walihamia Shule ya Sekondari ya Inyazura (kwa sasa Shule ya Upili ya Waadventista wa Nyazura) Mashariki mwa Zimbabwe, takribani kilomita 90 (maili 56) kutoka mji wa mpakani wa Mutare. Walikuwa wameitikia wito wa kaimu mkuu wa shule kuhamia Nyazura ili kuziba pengo. Shule hiyo ilianzishwa mnamo mwaka 1910 na ilikuwa mojawapo ya shule kongwe sana za Waadventista nchini Zimbabwe.3 Mnamo 1976 ilikuwa imefungwa wakati wa vita vya ukombozi, ikifunguliwa tena mnamo 1979, na akina Lale walikuwa ni sehemu ya mpango wa ufufuaji wake.

 

Akina Lale ndio tu walikuwa wameanza kufanya makazi yao ili wapate kufundisha pale ambapo, Jumanne, Februari 3, 1981, walishambuliwa na watu wawili wenye silaha na kuuawa kikatili. Ann alipigwa kichwani na stuli na kisha akapigwa risasi kwa karibu. Don alikimbia kwenda ofisini kuomba msaada lakini alifuatwa na mmojawapo wa watu wale wenye silaha ambaye alimpiga kifuani kwa kitu fulani butu.4 Don alianguka na wafanyakazi ambao walikuwa hapo walijaribu kumsaidia, lakini mshambuliaji alitishia kuwapiga risasi ikiwa wangethubutu kufanya hivyo. Walimtazama bila msaada alipokuwa akimpiga Don kwa rungu hadi akafa. Kisha mshambuliaji aliwalazimisha wafanyakazi kukariri kauli mbiu za kizalendo na kuwalazimisha kutoka nje ya jengo kabla ya kukimbilia gizani.

Mauaji ya akina Lale yalipeleka mawimbi ya mshtuko ulimwenguni kote, na mitandao mikubwa ya habari ilibeba habari hiyo. Wakati wa kifo cha wazazi wake, Tim alikuwa nchini Uingereza akisoma katika Shule ya Sekondari ya Stanborough wakati Andrew alikuwa nchini Zimbabwe. Tim alisafiri kwa ndege kwenda Zimbabwe kuhudhuria mazishi yao. Wanandoa hao walilazwa kupumzika kila mmoja karibu na mwenzake katika Makaburi ya Solusi huko Bulawayo, Zimbabwe.

 

Ibada ya ukumbusho ilifanyika katika kanisa la Stanborough Park mnamo Machi 1, 1981, na ilihudhuriwa na naibu meya wa Watford na mbunge wa eneo hilo. BBC ilimhoji mtoto wao, Tim, mara tu baada ya yeye na mdogo wake kurudi kutoka Zimbabwe. Alizungumza kwa ufasaha juu ya tukio hilo, imani yake kwa Mungu, na tumaini lake katika kurudi kwa Kristo hivi karibuni. Alisikika na mamilioni ya wasikilizaji kote Uingereza. Magazeti makubwa pia yalibeba kisa hicho katika vichwa vyao vya habari, na kanisa la Waadventista nchini Uingereza lilipata usikivu usio na kifani katika taifa ambalo wengi walikuwa hata hawajasikia kuhusu kanisa hili.5 

 

Zaidi ya miaka 40 imepita tangu tukio hili la tanzia, na mtoto wao, Tim, bado anazungumza akiwa na imani kwa Mungu na uongozi Wake. Hatuwezi kuelewa kwa nini mambo kama haya hutokea kwa wale wanaoyatolea maisha yao kushiriki injili, lakini hatutavunjwa moyo kuwafikia wengine kwa ajili ya Yesu bila kujali changamoto au hali. Haijalishi tuko wapi, tunafanya kazi "katika mwelekeo wa wajibu" kumfuata Yesu bila kujali anaongoza wapi.

Ufunuo 14:6 haitoi ufafanuzi dhahiri wa maudhui ya injili. Mtu anaweza na anapaswa kudhani kwamba ni injili ile ile ya wokovu kwa imani katika kazi ya ukombozi ya Kristo inayopatikana katika Agano Jipya lote. Ukweli ni kwamba hatutakiwi kusadiki chochote bila uthibitisho kwa sababu usomaji wa kitabu cha Ufunuo unadhihirisha uelewa wa Yohana wa injili ya milele.

 

 

1. MUHTASARI WA INJILI (UFU. 1:3-5)

Ni mwanzoni kabisa mwa kitabu ambapo Yohana anawasilisha habari njema ya wokovu kupitia kwa Kristo, na hivyo kuashiria umuhimu mkuu wa mada hii katika Ufunuo. Yohana anawasalimu wasikilizaji wake kwa jina la nafsi tatu za Uungu, zinazotambulishwa kama chanzo cha "neema" na "amani" (Ufu. 1:4). Haya ni maneno mawili ya msingi ya kisoteriolojia. Neema ni zawadi ya wokovu usiostahiliwa na amani inaonyesha upatanisho wetu na Mungu kupitia kwa Kristo. Mwishoni mwa salamu, Yohana anatoa wimbo wa sifa kwa Yesu na kumtambulisha kama Yeye "atupendaye" na "kutuosha dhambi zetu katika damu Yake" (aya ya 5). Hapa Yohana anaelezea jinsi ambavyo neema na amani vinaweza kutiririka kutoka kwa Uungu kuja kwetu, yaani kupitia katika kifo cha kujitoa kafara cha Kristo ambaye alitukomboa kutoka katika dhambi. Upendo wa kiungu unadhihirishwa katika tendo la kiungu la ukombozi lililowezekana kwa gharama ya uhai wa Yesu. Alikufa badala yetu. Hiki ndicho kiini hasa cha injili.

 

 

2. MWANAKONDOO NA UKOMBOZI

Uelewa ule ule wa wokovu unapatikana katika Ufunuo 5:9, 10, lakini wakati huu umekamilishwa kupitia kazi ya Mwanakondoo yule aliyechinjwa kwa ajili yetu, na hivyo kusisitiza tena fasiri yetu ya kirai "katika damu yake." Lugha ya kafara iliyowasilishwa katika Ufunuo 1:5, sasa inaonekana katika kifo cha kafara cha Mwanakondoo. Viumbe wa mbinguni wanaimba wimbo wa sifa kwa Mwanakondoo wakitangaza kustahili Kwake kwa kuwa "Ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa," (Ufu. 5:9). Dhana ya ukombozi inaonyeshwa kwa kutumia taswira ya ununuzi wa uhuru wa watumwa. Gharama kwa Uungu ilikuwa ni damu ya Mwanakondoo–kifo cha kafara cha Kristo. Ilikuwa ni kupitia katika kifo Chake ambapo Mwanakondoo aliyashinda majeshi ya uovu na kuwaokoa watu Wake. Injili ya milele ilionekana na inaendelea kuonekana wazi katika Ufunuo katika sura ya Mwana-Kondoo aliyechinjwa.

 

 

3. MWANAKONDOO NA WATU WA MUNGU

Kifo cha kafara cha Mwanakondoo hakifafanuliwi kupitia katika dhana ya ukombozi peke yake bali pia kwa kupitia ile ya utakaso. Hii ni sura mpya—wanadamu wako katika hali ya uchafu, wametengwa na Mungu na wanaelekea katika kutoweka, wakihitaji utakaso. Sabuni ni damu ya Mwana-Kondoo (Ufu. 7:14). Ni kwa kuikubali ahadi ya kiungu ya ufanisi wa kuokoa wa Mwanakondoo peke yake ndipo wanadamu wanapotangazwa kuwa huru kutokana na uchafu wa kimaadili na wa kiroho. Hivyo, damu ya Mwanakondoo inawawezesha watu wa Mungu kusimama mbele za Mungu na Mwanakondoo bila hofu huku wakiwatumikia (aya ya 15); tofauti dhahiri na waovu ambao hawawezi kusimama imara mbele za Mwanakondoo (Ufu. 6:15-17). Watu wa Mungu walimshinda joka kupitia katika damu ya Mwanakondoo (Ufu. 12:11) hasa pale walipomkubali kama Mkombozi. Mwishoni mwa pambano la ulimwengu, Kristo anaketi katika kiti cha enzi kama Mwana-Kondoo aliyechinjwa (Ufu. 22:1, 3), hivyo anatuhakikishia kwamba kifo chake cha kafara kitafaa milele kwa sababu ni udhihirisho mtukufu mno wa upendo wa Mungu.

Katika kila moja ya makala zetu tatu za hivi karibuni kuhusu huduma ya meno, tulitaja kwamba katika jitihada zetu za kutafuta kuwa na afya ya kinywa bora, ya kuridhisha, ya kuvutia, yenye kutenda kazi vizuri, kuna mambo kadhaa muhimu ambayo wataalamu wanatufanyia ambayo hatuwezi kujifanyia sisi wenyewe.

 

Kwa ajili ya afya bora ya kinywa, karibu kila mtu anapaswa kumtembelea mtaalamu wa meno kwa ratiba ya mara kwa mara, kwa ajili ya kila mtu binafsi. Kama wewe ni mmojawapo wa mamilioni ya watu ambao hawana daktari wa meno wa kawaida ama kwa sababu umechagua kuwaepuka, umehamia hivi karibuni, au kwa sababu ya kizuizi kingine, unaweza kuamua kurekebisha hali hii ili kwamba kinga na matibabu ya mapema, rahisi, ya kuridhisha, na ya gharama nafuu zipate kuwa sifa ya kawaida ya uzoefu wako wa utunzaji wa meno.

 

Kwa hiyo, mtu anamtambua na kumtathminije daktari wa meno? Kwanza, "daktari yeyote wa meno," hata mwenye uwezo mkubwa, anaweza kuwa si daktari kwa ajili yako. Haiba, matarajio, na mambo mengine kama vile sera ya kliniki lazima pia vipatane. Na bila shaka, kile sisi sote tunachokitaka ni daktari wa meno anayeaminika, mwenye ustadi, mwenye huruma ambaye hufanya kazi bora kabisa.

 

Kwanza njia kadhaa za kutochagua daktari wa meno: Tovuti za rufaa mtandaoni mara nyingi ni zaidi kidogo tu ya matangazo ya kulipiwa, kwa hivyo kuwa na shaka isipokuwa utapata tovuti ya tathmini yenye maoni mengi ya wagonjwa, ambapo wengi wao ni chanya. Pia usimchague daktari wa meno kwa kigezo cha bei. Katika matibabu ya meno kama ilivyo katika mambo mengine mengi, kitu chenye gharama ndogo sana wakati mwingine kinakuja kuwa ghali zaidi hatimaye na malipo ya juu hayahakikishi ubora. Matangazo yaliyorembwa yenye kuenea kila mahali yanaweza yasiwe ya kutegemewa, pia.

 

Kuwauliza marafiki wanaoaminika ambao wana uhusiano wa muda mrefu na daktari wa meno ni mwanzo mzuri. Hasa pale ambapo marafiki kadhaa wanampendekeza daktari wa meno yule yule. Unapowasiliana na ofisi ya meno kwa mara ya kwanza, unaweza kuanza kupata hisia za mitazamo ya timu ya hapo. Je, mpokeaji anasikiliza? Je, wanajibu maswali kwa furaha kuhusu malipo, muda, na kadhalika. Je, wanaelezea sera ya ofisi na je, zinapendeza?

 

Unapokutana na daktari wa meno je, anajiamini, ni mwema, mvumilivu, na mwenye kupenda kuwasiliana? Je, unaonyeshwa hali ya kinywa chako? Je, machaguo ya matibabu yanawasilishwa na matokeo ya muda mrefu kuelezwa? Je, unaalikwa kusaidia kufanya uamuzi? Je, anaelewa upungufu wako kuhusiana na fedha au ratiba, na anapendekeza njia za kushughulikia mahitaji yako binafsi?

 

Wakati wa kuonana kwako kwa mara ya kwanza, je unaarifiwa juu ya nini kitatokea na jinsi itakavyokuathiri? Je, maoni yako yanatafutwa pamoja na hisia zako, wasiwasi wako, au mashaka yako kuzingatiwa? Je, daktari huyu wa meno ana haraka au ni mwenye subira? Je, mafunzo yanatolewa kwa ajili ya usafi wa kinywa wenye ufanisi? Je, daktari wa meno anapiga eksirei na kuchunguza fizi zako, tishu laini, na kichwa na shingo? Je, daktari huyu wa meno ni mwangalifu asipate kukuumiza?

 

Mwishowe, unapaswa kuwa na uhakika kwamba ikiwa kutatokea dharura au shida katika siku zijazo, daktari wako wa meno atakuwa msikivu, mwenye kuhusika, na wa kuridhisha.

 

Afya njema ya kinywa ni sehemu muhimu ya afya ya jumla, na tunajua kwamba Mungu kwa rehema na upendo Wake, anatutakia afya njema ya mtu mkamilifu. Tunapokuwa na afya hii, ni rahisi zaidi kuwa na "kinywa kilichojaa kicheko na ulimi wenye kelele za furaha (Zab. 126:2).

José siku zote hufanya kila kitu ambacho mke wake, Ruthie, anamwambia afanye. Naam, mara nyingi.

 

Wakati huu ilikuwa ni tofauti. Ruthie alimketisha José na kumpa sharti/kauli ya mwisho. Hakuna hiari au kukawia. Jimbo la Maryland lilikuwa likimtuma msimamizi wa ustawi wa kijamii nyumbani kwao—mtu ambaye angekuwa akikagua kila kabati, akiangalia kila mlango, na kuhakikisha kuwa nyumba yao ingefaa kuwa maskani yanayokubalika kwa ajili ya watoto wa kulea ambao walihitaji sehemu mpya ya kuishi.

 

"Wataangalia bilula/koki zetu za maji, wataangalia friji, na kuhakikisha kuwa nimesafisha uvunguni mwa vitanda," Ruthie alimwambia. "Nao, wataangalia mlango ambao unaelekea katika chumba cha chini. Ule wenye komeo lililovunjika. Mlango huo ambao nimekuwa nikikuomba uurekebishe kwa miezi kadhaa. Mfanyakazi wa ustawi wa jamii atakuwa hapa muda fulani katika siku ya Jumanne alasiri, ambayo inamaanisha kuwa utapaswa kuurekebisha mlango huo Jumanne asubuhi."

 

Mpangilio wa muda ulikuwa ni mbaya sana.

 

 

MIPANGO ILIYOBADILISHWA

Kama mkurugenzi wa Ofisi ya Wanaojitolea wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Mchungaji José Rojas alikuwa amesaidia kuwatuma watu wanaojitolea zaidi ya 100,000 ulimwenguni kote. Kwa sababu hii, Mchungaji José alikuwa amealikwa kwenye jengo la Umoja wa Mataifa huko katika Jiji la New York katika siku ya Jumanne asubuhi kusherehekea "Mwaka wa Wanaojitolea" wa Umoja wa Mataifa.

 

Badala yake, Ruthie alikuwa "akihitaji" kwamba akae nyumbani na kurekebisha mlango wa chumba cha chini.

 

Siku ilikuwa imepangwa kwa makini! Angechukua treni kutoka Baltimore kwenda katika Jiji la New York na kufurahia kifungua kinywa kwenye mkahawa wa Windows on the World juu kabisa ya jengo la Kituo cha Biashara cha Ulimwengu. Alikuwa akitamani kula kwenye mkahawa katika maghorofa haya ya Twin Towers, na hii ilikuwa ndio nafasi yake! Basi, baada ya kuiona asubuhi ikiwasili kupitia katika madirisha ya juu kabisa ya jiji, angechua teksi kwa ajili ya safari fupi ya kwenda kwenye jengo la Umoja wa Mataifa na sherehe ile maalum.

 

"Kurekebisha mlango" haukuwa katika mipango ya José kwa siku ya Jumanne.

 

Walibishana kuhusu hilo. José alielezea jinsi ilivyokuwa muhimu kwake kuwa katika sherehe hiyo. Ruthie alimkumbusha jinsi ilivyokuwa muhimu kwake kwenda katika duka la vifaa vya ujenzi. José aliomba msamaha kwa kutokutengeneza mlango ule, na kisha akamkumbusha jinsi ilivyokuwa muhimu kwake kuwakilisha Kanisa kwenye sherehe hiyo. Ruthie alikubali ombi hilo la msamaha, lakini alibaki imara kuhusu haja ya José kukaa nyumbani na kuurekebisha mlango.

 

Yalikuwa ni mabishano mabaya kabisa katika ndoa yao, na huenda ndio wakati pekee ambapo Ruthie alikuwa ametoa madai yenye msimamo kama hayo. José alisikiliza, na kuamua kwamba kwa namna fulani, kuurekebisha mlango kulikuwa ni mapenzi ya Mungu.

 

José alikaa nyumbani.

 

Badala ya kifungua kinywa katika mkahawa wa Windows of the World, alishiriki kifungua kinywa na kutazama taarifa ya habari pamoja na Ruthie kwenye meza yao ya jikoni huko Maryland.

 

Siku hiyo ilikuwa ni Septemba 11, 2001 na habari za asubuhi ziliwajaza José na Ruthie hofu na shukrani. Walitazama kwa hofu ya kutia bumbuazi huku moshi ukipanda kutoka mahali pale ambapo muda mfupi tu uliopita jeti lilikuwa limepenya katika Mnara wa Kaskazini wa Kituo cha Biashara cha Ulimwengu cha New York, chini tu ya mkahawa ule. Siku hiyo ilipata maana kubwa zaidi pale walipokuwa wakitazama ndege ya United Airlines 167 ikijigonga kwenye ghorofa ya kusini la Kituo cha Biashara cha Ulimwengu, na kuua kila mtu kwenye mkahawa ule na wote waliokuwa karibu nao.

 

"Umeyaokoa maisha yangu," yalikuwa ndio maneno pekee ambayo José angeweza kupata yeye na Ruthie walipokumbatiana sana pale jikoni machozi yakiwatiririka. Sehemu ya siku iliyobaki ilijawa na maombi, kupiga/kupigiwa simu, taarifa za habari zaidi, vipindi vya maombi ya familia, na kuurekebisha mlango.

 

 

KUSAIDIA

Katika miaka aliyofanya kazi Kanisani huko Washington, D.C., Mchungaji José pia alijitolea kama mshauri wa sera za ndani kwa marais watatu tofauti wa Marekani. Umaizi wake ulithaminiwa na chama cha Democrat na Republican, na hata sasa mara nyingi alikuwa akitumia saa zake za mchana akifanya kazi kuhusu masuala ya sera za ndani katika ofisi ndogo katika Ikulu ya White House.

 

Jumatano asubuhi, Dkt. Sung Kwon, mkurugenzi wa Huduma za Jamii za Waadventista, alimwomba Jose aende pamoja naye New York kwa gari na kusaidia kuhudumia jiji lililokuwa katika hali ya wasiwasi mkubwa. Walipokuwa wakijiandaa kuondoka, habari zilikuja kwamba Konferensi ya Kaskazini Mashariki na Greater New York zilikuwa zimepata ahadi za wachungaji zaidi ya 50 ambao wangeweza kutembelea na kuzihudumia familia za wale waliopotea katika minara ile. Walimwongeza mkurugenzi mwenza wa Huduma za Waadventista za Chaplensia, Mchungaji Marty Feldbush kwenye gari lao.

 

Kule New York, Chapleni Feldbush alikutana mara moja na wachungaji wale na kuwapa mafunzo kwa ajili ya Kitambulisho Rasmi cha Ushauri cha Msalaba Mwekundu. Punde wachungaji hawa walitanda kote jijini kusaidia familia zilizoathiriwa na msiba katika minara ile. Baada ya mkutano wa pamoja na viongozi wa konferensi, Wachungaji Kwon na Rojas waliongoza kikundi kidogo kwenda "Mahali pa Kuanzia" pa Manhattan.

 

"Mahali pa Kuanzia" ilikuwa ni rundo kubwa la kifusi na vumbi lenye sumu. Mamia ya wahudumu wa dharura walikuwa wakienda polepole ndani yake, wakitafuta kwa hamu kubwa ishara yoyote ya waliookoka. Kwa sababu maafa haya yaliamsha hisia ya kujali katika mioyo ya maelfu kote ndani ya Marekani, usalama ukawa ni jambo la kushughulisha kwani watu wengi sana walitaka kusaidia. Baadhi yao walikuwa wamejifunza sana kuhusu utafutaji na uokoaji. Wengine walikuwa ni polisi, madaktari, wauguzi, au waendeshaji wa winchi. Wengine walikuwa ni wanasiasa.

 

"Tulianzisha vituo vya msaada vikiwa na maji ya chupa, asusa au vitafunwa, matunda, milo kamili, sharubati, na maeneo ya kulia machozi," Mchungaji José anakumbuka. "Ingawa nilifurahishwa hasa na mikahawa ambayo ilitoa michango ya milo yenye protini ya thamani kubwa, ninaamini waliojitolea ambao walikuwa ni muhimu zaidi ni wale ambao walijua kutoa bega kwa ajili ya mtu kuegemea huku akilia. Waitikiaji wa kwanza na watafutaji hawakuwa wakimkuta mtu yeyote akiwa hai katika rundo la kifusi. Wazima moto wangefanya kazi kwa saa nyingi ‘katika rundo hilo,’ kisha kuja kituoni kwa ajili ya chupa ya maji, na kuanza kuomboleza bila kujizuia mikononi mwa mtu ambaye hawakuwahi kukutana naye. Mtu fulani aliyefahamu. Mtu ambaye alisikiliza. Mtu ambaye alilia pamoja nao.”

 

Wafanyakazi wote walikuwa wakipumua vumbi hilo lenye sumu ambalo bado lilikuwa likipanda kutoka kwenye jengo hilo. Asbesto, kaboni, zege, jasi, na plastiki zilizochomwa zilionekana kuwa zilitoa mvuke uliokuwa wingu nene ambalo lilifanya koo lako kukereketa na macho yako kuwasha.

 

"Kulikuwa na benki ng’ambo ya barabara ambayo chumba chake cha chini kilitumika kama ‘chumba cha kuhifadhia maiti,’ " José anafuta machozi anapoelezea mahali hapo. “Lakini kulikuwa na miili michache sana iliyokuwa mikamilifu. Wengi walikuwa wamepondwa pondwa au kuunguzwa kwa moto, na wafanyakazi mara nyingi walikuwa wakileta sehemu tu za mwili. Ulikuwa ni wakati wa kutisha.”

 

Katika rundo hilo, wazima moto walipata mwanasesere wa dubu mdogo mwekundu, ukumbusho kutoka katika duka la zawadi  Kubwa Kabisa Duniani. Kisha wengine wawili. Dubu hawa wadogo wakawa nembo za matumaini katika Mahali pa Kuanzia. Kisha Jose alipata dubu wa nne, lakini huyu alikuwa na miguu mitatu tu. Mguu mmoja ulikuwa umeraruliwa katika mlipuko huo wa moto.

 

Dubu mmoja kwa sasa yuko katika Makumbusho ya Smithsonian huko Washington DC, wengine wawili wako katika makumbusho mengine ya shambulio la Septemba 11. Dubu wa nne, yule mwenye mguu uliopotea, yuko kama ukumbusho wa daima wa jinsi Mungu anavyofanya kazi katika maisha yetu kila siku.

 

"Dubu mdogo mwenye miguu mitatu," anasema Ruthie, "hunitoa machozi siku zote, na ninamshukuru Mungu kwa kumweka José nyumbani siku ile, Septemba 11, 2001."

Amelia alikuwa kijana wa kike aliyempenda na kumwamini Yesu kwa moyo wake wote. Kwa kawaida, alipata nguvu na furaha katika urafiki wao. Lakini hivi karibuni, alikuwa na wakati mgumu. Alipoteza kazi yake, mpenzi wake wa kiume aliachana naye, na mwanafamilia ambaye alimpenda sana alifariki. Alihisi huzuni na kupotea—kitu ambacho hakuwahi kukishuhudia hapo awali. Kwa nini mambo haya yote yananitokea? alijiuliza.

 

Usiku mmoja Amelia alikaa kitandani mwake, machozi yakitiririka mashavuni mwake. Alihitaji msaada na tumaini. Aliiona Biblia yake iliyokuwa kwenye kinara chake na alipoichukua, alifungua kurasa kwa kubahatisha—bila utaratibu maalum, akiomba apate kutiwa moyo. Macho yake yalifikia Yeremia 29:11: “ ‘Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi,’ asema Bwana, ‘ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.’ ” Kidole chake kilipokuwa kinafuatilia maneno hayo, alitabasamu huku machozi yake yakiendelea kumtoka. Aya hiyo ilikuwa ndiyo kile hasa alichokihitaji. Ilimwambia kwamba Mungu alikuwa anaelewa kile alichokuwa anakipitia na kwamba hata wakati maisha yalipokuwa magumu, Mungu alikuwa na mpango kwa ajili yake, mpango ambao ulijumuisha siku zijazo zilizojawa na tumaini.

 

Amelia aliendelea kusoma. Aligeukia Mwanzo na kusoma kisa cha Yusufu. Alikuwa na maisha magumu sana! Ndugu zake walimtendea vibaya na hata kumuuza kama mtumwa. Baadaye, aliwekwa gerezani kwa kitu ambacho hakukifanya! Lakini kamwe hakupoteza imani katika mpango wa Mungu kwa ajili yake. Kupitia miujiza kadhaa ya kushangaza, Yusufu alifanywa mtawala wa pili wa juu kabisa katika Misri yote na akaiokoa nchi nzima. Amelia aliweza kuona kwamba hata katika nyakati ngumu sana, Mungu angekuwa pamoja naye, akimtengeneza na kumwandaa kwa ajili ya kitu kizuri ambacho hakuweza kukiona bado.

 

Amelia alipovuta mablanketi yake usiku huo ili kujipa joto, alimshukuru Mungu kwa kuwa alikuwa amepata ahadi ya tumaini la kushikilia. [Mungu] Hangemwacha kamwe kupambana peke yake.

 

Juma lililofuata, Amelia alijiunga na kikundi cha kujifunza Biblia kanisani kwake pamoja na watu wengine ambao walikuwa wamekabiliwa na nyakati ngumu. Walizungumza juu ya mapambano yao na jinsi walivyopata nguvu katika Yesu. Mtu fulani alisoma Warumi 8:28, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Ingawa ilikuwa ni vigumu kuelewa, Amelia alijua kwamba kwa namna fulani Mungu angeleta kitu fulani kizuri kutoka katika kile alichokuwa anakipitia.

 

Maisha hayakuwa rahisi. Baadhi ya siku zilikuwa ngumu sana, na Amelia bado alijisikia kuwa na huzuni, ingawa alijua kuwa Mungu alikuwa pamoja naye. Siku moja alisoma kuhusu mwanamke mmoja katika Biblia ambaye alijaribu kutafuta furaha katika maeneo yasiyofaa, lakini Yesu alimpa kitu ambacho kingemfanya kuwa na furaha ya kweli milele. Baada ya kuzungumza na Yesu, mwanamke huyo alisisimka sana kiasi kwamba alikimbia na kuwaambia marafiki wake wote habari Zake—jinsi alivyojua kila kitu kumhusu lakini bado akamjali sawa vile vile. Maisha ya mwanamke huyo yalibadilika kabisa. Hili lilimpa Amelia wazo.

 

Alianza kujitolea katika makao ya wanawake na wasichana wasio na makazi. Alicheza michezo pamoja nao, akawaandalia chakula, akawapeleka kufanya ununuzi na kuwaongoza katika masomo ya Biblia ya kila juma. Alipokuwa akishiriki kisa chake mwenyewe cha nyakati ngumu, aliwaambia juu ya nguvu aliyokuwa anaipata katika urafiki wake na Yesu. 2 Wakorintho ikawa kipenzi chake: "Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.”

 

Amelia aligundua kwamba wakati alipokuwa akiwasaidia wengine, hakujisikia kuhuzunika sana! Huenda hili lilikuwa ndio "mema" ambayo Warumi 8:28 ilikuwa imeahidi, au labda ilikuwa na uhusiano fulani na kushiriki na wanawake na wasichana kwenye makao haya.

 

Amelia aliendelea kutafuta uongozi wa Mungu maishani mwake. Alipata aya katika Isaya 43:1-2 ambayo ilisema, “ ‘Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.’ ” Alipata faraja katika maneno hayo. Haijalishi ni wakati mgumu upi aliokutana nao, alijua ni nani angemtegemea.

 

Huzuni yake iligeuzwa kuwa furaha kwa kuwasaidia wengine; kuvunjika moyo kwake kuligeuzwa kuwa utambuzi; na ule mnong'ono mdogo wa mashaka akilini mwake uligeuzwa kuwa imani isiyotikisika kwa sababu alikuwa amepata nguvu na utambulisho wake katika Yesu. Alikuwa ni mtoto wa Mungu, aliyependwa na kuthaminiwa kupita kiasi.

Mchapishaji

Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

 

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review

Justin Kim

 

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa

Hong, Myung Kwan

 

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World

Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi

Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun,

Dong Jin Lyu

 

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review

Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

 

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani

Enno Müller, Beth Thomas

 

Wahariri waliopo Seoul Korea
Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

 

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali

Gabriel Begle

 

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi

Daniel Bruneau

 

Meneja wa Shughuli

Merle Poirier

 

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri

Marvene Thorpe-Baptiste

 

Wahariri /Washauri wengine

E. Edward Zinke

 

Meneja wa Fedha

Kimberly Brown

 

Mratibu wa Usambazaji

Sharon Tennyson

 

Mratibu wa toleo la Kanda (Adventist World)

Penny Brink

 

Bodi ya Utawala

Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong,

Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun

Byun; Hiroshi Yamaji; Joel Tompkins; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

 

Maelekezo ya Usanifu na Muundo

Types & Symbols

 

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:

Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

 

Tafsiri

Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

 

Msomaji wa prufu

Lilian Mweresa

 

Usanifu wa toleo la Kiswahili

Daniella Batista, Ashleigh Hite, Digital Publications

 

Uchapishaji wa Kidijitali

Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

 

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu

Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott

/Types & Symbols

 

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

 

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org

Tovuti: www.adventistworld.org

 

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

 

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

 

Vol. 19, Na. 11

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Allow Send-it to use cookies?

Send-it uses cookies to track how you use the application. Find out more about what data we collect and how we use the data in our privacy policy.