powered by
send-it.me

Adventist World-Kiswahili inamshukuru kila aliyejisajili kwa ajili ya jarida hilo, kupitia kwa chaneli ya WhatsApp. Tumefurahia kupokea jumbe kutoka kwako, na vilevile ushuhuda wa jinsi umetumia jarida hili linalotia moyo kuwafikia wengine kwa ajili ya Kristo!

Tungependa kukujulisha kuwa tunahamia jukwaa jipya katika mwaka mpya. Zaidi ya yote, tungependa uhame pamoja nasi. Adventist World-Kiswahili haitaki kumwacha nyuma yeyote aliyejisajili.

 

Badala ya kupokea ujumbe wa WhatsApp pamoja na toleo jipya kila mwezi, tunakupa kiungo kwa tovuti ya bure ambayo ni nzuri kwa simu, ambapo unaweza kuyasoma makala yote, kama kawaida. Chaneli ya WhatsApp na tovuti mpya zitafanya kazi kwa wakati mmoja kwa miezi kadhaa kabla ya kuhamia hatimaye kwa chaneli mpya.

Pia tutakiweka kiungo hicho kwenye ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi, ambapo unaweza kututumia jumbe na taarifa kuhusu jinsi makala hii inakufaidi wewe na jamii yako. Pia unaweza kututumia maoni na mapendekezo tutakayoangalia jinsi ya kuifanya makala hii iwafae zaidi wasomaji!

Ukipenda, unaweza kutuma baruapepe:
charles@digitalpublications.co.za

Moja ya manufaa ya tovuti mpya ya Adventist World-Kiswahili ambayo ni nzuri kwa simu, ni kwamba kutakuwa na lugha zingine nyingi za kuchagua, ikiwa ungependelea Kiingereza au lugha nyingine yoyote, unaweza kuangalia kama ipo, kando na ile ya kawaida ya Kiswahili.

 

Manufaa mengine ni kwamba ni rahisi kushiriki kiungo hicho kipya cha Adventist World-Kiswahili, kwa marafiki na familia. Tunakuhimiza ufanye hivyo, kwa sababu tayari inafanya kazi. Hebu iangalie sasa hivi.

 

Tunatumai kuwa na uhusiano mrefu na wa furaha na wasomaji wa Adventist World-Kiswahili.

 

Mungu akubariki,

 

Kundi la Adventist World-Kiswahili

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa prayer@adventistworld.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

Shabiki yeyote atakuambia kuwa kuna viwango mbalimbali vya kuthamini sanaa yoyote. Kama wapenda vitabu wanaonusa karatasi, wakusanyaji sarafu wanaouma chuma, au mashabiki wa vyakula wanaosoma asili ya kijiografia ya kiambato mahususi, sanaa inabeba shughuli katika kiwango cha kuthaminiwa. Kama watu wa kitabu, je, Waadventista wa Sabato hawapaswi kuthamini mafundisho ya Biblia katika kiwango bora zaidi? Zifuatazo ni njia saba za kufikia kiwango hicho bora zaidi:

 

 

Sikiliza. Kwa muda, sauti ilikuwa ikitoweka. Lakini sasa, katika enzi ya vitabu vya sauti na podikasti (sauti za kidijitali), sanaa ya kusikiliza inapendwa zaidi kuliko hapo awali. Kusikiliza Neno kunaelekeza katika siku za kale wakati ambao Maandiko yalisomwa kwa sauti kubwa kwa makutano. Kusikiliza kunahitaji muda, kujihusisha moja kwa moja na sauti, na kutulia kwa subira ili kuchakata kile ambacho kimesikiwa. Tafuta rekodi nzuri yenye ubora na usikilize, yaani uisikilize vizuri.

 

Soma. Katika ratiba zetu zenye shughuli nyingi, kutumia muda kusoma kifungu kila siku, kimya au kwa sauti, kunahitaji kujitolea na nidhamu. Mitindo ya usomaji inaweza kuwa tofauti: kusoma kwa haraka, kusoma polepole kwa sauti, kupitia haraka, kusoma kwa kutafakari na maombi, au kusoma huku ukipigia mstari/kuonyesha. Kwa tafsiri mbalimbali za Biblia zilizopo, jaribu kusoma toleo tofauti kila mwaka au zaidi.

 

Andika. Ikiwa imetumiwa na waandishi wa kale, njia ya kuandika aya za Biblia inakuza maana wakati mkono unanakili kila neno. Katika enzi ya skrini za kugusa, uandishi umekuwa sanaa adimu. Lakini unapotumika katika Maandiko, huamsha tena desturi hii ya kiroho na kuiga kile ambacho waandishi wa awali walipitia. Pata shajara nzuri na uunde toleo lililoandikwa kwa mkono la kitabu unachopenda cha Biblia.

 

Elewa. Pasipo desturi hii muhimu, kila kitu ni bure. Kuelewa kunahitaji kusoma, kutambua, kulinganisha, kutofautisha, kupigia mstari, kupangilia, kuchambua, na kutafuta kujua juu ya mipangilio ya mawazo kwenye Maandiko. Lakini kubwa zaidi, kunahitaji Roho Mtakatifu ili kutoa baraka ya kufasiri kile alichokifunua.

 

Kariri. Wengi, kama watu wazima, hupoteza sanaa hii. Lakini kukariri ni jambo linalohitajika zaidi na lenye manufaa kwa wale ambao wana kumbukumbu dhaifu. Kukariri Maandiko kunaimarisha moyo na kuboresha akili. Yesu alijifunza sehemu kubwa ya Agano la Kale na kutuhimiza kudai ahadi zake katika pambano la kiroho kwa ajili ya nafsi zetu.

 

Tafakari. Wakati ambapo dini za Mashariki zinatafuta kuweka akili katika hali ya utupu, Biblia inatufundisha kujaza akili. Kutafakari huchukua aya moja (iliyokaririwa) na kuirudia huku ukitilia mkazo neno tofauti kila wakati. Kwa njia hii, mtu hupata maana kamili ya aya kwa kuangazia kila neno.

 

Fanya. Je, haya yote hapo juu yana faida gani pasipo matumizi halisi katika maisha yetu? Kweli Neno la Mungu linaweza kufanywa kuwa lenye ufanisi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu pekee. Hebu Neno lililo hai litupe shauku na moyo wa kuanza safari zetu na Neno Lililoandikwa ili kufikia kiwango bora zaidi.

Mkutano wa madhehebu mbalimbali katika kijiji cha Nueva Union, kusini mwa Meksiko, hivi karibuni uligeuka na kuwa kanisa la Waadventista wa Sabato, shukran kwa kazi ya mchungaji na walei ambao waliendelea kuzuru eneo lililotengwa na kujifunza Biblia na wenyeji wa mahali hapo.

“Ilikuwa ni njia mwafaka zaidi ya kuziba pengo kati ya kanisa na jamii ya Viziwi, hasa wakati wa tukio linalosherehekewa kiulimwengu kama Krismasi . . . Natarajia kwamba kuona hili (tukio) kutawahimiza watu kutoka jamii ya Waadventista kujifunza zaidi kuhusu fursa tulizo nazo za kuifikia idadi ya watu ambao hawajafikiwa na hata kufikiria kujifunza lugha ya ishara ya Australia (Auslan).”

–Jessica Stekla, mchungaji mkufunzi wa Konferensi ya Greater Sydney, kuhusu lugha ya kwanza ya ishara kufasiriwa kwenye maigizo yaliyoitwa Road to Bethlehem. Uigizaji huu wa hadithi ya kuzaliwa kwa Yesu ulifanyiwa katika Chuo cha Kiadventista cha Mountain View huko Sydney, Australia. Mpango huo ulihusisha ushirika kati ya Huduma za Kikristo kwa Viziwi na Wenye Matatizo ya Kusikia na shule.

Kujifunza Biblia

Zaidi ya 240

Idadi ya watu waliopokea matibabu wakati wa tukio la afya la siku tatu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Dapcha nchini Nepal. Kikundi cha Wakorea kilitoa huduma za afya, shughuli za huduma ya watoto, utembeleaji wa nyumba kwa nyumba, unyoaji wa nywele bila malipo, na picha za familia. Timu hiyo ilianzisha kliniki ya muda iliyo na vifaa vya matibabu na teknolojia. Kliniki hiyo ilitoa uchunguzi maalumu, chanjo, ushauri, dawa, na elimu ya afya.

“Kituo hiki sio tu mkusanyiko wa vitu vya kubuni; ni ushuhuda hai wa safari yetu kama kanisa. Unatumika kama chanzo cha msukumo kwa washiriki wetu wa sasa na mlango kwa wengine kuelewa utume na maadili yetu."

–Edgar Bryan Tolentino, mratibu wa Roho ya Unabii na mkurugenzi wa Kituo cha Urithi wa Waadventista katika Divisheni ya Kusini mwa Asia-Pasifiki, juu ya Kituo kipya cha Adventist Heritage (Urithi wa Waadventista). Kituo hiki kiko Silang, Cavite, Ufilipino na huhifadhi na kuonyesha ukuaji, michango, na hatua muhimu za jamii ya Waadventista katika eneo hilo.

Zaidi ya 300

Idadi ya watu waliopokea matibabu wakati wa tukio la afya la siku tatu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Dapcha nchini Nepal. Kikundi cha Wakorea kilitoa huduma za afya, shughuli za huduma ya watoto, utembeleaji wa nyumba kwa nyumba, unyoaji wa nywele bila malipo, na picha za familia. Timu hiyo ilianzisha kliniki ya muda iliyo na vifaa vya matibabu na teknolojia. Kliniki hiyo ilitoa uchunguzi maalumu, chanjo, ushauri, dawa, na elimu ya afya.

“Tuna lengo linaloendelea la kulea vijana, na hasa, ni baraka kushuhudia kikundi cha vijana cha Athene kikikua na kuwa kanisa kamili lililopangwa lenye mwelekeo wa kimishonari. Mipango yetu inahusisha kugeuza kanisa kuwa mfumo wa vikundi vya vijana ndani ya eneo la Athene, ili kuongeza juhudi zao katika kuwafikia vijana wenzao.”

–Claudio Gulyas, mwenyekiti wa Misheni ya Ugiriki, juu ya ukuaji wa kikundi cha vijana cha Athene. Wakati wa ugonjwa tandavu viongozi wa kanisa waliunda huduma ya mtandaoni kwa vijana. Kikundi hicho kilibaki kimeunganishwa baada ya ule ugonjwa tandavu na kukua, na takribani vijana 30 wanakutana kila Sabato kwa ajili ya ibada na ushirika.

1,729

Idadi ya watu waliobatizwa kwenye hitimisho la mikutano ya uinjilisti huko San Fernando na Sitio Natampod, Namnam, Ufilipino. Tukio hilo lililoanza Novemba 26 hadi Desemba 2, lilikuwa ni juhudi za pamoja kati ya Misheni ya Mindanao-Kati na Redio ya Waadventista Ulimwenguni.

“Hiki [kituo cha redio] kinajihusisha na kutoa mafunzo na kuwaandaa wanafunzi wetu kuwa viongozi wa Kikristo wanaojiamini katika jamii zao, kushiriki visa vinavyowahusu wao wenyewe, na visa ambavyo jamii zao zinaweza kuunganishwa navyo hasa kwa kina na kulingana na maisha ya mtu binafsi."

-David Garrard, mkuu wa Chuo cha Mamarapha anayemaliza muda wake, kuhusu studio mpya iliyojengwa kwenye chuo hicho kwa msaada wa Faith FM. Chuo cha Mamarapha kiko Karragullen, Australia Magharibi. Kituo cha redio kinaruhusu aina zote za Waaustralia kushiriki visa vyao katika lugha yao wenyewe.

Taasisi ya Utafiti ya Jiosayansi (GRI), kituo cha utafiti wa kisayansi cha Kanisa la Waadventista wa Sabato, kiliandaa kongamano lake la kwanza katika bara la Afrika nchini Tanzania mwezi Novemba 2023.

 

Mikutano ya uwanda huo wa utafiti huenda mbali zaidi ya vikao na hotuba ili kuwaingiza washiriki katika uzoefu wa vitendo, kuwaonyesha moja kwa moja vipengele vya asili vinavyohusiana na uelewa wa kibiblia juu ya asili. Ingawa makongamano mengi ya jinsi hiyo yamefanyika katika historia ya miongo mingi ya GRI kote katika maeneo ya Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Ulaya, na Australia, tukio hili muhimu barani Afrika liliashiria tukio muhimu la kihistoria katika ushiriki wa Taasisi na huduma kwa kanisa la ulimwengu.

 

Uamuzi wa GRI kushirikiana na Divisheni ya Afrika Mashariki-Kati (ECD) ya Kanisa la Waadventista kwa ajili ya kongamano hilo ulikazia hadhi ya Divisheni kama kanda yenye nguvu sana katika elimu ya Waadventista. Ikiwa na makadirio ya wanafunzi 750,000 katika zaidi ya taasisi 3,400, ECD inayo sababu ya kujivunia mvuto mkubwa kabisa wa elimu ya Waadventista wa Sabato ulimwenguni. Ili kuboresha mvuto wake, watu 60 walichaguliwa kimkakati kwa ajili ya kushiriki katika mkutano huo, wakiwakilisha wahusika wakuu katika elimu, wakiwemo walimu wa sayansi wa shule za sekondari, maprofesa wa sayansi kutoka vyuo vya elimu ya juu, wakurugenzi wa elimu wa Unioni, viongozi wa vyuo vikuu na viongozi wa huduma ya kampasi za umma.

 

Tanzania ilichaguliwa kwa makusudi kama usuli wa mkutano huu kwa sababu inatoa fursa kuchunguza maeneo makuu muhimu kwa matumizi ya mfumo wa kibiblia katika kuelewa vielelezo vya asili, waandaaji walisema.

 

“Mkutano wa uwanda huo wa utafiti umeanza kuonyesha matokeo chanya,” mkurugenzi wa elimu wa ECD Andrew Mutero alisema. “Hii itakuwa na mvuto katika nchi 11 za Divisheni ya Afrika Mashariki-Kati. Sasa tumepewa mafunzo, tumefahamishwa, na tumehamasishwa sana. Tunakwenda kuanza kazi mara moja.”

 

Zilizoongeza uzoefu katika kazi zilikuwa hotuba kutoka kwenye jopo la kimataifa la wanasayansi wa GRI na wawakilishi kutoka katika Divisheni za Kanisa la Waadventista ulimwenguni. Mada zilitofautiana kutoka katika marekebisho ya ulimwengu hadi kuonyesha uwiano wa hali ya juu kati ya sayansi na imani. Vikao viwili vya warsha vilishirikisha vikundi vitatu tofauti—viongozi, wanafunzi, na walimu—na kusababisha kila kikundi kuweka maazimio na malengo yanayoweza kutekelezeka kwa mwaka ujao.

 

“Waliohudhuria walikuwa kundi zuri mno kufanya nalo kazi,” Ben Clausen, mwanasayansi mkuu wa GRI na mkurugenzi wa mkutano wa uwanda huo wa utafiti, alisema. “Malengo yalikuwa kujifunza jiolojia na biolojia mpya, kuelewa masuala ya wakati yakihusiana na mifano ya historia ya dunia, kukuza mtazamo mzuri kuhusiana na sayansi na imani, na kuongeza imani kwa Mungu na Neno Lake.”

 

Mafanikio ya mkutano huo yamefungua njia kwa ushirikiano wa baadaye kati ya GRI na ECD. Mipango ni pamoja na kuanzisha ofisi ya tawi ya GRI; kuendeleza mafunzo ya cheti kwa walimu katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha Afrika katika mkingamano wa imani na sayansi; na kuwa na mfululizo wa makongamano ya mafunzo katika Divisheni yaliyopangwa kwa mwaka ujao.

 

“Namshukuru Mungu kwa mkutano huo,” alisema Alfaxad Mussa Chacha, mwalimu wa biolojia na kemia katika Shule ya Sekondari ya Ikizu nchini Tanzania. “Pamoja, tulijifunza mengi zaidi kuhusu uumbaji, na nikiwa mwanabiolojia, nitatumia fursa ya kufundisha jenetiki kuonyesha jinsi tulivyoumbwa kwa jinsi ya kutisha na ya ajabu.”

 

Mwangwi wa kongamano hilo la GRI unavuma kupitia ECD, huku washiriki wakirejea katika nchi zao, njia mpya za kuelewa mkingamano wa imani na sayansi unaangazia ushuhuda wa kanisa kuhusu Muumbaji wetu mwenye upendo, waandaaji walisema. “Tukio hili limewezesha kizazi kipya cha waelimishaji na viongozi kubeba nuru ya maarifa katika jamii zao,” walisema.

Kundi la wanafunzi pamoja na wahadhiri kutoka Shule ya Meno ya Chuo Kikuu cha Loma Linda hivi karibuni walisafiri hadi Havana, Cuba, kushiriki katika maonyesho ya kwanza ya afya ya meno. Kliniki mbili za siku nne ziliratibiwa na Unioni ya Cuba ya Kanisa la Waadventista wa Sabato na Ofisi ya Masuala ya Kidini pamoja na maofisa wa afya ya umma nchini Cuba. Zaidi ya watu 300 walipokea huduma ya meno bure wakati wa maonyesho hayo, waandaaji walisema.

 

Gary A. Kerstetter, mkurugenzi na profesa wa Shule ya meno ya Chuo Kikuu cha Loma Linda, pamoja na timu iliyojumuisha wanafunzi wa mwaka wa tatu na wa nne wa udaktari wa meno, walifanya kazi ya kuziba, kusafisha, na kung’oa meno. Madaktari wa meno Waadventista na wataalamu wachache wa eneo hilo walisaidia kazi hiyo. Kliniki hizo zilifanyika katika Seminari ya Teolojia huko Havana (SETAC) na katika Kliniki ya Afya ya Umma katika Manispaa ya Boyeros huko Havana. Timu hiyo pia ilitoa elimu ya afya ya kinywa kwa kila mgonjwa.

 

“Tumeweza kuwa sehemu ya utume kwa kazi ya udaktari wa meno, kwa kutoa uzoefu wa kitabibu kwa wanafunzi wetu ambapo wanaweza kufanya taratibu zote kwa wagonjwa na pia kuwa na fursa ya uzoefu wa tamaduni katika nchi tofauti ambako wanaweza kusaidia watu katika mazingira mengine,” Kerstetter alisema.

 

Timu kutoka Loma Linda ilileta mashine ya eksirei inayoweza kubebeka, zana za meno, na vifaa, Kerstetter alieleza. “Tulikuwa na wagonjwa sita hadi wanane walioonekana kwenye viti vitano kila siku na waliithamini sana timu yetu kwa kazi waliyoifanya juu yao,” alisema.

 

Kliniki hizo zilikuwa za kihistoria na za pekee, alisema Orquídea Ferrer Hurtado, mkurugenzi wa Christian Medical Services Network, shirika ambalo hupanga wataalamu wa afya kupitia Wizara ya Afya ya Umma ya Cuba.

 

Ferrer, ambaye pia ni profesa wa kitivo katika Shule ya Udaktari wa Meno huko Havana, alisema uingiliaji kati ulioongozwa na timu ya Chuo Kikuu cha Loma Linda ulikuwa na maana kubwa sana kwake na wataalamu kumi wa afya waliojiunga kushiriki katika kliniki za meno. “Tuliweza kusaidia na kushiriki uzoefu wa kitaaluma na jinsi mambo yanavyofanyika hapa,” Ferrer alisema. “Walijifunza kutoka kwetu, na tulijifunza kutoka kwao, na hivyo ndivyo ilivyokuwa.”

 

“Ninamshukuru Mungu zaidi na wanafunzi hawa waliokuja kutusaidia, walifanya kazi iliyotukuka sana kwangu na kwa watoto wangu,” Yaremis Leyva Ross, mkazi wa eneo hilo, alisema.

 

“Maonyesho haya ya afya yamefungua njia hapa,” Heber Paneque, mkurugenzi wa afya union ya Cuba alisema. Waumini wa kanisa na watu katika jamii walikuwa miongoni mwa wagonjwa walionufaika na maonyesho ya afya ya meno. “Tunashukuru sana na kuona jinsi ilivyofurahisha watu wengi na tunaweza kuhisi kwamba mamlaka za serikali pia zilifurahishwa na maonyesho ya afya ya kinywa,” alisema.

 

Obed Carrera, meneja wa programu wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Loma Linda kwa Huduma ya Kimataifa ya Utume, alisema kumekuwa na safari kadhaa za kwenda Cuba katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Safari nyingi kati ya hizo zilijumuisha utume wa nyanja nyingi mara mbili kwa mwaka, lakini mwaka huu umeleta namna mpya ya huduma za matibabu, alisema.

 

Krystal Robinson, ambaye alisafiri kama muuguzi wa timu hiyo na amekuwa sehemu ya mipango ya safari za utume kwenda Cuba kwa miaka kadhaa, alisema safari ya hivi karibuni imekuwa baraka. “Wanafunzi wanakumbuka uthabiti mkubwa wa watu na wana furaha, shukrani, na nia ya kukupa chochote walicho nacho ili kuonyesha shukrani,” Robinson alisema.

 

“Imekuwa safari ya kubadilisha maisha yetu,” Kerstetter alisema. “Tunatumani kuwa na fursa zaidi za kuonyesha huruma kidogo ya kibinadamu kwa watu wa Cuba.”

Novemba 1, Hearts for Mission International (H4MI), kitengo kipya cha Huduma za Walei wa Kiadventista (ASi), kilianza safari ya pekee yenye uwezo wa kubadilisha maisha ya watu wengi katika Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara. Upasuaji wa kwanza kabisa wa moyo ulifanyika kwa mafanikio katika nchi ya Malawi na H4MI katika Hospitali ya Kiadventista ya Blantyre.

 

H4MI, pamoja na timu iliyojitoa ya watumishi ishirini wa utabibu na wafanyakazi kutoka Marekani na Kenya, wakiwemo madaktari wawili wa upasuaji wa moyo na mishipa wenye uzoefu mkubwa, walifanikisha jambo kubwa la kihistoria kwa kufanya upasuaji wa moyo mara mbili juma hilo.

 

Mpango huo unalenga kutoa suluhisho la kuokoa maisha la mishipa ya moyo kwa Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, eneo ambalo linakumbwa na vifo vingi vinavyohusiana na magonjwa ya moyo na lenye uwiano wa kushangaza wa mpasuaji mmoja tu wa magonjwa ya moyo kwa kila watu milioni 14.3. Nan Wang na Arega Fekadu Leta, madaktari wa upasuaji wa moyo, pamoja na timu iliyojitoa ya madaktari, wauguzi, na wahudumu wa hospitali na viongozi, waliongoza shughuli hizi muhimu.

 

“Hadi sasa, ni wagonjwa wale tu ambao wamemudu gharama ya ndege kwenda Afrika Kusini au India ndio waliweza kupata upasuaji wa kuokoa maisha,” Mkurugenzi Mtendaji wa H4MI Jason Blanchard alisema. “Idara ya ASI Missions Inc., H4MI, ilikuja Malawi ambapo inahudumu pamoja na serikali ili kutoa huduma kwa watu wake. Kwa kweli ni kisa cha matumaini kwa nchi,” Blanchard alisema.

 

“Kwa kugusa mioyo ya watu wachache hasa, tumetoka na kugusa moyo wa taifa na watu wake,” Wang aliongeza. “Safari hii ya utume pia imebadilisha timu ya moyo kwa namna mbalimbali. Sisi sote tumebadilishwa kabisa kwa sababu tumeona imani katika matendo. . . . Tutarudi!”

 

Eliza Frank, mama wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 33, alikuwa mkulima mdogo kabla ya kupata ugonjwa wa moyo wa baridi yabisi (rheumatic heart disease). Dalili zake, ikiwa ni pamoja na kukosa pumzi na mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, ilimlazimu Frank kuacha ukulima na kumtegemea mama na dada yake kwa msaada. Kwa kuwa na uwezo mdogo wa kupata matibabu, hali ya Frank haikuwa na tumaini lolote. Hata hivyo, Frank alikuwa mmoja wa wagonjwa wawili waliochaguliwa kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha maisha, na kuwa mtu wa kwanza nchini Malawi kupokea upasuaji wa moyo.

 

Upasuaji huo ulikuwa wa mafanikio makubwa, na sasa hali ya Frank inaendelea kuimarika katika hospitali ya Blantyre. “Hatumshukuru Mungu pekee bali pia timu yetu ya kushangaza ya wafadhili na wataalamu wa matibabu waliojitoa kugeuza ndoto hii kuwa ukweli usio na kifani,” viongozi wa H4MI walisema.

 

Naibu Waziri wa Afya wa Malawi, Halima Daud, alitembelea Hospitali ya Waadventista ya Blantyre ili kuonyesha msaada wake wa dhati kwa wagonjwa na kwa timu ya H4MI. “Serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kupeleka wagonjwa India kwa ajili ya upasuaji. Kama nchi, tumefurahishwa na maendeleo haya kwa sababu inaruhusu upasuaji huu kufanywa hapa nchini Malawi,” aliandika.

 

Bado kuna kazi kubwa ya kufanywa, viongozi wa H4MI walisema. Mamilioni ya watu wengine katika eneo hilo wanaugua magonjwa ya moyo na mishipa wakiwa na matumaini kidogo ya kupona. Utafiti wa hivi karibuni ulibainisha kuwa ugonjwa wa moyo na mishipa (CVD) unapatikana kwa wastani wa watu milioni 1.3 katika Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

 

H4MI imejitoa kuendelea na kazi ya kutoa huduma ya kubadilisha maisha na mipango ya kuweka kambi nyingi za moyo nje ya nchi kila mwaka pamoja na kufungua programu ya mafunzo ya kuwapa wenyeji elimu wanayoihitaji, viongozi walitoa taarifa. “Huu ni wakati muhimu sana, na matunda ya huduma hii mpya yataonekana kwa vizazi vijavyo,” walisema.

Kundi la waendesha baiskeli Waadventista hivi karibuni lilikamilisha safari ya majuma mawili kupitia kusini mwa Papua New Guinea (PNG) na kuingia Indonesia.

 

Timu ya Huduma ya Baiskeli ya Mpakani iliundwa na wafanyakazi saba kutoka Chuo Kikuu cha Waadventista cha Pasifiki, mmoja kutoka Konferensi ya Papua-Kati, na wana wawili wa washiriki. Safari yao ilianzia Daru na kuwapitisha katika vijiji mbalimbali, ambako walikaribishwa kwa furaha na wenyeji, ambao walionyesha ukarimu wao kupitia uimbaji na uchezaji wa kitamaduni. Katika kila kijiji, timu ilitumia fursa hiyo kupumzika na kushiriki ujumbe wa Yesu na wanakijiji.

 

Video ya dakika 19 inayoonyesha safari hiyo inahifadhi matukio muhimu, ikiwa ni pamoja na kuvuka Mto Morehead, kusindikizwa na jeshi la PNG, kukutana na mkuu wa uhamiaji wa mpakani, na kutembelea kanisa la Waadventista wa Sabato huko Sota, Indonesia.

 

Video hiyo pia ina mahojiano mafupi na kamanda wa Jeshi la Ulinzi la PNG, ambaye alisema, “Kama wanajeshi, tumekula kiapo. Kiapo hicho ni kumtumikia Mungu na kuwatumikia watu wa taifa hili. Ninahisi kuwajibika kusaidia [kanisa] kwa sababu naona kwamba [katika] eneo hili . . . [watu] wanahitaji mwongozo wa kiroho na ustawi wa kiroho. Nataka kubadili mawazo yao na mtazamo wao juu ya kufikiria maisha.”

 

Mwenyekiti wa Misheni ya Kusini Magharibi mwa Papua, Martin Sungu pia ameonyeshwa kwenye video, akitoa ukaribisho kwa waendesha baiskeli kabla hawajavuka mpaka. “Huu ni wakati wa kusisimua kuona uinjilisti wa awali ukianza kwa ajili ya maandalizi ya [programu] PNG kwa Kristo,” alisema.

 

 

KUHUSU PNG KWA KRISTO

PNG kwa Kristo ni kampeni ya uinjilisti iliyopangwa kufanyika nchini Papua New Guinea. Kwa jina la “Uzoefu wa utume wa maisha yote,” viongozi wameita PNG kwa Kristo “fursa ya pekee ya kuwaleta watu karibu na Yesu.” Mpango huu mkubwa utaenea nchini kote, ukijumuisha karibu maeneo 2,000 ya uinjilisti.

 

Kwa majuma mawili, kuanzia Aprili 26 hadi Mei 12, mikutano ya usiku itafanywa ili kuwashirikisha na kuwatia moyo watu binafsi katika safari yao ya kiroho. Wakati ambapo idadi kubwa ya wahubiri watakuwa wenyeji, kuna hitaji kubwa la watu wengine wa kujitolea kutoka Australia, New Zealand, na visiwa vya Pasifiki, viongozi wa kanda hiyo walisema.

 

Waandaaji walisema hawatafuti tu wachungaji na wainjilisti bali na mtu yeyote mwenye shauku ya kushiriki ujumbe wa Kristo. Mafunzo na rasilimali zitatolewa ili kuwaandaa washiriki wote, walisema.

 

“Lengo letu kuu ni kuwaleta watu kwa Bwana –Hilo ndilo hasa kusudi la PNG kwa Kristo,” alisema Gary Webster, mkurugenzi wa Idara ya Uinjilisti wa Hadhara katika Divisheni ya Kusini mwa Pasifiki ya Kanisa la Waadventista.

 

“Tunahitaji angalau wahubiri mia tatu kutoka kote Australia, New Zealand, na visiwa vya Pasifiki. Litakuwa tukio la ajabu na la kutia moyo, na ningependa kumtia moyo yeyote anayependa kuchangamkia fursa hii.”

 

Hivi karibuni, Webster alitembelea Goroka huko PNG ili kutoa mafunzo kwa baadhi ya wahubiri ambao watashiriki kikamilifu katika kampeni ya mwaka 2024.

 

“Roho anawatia nguvu huko PNG, na tunajua kwamba roho nyingi zitaletwa katika ufalme kupitia tukio hili,” alisema. “Kwa hiyo usikose fursa hii ya kuchangia kitu cha pekee katika kuwaleta watu karibu na Yesu.”

Je, umewahi kujiuliza kwa nini msalaba uliwashtukiza wanafunzi wa Yesu? Yesu mara kwa mara aliwaambia wanafunzi Wake kwa uwazi kwamba alipaswa “kupata mateso mengi . . . na kuuawa” (Mt. 16:21; tazama pia Mt. 17:22-23; 20:17-19). Wanafunzi walipuuzaje onyo la wazi kama hilo? Je, masikio yao yalikuwa yamefungwa?

 

Wanafunzi hawakutaka kuamini kwamba Yesu angekufa. Walipinga wazo hilo (tazama Mt. 16:22-23; Marko 8:32-33). Walimtaka Yesu awe mfalme wa kidunia, bila kuangalia au kwa kusahau unabii juu ya mateso ya Masihi; kwamba atachubuliwa wakati akiponda kichwa cha nyoka (Mwanzo 3:15), “atakatiliwa mbali” (Danieli 9:26), “alijeruhiwa kwa makosa yetu” na “alichubuliwa kwa maovu yetu” (Isaya 53:5). Aya hizi zilienda kinyume na kile wanafunzi walichokiamini juu ya Masihi na labda cha muhimu zaidi, kinyume na shauku yao kuu ya kwamba Yesu angewashinda Warumi na kuanzisha ufalme wa kidunia. Hawakuwa na “masikio ya kusikia.”

 

Labda umewahi kujiuliza, ni namna gani ninaweza kuwa na “masikio ya kusikia” kile anachosema Mungu kupitia neno Lake, Biblia? Ni kwa namna gani ninaweza kuisoma Biblia kwa njia inayoruhusu Biblia kujielezea yenyewe? Makala hii inashiriki hatua rahisi na za vitendo vya namna ya kuisoma Biblia kwa uaminifu, kwa kuanza na kutafuta uongozi wa Roho Mtakatifu kupitia maombi.1

 

 

OMBA NA TAFUTA MWONGOZO WA ROHO MTAKATIFU

Hatua ya kwanza ni kuichukua Biblia kwa mtazamo sahihi, kumwomba Mungu atuongoze ili tuweze kuona ng’ambo ya matakwa na matamanio yetu wenyewe. Mwombe Roho Mtakatifu akuongoze katika kweli yote (Yohana 16:13). Kwa maneno mengine, mwombe Mungu akuondolee matamanio na uelewa wako potofu na kukupa masikio ya kusikia.

 

Baada ya Kristo kufufuka kutoka katika wafu, alijitokeza kwa wafuasi Wake wawili kwenye njia ya Emau na “akaanza kutoka Musa na Manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe” (Luka 24:27). Wakiwa katika hali ya kuumizwa na kukata tamaa na kutafuta majibu, wanafunzi sasa walikuwa na masikio ya kusikia yale Maandiko yaliyosema kumhusu Yesu.

 

Tunahitaji kuwa na dhamira ile ile ya kumsikiliza Mungu kupitia Biblia—kusikia “Maandiko yote,” hata kama kuna aya inayopingana na imani au matamanio yetu. Ellen G. White anaandika: “Kama Yesu angekuwa nasi leo, angetuambia kama alivyowaambia wanafunzi Wake, ‘Hata bado nikali ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa’ (Yohana 16:12). Yesu alitamani kuwafungulia wanafunzi Wake mawazo ya kina na ukweli hai, lakini ubinadamu wao, uelewa wao uliofunikwa na upungufu, ulifanya kushindikana. Wasingeweza kunufaika na ukweli mkuu, mtukufu na makini. Uhitaji wa ukuaji wa kiroho unafunga mlango kwa miali mikali ya mwanga inayomulika kutoka kwa Kristo. Hatutafikia wakati ambapo hakuna mwanga unaoongezeka kwetu.”2

 

Mara nyingi, tafsiri potofu za Maandiko hazitokani na kichwa, bali moyo (tazama 2 The. 2:10, 12; 2 Tim. 4:1–4). Kwa hivyo, mwombe Mungu afungue moyo wako ili kupokea mafundisho Yake.

 


CHANGANUA AYA

Kuelewa aya kunahitaji kazi, ikiwa ni pamoja na kusoma si aya moja tu, bali kusoma aya moja kwa mwanga wa aya zingine zinazoizunguka.

 

Anza kwa kuchagua ibara, kipande msingi cha maana katika Biblia. Mara nyingine, Biblia hutambulisha ibara kwa nafasi zaidi kati ya mistari au kwa kujongeza mstari mwanzoni mwa sentensi. Mara nyingi, sura ya Biblia si sawa na ibara.

 

Kisha, changanua ibara kwa hatua nne zifuatazo. Kwanza, tambua wazo kuu la ibara. Mwandishi anajaribu kusema nini?

 

Pili, fikiria jinsi mwandishi anavyoendeleza wazo hilo. Je, muundo wa mantiki wa ibara na umbo la madai yake ni gani?

 

Tatu, tambua vipengele vya kihistoria na kitamaduni vinavyoweza kuathiri maana ya aya. Uelewa bora wa mwandishi, hadhira na hali ya kihistoria unaweza kutusaidiaje kuelewa aya vizuri zaidi?

 

Nne, angalia maneno yaliyo muhimu katika ibara. Je, kuna maneno ambayo tunahitaji kuyaelewa vizuri zaidi?

 

Baada ya hili, soma ibara hiyo hiyo katika tafsiri mbili au zaidi (ikiwezekana).

 

 

CHUNGUZA MUUNDO WA FASIHI

Ili kuelewa dhima ya aya katika kufikisha ujumbe wa kitabu na ujumbe wa jumla wa Maandiko, tunahitaji kuelewa muundo wa fasihi wa kitabu ambacho ibara yetu iko ndani yake. Ikiwa ujumbe wa ibara haujitoshelezi vizuri pamoja na ujumbe wa kitabu, hii inaonyesha kuwa hatufasiri ibara kwa usahihi.

 

Ibara ni kipande cha fumbo kilicho pamoja na vipande vingine vya Maandiko. Shida ya wanafunzi ilikuwa ni kwamba, walishindwa kuamini yote ambayo manabii walikuwa wameyasema kumhusu Yesu (Luka 24:25). Kwa mfano, ikiwa tunataka kuelewa maagizo ya Paulo kwamba wanawake wanyamaze kimya kanisani, tunahitaji kutazama aya zingine zinazozungumzia wanawake kanisani.

 

Tunapofanya hivyo, tunagundua kuwa mwongozo wa Paulo ulihusiana na utaratibu wakati wa ibada na si kuzuia wanawake kuzungumza (linganisha 1 Wakorintho 14:34-35 na 14:33, 40; Luka 2:36; Matendo 21:9).

 

Kuisoma vizuri Biblia na ufafanuzi wa Biblia hutoa habari juu ya muundo wa fasihi na kazi katika utangulizi wa kila kitabu cha Biblia. Utangulizi huo unaelezea ujumbe wa kitabu na muundo wa ujumbe huo. Kumbuka, hata hivyo, kwamba ufafanuzi na maelezo ya masomo yameandikwa kulingana na dhana za waandishi wao. Tafuta wale wenye mtazamo mpana juu ya Maandiko— wanaoamini kuwa Maandiko yameongozwa na Neno la Mungu (tazama 2 Timotheo 3:16). Na daima toa kipaumbele kwa kile Maandiko yenyewe yanasema. Maandishi ya wengine yanaweza kukusaidia kuelewa mafundisho ya Biblia, lakini kamwe yasitumike kuhukumu au kuchukua nafasi ya mafundisho ya Biblia.

 

 

ZINGATIA TANZU

Kisha, zingatia aina ya uandishi (tanzu) wa aya na kitabu iliyomo. Kwa mfano, zingatia ikiwa ni hadithi au mashairi au kitu kingine (k.m., fasihi ya hekima, maandishi ya unabii, au waraka). Hii inaonyesha utofauti muhimu wa jinsi aya inavyopaswa kueleweka.

 

Kwa mfano, simulizi (kama vile Mwanzo 1 au 1 na 2 Samweli) huelezea matukio ya kihistoria, lakini mara nyingi haituambii moja kwa moja somo gani tunapaswa kuchukua kutoka kwenye simulizi hizo. Ibrahimu, Yakobo, na Daudi walikuwa na mke zaidi ya mmoja, lakini Biblia haiungi mkono ndoa za wake wengi. Badala yake, visa hivi vinaelezea tu kwa usahihi yale yaliyotokea. Tunahitaji kutazama matokeo ya matendo hayo, ambayo vitabu vyenyewe vinaelezea, ili kuelewa somo na kutafuta mafundisho mengine yaliyo wazi ya Maandiko kuhusu ukamilifu wa Mungu (tazama Mwanzo 2:24).

 

Nyaraka (barua) katika Biblia, kwa upande mwingine, hutoa mafundisho maalum, lakini huandikwa kwa hadhira maalum ya awali (taarifa zaidi hapa chini). Kwa mfano, Paulo alipomwacha Timotheo awe mchungaji Efeso (1 Timotheo 1:3), Paulo alimwagiza kutowajumuisha wajane walio chini ya miaka sitini kupokea msaada wa kanisa na akaonyesha shauku yake kwamba wajane hao waolewe na kuzaa watoto (1 Timotheo 5:9-16).

 

Hata hivyo katika Korintho, alipendekeza kuwa watu ambao bado hawajaoa na wajane wasioe ikiwa wanaweza kujizuia (1 Wakorintho 7:1-9). Paulo hakujipinga mwenyewe. Paulo alikuwa akiongea katika muktadha tofauti wa kihistoria na kitamaduni huko Efeso na Korintho.

 

Aya za mashairi hutumia lugha ya kitamathali au sitiari kuweka ujumbe akilini mwetu, lakini mashairi hayadhamirii kutoa maana ya neno kwa neno. Yesu aliposema juu ya moto wa milele au usiozimika utakaoharibu waovu, alikuwa akirejelea lugha ya mashairi ya Isaya 34:9–15.

 

Aya hiyo inazungumzia uharibifu wa Edom kama moto wa milele ulioteketeza kila kitu milele. Ni wazi kwamba moto huo haukuendelea kuwaka milele kwa kuwa aya hiyo pia inasema kuwa wanyama na ndege wangekaa katika nchi hiyo.

 

 

CHUNGUZA MUKTADHA WA KIHISTORIA NA KITAMADUNI

Ni muhimu kuelewa maadili ya kitamaduni, desturi, alama, na vitendo vinavyohusiana na aya ili kuelewa maana yake kwa usahihi. Kwa mfano, tunashindwa kuelewa vizuri kisa cha Msamaria mwema tunaposahau kikwazo cha kitamaduni na kisheria kinachowazuia makuhani kugusa mwili wa marehemu yeyote isipokuwa jamaa zao wa karibu (tazama Mambo ya Walawi 21:1–4). Vivyo hivyo, tutaelewa vibaya vitendo vya Ruthu (tazama Ruthu 3:6–15) au maelekezo ya Paulo kuhusu kufunika kichwa (tazama 1 Wakorintho 11:2–16) ikiwa hatuelewi desturi za kitamaduni na kisheria za wakati huo.

 

Unaweza kujifunza zaidi kuhusu muktadha wa kihistoria na kitamaduni wa aya kutoka kwenye kamusi nzuri ya Biblia au ufafanuzi wa Biblia. Hata hivyo, daima weka kipaumbele kwa kile Biblia inachofundisha kuhusu historia na utamaduni unaohusiana na aya.

 

Kwanza, tunahitaji kuelewa aya katika muktadha wa historia ya binadamu. Kwa mfano, tunahitaji kuelewa nyaraka za Paulo katika muktadha wa historia ya kanisa kama ilivyoelezwa katika Matendo. Hatutaelewa Wagalatia bila kuelewa kilichotokea kwenye baraza la Yerusalemu (tazama Matendo 15). Vivyo hivyo, hatuwezi kuelewa vizuri Danieli 8 na 9 bila kuzingatia unabii wa Yeremia. Vile vile, kitabu cha Malaki kinaeleweka vyema katika muktadha wa maisha na huduma ya Nehemia.

 

Pili, tunahitaji kuelewa aya katika muktadha wa historia ya wokovu. Njia bora ya kuelewa hatua za Mungu katika uhusiano Wake na binadamu ni kusoma kisa cha Maandiko. Umaizi mzuri juu ya kisa hiki unapatikana katika magombo matano ya Mfululizo wa Pambano la Zama Zote yaliyoandikwa na Ellen White (Wazee na Manabii, Manabii na Wafalme, Tumaini la Vizazi Vyote, Matendo ya Mitume, na Pambano Kuu).

 

 

CHUNGUZA MAANA YA MANENO MUHIMU KATIKA AYA

Unaweza kuchunguza kwa kina maana ya maneno muhimu katika aya kwa kutumia orodha ya maneno au Biblia ya kidijitali.3 Orodha za maneno zinaorodhesha matumizi ya kila neno na mwandishi wa Biblia au katika Biblia yote.

 

Tunapoelewa namna ya maneno muhimu katika aya yanavyotumika katika sehemu zingine za Biblia, inatusaidia kuelewa vizuri dhana, watu au mada za Biblia. Kwa mfano, utafutaji wa neno “mchungaji” hutusaidia kuelewa kwamba Yesu alipojiita “mchungaji mwema” (Yohana 10:11), alidai kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa Yahweh, akija kuokoa kondoo Wake walioteswa na kutawanywa (tazama Zaburi 23; 80:1; Yeremia 23; Ezekieli 34).

 

Zaidi, kila mtu anayezungumza lugha zaidi ya moja anajua kwamba lugha tofauti mara nyingine hazina usawa kamili kwa maneno fulani. Kwa mfano, neno la Kigiriki teleios linamaanisha “kamili,” lakini pia “pevuka,” “kua," na “kuanzishwa.” Hivyo, “ukamilifu” katika Agano Jipya haimaanishi kabisa kitu sawa na inavyomaanisha katika Kiingereza. Maelezo mazuri yanaweza kukusaidia katika suala hili. Pia, kuna tovuti huru zinazotoa njia ya kufikia maneno ya asili ya Biblia yanayoweza kutumiwa hata na wale ambao hawawezi kusoma lugha hizo.4

 

 

SOMA BIBLIA NA WATU WENGINE

Mungu anatuagiza kukusanyika pamoja kusoma Maandiko na kutiana moyo (Ebr. 3:13; 10:25; 1 The. 5:27; 1 Tim. 4:13). Kuisoma Biblia na watu wengine ni muhimu kwa sababu inatusaidia kuona dhana na upofu wetu wenyewe. Tunaposoma Maandiko pamoja na kuyachunguza kwa umakini, tunaweza kusaidiana kuelewa kwa kina na kwa undani zaidi.5

 

 

TENDA KILE ULICHOJIFUNZA

Hatimaye, utii ni hatua muhimu katika kuelewa Maandiko. Yesu alisema kwamba wale wanaochagua kufanya mapenzi ya Mungu watapata kujua kweli (Yohana 7:17).

 

Hili lilikuwa jambo lililotokea kwa wanafunzi walipokuwa kwenye njia ya Emau. Walipomsihi Yesu akae nyumbani mwao, wakimaanisha kuwa wamekubali ujumbe Wake na wakitaka zaidi, “yakafumbuliwa macho yao” na wakamtambua (Luka 24:31). Kwa upande mwingine, Maandiko yanaeleza kwamba upungufu mkubwa wa wale watakaodanganywa mwishoni mwa nyakati hawatapungukiwa maarifa bali ukosefu wa upendo wa ile kweli (tazama 2 Wathesalonike 2:9–12).

 

Hatua ya kwanza kuelekea udanganyifu si ujinga bali ni ukosefu wa utayari wa kutii. Yesu aliwafananisha wale wanaosikia maneno Yake na kuyafanya na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mafuriko yalipokuja na upepo kuvuma, nyumba yake ilisimama imara. Wale wanaosikia maneno ya Yesu na hawayatendi, aliwafananisha na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. Upepo wa mafundisho ya uongo ulipovuma, nyumba yake ilianguka (tazama Mathayo 7:24–27).

Zaidi, Paulo anawaonya kwamba “utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo” (2 Timotheo 4:3-4).

 

Kadiri tunavyotenda kile tunachojifunza, ndivyo tunavyoelewa zaidi na kuanza kumpenda Mungu. Upendo ulioongezeka utawezesha ongezeko la uelewa. Tunapopitia uzoefu wa kweli ya Neno Lake, unazalisha hata ujasiri zaidi kwamba Neno Lake ni kweli na ahadi Zake ni hakika. Tunapopata uzoefu wa wema wa Neno la Mungu, hatutahitaji—kwa kweli, hatutaweza—kunyamaza. Kama vile wanafunzi wa Emau.

Roho Mtakatifu ni kiini katika utume wa Mungu. Kwa hiyo, tunahitaji uelewa wa kibiblia kuhusu utambulisho na asili ya Roho Mtakatifu. Fundisho hili la Biblia linashughulikia maswali muhimu yafuatayo: Je, Roho Mtakatifu ni nafsi au ni nguvu tu ya Mungu? Je, Roho Mtakatifu ni tofauti na Baba na Mwana (Kristo)? Je, Roho Mtakatifu ni Mungu kweli?

 

Ili kujibu swali la kwanza, lazima tukubali kwamba neno “nafsi” katika muktadha huu halimaanishi nafsi ya binadamu au aliye na ukomo wa kimwili kama wanadamu walivyo. Badala yake, tunamaanisha yule aliye na sifa binafsi ambazo watu pekee ndiyo wanazo kama vile uwezo wa kujitambua, mantiki na kuamua.

“Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi” (Efe. 4:30).

 

“. . . na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1 Kor. 2:11).

 

“Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye” (1 Kor. 12:11).

Roho Mtakatifu:

Anaweza kuwa  _________________.

__________________ vitu vya Mungu.

Akigawa karama kwa kila mmoja kama Yeye _________________

 

Haya na maandiko mengine ya kibiblia yanamwelezea Roho Mtakatifu pamoja na sifa za nafsi. Kani tupu au nguvu haiwezi kuhuzunika (inahitaji kujitambua), haiwezi kujua mambo ya Mungu (inahitaji mantiki) na haiwezi kuamua kutoa karama za kiroho kwa watu (inahitaji uamuzi).

“Kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kusema” (Luka 12:12).

 

“. . . kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum 8:26).

 

Ni nafsi pekee ndizo zinazoweza kuhuzunika (Efe. 4:30), kujua (1 Kor. 2:11), kupenda (1 Kor. 12:11), kufundisha (Luka 12:12), kuombea (Rum. 8:26), kushuhudia au kuwa shahidi (Yohana 15:26), kudanganywa na kujaribiwa (Matendo 5:3-4, 9), kusema (Matendo 8:29), kuonya (Neh. 9:30), kuongoza (Zab. 143:10; Matendo 8:29), wito wa huduma na kwenda (Matendo 13:2-4), kukataza au kuruhusu (Matendo 16:6-7), na kadhalika.

 

Hapa na mahali pengine, Maandiko yanamtambulisha Roho Mtakatifu kama nafsi, ikimrejelea Roho Mtakatifu kuwa na sifa ambazo zinapatikana kwa watu tu.1

“Lakini huyo Msaidizi, huyu Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote niliyowaambia” (Yohana 14:26).

 

Roho Mtakatifu (Msaidizi) ametumwa na ______ kwa jina la _____________.

 

“Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia” (Yohana 15:26).

Roho Mtakatifu (Msaidizi) ametumwa na ______________ kutoka kwa ______________.

 

Kwa kutumwa na Baba kwa jina la Yesu (Yohana 14:26) na kutumwa na Yesu kutoka kwa Baba (Yohana 15:26), Roho Mtakatifu hawezi kuwa Baba wala Mwana, bali ni tofauti na Baba na Mwana.

 

Kwa hiyo, Maandiko yanafafanua kwamba Roho Mtakatifu si sawa na Mwana (Kristo) wala Baba (au sehemu ya mmoja au wote wawili). Roho Mtakatifu ni nafsi bainishi (tazama pia, Mt. 12:32; Luka 3:21-22; Yohana 14:16).

 

Zaidi ya hayo, tutaona kuwa Maandiko yanamtambulisha Roho Mtakatifu kama mtu wa namna ya Mungu pamoja na Baba na Mwana, ambaye kwa jina Lake waumini wanabatizwa (Mathayo 28:19).

“. . . Roho Mtakatifu alinena vema na baba zenu, kwa kinywa cha nabii Isaya” (Matendo 28:25).

Kulingana na Biblia, maneno ambayo aliyanena Mungu katika Isaya 6:8-10, yalinenwa na ____ _____________.

 

Vivyo hivyo, Waebrania 3:7 inanukuu maneno yaliyonenwa na Mungu katika Zaburi 95:7-11 kwa kusema “kama Roho Mtakatifu anenavyo.” Maandiko haya na mengineyo yanamrejelea Roho Mtakatifu kama Mungu.

“Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako?

 

Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu” (Matendo 5:3-4).

 

Anania alipomdanganya Roho Mtakatifu, hakuwa amemdanganya ____________, bali ___________.

 

Kumdanganya Roho Mtakatifu, basi, ilikuwa kumdanganya Mungu. Hivyo, Maandiko yanamrejelea Roho Mtakatifu kama Mungu (tazama pia, Mathayo 28:19). Mungu pekee ndiye wa milele, mwenye maarifa yote (omniscient), na yupo kila mahali (omnipresent), na bado Roho Mtakatifu anarejelewa kuwa wa milele (Ebr. 9:14), mwenye maarifa yote (1 Kor. 2:10-11), na yupo kila mahali (Yohana 14:16) na hivyo lazima awe wa Mungu.

 

Kulingana na Maandiko, basi, Roho Mtakatifu ni nafsi (mwenye sifa binafsi), Roho Mtakatifu ni tofauti na Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu ni Mungu—mmoja wa nafsi tatu za milele za Mungu.2

Toleo hili la Adventist World linajadili somo lenye umuhimu mkubwa—Neno la Mungu. Maandiko Matakatifu ndiyo njia kuu ambayo Mungu huwasiliana nasi—ni Neno Lake, zawadi Yake kwetu kwa nyakati zote. Ni kupitia Maandiko ndipo Anafunua Yeye alivyo, jinsi gani anatupenda, historia yetu na mpango Wake wa wokovu, jinsi ya kuishi maisha yenye furaha, tumaini letu la baadaye na mengi zaidi. Kwa hakika, kama alivyosema Mtunga-zaburi, “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105).

 

Katika Injili ya Yohana, tunasoma kauli hii ya ajabu katika sura na aya ya kwanza: “Hapo mwanzo kulikuwako na Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, na Neno alikuwa Mungu” (Yohana 1:1).

 

Maelezo mazuri yaliyoje juu ya Yesu, Mwana wa Mungu na Mwana wa mwanadamu, mchanganyiko kamili wa binadamu na Mungu. Hatuelewi kikamilifu jinsi hii inavyowezekana, lakini tunajua kuwa iko hivyo. Na, Yesu Kristo ametupa maneno Yake ya uzima kupitia Maandiko Matakatifu, yaliyo hai, Neno la Mungu lenye nguvu (Ebr. 4:12). Akizungumzia Maandiko, Yesu alithibitisha, “hayo ndiyo yanayonishuhudia” (Yohana 5:39).

 

Biblia ni ujumbe wa Mungu uliotolewa kwa wanadamu, kwa lugha ya wanadamu, kupitia watu waliovuviwa na Mungu, kama 2 Petro 1:21 inavyoeleza: “bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”

 

 

MSINGI IMARA

Maandiko Matakatifu ni msingi ambao kwa huo ndiyo kama Waadventista wa Sabato tunategemeza imani zetu zote. Ndiyo maana Imani yetu ya Kwanza Kabisa ni “Maandiko Matakatifu.” Inasema: “Maandiko Matakatifu, Agano la Kale na Jipya, ni Neno la Mungu, lililoandikwa, lililotolewa kwa ufunuo wa Mungu. Waandishi waliovuviwa walinena na kuandika kama walivyoongozwa na Roho Mtakatifu. Katika Neno hili, Mungu amewapatia wanadamu ujuzi unaohitajika kwa ajili ya wokovu. Maandiko Matakatifu ni ufunuo wenye uwezo wa juu kabisa, wenye mamlaka, na usioweza kukosea wa mapenzi yake. Ni kipimo cha tabia, kipimo cha uzoefu wa kiroho, mfunuaji wa hakika wa mafundisho, na kumbukumbu ya kuaminika ya matendo ya Mungu katika historia.”1

 

Kuna maandiko mengi yanayothibitisha uzuri na nguvu ya Maandiko. Katika Mithali 30:5, 6 tunasoma ahadi na onyo hili: “Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.”

Isaya 8:20 inashuhudia, “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.”

Katika Yohana 17:17, tena tunamsikia Yesu akithibitisha umuhimu wa Maandiko anapowaombea wanafunzi Wake, akimsihi Baba yake wa Mbinguni “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”

 

Katika barua kwa Wathesalonike, mtume Paulo anawaambia waumini, “Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini” (1 The. 2:13).

 


KUAMINI KILE BIBLIA INACHOSEMA

Biblia inafunua ukweli wa Mungu na kutuleta karibu Naye tunapofuata mashauri Yake matakatifu yaliyoelezwa kwenye kurasa zake za thamani. Lakini ili kusikia kwa hakika Mungu anavyosema, lazima tutazame Maandiko tukiamini kwamba kwa hakika ni, “ufunuo wa mapenzi Yake wenye mamlaka ya juu kabisa na usiokosea.”2

 

Tunatahadharishwa katika kitabu, Pambano kuu:

“Ukweli ambao umefunuliwa kwa uwazi katika Biblia umetiliwa mashaka na kuwekwa giza na wasomi, ambao, kwa kujifanya kuwa wana hekima sana, hufundisha kuwa Maandiko yana maana ya kiroho ambayo ni fumbo, siri, isiyofahamika katika lugha iliyotumika. Watu hawa ni walimu wa uongo. Ilikuwa ni kwa tabaka kama hili Yesu alitamka: ‘Hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu’ (Marko 12:24). Lugha ya Biblia inapaswa kueleweka kulingana na maana yake ya wazi, isipokuwa pale ambapo ishara imetumiwa au kielelezo kimetumiwa. Kristo ametoa ahadi: ‘Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo.’ Ikiwa watu wangeielewa Biblia kama inavyosomeka, ikiwa wasingekuwepo walimu wa uongo wanaopotosha na wanaochanganya akili za watu, kazi ingefanyika ambayo ingewafurahisha malaika na ambayo ingeleta maelfu kwa maelfu kundini ambao kwa sasa wanatangatanga katika makosa.”3

Kwa masikitiko, leo hii katika sehemu fulani tunashuhudia ukosefu wa kuielewa Biblia na jinsi ya kuifasiri, pamoja na upinzani halisi dhidi ya Neno la Mungu.

 

Lakini, Kanisa la Waadventista wa Sabato linaamini katika uhalisia na mamlaka ya Neno la Mungu—Biblia Takatifu, na linazungumza kwa watu wote, kila mahali, kwa wakati wote. Kama inavyoonyeshwa katika hati yake rasmi iliyoidhinishwa, “Mbinu za Kujifunza Biblia,” Kanisa linakubali njia ya kihistoria ya kibiblia au njia ya kihistoria ya kisarufi ya kufasiri Maandiko tu, ikiruhusu Biblia kujifasiri yenyewe mstari kwa mstari, aya kwa aya, amri kwa amri, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.4

 

Kwa bahati mbaya, kuna wale wanaotumia njia ya ukosoaji ya kihistoria na njia nyingine za kibinadamu za ufasiri wa Kibiblia ambazo hazijajikita katika Mungu. Kwa kutumia njia ya kihistoria ya ukosoaji, msomaji ndiye anayeamua kuwa ukweli ni upi na upi siyo. Hii ni njia isiyoaminika sana ya kusoma Neno Takatifu la Mungu, kwa sababu, kama Yeremia 17:9 inavyoonyesha, moyo wa binadamu “ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?”

 

 

MUNGU AMETOA USHAHIDI WA KUTOSHA

Nakuhimiza kumruhusu Roho Mtakatifu kuwaongoza katika kuyaelewa Maandiko. Tumia tu njia ya kihistoria unapotaka kuelewa unabii wa Biblia. Si ile ya mwanzo (preterist), si ile ya mambo yajayo, si ile ya ukosoaji wa kihistoria, bali njia ya kibiblia ya kihistoria ya kuelewa Neno la Mungu.

 

Katika kitabu cha Spiritual Gifts tunasoma: “Mungu ametoa ushahidi wa kutosha unaoweza kuwa msingi wa imani ikiwa mtu anataka kuamini. Katika siku za mwisho dunia itakaribia kabisa kufilisikiwa na imani ya kweli. Katika kujifanya tu, neno la Mungu litachukuliwa kuwa lisiloaminika, wakati mawazo ya kibinadamu yatakubaliwa, ingawa yanapingana na ukweli dhahiri wa Maandiko.”5

 

Ndugu zangu, msije mkashawishiwa na wale walio ndani au nje ya kanisa wanaolipuuza, kulikashifu au kulidhalilisha Neno la Mungu. Kama Waadventista wa Sabato, tunasimama imara katika uelewa dhahiri na kukubali Neno la Mungu lote kama lilivyoandikwa.

 

Ninawatia moyo kutumia wakati pamoja na Mungu katika Neno Lake kila siku, mkiweka pembeni mawazo yote yaliyotangulia na kumwomba Roho Mtakatifu awaongoze. Mtapata thawabu kubwa.

“Kila andiko, lenye pumzi  ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” Neno la Mungu limejumuisha kila kitu muhimu kwa ajili ya kumkamilisha mtu wa Mungu. Ni kama ghala la thamani, lenye hazina iliyosheheni vito vya thamani; lakini hatuthamini utajiri wake, wala hatutambui haja ya kujitayarisha kwa hazina za kweli. Hatuoni umuhimu na haja kuu ya kujisomea wenyewe Maandiko. Wengi huzembea kujifunza ili kutimiza matamanio yao ya kidunia au kuendekeza anasa zinazopita. Mambo madogo yamefanywa kisingizio cha ujinga wa kutojua Maandiko.

 

 

MAELEKEZO MATAKATIFU

“Yalitolewa kwa pumzi ya Mungu,” “hutufanya kuwa na hekima kwa ukombozi,” kumtafsiria mtu wa Mungu “kamili, amekamilishwa apate kutenda kila jambo jema,” Kitabu cha vitabu kina madai ya heshima ya hali ya juu yanayochukua usikivu wetu. Mafundisho ya juu-juu tu hayawezi kuyafikia madai yaliyomo juu yetu, wala hayawezi kutupatia faida zote zilizoahidiwa.

 

Tunapaswa kutafuta kujifunza maana kamili ya maneno ya kweli na kujazwa na roho wa maneno matakatifu. Kusoma kila siku baadhi ya sura au kukariri baadhi ya Maandiko akilini, bila tafakuri ya kina ya maana yake, kutanufaisha kidogo.

 

Kujifunza ibara moja mpaka umuhimu wake uonekane kwa uwazi akilini, na uhusiano wake katika mpango wa wokovu umethibitika, ni wa thamani zaidi kuliko kusoma sura nyingi bila makusudi maalum na kutoka bila maelekezo chanya. Hatuwezi kupata hekima kupitia Neno la Mungu kama hatutaweka bidii ya maombi na umakini katika kujifunza. Ni kweli kwamba baadhi ya sehemu katika Maandiko ziko wazi sana kueleweka visivyo; lakini kuna maana nyingine nyingi ambazo haziwezi kuonekana kwa mara moja, kwa kuwa ukweli haujengwi kwa mtazamo wa nje tu. Ili kuelewa maana halisi ya aya hiyo, andiko linapaswa kulinganishwa na andiko lingine, uchunguzi wa kina na tafakari ya maombi mengi vinahitajika. Usomaji wa aina hii utakuwa na manufaa makubwa. Kama mchimba madini anavyogundua mwamba wa madini uliojificha chini ya sura ya nchi, kwa hiyo yeyote atakayetafuta Neno la Mungu kwa uvumilivu kama hazina iliyositirika, ataupata ukweli wa thamani kubwa, ambao ulisitirika kwa watafutaji wasio makini.

 

Lakini kama hutafanya mafundisho matakatifu ya Neno la Mungu kuwa kanuni na mwongozo wa maisha yako, ukweli hautakuwa na maana yoyote kwako. Ukweli huwa na maana pale unapofanyiwa kazi katika maisha. Kama Neno la Mungu litalaani baadhi ya tabia ulizoziendekeza, hisia ulizozilea, roho iliyojidhihirisha, usiende mbali na usimamizi mtakatifu; lakini mbali na uovu wa matendo yako na mwache Yesu asafishe na kuutakasa moyo wako. Kiri makosa yako, na kata shauri la kuachana nazo kabisa, ukiamini ahadi za Mungu na kuonyesha imani yako kupitia matendo yako. Kama ukweli wa Biblia utafanywa kivitendo katika maisha, utainua akili zetu kutoka ulimwenguni na katika mawazo hafifu. Wale waliosadikishwa kwa Maandiko watakuwa wanaume na wanawake wenye mvuto adilifu. Katika kutafuta ukweli wa mbingu uliofunuliwa, Roho wa Mungu husogezwa katika uhusiano wa karibu na moyo. Na uelewa wa mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa huikuza akili, huijaza, huiadilisha na kuijalia nguvu mpya, kwa kuleta uwezo kwa kukutana na ukweli wa ajabu. Hakuna usomaji ulio na manufaa katika kuipa nguvu akili, kukuza uwezo wa kufikiri, kama usomaji wa Neno la Mungu. Hakuna kitabu kilicho bora zaidi katika kuadilisha fikra na kutoa nguvu ya akili, kama Biblia, ambayo imekusanya kweli adilifu. Ikiwa Neno la Mungu lingesomwa kama inavyotakiwa, tungeona uwezo mkubwa wa akili, ustahimilivu wake katika lengo na uadilifu wa tabia.

 

 

USOMAJI WA KINA

Lakini usomaji wa Biblia umepewa kipaumbele cha pili na hasara kubwa imeendelea. Uelewa huchukua kiwango cha mambo yanayofahamika. Kama wote wangelifanya Biblia kuwa somo lao, tungeliona watu walioendelezwa vyema, wenye uwezo wa kutafakari kwa kina, ambao wangedhihirisha akili kubwa kuliko wale waliosoma kwa bidii sayansi na historia ya ulimwengu, mbali na Biblia. Biblia humkarimu mtafutaji halisi wa kweli nidhamu ya akili ya juu, naye hutoka katika tafakuri ya mambo ya Mungu hali amejazwa kiakili; nafasi ikiwa imenyenyekezwa, wakati Mungu na kweli yake iliyofunuliwa wameinuliwa. Ni kwa sababu wanadamu wamefahamu historia za thamani za Biblia, kiasi kwamba heshima kubwa hupewa mwanadamu na heshima kidogo hupewa Mungu.

 

Biblia inajumuisha kile ambacho kitamfanya Mkristo awe imara kiroho na kiakili. Mtunga zaburi anasema “kufafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga.” Biblia ni kitabu cha ajabu, ni historia inayotuonyesha karne zilizopita, bila ya Biblia tungebakia na dhana ya pamoja na hekaya kuhusiana na mambo yaliyotukia katika zama zilizopita. Ni unabii unaofunua ya siku za usoni. Neno la Mungu ndilo lifunualo kwetu juu ya mpango wa wokovu, likituonyesha njia ambayo kwayo tunaweza kuepuka kifo cha milele. Haitupatii historia ya ulimwengu huu pekee, bali pia maelezo ya ule ujao. Ina maelekezo kuhusu maajabu ya ulimwengu; na inadhihirisha juu ya fahamu zetu kuhusu tabia mwumbaji wa mbingu na nchi. Ndani yake ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu.

 

Utafiti wa vitabu vyote vya falsafa na sayansi hauwezi kufanyia akili na maadili kile ambacho usomaji wa Biblia unaweza kufanya, ikiwa utafanywa kivitendo. Yeye asomaye Biblia hufanya mazungumzo pamoja na wazee na manabii. Yeye huja karibu na kweli zilizositiriwa katika lugha iliyoinuliwa, inayoweka mvuto wenye nguvu na kuinua mawazo kutoka katika mambo ya duniani na kuyaelekeza katika utukufu ujao wa maisha ya milele. Ni hekima gani ya wanadamu inayoweza kulinganishwa na ufunuo wa ukuu wa Mungu? Mwanadamu mwenye ukomo asiyemjua Mungu, hutafuta kushusha thamani ya Maandiko, akidai kuwa ujuzi wake dhahania wa sayansi hauwezi kupatana na Neno la Mungu; lakini Neno hili takatifu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Maelezo ya Mhariri: Hadithi hii imetoholewa kutoka kwa Heart-warming Stories of Adventist Pioneers, na marehemu Norma J. Collins.

 

Heman na Eliza Gurney walikuwa waumini wa kwanza wa akina Miller na marafiki wa Joseph Bates. Walikuwa miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kuikubali Sabato na kuwa wafadhili wakubwa wa James na Ellen White, hata kugharamia nusu ya gharama ya uchapishaji wa maono ya Ellen White “To the Little Remnant Scattered Abroad” (Kwa Masalio walio Wachache Waliosambaa Nje).

 

Ingawa inajulikana kidogo kumhusu Gurneys, hadithi chache zimejitokeza kutoka kwa maisha ya Heman yanayohusisha mashua na mkono wa Mungu wa muujiza. Lifuatalo ni mojawapo ya tukio kama hilo.

 

 

MASHUA KURUDI NYUMBANI

Heman alikuwa mwashi akifanya kazi kwa Bw. Sherman na Bw. Hall huko West Island, karibu na pwani ya Fairhaven, Massachusetts, Marekani. Bw. Sherman alikuwa amemwambia kijana Heman ajisikie huru kuazima mashua yake wakati wowote aliotaka kwenda nyumbani kutembelea.

 

Akiwa amekumbuka sana kwenda nyumbani siku moja, Heman alipata ruhusa ya Bw. Sherman kuchukua mashua kwenda bara na kuwaona wazazi wake. Alipanga kurejea siku inayofuata. Ukungu tayari ulikuwa umetanda juu ya maji, lakini aliifahamu njia vizuri sana kiasi kwamba hakuogopa kupotea. Baada ya kusafiri maili tatu kama alivyodhania, kwa ghafla alisikia sauti ikipiga kelele “Geuza mwelekeo! Geuza mwelekeo!” ambayo inamaanisha, Toka njiani! Kwa haraka akikwepa ili kuona chini ya tanga, Heman aliona mashua ikiwa juu yake. Alijaribu kuondoka lakini akapita chini ya boriti la mashua. Milingoti na kamba zake zinazoishikilia zilizolewa mbali na mashua ilipinduka kwa sehemu.

 

Mabaharia kwenye mashua nyingine walimchomoa Heman kutoka baharini na kumburuta ndani. Alipata aibu alipokuwa akijaribu kueleza alichokuwa akikifanya kwenye mashua ndogo siku yenye ukungu sana. Watu wale walijaribu kuivuta mashua ndogo, lakini baada ya umbali mfupi kamba ilikatika, na wakalazimika kuiacha kwenye upepo na mawimbi. Heman alihisi kuugua. Alikuwa na uhakika kuwa ikiwa mashua itapatikana, itakuwa mwishoni mwa West Island, ikiwa imevunjika vipande vipande kwenye miamba.

 

Mashua iliyomkanyaga na kisha kumwokoa kutoka kwenye maji yenye kasi ilimpeleka New Bedford, Massachusetts. Akiwa na hofu kwamba marafiki zake huko West Island wangekuwa na wasiwasi juu yake, kwa haraka Heman alipita nyumbani kuchukua kofia nyingine—alikuwa ameipoteza ile aliyokuwa nayo alipoingia majini—kisha kwa haraka akaendelea na safari yake. Hisia zake za kukumbuka nyumbani ziligeuka kuwa hofu na kiwango fulani cha woga alipokuwa akijaribu kufikiria atakavyomwambia Bw. Sherman. Atawezaje kueleza kwamba mashua ya rafiki yake ambayo alikuwa ameazimwa ilikuwa imepotea au imevunjika vipande vipande kwenye miamba?

 

Takribani maili tano chini ya ufukwe, alijikuta mkabala na West Island. Kwa sasa ilikuwa inakaribia jioni, lakini alifanikiwa kupata mmiliki wa mashua wa eneo hilo ili kumchukua kwenda kwenye gati ya mashua ya Hall. Hili lilifanyika kwa usalama, na mtu aliyemrudisha alifanikiwa kurudi kabla ya giza ambalo lingemzuia kuona.

 

Heman hakujua vizuri kwa nini alijali, lakini aliamua kukagua mashua ya Sherman kwenye gati kabla ya kwenda nyumbani. Kulikuwa na ile mashua ndogo, imefungwa vizuri na kwa usalama katika mahali pake pa kawaida. Hakuweza kuamini macho yake! Itawezekanaje? Polepole aliichunguza kutoka mbele hadi nyuma. Ilionekana kama jambo lisilowezekana, lakini hakukuwa na uharibifu wowote. Ilileta mkanganyiko lakini cha kufurahisha ni Heman Gurney aliyelala usingizi mzito usiku huo licha ya siku yake ya kutisha.

 

Asubuhi iliyofuata, alijua lazima akutane na Bw. Sherman. Baada ya kusalimiana, alifanikiwa kugugumia, “Vizuri, ummm, naona ulipata mashua yako ikiwa salama.”

 

“Kupata mashua yangu?” aliuliza, akiwa ni mwenye mkanganyiko.

“Unamaanisha nini? Ipo hapa.”

 

Kwa kutanafusi, Heman alielezea yote yaliyotokea.

 

Bw. Sherman hakuwahi kufikiria juu ya mashua tangu Heman aondoke nayo; hata hakujua ilikuwa imepotea. Lakini bado ilikuwa mahali pake, bila uharibifu, salama na imara.

 

Miamba midogo-midogo inazunguka West Island. Wakati wa maji kupwa, baadhi ya miamba inaonekana, lakini wakati wa maji kujaa, inafunikwa. Kuna njia moja tu—takribani mita 11 upana—ambayo mashua inaweza kupita salama. Kwenye gati, mawe yalipangwa upande, kufanya njia rahisi yenye upana wa takribani mita tano (mita 4.5) ili kuvuta mashua.

 

Hiki kwa kweli kilikuwa ni kitendawili. Kijana na mzee kwa pamoja walijua hakukuwa na njia ya mashua kupita kwenye njia nyembamba inayoongoza kwenye nchi kavu. Hata kama ingekuwa hivyo, hakuna mtu aliyekuwepo kuiongoza na kuifunga.

 

Hakukuwa na shaka akilini mwa Heman kwamba “mjumbe asiyeonekana” alitwaa jukumu la mashua pale alipoiacha. Alishangazwa na kunyenyekezwa kufikiria kwamba malaika wa mbinguni waliteuliwa kumtunza.

 


MTU WA VITENDO

Heman S. Gurney alikuwa mtu wa maombi na vitendo. Mara kadhaa katika maandishi yake, Ellen White anamtaja kwamba alikuwepo wakati ombi likitolewa kwa ajili ya kuponya wagonjwa. Mada kuu ya maisha yake ilikuwa kuwaambia wengine kuhusu kuja kwa Bwana na kuwasaidia kuwa tayari.

Heman hakuwa na kipaji tu katika fuawe lake, bali pia alikuwa na sauti nzuri ya kuimba ambayo mara nyingi ilisikika alipokuwa akifanya kazi katika karakana yake ya uhunzi. Anajulikana katika jamii ya akina Miller na duru za Kiadventista kama mhunzi anayeimba, na alikuwa mwimbaji pendwa aliyeimba kama mwimbaji binafsi katika mikutano ya uinjilisti.

 

Kundi kubwa la wanaoshika Sabato lilikuwa limeanzishwa huko Memple, Michigan, na Heman na Eliza walihamia huko mwaka 1865. Kwa miaka 30 alikuwa mzee wa kanisa mahalia, akiangalia kundi, akifanya masuala yao kuwa yake. Hata alihudumu kama mwenyekiti wa Konferensi ya Michigan mwaka 1869. Alipendwa ndani ya kanisa na jamii.

 

Baadaye afya yake ilianza kudhoofika, na wakati ulifika alilazimika kukabidhisha majukumu yake kwa mtu mwingine. Alifariki Agosti 4, 1896, na akazikwa akiwa na uhakika wa “tumaini lenye Baraka” la kukutana na Bwana wake atakapokuja kuwachukua walio Wake.

 

Hadithi ya maisha ya mwanzilishi huyu aliyejitolea, kutoka mwanzo hadi mwisho ni, ukumbusho kwamba nguvu ya kanisa la Waadventista wa Sabato iko katika maisha na kazi za “watu wachache”—wale wasiojulikana na wasiosifiwa, lakini wanaokwenda kimya-kimya kutekeleza kazi ya Baba yao ya kuokoa roho kwa ufalme Wake.

Kujifunza desturi za enzi za kale za Mashariki ya Karibu kunaweza kuwa na manufaa katika kutambua mfanano na tofauti kuhusiana na maandiko haya ya Biblia. Mada uliyoileta inaweza kuwa mojawapo ya desturi hizo. Hapa, Biblia inatoa mtazamo wake maalum.

 

 

DHANA ZA ENZI ZA KALE ZA MASHARIKI

Katika enzi za Kale za Mashariki yote, wafalme walichukuliwa kuwa ni wana wa mungu/miungu. Huko Misri, Farao alichukuliwa kuwa mwana wa mungu na hivyo aliaminiwa kuwa ni mungu. Bado kuna mjadala iwapo katika sehemu zingine za Mashariki ya kale wafalme walichukuliwa kuwa ni miungu. Baadhi ya wasomi, wanaoshawishiwa na dhana za Mashariki ya kale, wamependekeza kwamba wafalme wa Israeli pia walichukuliwa kuwa wa kiungu. Ukweli ni kwamba nje ya Misri, ushahidi wa uungu wa wafalme si mwingi, kumaanisha kwamba ufalme wa kiungu si mtazamo wa kawaida huko Mesopotamia, Ashuru na labda Kanaani. Cheo cha “mwana wa mungu” kiliwatambulisha wafalme kama wawakilishi halali wa miungu, labda na sifa kadhaa na majukumu.

 

 

MFALME WA ISRAELI

Kwa ujumla wasomi wanakubaliana kwamba huko Israeli, cheo cha kifalme “mwana wa Mungu” hakimaanishi kwamba mfalme alikuwa wa kiungu, bali wakati wa sherehe ya kumweka mfalme madarakani, mfalme aliasiliwa kama mwana wa Mungu. Zaburi 2:7 inachukuliwa kuwa aya kuu: “Ndiwe Mwanangu, leo nimekuzaa.” Maneno haya yanachukuliwa kuwa fomula ya kuasili iliyotamkwa na muasili ili kumiliki kisheria. Huu ni msimamo wa kati katika tafsiri ya cheo hicho, ambao, ingawa unawezekana, unahojiwa na wengine. Hakuna ushahidi wa matumizi maalum ya hii “fomula ya kuasili” katika Agano la Kale na wala haikutumiwa hivyo katika Mashariki ya Kale.

 

Tunapata lugha ya jinsi hiyo huko Misri ikitumiwa kwa Farao, lakini katika jambo hili linaelezea dhana halisi la mfalme kama mungu.

Katika Zaburi 2:7, neno “mwana wa Mungu” linatumiwa kisitiari, kama linavyoonyeshwa na neno sambamba “leo nimekuzaa.” Hili si kuhusu kuzaliwa kwa kawaida au kuasili, bali ni kuhusu matumizi ya lugha kuonyesha wakati ambapo mtu, kwa kusema hivyo, “alizaliwa” kama mfalme kwa maana ya kuteuliwa na Mungu kama mtumishi wake kupitia kutiwa mafuta (aya ya 2).

 

Lugha ya kifamilia hutumiwa kuelezea uhusiano mpya uliowekwa kati ya Mungu na mfalme (2 Sam. 7:14; Zab. 89:27). Mfalme mpya “aliyezaliwa” yuko chini ya ulinzi na utunzaji wa Mungu. Labda mfano mzuri ni tangazo la Mungu la Israeli kama mwana wa Mungu (Kut. 4:22, 23), ambalo lilifanya wao kuwa watu wa Mungu. Dhana kuu ni uteuzi wa Mungu na si lazima kuasiliwa.

 

 

Mwana wa Mungu na Masihi

Kuna mifano kadhaa linganifu ya matumizi ya cheo “mwana wa Mungu” huko Israeli na mataifa mengine. Hata hivyo, wafalme walitekeleza majukumu mengi yaliyo sawa. Ni jambo lenye uwezekano mkubwa kwamba huko Israeli, cheo hicho kilikuwa na maana ya kimasihi tangu mwanzo, kikiashiria ujio halisi na wa pekee wa Mwana wa Mungu, ambaye alikuwa ni Mungu halisi (linganisha Zab. 45:6; Isa. 9:6). Mkondo wa kibiblia wa Mwokozi anayekuja unaanza na ahadi ya mwana iliyotolewa kwa Adamu na Hawa (Mwa. 3:15). Katika visa vya wazee wa imani, ahadi ya mwana inatoa kamba inayounganisha (kwa mfano, Mwa. 12:7; 15:3-4). Pamoja na kuanzishwa kwa ufalme, Mungu anaweka pamoja ufalme na ahadi ya Mwana wa kimasihi (linganisha 2 Sam. 7:12-14; 1 Nya. 17:11-13), ambayo inatimizwa katika Imanueli, Mwana wa mwanamke na Mwana wa Mungu (Mt. 1:23; Luka 1:32).

Matumizi ya mlo kamili wa mbogamboga ni sehemu muhimu ya Ujumbe wa Afya wa Waadventista. Chakula si sehemu pekee muhimu kwa mtindo wa maisha ya kiafya, ingawa inaonekana kuwa inapata umuhimu zaidi kuliko mazoea mengine ya kiafya—pengine ni kwa sababu chakula chetu ni dhahiri na kinaweza kupimika. Hii inaweza kusababisha mazungumzo makali na hata mabishano yanayoleta mgawanyiko. Tunapoteza sehemu bayana ya faida ya mazoea ya ulaji uliopimwa wa kiafya tunaporuhusu vita vya chakula kutugawa.

 

Uko sahihi kabisa; lazima tutilie mkazo faida za kuwa na uhusiano chanya na msaada wa kijamii.

 

Katika mwanzoni mwa miaka ya 1950, Abraham Maslow alipendekeza piramidi ya mahitaji ya binadamu, akisisitiza kwamba upendo ni muhimu kwa ukuaji mzima wa binadamu kama vile vitamini, madini, na protini. Kanisa letu ulimwenguni limejikita haswa katika faida za afya za kuwa na uhusiano tangu mwaka 2002, wakati Idara ya Afya ya Konferensi Kuu ilipoanzisha mpango wa afya ikitumia ufupisho wa CELEBRATIONS®: Choices, Exercise, Liquids, the Environment, Belief, Rest, Air, Temperance, Integrity, Optimism, Nutrition, Social Support1 (Chaguzi, Mazoezi, Vimiminika, Mazingira, Imani, Mapumziko, Hewa, Kiasi, Uadilifu, Matumaini mema, Lishe, Msaada wa Kijamii). Zingatia kuwa msaada wa kijamii ni mojawapo ya vipengele muhimu.

 

Kwa muda mrefu, watafiti wa sayansi ya jamii wamekuwa wakiandika zaidi kuhusu faida za uhusiano chanya wa kijamii. Hawako peke yao. Watafiti wa saratani wameonyesha kuwa wanawake walioko katika uponaji wa saratani ya matiti wanapunguza hatari ya kurudiwa na ugonjwa huo wanapopata msaada mkubwa wa kijamii kutoka kwa familia na marafiki. Utafiti wa ki-epidemolojia, kisaikolojia, kijamii na wa afya unaendelea kuthibitisha umuhimu na faida zote za kijamii katika maisha yetu kwenye magonjwa ya moyo. Watafiti maarufu wa mtindo wa maisha2 wanasisitiza upendo (uhusiano) kama dawa, kudumisha tabia njema!

 

Uhusiano wenye afya na muungano ni msingi katika kujenga uthabiti hasa kwa vijana. Uthabiti ni uwezo wa kudumisha kazi bora mbele ya msukosuko mkubwa wa maisha na ni lengo kuu la mkutano wa Youth Alive3 kwa kanisa letu unaowatia moyo vijana kuishi maisha kamili yenye afya bila tabia hatarishi. Sifa makinifu katika kukuza uimara ni kukuza uhusiano wa karibu na angalau mtu mmoja wa umuhimu (mzazi-mtoto; mwanafunzi-mwalimu; mume-mke).

 

Uhusiano binafsi, unaowezesha uhusiano na Mungu, unafungulia uwezekano wa umuhimu mkubwa katika uhusiano na wengine.

 

Tunapotekeleza Amri Kuu ya kwenda ulimwenguni kote kuhubiri, kufundisha na kuponya, Ellen White anatutia moyo kutunza uhusiano tunapofuata njia ya Kristo katika kuwafikia watu: “Ikiwa tutajinyenyekeza mbele za Mungu, na kuwa wema na wenye heshima na wenye adabu na wenye moyo mwepesi wa kuhurumia, kutakuwa na uongofu mia moja kwa ukweli ambapo sasa kuna mmoja tu.”4

 

Uhusiano mzuri na upendo na muunganiko ni ushahidi wa uhusiano wetu na Yesu kama alivyothibitisha, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:35). Na, tutafurahia maisha kwa ukamilifu!

“Ilikuwa kwenye mfuko wangu dakika chache zilizopita!”

 

Wapiga picha mara nyingi hubeba vitu vingi sana. Kamera, tripodi, lenzi ndefu, lenzi fupi, lenzi zumu, kisafisha lenzi, betri za ziada. Changamoto ni kuweka kila kitu unachoweza kuhitaji kwenye mfuko mdogo iwezekanavyo, wakati unajitahidi kuwa na mfuko mwepesi ili usikupunguzie mwendo unapopanda mlimani.

 

Kwa kuwa nilikuwa tayari nimetumia saa moja njiani na kufanya maamuzi kamili kuhusu nilichotaka kukipiga picha, niliacha mfuko kwenye gari na kubeba tripodi nzito peke yake, kamera moja, na lenzi mbili. Lenzi moja ilikuwa lenzi zumu, ikiruhusu nipige picha kwa upana au kuzumu ndani kidogo kwa ukaribu. Lenzi ya pili ilikuwa lenzi ndogo ya pembepana iliyotosha kwa urahisi kwenye mfuko wa jaketi langu.

 

Nilipanga kutumia lenzi ya pili kwa picha maalum, moja ambayo ingejumuisha majani mafupi ya dhahabu chini na yaliyo membamba juu ya mti wa msonobari. Kama ndivyo, picha ingeonyesha jinsi Mungu alivyoumba miti pamoja na majani kwa ajili ya kuishi katika miamba mirefu kando ya kilima kirefu sana.

 

Ndiyo, iliogopesha. Ili kupata picha hiyo, nililazimika kulala chini, kuegemea juu ya ukingo wa kilima, kuweka kila kitu sawa kwenye sehemu ya kutafutia mandhari na kisha kushikilia pumzi yangu nilipobonyeza shata ya kamera. Yote haya bila kusogeza tripodi.

 

Nilijaribu kupiga picha na lenzi yangu ya kawaida, lakini haikuweza kupiga picha pana zaidi. Kisha nikawa nachukua lenzi yangu ndogo kwa ajili ya pembepana kwenye mfuko wangu wa jaketi.

 

Haikuwepo!

 

 

HAIONEKANI

Mawazo yangu yaliangazia katika siku, kukumbuka mahali nilipokuwa, mahali nilipoiona lenzi hiyo kwa mara ya mwisho na nini ningekuwa nimefanya! Mbaya zaidi, nilianza kufikiria mahali ambapo inaweza kuwa imeanguka kutoka mfukoni mwangu, na umbali ambao ingeweza kuwa imeanguka chini. Mara moyo wangu ukahisi huzuni sana.

 

Ilikuwa bado kabla ya macheo, na hakuna mtu mwingine niliyeongozana naye katika kilele cha Wolf Creek Pass. Hivyo, niliacha kamera na tripodi pale vilipokuwa salama kutoka kwenye ukingo wa kilima chenye futi 2,000-na polepole nikatembea kurudi kwenye gari.

 

Nilitazama chini, ardhini ambapo miguu yangu ilisimama, kuzunguka mawe yote, na hata chini ya mimea michache iliyoota karibu na njia. Niliangalia vizuri, hadi mwisho mahali ambapo gari langu lilikuwa limeegeshwa kwenye kituo cha Wolf Creek. Eneo hili lina urefu wa futi 11,000, juu kutosha kupunguza pumzi yangu. Na kutembea kwangu.

 

Kwenye gari, nilifanya uchunguzi kamili wa gari na vifaa vyangu vya kamera. Niliangalia chini ya viti, katika buti la gari, na kuangalia kwenye kila mfuko na kasha la lenzi hadi nilipojua kwa hakika kwamba lenzi haikuwa ndani ya gari. Haikuwa lenzi ya gharama sana, nilijisemea, lakini bado ilikuwa imenigharimu kiasi cha fedha, na nilijua nisingeweza kumudu kupata mbadala.

 

Lenzi ilikuwa imepotea. Imetoweka. Ikiwa imejificha chini ya kichaka karibu na njia. Au, mbaya zaidi, ilikuwa imeanguka kutoka mfukoni mwangu. Niliwaza, ikiwa inaruka mawe na kupita juu ya miti yote mpaka chini ya bonde la futi 2,000 chini.

OMBI LILILOJIBIWA

Sina uhakika ni muda gani nilianza kuomba. Inawezekana ni wakati ule nilipogundua kuwa lenzi haipo. Kwa haraka ingekuwa, “Bwana, tafadhali nisaidie kuipata lenzi hii,” ombi la namna hiyo. Sasa nilikuwa nikiomba. Kwa kina. Kwa dhati. Kwa maneno mengi. Ombi la namna ya kudhamiria tumaini.

 

“Bwana. Ninahitaji lenzi hii leo na sina dola 300 ili kununua nyingine. Ninasikitika na kuhuzunika kwamba sikuwa mwangalifu. Ikiwa bado ipo hapa pembezoni mwa kilima, tafadhali nionyeshe. Tafadhali nionyeshe . . .”

 

Nilifunga gari na kuanza safari ndefu na ngumu kurudi kwenye kamera yangu na tripodi.

 

Utafutaji wangu na maombi vilichukua muda mrefu, mpaka watalii walianza kufika. Wengi wao walitazama uzio wa usalama chini kwenye bonde, wakijipiga picha wenyewe kwa kamera ya mbele, wakirudi kwenye magari yao, na kuondoka. Wenzi fulani walikuwa tofauti. Walikuwa “wakitafiti,” na wakapita karibu nami walipoelekea kwenye ukingo ambapo tripodi yangu ilikuwepo. Nilijiunga nao, na waliponiuliza, nikawaonyesha mahali nilipofikiri kuwa ni bora kwa picha yao ya kamera ya mbele ambayo ingewafanya waonekane kama mbuzi wa mlimani.

 

Nilifurahia mazungumzo, lakini daima nilikuwa nikigeuza macho yangu kwenye maeneo ambayo ningeweza kuwa nimeangusha lenzi yangu. Hakukuwa na kitu.

 

Niliwasaidia wenzi hao kuseti picha bora sana kwa ajili ya kamera ya mbele na kisha kuwaonyesha picha niliyokuwa nimeitarajia—majani madogo ya njano chini, mti mwembamba unaokua kwenye mwamba juu, jabali refu hadi kwenye konde la majani chini sana. Walipenda.

 

Nilipoigeukia tripodi yangu na kamera, kiatu changu kiligonga jiwe dogo na kukirusha kwenye jabali. Macho yangu yalifuatilia, na hapo, upande wa kulia wa mti mdogo wa msonobari, kulikuwa na kipande kidogo cha kasha la lenzi nyeusi kilichopiga kelele “Canon.”

 

Sote watatu tulifurahia!

 

Nilitembea polepole sana, nikitambua kuwa mwendo wowote unaweza kuondoa lenzi kutoka kwenye mahali ilipokuwa. Kipande kimoja cha mzizi wa mti wa msonobari kilizuia kuidondosha kutoka juu futi 2,000. Kuiona, na kisha kuipoteza, ingekuwa mbaya zaidi kuliko kutoipata kabisa!

Sasa nilitambaa, nikienda polepole, pamoja na marafiki wawili wakinipa moyo kwa kuninong’onezea, mpaka lenzi ilipokuwa yangu tena!

 

“Ni lazima unamjua Mungu vizuri sana,” rafiki alisema kwa tabasamu.

 

“Ananijua,” nilijibu. “Na mimi najifunza.”

 

Wenzi hao waliondoka, na nikaketi karibu na kamera yangu kwa muda mrefu. Nilitafakari. Niliomba Maombi Makubwa; Maombi ya Shukrani. Maombi ya Urafiki. Maombi ya Sifa. Yote yaliombwa kwa sauti kwa Rafiki yangu wa karibu.

 

Nikaenda juu kwenye tripodi yangu, nikabadilisha lenzi, na kupiga picha. Ni picha Yake. Yule anayejali. Hata kuhusu lenzi ndogo za pembepana.

Mama, kwa nini tunaenda nyumbani kwao Halima?” Clara alikuwa na hamu ya kutaka kujua. Hakuwahi kufika kwenye nyumba ya familia ya wakimbizi hapo awali. “Naam, mpenzi,” Mama akajibu huku akiongoza gari kukata kona za barabara, “familia yake ina furaha kwa jinsi ambavyo tumekuwa tukiwasaidia kuweka mambo yao vizuri na wanataka kusema asante!”

 

“Ni kama nina wasiwasi,” Clara alinong’ona. “Kwa nini mpenzi?” Mama aliuliza. “‘Siwajui,” Clara alijibu. “Itakuwaje kama sijui cha kusema? Itakuwaje kama hawawezi kunielewa?”

 

“Ni wema, Clara,” sauti ya Mama ilikuwa ya kutia moyo. “Halima ana binti wawili wa rika lako. Nadhani utawapenda.”

 

Ilikuwa vigumu kwa Clara kueleza alivyokuwa akihisi kwa Mama. Mama alikuwa akiisaidia familia ya Halima kwa muda kwa vitu walivyohitaji. Clara alikuwa amesaidia hata kuchagua vifaa vya usafi kwa ajili ya familia hiyo. Hiyo ilifurahisha. Na alipanga nguo zake na midoli na kuchagua vitu ambavyo alitaka kuwapa watoto wa Halima. Lakini kwenda nyumbani kwao? Hilo lilikuwa jambo tofauti kabisa!

 

Familia ya Halima walikuwa wakimbizi Waislamu kutoka Afghanistan. Clara hakuwa na uhakika kabisa hiyo ilimaanisha nini. Alijua kwamba walikuwa na imani tofauti na yeye na alijiuliza kama angeona sanamu zozote katika nyumba yao.

 

Clara alichezacheza kwa woga na mkanda wake wa kiti. “Clara, usijali! Utakuwa sawa,” Mama alimhakikishia kutoka kwenye kiti cha mbele cha gari. “Ni watu wema!”

 

“Je, ni lazima nile tukiwa huko?” Clara alikuwa na wakati mgumu kujaribu vyakula vipya. “Itakuwaje kama sivipendi?”

 

“Kidogo tu,” Mama alimthibitishia. “Kunapaswa kuwa na wali na mkate, kwa hivyo hakika utakuwa na kitu cha kula!” “Lakini vipi ikiwa sijui la kuzungumza nao?” Clara aliuliza. Alikuwa na aibu kwa watu wageni. “Jihusishe pamoja nao na tabasamu.

 

Utafanya marafiki wajisikie vizuri,”

 

Mama alinyoosha mkono wake nyuma na kushika mkono wa Clara. “Hebu tuombe juu ya hili, mpenzi.” “Sawa,” Clara aliitikia kwa sauti ya chini. Mama aliomba, “Yesu Mpendwa, Clara ana wasiwasi kuhusu kumtembelea Halima na familia yake. Tafadhali kuwa pamoja naye na umpe amani yako. Msaidie kufahamu kwamba Unampenda na utamtunza. Na Yesu, tafadhali tusaidie kuwa baraka kwa Halima na familia yake.”

 

Punde Mama alisimama mbele ya safu nyingi za nyumba zilizo na njia fupi za kuingia. Zilionekana za ajabu kwa Clara. Haikuwa kama nyumbani kwao milimani kwenye barabara ndefu na miti mingi. Mama alimkumbatia Clara huku wakishuka kwenye gari. “Utakuwa sawa, mpenzi,” alimthibitishia. Kisha wakatoa zawadi yao kwa ajili ya familia ya Halima kutoka kwenye buti la gari na kutembea kuelekea mlango wa mbele.

 

Halima aliwakaribisha kwa tabasamu. Clara aliitazama nyumba kwa mshangao mkubwa. Haikuonekana kama vile alivyotarajia.

 

Kulikuwa na zulia la rangi na michoro ya kupendeza juu yake. Makochi meupe ya ngozi, meza ndogo za vioo na dhahabu, na kioo kikubwa kilichokuwa ukutani kilikifanya chumba hicho kionekane angavu na cha kuvutia. Hakukuwa na kitu chochote cha kutisha, lakini vyote vilikuwa tofauti sana na nyumbani kwa Clara kwenye samani za mbao, piano, na kochi laini la kahawia.

 

“Huyu ni Beheshta na Samira,” Halima alisema, akiwaashiria wasichana wawili wadogo. Walikuwa warembo na ngozi yao ya rangi ya kahawia na nywele nene nyeusi. “Je, ungependa kuja chumbani kwetu?” Yule mkubwa aliuliza huku akitabasamu, “Nenda,” Mama alimsukuma Clara taratibu. Clara aliwafuata taratibu wale wasichana wawili juu ghorofani akijaribu kukumbuka majina yao. Wasichana hao walimkaribisha chumbani kwao.

 

“Je, unataka kufanya ufundi na sisi?” Beheshta alishika kisanduku cha shanga za rangi angavu.

 

“Sijui jinsi ya kufanya,” Clara alisema, akitazama chini kwenye vidole vyake vya miguu. Kusema kweli, hakupenda shanga. Kila mara zilianguka kutoka kwenye uzi kabla hajamaliza, na hii ilimfanya ajisikie vibaya.

“Tutakuonyesha,” Samira alicheka. “Siyo ngumu.” Alichomoa baadhi ya waya nyembamba na kumuonyesha Clara jinsi ya kuzifunga zile shanga.

 

Mwanzoni, vidole vya Clara vilihisi kulegea kwa kutumia shanga hizo ndogo lakini ikawa rahisi alipokuwa akifanya mazoezi.

 

Haikuchukua muda mrefu Mama akawaita Clara na wasichana waje kula. Clara alijisikia furaha alipotazama chakula kilichokuwa mezani. Kulikuwa na chakula chenye harufu nzuri, lakini pia kulikuwa na mkate na wali na saladi. Baada ya chakula cha jioni, wasichana walirudi ghorofani kuchora picha. Clara alipenda jambo hilo zaidi na alishangazwa Mama aliposema ulikuwa wakati wa kurudi nyumbani.

 

“Mama, Waislamu ni nini?” Clara aliuliza walipokuwa wakiendesha kuelekea nyumbani. Alishangaa kidogo! Hawakuwa tofauti kama alivyofikiria. “Ni watoto wa Mungu kama sisi tulivyo. Wanaamini katika Mungu Muumbaji na kumwita Mwenyezi Mungu (Allah),” Mama alieleza. “Lakini hawaamini kwamba Yesu alikuwa Mungu. Wanafikiri kuwa alikuwa nabii mkuu. Pia wanafuata kitabu kiitwacho Kurani badala ya Biblia.”

 

“Kwa hiyo wanamwamini Mungu?” Clara alitaka kujua. “Ndiyo,” Mama alijibu, “lakini hawaelewi kikamilifu upendo wa Mungu au jinsi Yesu alivyokuja kutuokoa kutoka katika dhambi zetu. Tumepewa jukumu la kuwaonyesha upendo wa Yesu.”

 

Ilibidi Clara afikirie hilo kidogo. “Nimefurahi sana kwenda kuwatembelea Halima na familia yake!” hatimaye alisema. “Beheshta na Samira ni wema.” Mama alitabasamu.

 

“Kwa hiyo, unafikiri ungependa kuwatembelea tena?” Clara alicheka. “Nafikiri naweza kufanya hivyo. Tulikuwa na wakati mzuri wa furaha pamoja.”

Mchapishaji

Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

 

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review

Justin Kim

 

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa

Hong, Myung Kwan

 

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World

Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi

Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun,

Dong Jin Lyu

 

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review

Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

 

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani

Enno Müller, Beth Thomas

 

Wahariri waliopo Seoul Korea
Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

 

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali

Gabriel Begle

 

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi

Daniel Bruneau

 

Meneja wa Shughuli

Merle Poirier

 

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri

Marvene Thorpe-Baptiste

 

Wahariri /Washauri wengine

E. Edward Zinke

 

Meneja wa Fedha

Kimberly Brown

 

Mratibu wa Usambazaji

Sharon Tennyson

 

Mratibu wa toleo la Kanda (Adventist World)

Penny Brink

 

Bodi ya Utawala

Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong,

Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun

Byun; Hiroshi Yamaji; Joel Tompkins; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

 

Maelekezo ya Usanifu na Muundo

Types & Symbols

 

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:

Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

 

Tafsiri

Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

 

Msomaji wa prufu

Lilian Mweresa

 

Usanifu wa toleo la Kiswahili

Daniella Batista, Ashleigh Morton, Digital Publications

 

Uchapishaji wa Kidijitali

Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

 

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu

Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott

/Types & Symbols

 

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

 

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org

Tovuti: www.adventistworld.org

 

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

 

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

 

Vol. 20, Na. 2

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Allow Send-it to use cookies?

Send-it uses cookies to track how you use the application. Find out more about what data we collect and how we use the data in our privacy policy.